Correspondance Course - Lesson 04

Swahili

INJILI

Somo la 4

Somo: Isaya 55

Habari Njema

Kila mtu anafurahi kusikia ‘habari njema’. Na hivi ndivyo hasa habari ya Injili ilivyo. Neno Injili maana yake ni “Habari Njema”

Vitabu vinne vya kwanza vya Agano Jipya mara nyingi vinaitwa ‘Injili’, kwa sababu ya habari njema iliyopo ndani yake. Ni habari njema inayomhusu Bwana Yesu Kristo. Alikuwa ni Mwana wa Mungu na alizaliwa na bikira Mariamu...

 

 

 

Hivi ni sehemu tu ya habari njema!

Yesu hakutuonesha tu jinsi Mungu alivyo, na upendo na wema wake, bali ametuonesha pia uweza wake katika miujiza aliyofanya. Lakini kitu cha kushangaza kuliko vyote ni kwamba, Yesu hakuwahi kufanya dhambi. Kwa kuwa hakukosa, alifufuliwa katika wafu.  Ni mtu pekee ambaye amewahi kufufuliwa kutoka kwa wafu, anayeendelea kuishi.

Hii sio Habari Njema kwa Bwana Yesu Kristo tu, ni Habari Njema kwetu sisi wote. Kwa kufa na kufufuliwa kwake, Yesu ameifungua njia kwetu sisi wanadamu wadhambi, ya kuweza kusamehewa dhambi zetu. Ametupa tumaini la uzima baada ya kufa. Kwa hiyo habari njema ni kwamba, sio lazima kwetu kuendelea kuishi katika hali mbali tuliyonayo. Mungu ametuonesha njia ya kutuwezesha kuiepuka dhambi na mauti.

Lakini kuna zaidi ya hilo

Bwana Yesu Kristo yupo mbinguni kwa sasa, lakini muda si mrefu atarudi tena duniani. Katika Ufunuo tunaambiwa: “Tazama, yuaja na mawingu, na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma, na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam, Amima” (Ufun.1:7).

Atakaporudi katika dunia hii, Yesu Kristo atausimamisha Ufalme wa Mungu hapa ulimwenguni. Dunia itakuwa wakati huo mahali tofauti kabisa. Tunaambiwa kutakuwa:

  • Hakuna tena vita
  • Hakuna tena njaa
  • Hakuna tena majonzi
  • Hakuna tena dhambi
  • Hakuna tena mauti

Bwana Yesu Kristo atakapokuwa ndiye Mtawala-Mkuu wa dunia, haki itastawi na kutakuwa na amani. Ardhi itakuwa ikizalisha sana, hivyo kwamba njaa itatokomea moja kwa moja. Mauti itamezwa na ushindi. Nabii Isaya, akiusemea wakati huo, anasema:

“BWANA Mungu atafuta machozi katika nyuso zote, na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote, maana BWANA amenena hayo” (Isaya 25:8).

Mungu atatupa nafasi katika Ufalme wake huo duniani. Ni zawadi kubwa sana hii anayoitoa kwetu. Kwa vyovyote kuna masharti yake, na ndio maana tunahitaji kulisoma Neno la Mungu, Biblia, ili tuweze kujua kile Mungu anachokitaka tufanye kwa sasa katika maisha yetu.

Injili ilifahamika kwa watu wakati wa Agano la Kale

Tunaambiwa kuwa, Injili ilihubiriwa kwa Ibrahimu! (Wagalatia 3:8). Kutokana na imani na utii aliokuwa nao, Mungu alifanya ‘maagano’ naye ya muhimu sana. Alimuahidia urithi wa nchi ya Israeli milele. Ibrahimu alizeeka na kufa bila ya kurithi kipande chochote cha ardhi Mungu aliyomuahidi.

Hata hivyo tunajua ya kuwa, Mungu huwa anazitimiza ahadi zake zote. Kwa hiyo, ili Ibrahimu aishi katika nchi Mungu aliyomuahidia, ni lazima Ibrahimu afufuliwe kutoka kwa wafu. Ibrahimu aliamini juu ya ufufuo, kwa hiyo aliahidiwa uzima baada ya kufa (Waebrania 11:19).

Nchi hiyo ambayo Ibrahimu aliahidiwa, ndiyo itakayokuwa kitovu cha Ufalme unaokuja. Ibrahimu atafufuliwa kutoka kwa wafu, na kuwa katika Ufalme wa Mungu katika dunia, Bwana Yesu Kristo atakaporudi. Kwa hiyo Ibrahimu aliifahamu Habari Njema ya Ufalme unaokuja na aliutazamia (Waebrania 11:10).

Mfalme Daudi naye aliutazamia wakati ambao ‘mzao’ wake angetawala kutoka katika Yerusalemu. Utajifunza mengi zaidi kuzihusu ahadi za Mungu kwa Ibrahimu na Daudi katika masomo ya mbele.

Bwana Yesu Kristo atarudi lini?

Hatuifahamu siku ya kurudi kwa Yesu. Lakini tunajua, kutokana na matukio yanayotokea duniani leo, kuwa muda sio mrefu atarudi. Kwa miaka kama 2000 iliyopita, Wayahudi hawakuwa na nchi ya kwao wenyewe. Sasa wamerudi katika nchi yao ya kale, na katika mwaka 1948 walianza kuwa na taifa lao tena. Hiki ni kitu kilichoahidiwa kutokea kabla ya kurudi kwa Bwana Yesu.

Dunia leo imejaa machafuko na uovu ni mwingi, watu wengi wanajifanyia tu wanavyopenda; hawataki kujizuia. Kuna vita, njaa na magonjwa ya kutisha duniani kote. Ugaidi nao umekuwa tatizo lililo katika kuongezeka. Watu wanahofia maisha yao, kama Yesu alivyosema ingetokea. Alisema, watu wangevunjika: “Mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu” (Luka 21:26).

Yesu aliendelea kusema, mambo haya yote yatakapokuwa yakitokea, ujio wake utakuwa karibu sana. Utajifunza zaidi juu ya hili katika masomo yanayokuja.

Yesu atarudi na kuwa Mfalme wa dunia

Yesu alimwambia Pontio Pilato kuwa, alizaliwa kuwa Mfalme. Juu ya msalaba wake waliandika: “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi”. Lakini hawezi kuwa Mfalme wa Wayahudi tu. Atakuwa Mfalme wa dunia nzima. Mungu alisema hili miaka mingi nyuma: “Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia” (Zaburi 72:8).

Nini kitatokea wakati Yesu Kristo akirudi hapa duniani?

Atawafufua waliokufa na kuwahukumu. Ni wale tu walio vile Mungu anavyotaka, watakaopewa uzima wa milele, na sehemu katika huo Ufalme wa Mungu. Hao watamsaidia Yesu katika kuitawala dunia.

Katika wakati huo, Yerusalemu itakuwa ni Mji Mkuu wa dunia, na Yesu Kristo atakuwa Mkuu wa dunia yote. Utakuwa ni wakati wa furaha kuu. Yesu aliwaambia wanafunzi wake wauombee wakati huo kwa Mungu, wakisema: “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni….kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu na utukufu, hata milele” (Mathayo 6:9-13).

Baada ya miaka elfu moja, hakutakuwa tena na dhambi wala mauti. Mungu atakuwa, ‘yote katika wote’ – kama alivyopanga tangu mwanzo, kwa maana: “Dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yanavyoifunika bahari” (Habakuki 2:14).

Ujumbe wa maana sana kipekee ni kwamba, tunaweza kuwa na nafasi katika Ufalme huo huo.

Tunawezaje kupewa sehemu katika Ufalme huo wa Mungu unaokuja duniani?

Tunahitaji kutambua jinsi watu wote walivyo wadhambi, na kuchukua hatua kibinafsi juu ya hali yetu hii. Wakati mtume Paulo alipokuwa Athene, alisema:

“(Mungu) Anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu, kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua, naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu” (Matendo 17:30,31).

Mungu anawaamuru watu wote kutubu. Kutubu ni kuacha kujipendeza mwenyewe na kujaribu kumpendeza Mungu. Sisi wote ni wadhambi, kwa hiyo tuna wajibu wa kutubu na kubatizwa katika maji. Ni lazima tujaribu kuishi kwa namna alivyosema Yesu. Kwa wale wanaofanya hivi, Yesu Kristo atawapa uzima usio na mwisho atakaporudi.

(Utakuwa umegundua kuwa, Injili haihusu kwenda mbinguni, hilo sio Biblia inalofundisha. Injili inahusu uzima wa milele katika Ufalme wa Mungu katika dunia)

Muhtasari

  1. Biblia yote inahusu Injili (au Habari Njema). Watu waaminifu katika Agano la Kale na Agano Jipya walielewa maana ya Injili.
  2. Ili kuwaokoa watu, Yesu aliishi maisha makamilifu na kufa kwa hiari.
  3. Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, na baadaye kidogo Yesu alipaa mbinguni.
  4. Bwana Yesu atarudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.
  5. Yesu atawafufua waliokufa na kuwahukumu. Wale watakaokubalika watapewa uzima wa milele katika Ufalme wake hapa duniani.

Mistari ya kusoma: Isaya 45:18, Zekaria 9:9, Mathayo 25:31-34, 1 Wakorintho 15:28.

Jifunze kwa moyo: Mwanzo 12:1-3

“BWANA akamwambia Abramu, toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, nenda mpaka nchi nitakayokuonyesha, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka, nami nitawabariki, wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”.

 

Swahili Title
Injili - Somo la 04
English files
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission