Somo la 6
MUNGU ALIUPENDA ULIMWENGU
SOMO: Isaya 53
Dunia ina matatizo gani?
Ni kweli kuna matatizo katika dunia tunamoishi. Kila siku tunasikia habari za kutisha za ukatili na vurugu duniani kote, na matishio ya vita. Magonjwa ya ajabu-ajabu yanasambaa kwa haraka, na wengi wanakufa kwa njaa wakati wengine wana chakula kingi zaidi ya mahitaji yao. Wafalme na watawala wengine hawaonekani hasa kuguswa na matatizo ya wale wanaowaongoza.
Maisha ya dhiki yamekuwa ya wakati wote, kwa sehemu kubwa. Tumeyazoea, tunachukulia kama ndivyo ilivyo. Lakini, kama tukitulia na kufikiri, tunajikuta tukijiuliza, âNi kwa nini?â
Kwa hakika, hapo Mungu alipoiumba dunia na kuifanya iwe mahali pazuri sana pa watu kuishi, alikuwa amekusudia pawe mahali bora zaidi, kuliko dunia hii ya shida na mashaka tunamoishi ndani yake leo.
Mwanzo wa shida
Hapo mwanzo Mungu alipomuumba mtu wa kwanza, aliyeitwa Adamu, alimfundisha Njia zake. Alimpa pia Adamu amri ndogo, na kama ambavyo baba yeyote anavyotazamia wanawe wamtii, naye Mungu alitegemea utii kutoka kwa Adamu. Mungu alimwambia:
âMatunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakikaâ (Mwanzo 2:16,17).
Adamu hakumtii Mungu; alianguka kwenye dhambi. Kutokumtii kwake hatimaye kulileta mauti, kama Mungu alivyosema. Dhambi yake ilimpa urahisi wa kuendelea kukosea, na tangu hapo kila mwanadamu ameona rahisi kumkiuka Mungu. Katika Warumi 5:12 tunaambiwa:
ââ¦..kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti, hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambiâ.
Kwa hiyo Adamu alifanya dhambi, na kwa kuwa mdhambi, alikufa. Ni vizuri kugundua hapa ya kuwa, Mungu hakuwaahidia Adamu na Hawa kuwa wangekwenda mbinguni baada ya kufa. Kuwaahidi hivyo ingekuwa kuwazawadia. Walichopewa ilikuwa ni hukumu ya kifo; adhabu, sio tuzo.
Inatokea na sisi, pia
Nasi tunamkiuka Mungu na tunakufa. Uliposoma Sura ya Isaya 53, uligundua maneno katika msitari wa 6, yanayosema:
âSisi sote kama kondoo tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyeweâ.
Nabii Yeremia naye anatuambia kitu hicho-hicho kwa maneno mengine, anaposema:
âMoyo (wa mwanadamu) huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufishaâ (Yeremia 17:9).
Tunayasoma mambo haya katika Biblia, na tunajua kutokana na tunavyojisikia wenyewe, kuwa ni kweli. Mtume Paulo alisema:
âKwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu halikai neno jemaâ (Warumi 7:18).
Wote sisi tunastahili kukubaliana na Paulo. Kwa namna fulani sisi wote tunakuwa tunashindwa kuwa wema kama tunavyotaka. Wapo wengi pia ambao hawataki hata kule kuwa wema.
Ufumbuzi ni nini?
Kabla ya kuanguka kwenye dhambi, Adamu aliishi kwa mahusiano mema na Mungu. Sasa, urafiki huo ulivunjika baada ya kuwa mdhambi. Ushirika wake na Muumba wake usingeweza kuendelea; Mungu ni Mtakatifu sana.
Adamu inawezekana hakujua ni balaa gani alikuwa analianzisha. Kuanzia hapo aliendelea kumkiuka Mungu, na mpaka sasa kila anayetokana naye, ukiwepo wewe na mimi, amezifuata nyayo zake na kufanya dhambi (ukimweka pembeni Yesu tu). Na kwa kuwa sisi wote tumekuwa wadhambi kiurithi, wote tumefarakana na Mungu.
Tokea hapo, tunapozaliwa, tunakuwa ni uzao wa Adamu na tunarithi matokeo ya dhambi yake. Tu-viumbe wa kufa tangu tunapotungwa mimba, na tunapozaliwa tunafanya mambo yawe mabaya zaidi kwa kuongeza dhambi zetu wenyewe. Hii ni hali mbaya sana! Hakuna anachoweza kufanya mtu kujiokoa mwenyewe.
Wokovu ni kwa neema ya Mungu
Mungu kwa upendo na huruma yake, hakuwaacha wanadamu waishie wote kwenye kufa kwa dhambi zao. Ameweka njia ambayo watu wanaweza kumjea na kuwa na uzima. Tunasoma katika Yohana 3:16 kuwa:
âMungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa mileleâ.
Mtume Paulo anasema: âMmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imaniâ (Waefeso 2:8).
Neema ya Mungu ni upendo wake anaotupa bure, wa kutusamehe dhambi zetu, kwa ajili ya Kristo. Ametimiza hilo kwa upande wake kwa kutupa Yesu; ametufungulia njia, tusipotee. Hili linawezekana, kwa njia ya imani.
Biblia inapoongelea kwa njia ya imani, inamaanisha kuamini na kuweka tumaini. Kama hatuliamini Neno la Mungu, ni kwamba haiwezekani tukawa na imani inayolitumaini. Katika hali hiyo, hatuwezi kuwa na ushirika katika hiyo neema yake. Neno linasema:
âPasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu), kwa kuwa mtu amwendeaye (âamwaminiyeâ) Mungu, lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutaoâ (Waebrania 11:6).
Yesu na msalaba
Yesu hakutenda dhambi. Alifanya wakati wote mambo yale yanayompendeza Mungu. Hata hivyo walimsulubisha! Mungu hakumwokoa kisimpate kifo hicho cha kutisha. Msitari tuliounukulu kutoka Isaya 53 unaendelea kusema:
âNa BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi soteâ.
Biblia inatufundisha wazi-wazi kuwa, kupitia katika kifo cha Yesu msalabani, kwa kuyatii mapenzi ya Baba yake, tunaweza kusamehewa dhambi zetu, na kuwa na tumaini la uzima.
Kuna kitu kizuri sana cha ajabu katika hili; katika huu upendo wa Mungu katika kumtoa Mwanawe, na katika upendo wa Yesu kwa kutii mapenzi ya Baba yake. Kwa kuamini Habari Njema iliyoko ndani yake, tunaweza kuwa na uzima. Watu hawalishiki hili vizuri. Tutalirudia tena na tena katika uchunguzi wetu wa Kimaandiko, kwa maana dhana hii ndiyo kiini cha tumaini la wokovu; tumaini la Mkristo.
Uko upande upi?
Namna moja ya kuutafakari wokovu ni kufikiria familia. Adamu alikuwa kiongozi wa familia ya âwanadamuâ na kutokana naye (na mke wake, Hawa), sisi wote tumezaliwa. Adamu alifanya dhambi na kuleta mauti kwa jamii ya mwanadamu, na kwa hiyo watu wote tunakufa.
Bwana Yesu Kristo alichepuka na kuanzisha familia nyingine. Aliweza kufanya hili kwa kuivunja nguvu dhambi. Ilihitajika dhabihu kamilifu kuweza kuishinda laana ambayo Adamu na Hawa walikuwa wameileta kwa wanadamu. Yesu alikuwa ndio hiyo dhabihu kamilifu.
Kwa hiyo familia ziko mbili: familia ya Adamu na familia ya Kristo. Sisi wote tunakuwa tumezaliwa katika familia ya Adamu, na tunapokufa tukiwa ndani ya familia hiyo ya Adamu, tunapotea milele. Inatubidi tufanye kitu!
Kristo anatutaka tujiunge na familia yake yeye, na tunaweza kufanya hivyo kwa kujifunza juu yake tunapolifahamu kusudi la Mungu, na kubatizwa. Ubatizo (kama utakavyojifunza baadaye), ni ishara ya kufa kwake Yesu na kufufuka tena. Kwa hiyo tunakufa ili kujitoa katika familia ya Adamu, na kujiunga na familia ya Kristo tunapoibuka kwenye maji ya ubatizo.
Kama ukisoma Warumi 6:12, 18-21, utaona vile mtume Paulo anavyolitumia wazo hili la familia.
Tunapaswa kumshukuru sana Mungu na Bwana Yesu kwa kutuwezesha kutoka katika familia hiyo ya Adamu.
Kumwamini
Tumeshaona kuwa, kama tunapenda kumpendeza Mungu, ni lazima tuamini yale aliyofanya kwa ajili yetu kupitia katika kifo cha Yesu Kristo. Katika Yohana 3:16 tumeambiwa: âIli kila (mtu) amwaminiye (Yesu) asipotee, bali awe na uzima wa mileleâ.
Hili halina maana ya kusema tu kwamba, âNimemwamini Yesuâ, kwa hiyo nitaokolewa na dhambi na mauti. Inaweza ikaonekana kihivyo unapoanza kufikiri, lakini hebu tulia na kulifikiria jambo hili vizuri. Tunapokuwa kikweli tumeamini kitu, tunakifanyia kazi. Kama tunauguliwa na mtoto na tunaamini daktari anaweza kutusaidia kumponya, hatusemi tu, âNamwamini daktariâ, na kuishia hapo. Tunampeleka mwanetu kwa daktari, na kwa kuwa tunamwamini daktari wetu, tunafanya lolote analotuambia.
Sasa, ni hivyo ilivyo kumwamini Yesu. Kama ni kweli tumemwamini, tutajitahidi kujua kile anachotutaka tufanye na tutakifanya kwa uwezo wetu wote. Kumwamini Mungu kunaanzia katika kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji, kama alivyoamuru. Ni pale tu tunapofanya hili, ndipo tunapoweza kuwa miongoni mwa wale ambao hawapotei; miongoni mwa wale watakaopata, âuzima wa mileleâ.
Tuzo ya uzima wa milele
Maisha katika Ufalme wa Mungu ni tuzo ya Mungu kwa wale wanaoliamini Neno lake, na kujitahidi kumtii. Hawa ni watu wanaomuomba Mungu kila siku wakisema, âUfalme wako ujeâ. Yesu atakaporudi, atausimamisha huo Ufalme wa Mungu. Atakikalia âkiti cha enzi cha Daudiâ, baba yake, na kuitawala dunia nzima. Hapo ndipo wanaume kwa wanawake waliomngoja wakijitahidi kuishi kwa namna walivyoamuriwa, watakapopewa zawadi kubwa kuliko zawadi yoyote mtu anayoweza kupewa; uzima usio na mwisho katika Ufalme wa Mungu. Hawatakufa tena.
Hao wataishi milele na kumsaidia Bwana Yesu katika jukumu lake la kuitawala dunia. Ndipo watakapoimba maneno haya tunayoyasoma katika Ufunuo, wakisema:
âWastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu, kwa damu yako, watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchiâ (Ufun. 5:9,10).
|
Muhtasari
|
Kifungu cha kusoma: Waefeso 2
Jifunze kwa moyo: Yohana 3:16
âKwa jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa mileleâ.