Correspondance Course - Lesson 05

Swahili

Somo la 5

MUNGU NA UUMBAJI

Masomo:  Mwanzo 1,  2 : 1 – 7

Uumbaji

Katika kifungu cha kwanza cha Biblia, Mwanzo 1, umeshasoma juu ya siku saba  za uumbaji. Jedwali hapa chini linaonesha kazi ya kila siku:

Siku

Tukio

Kilichofanyika

  1.  

 

Nuru inatokea; kunakuwa na mchana na usiku

      2.

Maji yanajitenga, anga linajitanda

  3.

 

 

Nchi kavu inatokea; majani, miti na mimea inaota

 

 

  4.

 

Jua, mwezi na nyota vinatokea

  5.

 

Samaki wanatokea baharini, ndege angani

 

  6.

Wanyama wanaumbwa, na mwisho kabisa mwanadamu, wa kiume na wa kike

  7.

 

Mungu anapumzika.

 

Kila kitu kilifuata utaratibu wake. Kwa mfano, mimea na miti haikuwekwa mpaka siku ya tatu, wakati nchi kavu ilipokuwa imewekwa kwa ajili yao. Wanyama waliumbwa siku ya sita, wakati chakula kikiwa kimeshapatikana kwa ajili yao.

“Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana”.

Popote pale tulipo, kila siku tunaona uzuri wa kazi ya Mungu. Mwanadamu amegundua vitu vya ajabu kama ndege za kusafiria angani na madawa, lakini utaalamu unaotumika kuvibuni na kuviunda vitu hivi, si chochote ukilinganisha na ustadi na uweza ulioviumba vitu hivi vyote kwa umahiri mkubwa.

Mchana unafuata usiku, misimu inafuatana, na hatuwi na mashaka kama mambo hayataendelea kuwa hivyo. Kazi anayoifanya mtu anaweza kuikosea, lakini kazi ya Mungu haikosewi.

Wakati kazi nyingi wanazofanya watu zinakuwa na kasoro nyingi, kila anachokiumba Mungu, sio tu kama kinafaa kwa lengo alilolikusudia, bali pia kinapendeza. Ua dogo kabisa la rangi na kwa umbo lake, uwezo wake wa kujizalisha ni muujiza. Ni hivyo hivyo kwa kindege kidogo na vibawa vyake vinavyokiwezesha kuruka. Kinaweza kuruka kwa kuijua njia yake kwa maelfu ya kilometa, kikizunguka kwenda kwenye makazi yake ya msimu wa baridi kali.

“Wewe Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote?”

Miungu isiyo miungu

Katika nyakati zote tangu kale, mwanadamu amekuwa akiona maajabu ya asili, lakini, badala ya kumuabudu Mungu aliyeviumba vitu vyote, wamekuwa wakiviabudu vitu alivyoviumba! Hata watu wa Mungu, Wayahudi, wamefanya hivyo kwa nyakati mbalimbali. Watu wameliabudu jua, mwezi na nyota, na kufikiri kuna mizimu inayoishi kwenye maji na upepo, kwenye miti na mawe. Hili ni jambo ovu sana kufanya na Mungu analilaani. Hebu soma kitu mtume Paulo anachokisema juu ya hili katika Warumi 1:20–23. Anasema:

“….wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu (‘anayekufa’), na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo” (ms.23).

Kwa vyovyote watu walipoiomba miungu hiyo ya uongo, haikuweza kujibu kamwe. Iwezeje kujibu wakati sio miungu lolote? Kuabudu miungu ya uongo ni jambo ovu sana, na kumeleta matukio mabaya sana, kufikia hata kuwapitisha watoto kwenye moto. Hata Wayahudi, ingawa walikuwa wamepewa mafunuo ya Mungu kwa Sheria yake ya Haki, walikuwa na hatia ya kuabudu sanamu; kuabudu miungu ya uongo. Mungu alikuwa amewaonya dhidi ya hili, katika Kumbukumbu la Torati 4:15-19.

Sasa tazama Ezekieli 14:1-5. Ona vile Mungu alivyosema juu ya hawa ‘waabudu sanamu’ katika mstari wa 3, kuwa, walikuwa: “Wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao”. Nasi tutaendelea kufanya hivi tusipoangalia. Kama kuna kitu katika maisha yetu tunachokifiri ni cha maana zaidi kumpita Mungu aliyetuumba, kitu hicho ni ‘sanamu’; ni kinyago moyoni mwetu. Kama tunataka kumpendeza Mungu, inatubidi kuachana na sanamu; inatubidi tujitenge na wanaoabudu miungu ya uongo. Paulo analiongelea hili katika waraka wake wa pili kwa Wakorintho, ambapo anasema:

“Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana ushirika gani kati ya nuru na giza?” (2 Wakorintho 6:14).

Endelea kusoma mpaka mwisho wa kifungu hiki kwa Wakorintho, kisha fungua waraka wake kwa Wathesalonike. Waumini Wakithesalonike, walimgeukia Mungu na kuziacha: “Sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli. Na kumngojea Mwanawe kutoka Mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu inayokuja” (2 Wathes.1:9,10).

Ulimwengu wanadamu waliouchafua

Watu wanafanya uovu mkubwa wanapoabudu sanamu, na watu wanafanya uovu wanapoichafua dunia iliyoumbwa na Mungu. Hapo mwanzo, dunia yetu ilikuwa ni mahali pazuri zaidi kuliko ilivyo leo. Wanadamu wamefanya mengi kuharibu uzuri wake. Wanakata miti ovyo ovyo na kusababisha majangwa palipokuwa pameota misitu. Wameichafua hewa kwa mioshi ya sumu, na kuchafua chemchemu na mito kwa takataka za sumu kutoka kwenye viwanda vyao. Kwa njia hizi na zingine, dunia yetu inaharibika.

Lakini bado ni dunia ya Mungu, na hataruhusu watu waendelee kuiharibu moja kwa moja. Katika Matendo ya Mitume, mtume Paulo anasema, Mungu:

“Ameweka siku atakayowahukumu walimwengu” (Matendo 17:31).

Siku inakuja ambapo Mungu atamtuma Yesu arudi kuyaweka mambo sawa; kuitawala dunia. Utawala wake wa busara na miongozo yake ya haki, itairudisha dunia katika uzuri wake wa kwanza. Mungu amesema: “Hakika yangu, kama niishivyo, ndivyo dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA” (Hesabu 14:21).

Mungu mwenye uweza wote

Zaburi ya 90:2 inasema: “Tangu milele hata milele ndiwe Mungu”. Hiki ni kitu ambacho akili zetu haziwezi kukielewa. Tunajua kutokana na namna tunavyoishi maisha yetu kuwa, mambo yote yana mwanzo na mwisho, na tumezoea kuna kuzaliwa na kufa. Lakini, Bwana Mungu yeye amekuwako nyakati zote na ataendelea tu kuwako. Tunapaswa tuwe na imani kuwa, hivi ndivyo ilivyo. Mwandishi kwa Waebrania anasema: “Mtu amwendeaye Mungu (‘anayemwamini Mungu’) lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao” (Waebr. 11:6).

Tunaweza kuangalia vitu vya ajabu tunavyoviona katika mazingira tulimo, na kujifunza kitu kuhusu uweza wa Mungu na hekima yake. Lakini, hatuwezi kuona katika dunia inayotuzunguka, jibu la kusudi la Mungu katika kuiumba dunia, na mipango aliyonayo kwa mambo yake ya mbeleni. Hatuwezi kujua anavyowataka wanadamu waishi.

Ni kwa Neno lake tu tunavyoweza kuyajua mambo haya. Ili kumjua Mungu, ni lazima tuje kwenye Biblia. Biblia inatuambia ya kwamba, YEYE ni Mkuu sana na ni mwema. Inatuambia kuwa anao mpango na dunia yake. Katika kujifunua kwa Musa, alijitambulisha kuwa, YEYE ni:

“BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi, wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe” (Kutoka 34:6,7).

Mungu ana rehema na upendo, lakini pia ni wa kweli na haki. Anatutegemea tumtukuze na kumtii.

Hapo mwanzo

Kuna watu wengi wanaoamini kuwa, dunia yetu hii ya ajabu ilitokea hivi hivi tu. Wanafikiri uhai ni kitu kilichoanza tu, na tokea hapo, baada ya mamilioni ya miaka, mambo yakajipanga yenyewe katika utaratibu na uzuri wa dunia tunayoiona leo. Kwa hiyo wanasema, viungo vyenye uajabu kama macho yanayoona na masikio yanayosikia, vilitokea kwa bahati tu.

Miaka si mingi iliyopita, wana-sayansi karibu wote waliamini tunatokana na “mabadiliko ya pole pole” yaliyotokea yenyewe (Evolution, kama nadharia hiyo inavyoitwa). Walisema dunia hii tunamoishi leo ni matokeo ya mpasuko na mabadiliko ya taratibu ya mamilioni ya miaka. Kwa siku hizi, hata hivyo, wana-sayansi wengi maarufu wanarudi kwenye mawazo ya kwamba, hayakutokea tu. Kuna Muumba wa yote. Biblia inasema:

“Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”.

Haituambii namna alivyofanya, na kama ingetuambia, inawezekana tusingeelewa. Tuna wajibu wa kulipokea Neno la Mungu kwa imani. Kitu kimoja ni hakika: hatuwezi kuamini Biblia inachofundisha kumhusu Mungu aliyeviumba vitu vyote, na wakati huo huo tukaamini kuwa dunia hii ilitokea tu:

“Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake” (Zaburi 33:6).

Tuliona katika Mwanzo 1 jinsi Mungu alivyoiumba dunia, na kuwaumba  mwanamume na mwanamke katika siku ya sita. Sasa hebu soma Mwanzo 2:15 mpaka Mwanzo 3:24. Mistari hii inaeleza hadithi ya kusikitisha. Hapo mwanzo kila kitu baada ya kuumbwa kilikuwa ‘chema sana’. Baada ya hapo Adamu na Hawa hawakumtii Mungu, na kutomtii kwao kukaleta dhambi na mauti duniani.

Kwa upendo wake kwa wanadamu, miaka mingi baadaye Mungu alimtoa Mwanawe, Bwana Yesu Kristo. Yesu aliweza, kwa maisha yake makamilifu na kwa kifo chake msalabani, kuifungua njia kwa Mungu kuweza kusamehe dhambi. Yesu ametuletea tumaini la uzima. Utasoma juu ya hili katika somo litakalofuata.

Sisi ni sehemu ya uumbaji wa Mungu

“Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba” (Zaburi 95:6).

Kuweza kuja mbele ya Mungu kumwabudu na kumsifu, ni fursa ya kipekee iliyo ya maana sana. Yesu anaongelea wale wanaokuja kumwabudu Mungu ‘katika roho na kweli’, na kusema, “Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu” (Yohana 4:23). Mungu anataka awabariki watu wanaompenda; wanaopenda kumwamini na kumtii, waifurahie dunia hii aliyoiumba.

Mungu anawataka watu wamruhusu YEYE ayaongoze maisha yao. Anawaandaa watu hao kwa ajili ya wakati watakapoweza kumtumikia milele katika Ufalme wake, Yesu atakaporudi duniani. Kama tukilisoma Neno lake na kumtukuza na kumtii sasa, katika siku hiyo inayokuja tutakuwa kati ya wale watakaosema:

“Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemngojea…..tushangilie na kuufurahia wokovu wake” (Isaya 25:9).

Muhtasari

  1. Hii dunia iliumbwa na Mungu.
  2. Ni YEYE pekee astahiliye kuabudiwa.
  3. Nadharia zote za watu juu ya dunia ilivyoanza ni uongo, kama zinamkana Mungu kuwa siye Muumbaji.
  4. Tunaweza tu kufahamu juu ya Mungu na kusudi lake kwa dunia hii kwa kuisoma Biblia.
  5. Biblia inatufundisha tunavyoweza kuishinda dhambi na mauti kwa kupitia kwa Yesu, na kuwa na sehemu katika Ufalme wa Mungu unaokuja.

Mistari ya kusoma:  Zaburi 24 , Zaburi 102:25–28, Warumi 1:18-23, Mwanzo 2:15, 3:24.

Jifunze kwa moyo:  Waebrania 11:3

“Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri”.

Swahili Title
Mungu na Uumbaji - Somo la 05
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission