Correspondance Course - Lesson 07

Swahili

Somo la 7

KURUDI KWA BWANA YESU DUNIANI

SOMO: Matendo 1

Miaka 2000 iliyopita

Bwana Yesu alisulubiwa miaka elfu mbili iliyopita. Wafuasi wake walivunjika moyo na kuchanganyikiwa. Matumaini yao yote kwake yalivunjika, alivyokuwa amekufa na kulazwa kaburini.

     Siku ya tatu, Yesu alitoka kwenye kaburi lile akiwa hai!     

Lakini:

Lilipotokea hili, wafuasi wake waliyakumbuka maneno aliyokuwa amewaambia kabla ya kufa:

“Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi….lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha” (Yohana 16:20).

Watakuwa walifurahi kiasi gani kumwona Bwana wao mpendwa tena! Tunaambiwa: “Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana” (Yoh. 20:20). Kwa hakika, furaha yao ilikuwa kubwa sana.

Yesu alipokwenda mbinguni

Sasa hebu soma tena mistari nane ya kwanza ya Matendo 1. Jaribu kupata picha jinsi mitume walivyokuwa katika hizo siku arobaini, Yesu alipokuwa yupo nao tena kwa mara nyingine. Wafikirie tena mwishoni mwa siku hizo arobaini, wakiwa wamesimama juu katika miteremko ya kijani ya Mlima wa Mizeituni, wakiwa na Yesu katikati yao. Ghafla anatwaliwa pale walipo na kupaa mbinguni.

Watakuwa walimtazama sana kwa jinsi alivyoondoka duniani, na kutokomea mawinguni, wasimwone tena. Walikuwa wameachwa ukiwa tena.

Hata hivyo, safari hii hawakufadhaika wala kujiuliza. Hapana! Luka anatuambia tu: “….. alijitenga nao, akachukuliwa juu mbinguni. Wakamwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu” (Luka 24:51,52).

Siri ya furaha yao

Ni kwa nini baada ya kutengana nao mara hii ya pili walikuwa na furaha kubwa?

Sababu moja ni kwamba, Yesu alikuwa amewaahidi kitu. Alikuwa amewaambia: “Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20). Hili lilikuwa na maana kuwa, ingawa walikuwa hawawezi tena kumwona, yeye alikuwa pamoja nao na angeendelea kuwajali siku zote.

Lakini, hiyo haikuwa sababu pekee ya furaha yao. Walipokuwa wakimwangalia akipaa kwenda mbinguni, kuna malaika wawili waliowajea na ujumbe na kuwaambia:

“Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo 1:11).

Wanafunzi wale wote walipokuwa wakirudi Yerusalemu kwa kutii maagizo ya Bwana wao, walikuwa na uhakika kabisa ya kuwa, Yesu mwenyewe angerudi duniani. Hiki kilikuwa ni kitu cha kuwafariji na kuwatia furaha.

Maneno ya Yesu

Yote haya yalitokea miaka 2000 iliyopita, na Yesu bado hajarudi. Lakini tunajua atarudi kwa kuwa ndivyo alivyosema.  Katika Luka 21:27 anaongelea kurudi kwake mawinguni, akiwa na ‘nguvu na utukufu mwingi’. Utakuwa umegundua kuwa, alipokuwa akipaa aliinuliwa, na “wingu likampokea” (Matendo 1:9), na kwamba malaika walisema atarudi, “…jinsi hiyo hiyo” walivyomwona akienda zake” (ms.11).

Mifano mingi aliyotoa Bwana Yesu iliongelea pia kurudi kwake. Chukua kwa mfano, mfano katika Mathayo 25:1-13. Huu unamsemea ‘bwana-harusi’, na hatuna tatizo katika kuuelewa. Bwana harusi huyo, hakuna shaka, ni Bwana Yesu Kristo, na simulizi hilo linatutahadharisha kuwa, atakapokuwa akirudi, watakuwepo watu watakaokuwa hawajajiandaa kumpokea. Kwenye mstari wa 13 tutambue kuwa hasemi, ‘hamjui kama Bwana wenu atarudi au la’. Hakuna mashaka juu ya hili, ujio wake ni kitu cha uhakika. Analosema ni: “Hamwijui siku wala saa”.

Ushuhuda wa Petro

Siku chache baada ya Yesu kupaa mbinguni, tunasoma juu ya Petro akiwa hekaluni, Yerusalemu, akiwahutubia kwa kishindo Wayahudi waliohusika katika kumsulubisha Yesu. Katika Matendo 3:19,20 anawaambia:

“Tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakazi za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani”.

Petro alisemea tena ujio wa mara ya pili wa Kristo, katika barua aliyoandika baadaye kwa waumini. Akiwasemea wale wasioamini katika 2 Petro 3:4 anasema kuwa, watahoji wakisema: “Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali hiyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa”.

Unaweza ukawa umewasikia watu wakitumia maneno kama hayo. Lakini ni Mungu mwenyewe aliyeahidi kumtuma Bwana Yesu, na tunajua ya kuwa ataitimiza ahadi yake. Petro anaendelea katika mstari wa 9 na wa 10 kusema:

“Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie (‘waifikie’) toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi”.

 

Ushuhuda wa Paulo

Yesu mwenyewe alimtokea mtume Paulo na kumtuma aende kuwahubiri wengine. Paulo anadai kuwa Injili aliyokuwa akiihubiri alipewa na Yesu Kristo. Paulo alifundisha juu ya ujio wa mara ya pili wa Bwana Yesu Kristo. Katika 2 Timotheo 4:1 tunasoma Paulo akimwambia Timotheo:

“Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa kwa kufunuliwa kwake…….”

Aliandika pia barua mbili kwa kanisa katika Thesalonike. Utaziona nyaraka hizi ndani ya Biblia yako. Ndani yake kuna vifungu vinane vifupi-vifupi, na kuna kitu cha kushangaza ndani yake; katika kila kifungu, Paulo anataja ujio wa Yesu.

Katika 1 Wathesalonike 4:16, anaongelea ufufuo wa wafu katika ujio wa Yesu:

“Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu, nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza”.

Katika 2 Wathesalonike 1:7,8  Paulo anazungumzia:

“Kufunuliwa kwake Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake, katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana Yesu Kristo”.

Hapa anamwongelea Yesu akirudi kuwaadhibu watu, lakini kama tukiendelea kusoma tutaona kuwa, anawaongelea pia watu wengine ambao, ujio wake utakuwa tukio kubwa la shangwe kwao, kwa kuwa atakuwa anakuja, “Kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile” (ms. 10).

Yesu  atafanya nini atakaporudi?

Ujio wa Yesu utayabadili maisha ya kila mtu, atakayekuwa akiishi wakati huo. Litakuwa ni tukio kubwa sana kwa:

  1. Waumini wanaomsubiri na kumtazamia.
  2. Wote watakaokuwa wanaishi wakati huo, wasioijua Injili ya kweli.
  3. Taifa la Wayahudi.

Tuyaangalie haya moja baada ya jingine:

a. Waumini wa kweli wanaomtazamia na kumngoja (Watu walio katika Kristo):

Yesu atawafufua katika wafu wale wote waliokufa katika imani, na kuwakusanya pamoja waumini walio hai:

“Angalieni, nawaambia ninyi siri, hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho, maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika” (1 Wakorintho 15:51,52).

Wale ambao wamekuwa si waaminifu watakataliwa, lakini kwa waliokuwa waaminifu, kutakuwa ni shangwe kuu; Yesu atawapa uzima wa milele. Paulo anatuambia katika Wafilipi, Yesu ataubadili: “Mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu” (Wafilipi 3:21).

Kama ilivyo kwake, watashirikishwa uzima usio na mwisho; usio na maumivu na machungu yoyote. Watamsaida Yesu katika kazi kubwa ya kuyafundisha mataifa yote juu ya Mungu, na kuwaongoza watu wa dunia waweze kuuitikia upendo wake, na kwenda katika njia zake.

b. Watu wa dunia:

Wakati atakapokuwa akirudi Yesu, hukumu za Mungu zitamwagwa juu ya watenda maovu, na kutakuwa na dhiki kubwa duniani. Hili linasikitisha, lakini haliepukiki. Bila ya Mungu kuitikisa dunia, dunia haitaweza kamwe kumgeukia YEYE na kumkubali Bwana Yesu kuwa Mfalme wake anayemweka.

Baada ya hukumu hizo za Mungu kumwagwa, watu wa dunia watakuwa tayari kumkubali Yesu kuwa Mfalme wao. Naye atausimamisha utawala wa Mungu katika dunia; Ufalme wa Mungu. Uongozi wake utakuwa wa upendo na hekima, wenye kuwajali maskini na wanyonge. Hebu ifungue Zaburi ya 72 na uisome yote. Itakupa picha ya utawala wake. Inasemea vile atakavyowahurumia wenye shida, na wale wasio na msaada.

Watu wa dunia watakaopona katika hukumu hizo za Mungu, wataishi katika Ufalme wa Mungu na kupata mibaraka mingi. Watakuwa, hata hivyo, wakivutwa bado na dhambi, na hatimaye watakufa kama inavyowatokea watu leo. Hata hivyo maisha yao yatakuwa marefu zaidi, na wakati wakiishi watakuwa wakifundishwa Njia za Mungu. Fursa itakuwapo bado kwao ya kuipokea miongozo ya Bwana Yesu, au kuikataa.

Itakapofikia mwisho wa kipindi cha miaka 1000 cha utawala wa Yesu, kutakuwa na ufufuo wa pili na hukumu kwa wale walioishi katika dunia katika kipindi hicho cha miaka elfu moja. Wengi wao watapewa uzima wa milele, na wengine watakataliwa milele. Hatimaye, mauti yatakuwa yametokomezwa; hakutakuwa tena na kufa.

c. Itakuwaje juu ya Wayahudi?

Yesu atarudi katika wakati ambao Taifa la Israeli wapo kwenye hekaheka kubwa. Watakuwa wamezungukwa na maadui pande zote. Yesu, kwa uweza wa Kimungu, atawashinda hao wanaopigana nalo. Ndipo Wayahudi walio wengi watakapotambua hatimaye ya kuwa, Yesu alikuwa ndiye Mfalme na Mwokozi wao kweli waliyeahidiwa, na ambaye walimsulubisha! Nabii Zekaria anasema: “Watamtazama yeye ambaye walimchoma, nao watamwombolezea” (Zekaria 12:10). Ndipo sasa watakapomkubali kwa furaha awe Mfalme wao.

Bwana Yesu atausimamisha Ufalme wa Mungu, na Wayahudi watakuwa wakati huo ‘Taifa Kiongozi’ juu ya mataifa yote. Mji wao Mkuu, Yerusalemu, utakuwa ‘Makao Makuu’ ya dunia, na kuwa ‘kitovu’ cha Ibada ya Kweli kwa watu wote. Utakuwa ni wakati wa furaha sana kwa Wayahudi, baada ya mateso yao yote ya miaka mingi. Upendo, furaha na amani ya hali ya juu vitatiririka kwa dunia kutoka katika Makao hayo Makuu mapya!

Kitatokea nini kwako wewe na mimi?

Usome tena mfano ule wa wanawali kumi katika Mathayo 25:1-13. Kama tuna akili nzuri kama wale wanawali wenye busara katika kielelezo hicho, tutajifunza Neno la Mungu, na kujiandaa sasa kwa ujio wa Yesu. Bwana Yesu alipomwambia mtume Yohana, “Naam, Naja upesi” (Ufunuo 22:20), Yohana alimjibu, “Na uje, Bwana Yesu”.

Tujiulize, tutakuwa kama mtume huyu na kulifanya jambo hili la kurudi kwa Bwana Yesu liwe jambo la kuombea?

Muhtasari

  1. Yesu Kristo anarudi duniani.
  2. Tunaweza kuwa na uhakika juu ya hili, kwa kuwa alisema hivyo mwenyewe, na malaika na mitume walisema hivyo pia.
  3. Atakapokuja atawapa wafuasi wake waaminifu uzima wa daima.
  4. Ataifanya Israeli kuwa Taifa Kuu kati ya mataifa.
  5. Atawafundisha watu wote wa ulimwengu Njia za Mungu.
  6. Kama tuna busara, tutajiandaa sasa kwa ujio wake huo.

Vifungu vya kusoma:     1 Wathesalonike 4,  Danieli 12:1-4,  Mathayo 25:1-13

Jifunze kwa moyo:          Matendo 1: 11

“Malaika wakasema: “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni”.

 

Swahili Title
Kurudi kwa Bwana Yesu Duniani - Somo la 07
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission