Correspondance Course - Lesson 08

Swahili

Somo la 8

ISHARA ZA KURUDI KWA YESU

SOMO: Luka 21

Yesu atarudi tena hapa duniani. Biblia inatuambia hili wazi wazi sana, kama tulivyoona katika somo lililopita. Kuja kwake ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa dunia yetu. Yesu atakuwa ‘Mfalme wa Wafalme’, akiongoza dunia kutoka katika Kiti chake cha Enzi katika Yerusalemu. Hii ilikuwa ahadi ya Mungu kwa Wayahudi katika Agano la Kale, na ni ujumbe muhimu sana wa Agano Jipya kwa watu wote. Wafuasi wa mwanzo wa Bwana Yesu waliutazamia wakati wa kuja mbeleni, wa:

“Kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana,” atakapomtuma “Yesu Kristo” (Matendo 3:19, 20). Neno lililotafsiriwa ‘kuburudishwa’ hapa, maana yake hasa ni ‘kurudishiwa-upya’(‘refreshing’-kwa Kingereza); ni kurudishiwa mambo upya au kuwekwa mwanzo-mpya, kutakakotokana na kurudi kwa Bwana Yesu.

Kurudi kwa Yesu kutakuwa ni tukio kubwa kuliko yote yaliyotokea, tangu kuumbwa kwa dunia. Kutayabadili maisha ya wote wanaoishi katika dunia hii. Kwa hiyo tunaweza kujiuliza, “jambo hili litakuwa lini?”

Hatuijui siku yenyewe. Yesu mwenyewe alisema: “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo 24:36). Lakini Mungu ametupa ishara zilizo wazi sana katika Neno lake. Yesu anatupa baadhi ya hizi katika Sura hiyo ya Mathayo 24 anaposema:

“Myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni” (Mathayo 24:33), yaani Ufalme wa Mungu umekaribia sana.

Mtu aliye safarini, anatambua anapoona alama fulani njiani au kibao kuwa, anakaribia mwisho wa safari yake. Kwa namna kama hiyo, ishara tunazoziona katika dunia zinatutambulisha kuwa, tunakaribia kabisa wakati wa kurudi kwa Kristo.

Wanafunzi wa Yesu walipomuuliza Yesu: “Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?” (Mathayo 24:3), Yesu aliwapa ishara kadhaa. Aliwaambia kuwa Yerusalemu ingeharibiwa (hili lilitokea miaka kama 40 tu baadaye, katika mwaka wa 70 Baada ya Kristo), na Wayahudi kukatawanywa. Aliendelea kuongelea juu ya kurudi kwake kwa kuwapa ‘ishara’ za kuchunguza. Zipo pia kwa ajili yetu leo.

Ishara kwamba tunaishi katika siku za mwisho:

  1. ISHARA KUHUSU WAYAHUDI

Biblia inasema kuwa, katika siku za mwisho:

  1. Wayahudi watarudi katika nchi ya Israeli
  2. Israeli litakuwa ni taifa tena
  3. Jiji la Yerusalemu litawekwa huru kutoka kwa maadui zake

   Maelezo:-

  • Wayahudi walikuwa wametawanywa dunia nzima katika mwaka wa 70 B.K. Tokea wakati huo, kwa karibu miaka 2000, hawakuwa na nchi iliyokuwa yao wenyewe. Lakini katika nyakati zetu hizi tumewaona wakiirudia Nchi ya Israeli, na kwa kufanya hivyo kuutimiza unabii wa Biblia:

“Tazama, zinakuja, anasema BWANA, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema BWANA, nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki” (Yer.30:3).

  • Katika mwezi Machi 1948, ingawa kulikuwa na upinzani mkali sana kutoka kwa Waarabu, Taifa la Israeli lilianzishwa, kinyume na vikwazo vyote. Nchi hiyo tangu hapo imechukua nafsi yake kati ya mataifa ya ulimwengu. Mungu alishasema  hili lingetokea kupitia kwa nabii Ezekieli, zamani sana:

“Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nani nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe, nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli” (Ezek. 37:21,22).

  • Yerusalemu sasa ni Makao Makuu ya Wayahudi. Soma maneno ya Yesu katika Luka 21:24, yanayoongelea kutawanywa kwa Wayahudi. Tambua hapa ya kuwa Yesu alisema, Yerusalemu utakanyagwa na mataifa, hata ‘majira ya mataifa yatakapotimia’. Unaona vile msitari huu unavyosisimua?

Katika mwezi Mei 1967, Wayahudi walipambana katika vita ya siku sita, na kuiweka Yerusalemu huru kutoka kwa maadui zake. Jiji hili ‘halikanyagwi’ tena na mataifa (halimilikiwi), bali liko mikononi mwa Wayahudi. Hakika ni ishara kali kabisa ya kuwa ujio wa Bwana umekaribia.

  1. ISHARA KATIKA DUNIA TUNAMOISHI

Kila mahali duniani kuna matatizo; matatizo ambayo viongozi wa mataifa hayo wanashindwa kuyatatua:

  • Wapo mamilioni ya watu wanaokufa kwa njaa, wakati wengine wanashiba na kusaza na kutupa.
  • Kuna matatizo ya uchafuzi wa mazingira. Watu wanaiharibu dunia wanayoishi ndani yake kwa choyo na uzembe.
  • Kuna matatizo ya ukuaji wa idadi ya watu. Ukuaji kwa baadhi ya nchi ni mkubwa mno kuliko uwezo wa serikali zake kumudu.
  • Kuna miogogoro ya kivita kila mahali inayoleta mateso na vifo.

Yesu aliyaona haya mapema. Alisema, “Kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota, na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake” (Luka 21:25).

Hili limekuwa kweli tukiangalia matatizo yanayoikabili dunia leo. Watu wanashindwa kujua wafanyeje. Katika msitari unaofuata Yesu anaendelea kusemea mioyo ya watu kuvunjika kwa hofu, “…na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu” (Luka 21:26). Siku hizi watu wanaogopa: wanahofia vita vya kinyuklia, na ajali za kinyuklia kama ile iliyotokea Japani mwaka 2011. Kuna hofu kubwa juu ya ugaidi, utekaji nyara, ujambazi, ukatili, uharibifu wa mali n.k. Viongozi wanababaika tu na kushindwa kujua hasa la kufanya!

Imekuwa kama vile hakuna suluhu ya matatizo haya, lakini hebu ona kile Yesu anachosema katika msitari uliofuata mbele:

“Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Luka 21:27).

Ni hakika tunaikaribia sana siku ya kurudi Bwana Yesu.

Kutokumwamini Mungu na Neno lake

Mtume Paulo, akiwasemea watu kwa wakati wake, alisema: “Kumcha Mungu hakupo machoni pao” (Warumi 3;18). Hivi si ndivyo ilivyo kwa watu hivi leo? Watu walio wengi hawataki kuusikia UKWELI ulio katika Neno la Mungu; hawataki kufahamu habari ya Yesu kurudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu.

Wanapendezwa zaidi na kwenda njia zao wenyewe, na kumsikiliza yeyote anayewaambia, sio lile lililo kweli, bali lile wanalopenda kusikia. Imeandikwa, watu kama hao wana ‘masikio ya utafiti”. Tafsiri hii ya Kiswahili sio sahihi sana hapa. Tafsiri sahihi ingekuwa, “wana masikio yanayowawasha” (kwenye Kingereza ni ‘itching ears’. Paulo anasema:

“Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima, ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti (‘masikio yanayowawasha’); nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo” (2 Timotheo 4:3,4).

Mtume Petro naye alisema, katika siku za mwisho watu watalibeza Neno la Mungu. Anasema watalidhihaki wakisema, “Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake?” (2 Petro 4:3,4). Naona ni kama hivi ndivyo hasa watu wanavyosema siku hizi.

Ukiukaji wa Sheria.

Katika wakati Israeli walipokuwa wakiongozwa na Waamuzi, tunaambiwa: “Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli, kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe” (Waamuzi 17:6). Matokeo ya hili yalikuwa ni mauaji, uporaji, ubakaji na vurugu za aina zote. Ni hivyo ilivyo leo. Watu  hawaijali Sheria za Mungu na wanazivunja sheria za mataifa yao kila siku. Kujizuia na kujidhibiti kimienendo ni kudogo sana.

Watu wamekuwa wachoyo sana na kuwa wapenda fedha. Hawajali wengine wanavyoteseka, mradi wanapata kile wanachokitaka, iwe mali au madaraka. Paulo alisema ndivyo ambavyo ingekuwa katika ‘siku za mwisho’:

“Lakini ufahamu neno hili ya kuwa, siku za mwisho kutokuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha. Wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani….. wasiojizuia… wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu” (2 Timotheo 3:1-5).

Wakati wa taabu.

Nabii Danieli aliongelea ujio wa wakati wa taabu ambao mfano wake haujakuwapo. Huo ndio wakati tulio nao. Tunasikia mengi kuhusu ‘uchumi’ siku hizi. Ni uchumi imara unaoweza kuboresha maisha ya watu katika jamii. Unapodorora, hali za watu zinakuwa mbaya.

Katika mwaka 1973 Waarabu waliishambulia Israeli, lakini hawakuweza kuiangamiza. Baada ya hapo walipandisha sana bei ya mafuta yao na kuzorotesha uchumi wa mataifa mengi. Mataifa mengi bado yanategemea mafuta ya Mashariki ya Kati kwa uchumi wake. Matokeo, matajiri wameendelea kutajirika wakati maskini wakiendelea kudhoofika zaidi.

Kila taifa linaumia kunapokuwa na mitikisiko ya kiuchumi. Inasababisha watu kupoteza kazi na masononeko kila mahali. Inaonekana matatizo yaliyo mengi hayana ufumbuzi; kumekuja wakati wa taabu aliousemea Danieli:

“Kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati  huo huo……Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima  wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele” (Danieli 12:1,2).

Taabu zilizopo zinaonesha tulivyo karibu na kurudi kwa Yesu.

Israeli na mataifa.

Waisraeli wanazungukwa na maadui. Mataifa ya Kiarabu yamekuwa yakinuia kuliangamiza Taifa la Kiyahudi na kuitwaa tena nchi ile, ambayo wanaihesabia kuwa ni yao. Kuna mivutano isiyoisha na vita katika mipaka ya Israeli wakati wote.

Waarabu wanadai ndio wenye haki ya nchi hiyo, lakini ni Mungu aliyemuahidia Ibrahimu, Isaka na Yakobo hapo kale, na uzao wao, kuwa urithi wao wa milele. Migogoro itaendelea na mataifa yote hatimaye yatavutwa kwenye vita vitakavyotokea.

Hapo ndipo Kristo atakaporudi. Yapo karibu kutokea haya; ujio wa Kristo u-karibu. Akiongelea nyakati hizi, mtume Petro anawaasa wale wanaoyafahamu mambo haya, akihoji: “Imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa?” (2 Petro 3:11).

Ni kitu ambacho sisi wote tunapaswa kujihoji wakati wote.

Muhtasari

Hatujui siku wala saa Bwana Yesu atakaporudi duniani kutoka mbinguni, lakini kuna ishara nyingi zinazoonesha atarudi karibuni. Baadhi yake ni hizi:

  1. Kurudi kwa Wayahudi kwenye nchi yao.
  2. Kuanza upya kwa Taifa la Israeli, mwaka 1948.
  3. Yerusalemu kuwa mji mkuu wa Israeli tangu mwaka 1967.
  4. Uwepo  wa matatizo mengi duniani.
  5. Watu kuwa na hofu ya  yanayoipata duniani.
  6. Vurugu na kuongezeka kwa ukatili.
  7. Uwepo wa taabu ambazo hazijatokea nyuma.
  8. Maadui wa Israeli kujiandaa kuipiga.

Mistari ya kusoma: Yeremia 31:10,  Ezekieli 5:5,  Yoeli 3:1, 2,  9-18

Jifunze kwa moyo:  Luka 12:40

“Ninyi jiwekeni tayari kwa kuwa, saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu”.

Swahili Title
Ishara za kurudi kwa Yesu - Somo la 08
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission