Somo la 10
MUNGU ANAVYOIONA HISTORIA
SOMO: Danieli 2
Mungu hatazami historia kwa namna tunavyoitazama sisi. Ile watu wanayoiona kama dola yenye nguvu sana, inaweza kuwa si chochote machoni pake. Kwa upande mwingine, mtu anayeonekana mkimya, mwenye unyonge, anayedharauliwa na wenzake, anaweza kuwa wa thamani kubwa machoni pa Mungu.
Biblia ni kitabu cha historia cha Mungu, na Wayahudi ni watu wake. Mpango wa wokovu wa Mungu kwa wanadamu umejengekea kwa Wayahudi, ingawa kwa njia ya Kristo umetanuka kuyafikia mataifa yote. Kwa sababu hiyo, basi, historia katika Biblia inawahusu zaidi Wayahudi.
Katika Biblia kuna maelezo mafupi ya watu kadhaa wa muhimu:

ADAMU: Adamu alikuwa mtu wa kwanza. Mungu alimuumba akiwa mwema kabisa, lakini hakumtii Mungu. Tangu wakati huo, watu wote wamemkiuka Mungu na wanaendelea kumkiuka kwa namna moja au nyingine, na wote wanakufa.
NUHU: Nuhu alizaliwa zaidi ya miaka elfu moja baada ya Adamu. Katika siku zake, wanadamu walikuwa wamekuwa waovu mno kiasi kwamba, Mungu alituma gharika na kuwaangamiza wote, akibakia Nuhu na familia yake tu. Nuhu alimwamini Mungu na kumtii (Mwanzo 6).
IBRAHIMU: Ibrahimu anaitwa katika Biblia âRafiki wa Munguâ. Mungu alimwambia aiache nyumba yake kule Uru, aende kuishi Kanaani, na Ibrahimu alimtii. Mungu alifanya naye Maagano ya muhimu sana (Mwanzo 12).
ISAKA: Isaka alikuwa mwana wa Ibrahimu, aliyezaliwa ki-muujiza wakati Ibrahimu na mke wake, Sara, wakiwa wazee sana kuweza kupata watoto (Mwanzo 21).
YAKOBO: Yakobo alikuwa mwana wa Isaka. Mungu alimbadilisha jina na kumwita âIsraeliâ, maana yake, âMkuu pamoja na Munguâ. Yakobo alipata wana kumi na wawili.
YUSUFU: Yusufu alikuwa mmojawao wale wana kumi na wawili wa Yakobo. Kaka zake walimuonea wivu, na kumuuza apelekwe Misri kuwa mtumwa. Yalimpata majaribu mengi, lakini Mungu alimbariki; akawa wa pili kwa ukuu, kimamlaka Misri.
Baada ya hapo, familia yote ya Yakobo ilijiunga na Yusufu kule Misri (Mwanzo 46). Miaka mingi baadaye, wakiwa wameongezeka na kuwa taifa la Kiyahudi, walifanywa kuwa watumwa na Wamisri.
MUSA: Wazazi wa Musa walikuwa Wayahudi, lakini alilelewa na kuwa mwana wa binti Farao, mfalme wa Misri. Mungu alimtumia Musa kuwatoa Waisraeli Misri, na kuwaleta katika nchi ya Kanaani, aliyokuwa amewaahidia.
Mungu aliwapa watu hawa Sheria za hekima na haki, lakini hawakupenda kuzitii. Walizipenda zaidi ibada za Kimisri; ibada za sanamu.
|
SANAMU Sanamu ni kitu chochote kinachoabudiwa; badala ya Mungu wa Kweli. Watu wameabudu vitu vingi- jua, miti, vinyago, mawe, picha za vitu, mali n.k. Vyote hivi ni miungu ya uongo; haviwezi kusaidia, haviwezi kuokoa. |
Baada ya miaka 40 ya kuzagaa-zagaa nyikani, ambapo waliokuwa watu wazima karibu wote walikufa kwa kukosa imani, uzao wao ulifika katika nchi Mungu aliyokuwa amewaahidia.
YOSHUA: Ndiye aliyewaingiza watu hao katika nchi ya ahadi, nchi ya Kanaani.
Waamuzi ulingoni
Kwa miaka kama 400 Wayahudi waliongozwa kwa vipindi tofauti-tofauti na Waamuzi, lakini Mungu ndiye aliyekuwa Mfalme wao. Mara kwa mara walizivunja amri zake, na aliwaadhibu kwa kuleta mataifa ya nje kuwapiga. Matatizo yalipowazidia, walimgeukia Mungu na aliwaokoa kwa kutuma Waamuzi.
Watu wataka Mfalme
Badala ya kuishi kwa furaha wakimtii Mungu, Wayahudi waliomba wapatiwe mfalme. Hawakuwa wakimtaka Mungu. Walitaka mfalme wanayeweza kumwona, kama ilivyokuwa kwa mataifa mengine.
SAULI: Alikuwa ndiye aliyekuwa mfalme wa kwanza. Hakumpendeza Mungu; hakuwa mtiifu. Mfalme wa pili, Daudi, anaitwa katika Biblia âmtu anayefanana na moyo wa Munguâ. Huyu alikuwa mtiifu sana. Alipewa ahadi za kipekee sana na Mungu, za kutimizwa na Bwana Yesu Kristo (2 Samweli 7).

Daudi alifuatiwa katika kiti chake cha enzi na mwanawe, Sulemani, lakini Israeli walikuwa bado ni Ufalme wa Mungu, kama tulivyoona katika 1 Nyakati 29: 23.
Ufalme unagawanyika
Baada ya Sulemani, Ufalme ulijigawa sehemu mbili. Ufalme wa Kaskazini ukaitwa Ufalme wa Israeli na ule wa Kusini ukaitwa Yuda. Watu wa Israeli upande wa kaskazini walikuwa waovu sana kiasi kwamba, Mungu aliwaleta Waashuru juu yao. Waliwachukua mateka, na hawakuirudia tena nchi yao.
Ufalme wa Yuda, kusini, hawakuwa na unafuu wa maana. Baada ya muda walibebwa nao mateka kupelekwa Babeli. Tokea wakati huo hakujawa na mfalme tena. Baadhi ya watu wa Yuda waliirudia nchi yao ya Israeli baada ya miaka 70.
Agano Jipya
Hatimaye, kama miaka 400 baada ya Yuda kurudi na Agano la Kale kufungwa, Mungu alimtuma Mwanawe mwenyewe, Bwana Yesu Kristo. Agano Jipya linatupa simulizi juu ya Yesu, na jinsi kanisa la Kikristo lilivyoanza.
Ndugu zake wa Kiyahudi karibu wote walimkataa Yesu. Baada ya hapo Mungu alitoa âofaâ ya uzima kupitia kwa Yesu kwa mataifa yote, kwa nia ya Agano Jipya. Humo tunasoma vile hao Wakristo wa kwanza walivyosafiri mbali wakihubiri juu ya namna mpya ya maisha. Kuhubiri kwa namna hiyo bado kunaendelea kufanywa hata sasa.
Picha ya Falme za Dunia
Kabla hujajifunza somo linalofuata, hebu jaribu kuichunguza kwa makini picha inayofuata.
![]() |
|
Maono yaliyohusu picha hii, ni historia inayouhusu ulimwengu, kuanzia wakati wa Dola ya Babeli, kushuka mpaka nyakati zetu hizi, na kuendelea mbele. Yanahusu vile Mungu anavyotambua mataifa na kuziongoza nchi, na ameelekeza lini Ufalme wa Mungu utakuja.
Unakumbuka vile Waisraeli (wa Yuda) walivyochukuliwa mateka kwenda Babeli? Miongoni mwao alikuwapo kijana mmoja aliyeitwa Danieli.
Usiku mmoja, Nebukadreza, aliyekuwa mfalme wa Babeli, alipata ndoto moja ya ajabu sana. Ndoto hiyo ilitumwa kwake na Mungu, na Danieli alimfafanulia maana yake.
Mfalme aliona sanamu kubwa sana, iliyokuwa ikifanana na picha ya mtu. Sanamu hiyo ilisimama badala ya dola nne kubwa: Dola ya Babeli, Dola ya Wamedi na Waajemi, Dola ya Wayunani, na Dola ya Warumi. Zote hizi katika historia ya dunia zilishamiri kwa vipindi fulani, moja baada ya nyingine na kupita. Tunaweza kusoma habari zake katika vitabu vya Historia vya kawaida.
Kile kichwa cha dhahabu kiliwakilisha ufalme wa Babeli, ambao ulikuwa umenawiri sana. Kifua na mikono katika sanamu yalikuwa ni madini ya fedha, na yaliwakilisha dola ya Wamedi na Waajemi. Chini yake tumbo na kiuno ilikuwa shaba, ikiwakilisha dola ya Wayunani.
Hatimaye ilikuja dola ya Warumi iliyokuja kuutawala ulimwengu. Iliwakilishwa na miguu ya chuma; chuma kwa sababu ilikuwa kali na ya kikatili, yenye nguvu sana. Dola hii ilipanuka na kuenea maeneo ya mbali zaidi kuliko dola zote, na miongozo yake ya kisheria ni msingi na Sheria za mataifa mengi hata leo. Ni katika wakati huu wa dola ya Kirumi alipozaliwa Bwana Yesu na ni askari wa Kirumi waliomsulubisha.
Baada ya mamia ya miaka Dola ya Warumi nayo ilisambaratika. Hakujatokea dola inayojulikana juu ya mataifa, kwa namna ilivyokuwa.
Kwa miaka kama 1500, dunia imekuwa kwenye nyayo za sanamu ile ya Nebukadreza. Ni mchanganyiko wa chuma na udongo; mataifa yenye nguvu na mataifa dhaifu. Ndivyo ilivyo leo.
Alafu, katika ndoto, Nebukadreza aliona jiwe dogo ambalo, âLilichongwa mlimani bila kazi ya mikonoâ (Dan. 2:45). Hilo liliipiga sanamu hiyo kwenye miguu yake, na kuivunja vipande vipande. Kisha lilikua likawa mlima mkubwa, ulioijaza dunia yote. Jiwe hilo lililotoka juu, lililokatwa âbila ya kazi ya mikonoâ ni kielelezo cha Yesu, ambaye hakuwa na baba wa kibinadamu. Atakaporudi duniani, atazivunja-vunja falme za kibinadamu, na kuusimamisha Ufalme wa Mungu, utakaokua na kuijaza dunia yote.
Kwa sasa tupo katika nyakati za hicho chuma na udongo, wakati wa mitengano. Baadhi ya mataifa ni tajiri na yenye nguvu, na yaliyo mengi ni madhaifu. Yanakubaliana katika baadhi ya mambo tu. Wamegawanyika, hakuna umoja, kama ambavyo vipande vya chuma visivyoweza kuungana na udongo. Haviwezi kushikamana. Muda si mrefu Yesu atarudi. Atazivunja tawala za kibinadamu, na kuusimika utawala wa Mungu, utakaoenea ulimwenguni pote.
Mengi ya yale yaliyoelezwa kuihusu ndoto ya Nebukadreza, yametimia na sasa ni historia. Tunaweza kuwa na uhakika ya kwamba kipande kilichobaki cha mwisho (cha wakati tulio nao), nacho kitatimia. Kumbuka: Ufalme unaozungumziwa ni wa hapa duniani.
|
Muhtasari
|
Vifungu vya kusoma: Kuna vifungu vingi vinavyotajwa katika somo hili. Jaribu kuvisoma vyote; vitakuza uelewa wako. Baada ya hapo soma Matendo 7.
Mstari wa kuushika: Danieli 2:44.
âNa katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake, bali atavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na mileleâ.
