Somo la 11
UFALME WA MUNGU â AMANI DUNIANI
SOMO: Isaya 35
Amani Duniani â Lini?
Yesu alipozaliwa, malaika waliimba kwa shangwe. Maneno ya wimbo wao yameandikwa katika Luka 2:14: âAtukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhiaâ.
Hata hivyo tangu wakati huo hadi sasa, hakujawahi kuwa na amani ya sawasawa inayodumu katika dunia. Haitaweza kuwapo, mpaka hapo Yesu atakaporudi duniani kuusimamisha Ufalme wa Mungu. Agano la Kale linatuambia mengi kuhusu Ufalme huo, na linatupa vidokezo vingi vya wakati wa amani na neema utakaoletwa na Ufalme huo.
Ukubwa wa Ufalme huo
Hebu iangalie Zaburi ya 72. Katika Zaburi hii tunapewa picha kwa njia ya maneno, ya wakati Ufalme wa Mungu utakaposimamishwa katika dunia. Lakini, kwa sasa, angalia hasa mstari wa 8 unachosema:
âNa awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya duniaâ.
Hapa tunaambiwa kuwa, Ufalme atakaousimamisha Yesu, wenye chimbuko lake katika Israeli, utaenea dunia nzima. Tunaona kitu kama hicho katika Zaburi 2:8, ambapo Mungu anasema na Yesu, akimwambia:
âUniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yakoâ.
Hebu tutazame mstari mmoja zaidi. Katika Zekaria 14:9 tunaambiwa:
âNaye BWANA atakuwa Mfalme juu. ya nchi yote, siku huyo BWANA atakuwa mmoja, na jina lake mojaâ.
Utawala wa Kristo
Yesu Kristo atatawala kutokea Yerusalemu, makao yake makuu, ambayo kuna wakati aliyaita, âMji wa Mfalme Mkuuâ (Mathayo 5:35). Sheria zake ndipo zitakapotokea na kuenea duniani mwote. Katika Isaya 2, tunaambiwa: âKatika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemuâ (Isa 2:1-4).
Ufalme mzuri
Kama ungetakiwa kusema ni hali gani ungependa kuiona kwenye dunia iliyo bora, ungesemaje? Natumaini, kati ya mambo ambayo ungeyatamani sana yangekuwa ni: mazingira ya amani; kusiwe na hofu, kuwe na ufanisi na utulivu wa kuweza kuyafurahia matunda ya kazi zako n.k. Ungeweza pengine kuwa na mawazo ya kitu kama kile nabii Mika anachotupa, akisema:
âNaye (Yesu Kristo) atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali, nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe mundu, taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake, wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hiviâ (Mika 4:3,4).
Lakini kabla hakujawa na amani, itakuwa lazima kuwe na jitihada ya makusudi kati ya watu, ya kutembea katika Njia za Mungu. Wakati wote watu wanapokuwa wakiziendea njia zao wenyewe, ni lazima kuwe na matatizo. Kwa hiyo jambo kubwa la kwanza atakalofanya Bwana Yesu litakuwa kuyafundisha mataifa yote Njia za Mungu.
Lakini unaweza kusema, wapo tu ambao hawatakuwa tayari kumsikia. Hilo ni kweli, lakini, hao wasiomtii wataadhibiwa. Tunasoma katika Isaya 11:4 kuwa: âKwa pumzi ya midomo yake atawaua wabayaâ.
Kumbuka, Yesu atakapokuja tena, atakuwa na uweza wote.
Ni nani watakaokuwa katika Ufalme huo?
-
Kwanza kutakuwa na watawala. Hawa watakuwa ni wanaume na wanawake ambao wamekuwa wafuasi. Hawa ni wote waliomfuata Yesu katika nyakati zote mpaka anaporudi. Sasa watakuwa wamepewa uzima usio na mwisho na Yesu katika kuja kwake. Watakuwa Wafalme na Makuhani, wakimsaidia Yesu kuitawala dunia. Watakuwa watu ambao hawafi; watu wasioweza tena kufa:
âNao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake, kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchiâ (Ufunuo 5:9,10).
-
Watakuwapo pia Wayahudi waliompokea Yesu kuwa Mfalme wao. Yerusalemu itakuwa ni Makao Makuu ya dunia nzima. Mataifa yote yataielekea, kwa kuwa ndipo Sheria ya Mungu itakapokuwa ikitokea.
âWakati ule utauita Yerusalemu kiti cha enzi cha BWANA, na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la BWANA, wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbayaâ (Yeremia 3:17).
Kristo atakuwa miongoni mwao na watakuwa wamebarikiwa sana. Lakini watakuwa bado wakifa; watakuwa hawajapata uzima wa milele.
-
Kristo atakapokuja, hukumu za Mungu zitakuwa kali, na watu wengi watakufa. Wale watakaoachiwa kuendelea kuishi popote pale walipo katika dunia, watakuwa chini ya mamlaka ya Yesu, wakijifunza kufanya yale yanayompendeza Mungu. Neno la Mungu kwa Isaya linasema:
âHukumu zako zikiwapo duniani, watu wakaao duniani hujifunza hakiâ (Isaya 26:9).
Neema kwa wote
Kutokana na mazingira bora kabisa yatakayokuwapo, kutakuwa na mibaraka kwa kila mtu. Zaburi ya 72:16 inasema:
âNa uwepo wingi wa nafaka juu ya milima, matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoniâ.
Juu ya milima kwa kawaida huwa hakuna kitu. Kama kunaweza kuwa na nafaka nyingi katika vilele vya milima, tunaweza kujua kwa kiasi gani mavuno yatakuwa mengi mabondeni. Zaburi ya 67:6 inatoa picha ya wakati huo, ikisema: âNchi imetoa mazao yake, MUNGU, Mungu wetu ametubarikiâ.
Hata majangwa yatakuwa kijani siku hizo. Soma mistari miwili iliyopo tena katika Isaya inayosisimua, inayotuambia:
âNyika na mahali palipo ukiwa patafurahi, jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimbaâ (Isa 35:1, 2).
Kuponywa kwa akili na mwili
Pamoja na mibaraka hii, kutakuwa na mibaraka ya afya bora na nguvu.
Yesu alipoishi duniani miaka 2000 iliyopita, aliwapa afya wengi waliokuwa wagonjwa, kwa kutumia uweza aliopewa na Mungu. Katika Ufalme wa Mungu, uweza huo utaonekana tena. Endelea kusoma Isaya 35 mstari wa 6:
âNdipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimbaâ.
Tunaweza pia kuona kwamba, watu wale wanaokufa (wasiopata uzima wa milele), wataishi maisha marefu zaidi kuliko wanavyoishi sasa. Nabii Zekaria anatuambia hivyo ndivyo itakavyokuwa. Anasema:
âWazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zakeâ (Zek. 8:4,5).
Mistari hii inaiongelea Yerusalemu, lakini, kama tulivyoona, mibaraka ya Ufalme huo itaenea maeneo yote ya dunia.
Neno thabiti la Mungu
Pengine unasema: âHaya yote yanaonekana mazuri sana, lakini nina shaka hayawezi kutokeaâ. Kama ahadi hizi tunazozisoma zingewategemea wanadamu, kwa hakika tusingeweza kuziwekea tumaini. Hata mtu anayeonekana kuwa mkweli sana, anaweza kushindwa kutekeleza anayowaahidi wengine kwa sababu ya udhaifu wa kibinadamu.
Lakini ahadi hizi zinatoka kwa Mungu, na kwa sababu hiyo tunaweza kuzitumainia kabisa. Hebu soma Isaya 55:6-11. Katika mstari wa 11 Mungu anasema:
âNdivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu, halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolitumaâ.
Kwa hiyo tunaweza kuutazamia kwa matumaini mema wakati huo unaokuja wa utukufu, unaoletwa na Mungu aliye juu mbinguni. Utakuwa wakati wa furaha na, âAmani duniani, kwa watu aliowaridhiaâ (Luka 2:14).
Utimilifu mkubwa zaidi
Kipindi cha Ufalme kitakachochukua miaka elfu moja, kitakuwa kipindi kizuri ajabu, lakini hakitakuwa kikamilifu. Mtu wa kawaida anayeishi katika enzi hiyo ya Ufalme, bado atakuwa na hulka ya ubinadamu-wake, inayopata urahisi kukosea na kushindwa. Bado watu watazeeka na kufa. Tunaambiwa pia kwamba, yapo mataifa yatakayofanya uasi dhidi ya utawala wa Bwana Yesu, utakapokaribia mwisho wa kipindi hicho.
Bwana Yesu atawashinda vibaya. Hakuna shaka juu ya hili. Waliokufa watafufuliwa na Yesu, na hukumu itapita. Wakati huo, wale ambao wamekuwa waaminifu katika wakati huo wa Ufalme, watapewa nao tuzo yao ya uzima wa milele.
Baada ya hapo, dunia yote itajazwa utukufu wa Mungu, naye Muumba Mkuu wa yote atakuwa âyote katika woteâ (1 Wakorintho 15:28).
Muhtasari
-
Yesu atakuja tena na kuwa Mfalme wa dunia.
-
Makao yake makuu yatakuwa Yerusalemu.
-
Dunia itakuwa mahali pa amani na neema, afya bora na furaha.
-
Katika Ufalme wa Yesu, kila mtu atajifunza kuzitii amri za Mungu.
-
Katika Ufalme huo kutakuwa na:
-
Watu wasiokufa: Ni wale waliomfuata Yesu na kumtii Mungu katika maisha yao ya sasa. Wakiwa wamepewa uzima usio na mwisho, hawatapatwa na machungu, wala kulazimika kupambana na dhambi tena. Ndio watakaomsaidia Yesu kutawala na kuiweka sawa dunia na watu wake katika Ufalme wa Mungu.
-
Watu wa kawaida (wanaokufa) watakaokuwa wameokoka kwenye zile hatari na hekaheka za hukumu za Mungu juu ya dunia iliyojaa uovu. Watajifunza kumtumikia Mungu na kumcha na kumwabudu.
-
Vifungu vya kusoma: Zaburi 72; Mika 4: 1-7
Kujifunza kwa Moyo: Zaburi 22: 27, 28
âMiisho yote ya dunia itakumbuka, na watu watamrejea BWANA, jamaa zote za mataifa watamsujudia. Maana ufalme una BWANA, naye ndiye atawalaye mataifaâ.
|
KURUDI KWA KRISTO DUNIANI |
KRISTO ANAUKABIDHI UFALME |
|
|
WAKATI TULIO NAO |
UFAMLE WA MUNGU DUNIANI (Miaka 1000) |
MUNGU ANAKUWA âYOTE KATIKA WOTEâ |
|
Falme za wanadamu
Mwisho wa falme za wanadamu; waumini wanafufuliwa. |
KRISTO ANATAWALA DUNIA AKIWA NI MFALME
Watu wasiokufa na watu wanaokufa. |
Watu wasiokufa tu!
Mwisho wa dhambi zote na mauti.
|
|
Jedwali la falme za wanadamu na Ufalme wa Mungu. |
||