Ahadi za Mungu kwa Ibrahimu - Somo la 12

Swahili

Somo la 12

AHADI ZA MUNGU KWA IBRAHIMU

SOMO: Mwanzo 13

Miaka ipatayo 2000 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, aliishi mtu mmoja aliyeitwa Abram, anayezungumziwa katika Biblia kuwa alikuwa ‘rafiki wa Mungu’ (Isaya 41:8). Aliishi Uru, mji uliokuwa katika Mesopotamia, katika nchi tunayoiita leo Iraki, kama maili 800 mashariki ya nchi ya Israeli.

Watu wa Uru hawakujua lolote kumhusu Mungu wa Kweli; waliabudu miungu mingi ya uongo, mkubwa kati yao akiwa ni mungu-mwezi.  Mabaki ya hekalu alilojengewa yamegunduliwa katika eneo hilo.

Ujumbe kutoka kwa Mungu

Siku moja Abram alipokea ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tunaweza kuusoma ujumbe huo katika Mwanzo 12:1 ambapo Neno linasema: “BWANA akamwambia Abram, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha”.

Alikuwa anaambiwa aiache nchi alimozaliwa, aende kuiendea nchi asiyoijua ambayo Mungu angemuonesha. Sijui tungejisikiaje tungepewa agizo kama hilo, na hasa tukizingatia kuwa, usafiri nyakati hizo ulikuwa kitu kigumu sana na cha hatari kuliko ilivyo sasa.

Mungu alipomwagiza Abram afanye hilo, alimwambia pia: “Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka.  Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” (ms.2,3).

Abram aliziamini ahadi zile Mungu alizompa, na kumttii.  Mwandishi kwa Waebrania anatuambia, Ibrahimu (Jina  lingine alilopewa Abram baadaye):

 â€œAkatoka asijue aendako” (Waebr.11:8).

Baada ya siku nyingi, aliifikia nchi ya Israeli, wakati huo ikiitwa nchi ya Kanaani, akiwa na mke wake, Sara, na mwana wa ndugu yake aliyeitwa Lutu.  Sasa isome Mwanzo 13. Utaona vile Lutu alivyochagua nchi iliyokuwa bora zaidi, na Abram kubakia akitafuta malisho kwa shida kwa ajili ya mifugo yake katika sehemu ya nchi iliyokuwa kame zaidi.  Lakini Mungu alikuwa na Abram, na akaipanua ahadi ile aliyompa awali kule Uru, akimwambia:

“Nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele. Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi” (Mwanzo 13:15,16).

Hapa Mungu alikuwa akimwahidia Ibrahimu kuwa, nchi hiyo yote ingekuwa urithi wake wa milele. Ili Ibrahimu aweze kuimiliki nchi hiyo milele, ilibidi awe anaishi milele; kwa hiyo Mungu alikuwa hapa akimwahidia uzima wa milele. Nchi aliyokuwa akiahidiwa ilikuwa ni nchi aliyooneshwa; nchi kwa sasa tunayoiita Israeli.

Pamoja na hilo, Mungu aliahidi urithi wa nchi hiyo pia kwa ‘uzao’ wake. Kwa wakati huo, Ibrahimu na Sara hawakuwa na watoto. ‘Uzao’ huo ulikuwa ukimhusu ‘Mwana’ mmoja maalumu, ambaye angeimiliki nchi hiyo pamoja na Ibrahimu. Mungu aliahidi pia kwamba uzao ambao ungetokana na Ibrahimu ungekuwa taifa kubwa.

Mungu afanya Agano na Ibrahimu

Fungua Mwanzo 15. Hapa utaona kuwa, Mungu anazirudia tena ahadi zake kwa Ibrahimu na kuziongezea.

Miaka ilikuwa inakwenda, na Ibrahimu alikuwa akizeeka.  Mwana aliyeahidiwa alikuwa hajampata. Kwa mara nyingine tena Mungu anamhakikishia kuwa angepata mtoto, na kwamba wazaliwa wake wangekuwa wengi kama nyota za mbinguni. Katika mstari wa 6 tunaambiwa, Ibrahimu: “Akamwaamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki”.

Ibrahimu, kama tulivyo nasi, hakuwa mkamilifu. Hata hivyo, alimwamini na kumtumaini Mungu, na kwa sababu hiyo Mungu alimfurahia.  Mungu alifanya sasa Agano na Ibrahimu; mapatano yasiyoweza kamwe kubatilika.  Agano hili lipo katika Mwanzo 15:8-18.

Kwa nyakati hizo za Ibrahimu, Agano lilikuwa likifanywa kwa mnyama kuchinjwa. Mnyama huyo aligawanywa vipande vipande, na watu wawili waliokuwa wakifanya Agano walitembea kati ya hivyo vipande.  Katika tukio hili, utukufu wa Mungu ulipita kati ya vipande hivyo, na kwa hiyo Ibrahimu alitambua ya kwamba Agano hilo lingekuwa thabiti.

Mwana aliyeahidiwa

Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka 100 na mke wake 90, wakati hatimaye Mungu alipomtimizia mojawapo ya ahadi zake. Walimpata mwana, waliyemuita Isaka.

Katika Mwanzo 22 utaona kielelezo cha ajabu cha imani aliyokuwa nayo Ibrahimu kwa Mungu.  Soma mistari 14 ya kwanza.  Mungu alimtaka Ibrahimu amtoe mwanawe, Isaka, awe sadaka. Hili lilikuwa ni jaribu kubwa maana

Mungu alikuwa ameahidi kuwa kupitia kwa Isaka, uzao wa Ibrahimu ungekuwa taifa kubwa.

Ibrahimu alifanyaje? Alijua kuwa Mungu angeweza bado kuzitimiza ahadi zake, na kwa hiyo mwandishi wa Waebramia anatuambia:

“Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye aliyeambiwa, katika Isaka uzao wako utaitwa, akimhesabu ya kuwa Mungu  aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko  kwa mfano” (Waebr. 11:17-19).

Ibrahimu alikuwa tayari hata kumtoa mwanawe mpendwa, akijua ya kuwa Mungu angeweza kumrudishia uhai. Ndio maana tunaona jinsi Mungu alivyopendezwa na Ibrahimu, kwa jinsi alivyomtumaini na kumtii. Katika Mwanzo 22:15–18 Mungu alimpa tena ahadi ya ziada.

Mzaliwa Mkuu kuliko Isaka

Haya mambo yalitokea kama miaka 4,000 iliyopita, na juu-juu  hayaonekani kama mambo ya sisi kuyajali sana. Lakini, Ibrahimu alipata ‘Mwana’ baadaye ambaye alikuwa ‘Mkuu’ zaidi kuliko Isaka. Mstari wa kwanza wa Agano Jipya unamzungumzia, ukimtaja. Ni “Yesu Kristo, Mwana wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu” (Mathayo 1:1).

Kwa hiyo, Yesu naye alikuwa ‘Mwana’ aliyeahidiwa kwa Ibrahimu. Paulo anatuambia hili katika Wagalatia 3:16, akisema:

“Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja: kwa mzao wako, yaani, Kristo”.

Kwa hiyo, ahadi alizopewa Ibrahimu kwamba angeishi milele katika nchi ya Israeli na kuwa ‘mbaraka kwa mataifa yote’, zilikuwa pia ni ahadi zilizofanywa kumhusu Bwana Yesu Kristo.

Atakapokuja tena kuitawala Israeli na dunia kutokea Yerusalemu, tutaona ahadi hizi zikitimilika, na kubwa zaidi ni kwamba, nasi tunaweza kuwa na sehemu katika ahadi hizo. Kama tukimwamini Yesu na tukafanya kile anachotutaka tufanye, tunaweza nasi kuwa washiriki wa ahadi hizi, kwa kuwa tunaweza kuwa ‘wana’ wa Ibrahimu pia.

Katika mstari wa mwisho wa Wagalatia 3 tunaambiwa: “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi” (Wagalatia 3:29).

Kuwa na sehemu katika ahadi hizo ni kuweza kupata uzima wa milele, na kumsaidia Yesu Kristo katika kazi kubwa inayokuja ya kuleta ufanisi, amani na furaha duniani. Tunawezaje kuwa watu wa ‘uzao wa Ibrahimu’? Jibu ni- kwa kuamini na kubatizwa katika Yesu Kristo. Hiki ndicho hasa Paulo anachosema katika Wagalatia 3:26–29, anaposema:

“….Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi”.

Utakumbuka kuwa mojawapo ya ahadi ya ziada aliyopewa ilikuwa kwamba:

“Na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia” (Mwanzo 22:18).

Ahadi hii itatimia hapo Yesu atakaporudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu.

Ibrahimu je?

Lakini unaweza ukawa unafikiri, Ibrahimu je, itakuwaje juu yake? Hakuwahi kuzitimiziwa zile ahadi na alikufa! Hilo ni kweli. Lakini ahadi za Mungu haziwezi kushindwa. Yesu atakapokuja, atamfufua Ibrahimu na Isaka kutoka kwa wafu, na wengi wengineo, na wataishi milele katika dunia, wakiifurahia hiyo mibaraka Mungu aliyowaahidia zamani hizo.

Utambue hapa ya kuwa, Mungu hakumwahidia Ibrahimu mahali au urithi katika Ufalme ulioko juu mbinguni. Alimwahidia nchi aliyoiona  na kuishi ndani yake.

Muhtasari

  1. Ibrahimu aliitwa na Mungu kuondoka Uru, aende kwenye nchi asiyoijua.
  2. Nchi hiyo ilikuwa ni nchi ya Israeli, na aliahidiwa kuwa ingekuwa yake milele.
  3. Mungu alimwahidi Ibrahimu pia kupata mwana, na kwamba uzao wake ungeongezeka na kuwa taifa kubwa. Mwanawe huyo aliahidiwa kuwa mbaraka kwa mataifa yote.
  4. Ibrahimu alimpata huyo mwana, Isaka, aliyezaliwa kwa muujiza wakati wazazi wake wakiwa wazee. Yesu Kristo naye ni mwana wa Ibrahimu, naye alizaliwa kwa muujiza kupitia kwa mwanamke aliyekuwa bikira.
  5. Kama tunakuwa ‘Wa-Kristo’ kwa kumwamini na kubatizwa, tutakuwa tunahesabiwa kuwa wana wa Ibrahimu, na kuwa washiriki wa ahadi alizopewa.
  6. Ahadi hizi zitatimia Yesu atakaporudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu.

 

Pendekezo:

Mada hii inayohusu uzao wa Ibrahimu ni ngumu kidogo kueleweka kwa mara ya kwanza, lakini ni ya muhimu sana. Unaonaje ukiisoma tena kwa mara nyingine sasa!

Kifungu cha kusoma:     Waebrania 11 (Zingatia hasa ms. 39, 40).

Kujifunza kwa moyo:     Wagalatia 3:27 – 29.

 

Jedwali la ahadi za Mungu kwa Ibrahimu

Rejea katika Mwanzo

Mungu alichomuahidi Ibrahimu

          Muhtasari

12:2

 

 

12:3

 

 

 

12:7

 

 

13:16

Ibrahimu angekuwa taifa kubwa na Mungu angembariki.

 

Katika Ibrahimu mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.

 

 

Nchi alimoishi Ibrahimu ingefanywa kuwa mali yake na uzao wake milele.

 

Wazaliwa wa Ibrahimu watakuwa kama mavumbi ya nchi kwa wingi.

Ibrahimu alikuwa Myahudi wa kwanza.

 

 

Kupitia katika uzao wa Ibrahimu, tunaweza kupata mbaraka wa wokovu na sehemu katika Ufalme wa Mungu unaokuja duniani.

 

Hii ilikuwa ni nchi ya ISRAELI.

 

 

Ingawa kumekuwa na majaribio kadhaa ya kuwaangamiza Wayahudi, bado wapo na ni wengi hata leo.

Angalia pia Mwanzo 15:18, 17: 6-8, 22: 16 - 18

 

Swahili Title
Ahadi za Mungu kwa Ibrahimu - Soma la 12
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission