Wayahudi katika Historia - Somo la 13

Swahili

SOMO LA 13

MASOMO YA WAKRISTADELFIA KWA NJIA YA POSTA

 

WAYAHUDI KATIKA HISTORIA

(Sehemu ya 1)

 

SOMO: Mwanzo 37

 

Mwanzo wa historia yao

Habari za Wayahudi zinaanza hasa ni yule mtu mmoja aliyekuwa mtu wa imani sana, aliyeitwa Ibrahimu. Alipata mtoto wa kiume wakati wa uzee wake, aliyeitwa Isaka, na Isaka akawa na mwana aliyemwita Yakobo, aliyepewa jina la Israeli baadaye. Yakobo alipata wana kumi na wawili wa kiume, ambao ni mababa wa makabila kumi na mawili ya Israeli.

 

Mwana wa kiume wa pili kutoka mwisho aliitwa Yusufu, na historia ya maisha yake tunayoipata kwenye Biblia ni ya kusisimua wakati wote tunapoisoma. Lakini ni zaidi ya kuwa historia; inatupa simulizi juu ya matukio muhimu kuhusiana na watu wa Biblia, Wayahudi. Ndani yake tunapata kielelezo cha ajabu cha vile mkono wa Mungu unavyoyaongoza masuala yanayohusu watu wake.

 

Tunaweza kukumbuka vile kaka zake Yusufu walivyomuuza kuwa mtumwa kutokana na wivu, na vile baada ya kupatwa na majaribu mengi, Yusufu alivyopanda cheo kuwa mtawala wa Misri. Baada ya hapo, kutokana na njaa kali katika nchi ya Kanaani, baba yake na ndugu zake walihamia Misri kulikokuwa na chakula kwa wingi.

 

Kwa muda, Wayahudi (wanaoitwa pia ‘Waisraeli’ au ‘Wana wa Israeli’) walikuwa na raha kule Misri. Lakini baada ya Yusufu kufa, miaka ilivyopita, kwa kadri Wayahudi ilivyoongezeka kuwa wengi haraka, Wamisri walianza kuwahofia na kuwatesa kwa kuwafanya watumwa.

 

Uhuru wa watumwa

Pengine unaifahamu hadithi ya namna Mungu alivyowatoa watumwa wa Kiyahudi Misri, chini ya uongozi wa mtu aliyeitwa Musa, na kuwapitisha kwenye eneo lenye ukame na jangwa, mpaka kwenye mipaka ya nchi ya Israeli. Safari yao hiyo ndio wazo kuu la Kitabu cha Kutoka.

 

Katika msafara huo mrefu na wa hatari, Mungu aliwalisha na kuwakinga. Nabii Ezra akimsifu Mungu kwa hilo anasema: “Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao. Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; na nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba” (Nehemia 9:20,21).

 

Mungu anatoa Sheria

Baada ya kuivuka Bahari ya Shamu, walipokuwa wakiendelea na safari kuiendea nchi Mungu aliyowaahidia, waliufikia Mlima Sinai. Hapo kitu cha kipekee sana kilifanyika. Watu waliambiwa na Mungu wajikusanye chini ya mlima huo, na hapo Mungu alitoa tamko, kuwaambia:

 

“Ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu”

(Kutoka 19:5).

 

Na watu waliitikia, wakisema: “Hayo yote aliyosema BWANA tutayatenda” (Kutoka 19:8).

 

Baada ya hapo Mungu alimpa Musa sheria zake, na Musa akawapa watu. Kwa hakika Sheria hizo zilikuwa ni za maana sana, ambazo hakuna taifa lingine lililowahi kuwa nazo, na kama Wayahudi wangezizingatia ipasavyo, wangekuwa watu wenye raha kuliko watu wote katika dunia hii.

 

Kama ishara kuwa walikuwa ni watu wake maalumu, Mungu aliwaagiza wawe wakiitenga siku ya mwisho ya juma kwa kuifanya takatifu. Siku hiyo iliitwa Sabato; walitakiwa wapumzike siku hiyo na kuufikiria wema wa Mungu kwao.

 

Lakini hawakuzishika amri za Mungu. Hawakuweza kuzitii zote ilivyotakiwa. Ni jambo Mungu alijua lingetokea, hata hiyo aliliweka kuwalenga watambue na kujifunza kuwa, wasingeweza kujiokoa wenyewe. Ni hivyo hivyo na sisi leo; kwa sheria hakuna anayeweza kupata haki mbele ya Mungu. Walimkiuka Mungu mara nyingi, na hawakuifanya Sabato kuwa siku maalumu, kama walivyoagizwa.

 

Hatimaye waliifikia nchi ya Israeli na Mungu kuwa Mfalme wao. Aliwapa makuhani wa kuwafundisha njia zake, na waamuzi wa kuwatawala.

 

Wayahudi wataka mfalme

Miaka karibu 400 ilipita. Wayahudi wakawa hawaridhiki, na wakataka wawe na mfalme kama mataifa yaliyowazunguka; mfalme wanayemwona. Kwa kuomba mfalme, walikuwa wakimkataa Mungu kuwa mfalme wao. Wakati Samweli akiwa mwamuzi wao, alimwambia Mungu vile walivyokuwa wakiomba mfalme, Mungu akasema:

 

“Hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao” (1 Samweli 8:7).

 

Mungu aliwapa walichokitaka. Unaweza kupenda kujisomea mwenyewe simulizi la kusisimua la kusimikwa kwa Sauli kuwa mfalme wa kwanza wa Israeli. Utalipata katika l Samweli 8 na 9.

 

Ufalme unagawanyika

Sauli alifuatiwa na Mfalme Mkuu, mfalme Daudi, utakayesoma zaidi habari zake katika somo la mbele. Baada ya utawala mrefu wa miaka 40, Daudi alifariki, na mwanawe Sulemani akawa mfalme mahali pake.

 

Sulemani alitajirika sana; aliwatoza wananchi wake kodi kubwa. Hili liliwafanya wasiridhike naye. Sulemani alipokufa wananchi walikuja kwa mwanawe, Rehoboamu, kumwomba awape unafuu wa kodi. Utasoma katika l Wafalme 12, vile Rehoboamu alivyowasikiliza rafiki zake vijana, badala ya kupokea ushauri wa wazee wa hekima, waliokuwa washauri wa baba yake.

 

Walipokuja watu kumuuliza mfalme Rehoboamu kama amewakubalia ombi lao, Rehoboamu hakuwajibu kwa busara. Aliwajibu kama vile vijana walivyomshauri, kwa kuwaambia:

 

“Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kogwa lenu. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa ng’e”

(1 Wafalme 12:14).

 

Haishangazi raia kumwasi mfalme kama huyo! Makabila 10 ya Israeli yalijitoa na kuanzisha ufalme wa kwao wenyewe, chini ya bwana mmoja aliyeitwa Yeroboamu. Ni Yuda tu (kabila lililokuwa la Rehoboamu), na kabila dogo la Benyamini, waliobakia katika uaminifu kwa Rehoboamu. Kuanzia wakati huo kwenda mbele, tuna historia mbili za falme mbili tofauti katika Biblia.

 

Kuna historia ya makabila 10 yanayotajwa mara nyingi kwa jina la ‘Israeli’ (au Ufalme wa Kaskazini), na historia ya makabila mawili yanayoitwa ‘Yuda’ (au Ufalme wa Kusini). Ufalme wa Israeli ulikuwa kaskazini mwa nchi, na Yuda kusini.

 

Ukaidi wa Wayahudi

Katika Kitabu cha kwanza na cha pili cha Wafalme, tunasoma habari ya kusikitisha jinsi Wayahudi walivyomkiuka na kumsahau Mungu, kwa kuziacha njia zake. Mambo yalikuwa mabaya kiasi kwamba, hatimaye Mungu aliazimia kuwaadhibu watu wake, kulingana na tahadhari alizokuwa ametoa, kwa kuwafanya waondolewe kwenye nchi yao wakawe watumwa.

 

Utaweza kuona kutoka katika maneno kwenye 2 Nyakati 36, jinsi Mungu alivyokuwa amefanya kila aliloweza kuwarudisha watu kwenye njia zake, bila mafanikio. Kifungu kinasema:

 

“Naye BWANA, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema na kuwatuma, kwa sababu aliwahurumia watu wake na makao yake, lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu na kuyadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya BWANA juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya” (2 Nyakati 36:15,16).

 

Adhabu ilibidi ije!

 

Ufalme wa Israeli Wagawanyika

UFALME WA ISRAELI

(wa pamoja).

 

 

 

 

UFALME WA KASKAZINI WA ISRAELI UFALME WA KUSINI WA YUDA

(Makabila 10) (Makabila 2)

CHINI YA YEROBOAMU CHINI YA REHOBOAMU

 

WAFALME WENGINE WAFALME WENGINE

 

 

WALITEKWA NA KUTAWANYWA WANATEKWA KUPELEKWA UTUMWANI

NA WAASHURU BABELI

(Hawakurudi tena) (Walirudi baada ya miaka 70)


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ukiukaji wa namna hiyo ilibidi utolewe adhabu. Ufalme wa Kaskazini ulitekwa kwanza. Mfalme wa Ashuru alikuja na kuipiga Israeli na kuwateka watu na kuwapeleka Ashuru, na hawakuwahi kuirudia nchi yao tena wakiwa kama taifa.

 

Baadaye Ufalme wa Yuda nao ulitekwa na mfalme wa Babeli, lakini Mungu aliahidi kuwa baada ya miaka 70 wangeirudia nchi yao. Wengi wao walifanya hivyo baada ya miaka hiyo 70, wakitiwa moyo na manabii wa Mungu, na wakalijenga upya hekalu la Mungu katika Yerusalemu. Vitabu vitatu vya mwisho vya Agano la Kale vya Hagai, Zekaria na Malaki, viliandikwa wakati huo.

 

Kati ya Agano la Kale na Jipya

Baada ya manabii hao watatu (Hagai, Zekaria na Malaki), kulipita kipindi kirefu cha kama miaka 400, ambacho Wayahudi hawakupata ujumbe wowote wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Mungu hakusema nao. Nabii Amosi alikuwa ametabiri juu ya kipindi hicho, miaka mingi nyuma:

 

“Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA” (Amosi 8:11).

 

Kipindi hiki cha miaka 400 kinakuja kati ya kitabu cha mwisho cha Agano la Kale (Malaki), na kitabu cha kwanza cha Agano Jipya (Mathayo). Ndio maana, alipotokea Yohana Mbatizaji, kulikuwa na msisimko mkubwa sana kati ya watu. Baada ya mamia ya miaka ya ukimya, Mungu alikuwa anasema tena na watu wake.

 

 

 

Myahudi wa muhimu kuliko wote

Yohana Mbatizaji alitumwa na Mungu kuiandaa njia ya mtu aliyekuwa mkubwa zaidi yake. Mungu alikuwa anataka kumtuma Mwanawe mwenyewe kuwaokoa watu wake. Na, kwa hiyo, katika nchi ya Israeli, miaka 2000 iliyopita, Bwana Yesu Kristo alizaliwa. Mara nyingine huwa tunasahau kuwa Yesu alikuwa Myahudi!

 

Unajua yaliyotokea kumhusu Yesu. Baada ya Wayahudi kumsikia na kuyaona matendo yake ya ajabu, walimkataa. Walimshawishi Pilato amsulubishe. Pilato hakuweza kuona kosa katika tuhuma zao. Hata hivyo, kwa kuwaitikia, aliwajibu kwa kusema: “Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki.” Wayahudi walimjibu na kusema: “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu” (Mathayo 27:24,25).

 

Hakukuwa na hatia mbaya zaidi kuliko hii mbele ya Mungu; waliimwaga damu ya Mwana wa Mungu, isiyo na hatia. Hata hivyo, kutokana na mahubiri ya nguvu ya mitume, Mungu aliwapa tena fursa. Wayahudi walio wengi hawakuijali fursa hiyo ya kurehemewa, na adhabu kali ilibidi ifuate. Ilikuwa ya kutisha sana.

 

Watu wasio na kwao

Miaka kama 40 baada ya kufa kwa Yesu, majeshi ya Kirumi yalikuja na kuwapiga Wayahudi. Ulikuwa wakati wa mateso makali sana. Machungu ya vita hiyo yalikuwa kati ya mabaya kuliko yote katika Historia. Jiji la Yerusalemu lilitekwa na Warumi, na Wayahudi waliookoka walitawanywa katika mataifa yote ya dunia.

 

Mungu alikuwa amewaonya Wayahudi tangu zamani kwamba, hili lingetokea kama wangeziacha njia zake: “BWANA atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata nchi hii ya dunia” (Kumb. La Torati 28:64).

 

Na kwa hiyo, kwa miaka kama 2000 iliyopita, Wayahudi walikuwa hawana nchi ambayo ni yao wenyewe. Na mbaya zaidi, wamepata mateso mengi ya kutisha sana. Laana mbaya sana za Kumb. la Torati 28 zimewashukia. Sehemu ya mateso haya yametokea katika miaka ya karibuni. Wengi wetu tutakuwa tunajua juu ya kambi za mateso alizoziweka Hitler, kiongozi wa Ujerumani, wakati wa vita kuu ya pili (1939 – 1945).

 

Zaidi ya Wayahudi milioni sita waliuwawa kikatili sana; ukatili ulioitetemesha dunia nzima. Soma tena Kumb. La Torati 28:64-67, na utayashangaa maneno hayo yaliyoandikwa na Musa zaidi ya miaka 3,000 iliyopita. Yamekuja kutokea hivyo-hivyo katika nyakati zetu hizi!

 

Ni simulizi la kuhuzunisha, lakini hatujafikia mwisho. Tunapaswa kujisikia vizuri bado katika kulisoma Neno la Mungu; tunaambiwa, hatimaye mambo yatakuwa mazuri.

 

Vipindi katika Historia (Miaka ni ya makadirio):

 

 

  1. Miaka 3500 iliyopita.

 

 

 

  1. Miaka 2500 iliyopita.

 

 

  1. Miaka 2000 iliyopita

 

 

  1. Leo

 

Mungu aliwatoa Wayahudi Misri, na kuwapa nchi ya Israeli waishi humo. Aliwafundisha njia zake. Badala ya wao kuwa kielelezo kwa mataifa mengine, Wayahudi walifuata uovu wa mataifa hayo.

 

Mungu hatimaye aliwaadhibu kwa kuwatoa wawe mateka. Watu wa Yuda uliirudia nchi yao baada ya miaka 70, lakini bado waliendelea kumkiuka Mungu.

 

Baada ya kusulubiwa kwa Yesu Kristo, Wayahudi waling’olewa katika nchi. Kwa miaka kama 2000 wamekuwa hawana makao, tena wakibaguliwa na kuteswa.

 

Mungu anawarudisha tena watu wake katika nchi ya Israeli (Utasoma zaidi juu ya hili katika somo linalofuata).

 

Vifungu vya kusoma: Kumb. la Torati 28, 2 Nyakati 36:11 – 23.

 

 

 

Jifunze kwa moyo: Isaya 43:11,12

“Mimi, naam, mimi ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu mgeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, nami ni Mungu”.

 

 

 

 

 

Swahili Title
Wayahudi katika historia (1)
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission