Wayahudi katika Historia - Somo la 14

Swahili

Somo la 14

WAYAHUDI KATIKA HISTORIA (Sehemu ya 2)

Somo:  Ezekieli 37

Bonde la mifupa-mikavu

Ezekieli alipewa maono ya ajabu. Yapo katika Ezekieli, Sura ya 37. Yalikuja kwa awamu tatu:

1. Ezekieli alioneshwa bonde lililojaa mifupa mikavu sana.

2. Ezekieli alitakiwa ‘atoe unabii’; aiamuru mifupa, na alipofanya hivi, kukawa na mshindo mkubwa, mifupa ile ikasogeleana na kujiunga, ikawa ni sanamu tupu za mifupa ya watu. Alivyoendelea kuzitazama, kukawa na mishipa inatokea juu yake, kisha nyama na ngozi zikazifunika. Mifupa hiyo ilikuwa sasa ni mizoga ya watu waliokufa (bado).

3. Mungu sasa akamwagiza Ezelieli atoe unabii kuutaka upepo uje ili miili ile ijazwe pumzi. Ezekieli alipofanya hivyo pumzi iliiingia, miili ikawa hai, na kuwa Jeshi Kubwa mno.

 

Sasa likawa, ni kwa ajili gani? Ezekieli anaambiwa:

“Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli, tazama, wao husema, mifupa yetu imekataliwa mbali kabisa” (Ezek. 37:11).

 Awamu ya 1:

Mifupa mikavu inamaanisha: Israeli isiyo na matumaini, iliyotawanywa ulimwenguni kote na kuteswa.

Mungu anaendelea kusema katika mstari wa 12:

“Tazama, nitafufua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli”.

Awamu ya 2:

Mifupa kujiunga na kupewa miili kunamaanisha,  Mungu kuwarudisha watu wake waliotawanyika katika nchi ya Israeli.

 

 

Mwishowe, kuhusu kuwapa uhai, Mungu anasema:

“Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, nimesema hayo na kuyatimiza” (ms. 14).

Awamu ya 3:

Miili isiyo na uhai kupewa pumzi ya uhai maana yake:

Mungu atawapa watu wake Roho yake, watambue kwamba ni yeye anayetawala.

Tuziangalie zaidi hizi awamu:

Ya kwanza

Hili lilishatokea. Waisraeli walitawanywa na walikuwa katika hali ya kukata tamaa, unabii wa Kumb. La Torati 28:65 – 67 ukiwa unatimia. Ulisema:

“Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha uwayo wa mguu wako, lakini BWANA atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika; na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yake; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako, asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! kwa kicho cha moyo wako (‘kwa hofu ya moyo wako’) utakavyokucha (‘utakavyohofu’), na (kwa) kuona kwa macho yako utakavyoona”.

              (Hapa msitari wa mwisho tafsiri ya Kiswahili ilikosewa sana!)

Ya pili

Ni hivi karibuni tu wana wa Israeli wamekuwa wakirudi katika nchi yao. Katika mwaka 1917 Azimio la Balfour lilisainiwa huko Uingereza, la ahadi ya kwamba Waingereza wangeifanya Palestina (inayoitwa sasa Israeli) iwe makao ya kitaifa kwa Wayahudi.

Hitler alipoingia madarakani Ujerumani alinuia kuwaangamiza Wayahudi wote, na zaidi ya Wayahudi milioni 6 waliuawa katika mazingira ya kutisha sana. Kutokana na mateso yao walijawa na tamaa kubwa ya kurudi Israeli na kuwa na nchi ya kwao wenyewe, mahali ambapo wangejisikia huru kutokana na mateso.

Katika mwaka 1948, baada ya mapambano makali, Israeli ilijitangaza yenyewe kuwa ni taifa. Kinyume na matarajio ya wengi, Waisraeli wameendelea kuwa taifa mpaka sasa. Imewezekanaje? Sababu ni kwamba, Mungu alisema wangekuwa taifa tena (kumbuka Ezekieli 37:12).

Naye Yeremia alitabiri hivi:

“Maana mimi ni pamoja nawe, asema BWANA, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa…………” (Yer. 30:11)

“Aliyemtawanya Israeli atamkusanya na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake. Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye” (Yer. 31:10,11).

Awamu hii ya 2 imekuwa katika kutimia kwa sasa!

Text Box: Vipi ya tatu?Taifa la Israeli wanatambua kuwa Mungu ndiye anayetawala? Kwa bahati mbaya, sivyo. Wakati unakuja, hatahivyo, wakati ambao taifa la Israeli litamgeukia Mungu. Tunapewa sababu katika Zekaria 14:1-4. Wakati unakuja ambao mataifa yote yatajikusanya kinyume na Israeli. Kutokana na mambo yanayotokea duniani kwa sasa, hili haliwezi kuwa mbali.

Ni hapo hali ya mambo itakapokuwa ya kukatisha tamaa kabisa kwa Israeli, jambo la ajabu la kusisimua litakapotokea. Tunaambiwa:

“Hapo ndipo atakapotokea BWANA, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita” (Zekaria 14:3).

Mstari unaofuata unatuonesha Mungu atakavyowasaidia; atamtuma Yesu arudi! Tunaambiwa: “Na siku iyo miguu yake (Yesu) itasimama juu ya mlima wa Mizeituni………..”(ms. 4).

Hebu fikiria jinsi Wayahudi watakavyojisikia, watakavyotambua lililotokea; kumwona Yesu Kristo, waliyemsulubisha, amerudi sasa kutoka mbinguni, na kuwaokoa! Kwa vyovyote watamtambua na kumkubali. Nabii huyu Zekaria anatuambia:

“Nao (Wayahudi) watamtazama yeye ambaye walimchoma, nao watamwombolezea kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee” (Zek. 12:10).

Kwa hiyo Waisraeli ni lazima wabadilike. Watalazimika kuitambua dhambi yao waliyoifanya kama taifa katika kumuua Bwana Yesu, na watamkubali sasa awe kiongozi wao. Katika Ezekieli 37:23 inatajwa pia kwamba ‘watatakaswa’. Katika Ezekieli 36, ujumbe kama huo unatolewa:

Awamu ya 1

 

Awamu ya 2

Awamu ya 3

Israeli wanatawanywa na kuadhibiwa kwa uovu wao.

Mungu anawakusanya tena.

Israeli wanabadilishwa.

Ezekieli 36:16-20

 

Ezekieli 36:21–24

Ezekieli 36:25 – 28

Uanzishwaji wa Ufalme wa Mungu duniani tena

Wayahudi watakapokuwa wametubu, Yesu atashika mamlaka kutoka Yerusalemu. Yesu atakapokuwa Mfalme, na Sheria ya Mungu itakapokuwa inaiongoza dunia, dunia itabadilika. Lakini wakati huo wa amani utafikiwaje?

Katika nyakati zote katika historia ya mwanadamu, mataifa yamekuwa yakienda kwa kuzifuata njia zake yenyewe. Yamekuwa yakijifanyia yanachotaka na kumpuuza Mungu; na ndivyo yanavyofanya hata sasa. Wakati Bwana Yesu Kristo atakapokuwa Mfalme katika Yerusalemu, atayataka mataifa yote yamche Mungu na kumtukuza, kama tunavyosoma katika Ufunuo 14:7. Mataifa yale yatakayomkubali Bwana, yatabarikiwa sana katika Ufalme huo.

Lakini Bwana Yesu Kristo atakuwa pia na uwezo wa kuliadhibu taifa lolote linaloasi. Katika Zekaria 14 tunaambiwa kwamba, taifa lolote likikataa kwenda Yerusalemu kuabudu halitapata mvua (ms.17,18). Na kama taifa kama Misri, ambalo kawaida hupata mvua ndogo sana, lisipotii, litapigwa pia na tauni.

Kwa hiyo itakuwa ni wakati wa amani na furaha kwa ulimwengu wote. Kuna vielelezo vingi vya kusisimua katika Biblia juu ya wakati huo. Kimojawapo kipo katika Isaya 11:6,9:

“Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi, ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza….. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu, maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari”.

Mtume Paulo alipokuwa akiwaandikia Warumi (ambao ni watu wa kimataifa kama sisi), alitumia kielelezo cha mti wa Mzeituni ili kuonesha kuwa, watu wa kimataifa wanaweza kujiunga na hatma iliyoahidiwa kwa Wayahudi.

Soma hili kwa ajili yako mwenyewe katika Warumi 11 (na hasa msitari wa 13– 25). Angalia maonyo hayo yanayotolewa.

MATAIFA NA WAYAHUDI KATIKA MPANGO WA MUNGU (Warumi 11).

 

   Mzeituni ukiwa unasimama   badala ya Israeli

    Baadhi ya matawi yamekatwa. Matawi hayo yanawakilisha Waisraeli wasiomwamini  Mungu. (ms. 17 – 20).

Matawi kutoka kwenye Mzeituni pori yanaweza kupachikwa. Matawi hayo ni waumini wa kimataifa wanaojiunga (ms. 17).

Baadhi ya matawi ya kiasili yanaweza kurudishiwa tena. Mungu anaweza kuwapachika tena Wayahudi wanaomgeukia tena na kumwamini  (ms. 23).

Vifungu vya kusoma: Ezekieli 36-37,  Zekaria 14,  Warumi 11.

Mstari wa kushika     : Zaburi 72:8

“Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia”.

Swahili Title
Wayahudi katika historia (2)
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission