Somo la 18
KIFO CHA YESU
SOMO: Marko 14 na 15
Tatizo la Dhambi
Ni dhahiri kuwa, dhambi ni janga kubwa kwa mwanadamu. Ni tatizo ambalo hata mtu anayeonekana mkweli sana, anashindwa kulitatua. Hakuna mtu anayeweza kuishinda dhambi kwa jitihada zake mwenyewe. Biblia yote inahusu namna Mungu alivyotoa jawabu kwa tatizo hili.
Mungu alimtoa Mwanawe, Bwana Yesu Kristo, awe dhabihu inayokubalika kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu, na Bwana Yesu alifanya kazi pamoja na Baba yake kufanikisha jambo hilo. Yesu alijitoa mwenyewe kwa utii kuwa hiyo dhabihu, kwa kuivunja nguvu ya dhambi kati ya watu. Hili limewezesha wale wanaomfuata, wa enzi zote, kujaribu kama yeye kupambana na dhambi kwa kufuata mfano wake.
Dhabihu ya Bwana Yesu imemwezesha Bwana Yesu Kristo mwenyewe kuyaepuka matokeo ya hukumu ya kifo iliyotolewa, iliyorithiwa kutoka kwa Adamu. Hili limewezesha wafuasi wa kweli wa Yesu kusamehewa dhambi zao, na hatimaye nao watapata uzima wa milele. Yesu alikuwa, katika yote ni mkamilifu; hakufanya dhambi yoyote.
Utabiri juu ya mateso ya Bwana Yesu Kristo
Tunaweza kusoma juu ya mateso aliyoyapata Bwana katika Injili zote. Lakini, tunapata picha iliyojaa zaidi tunaposoma pia vifungu vilivyotabiri mateso hayo.
Hebu fungua Zaburi ya 22. Zaburi hii inatuwezesha kuelewa jinsi Yesu alivyokuwa akijisikia, alipokuwa akiwambwa msalabani:
Sio tu uchungu, bali pia aibu ya kusulubiwa ilimlemea sana Yesu. Isome Zaburi hii kwa uangalifu na utaona pengine kuwa, maneno yake yanatusaidia kuyaelewa hasa yaliyompata Bwana Yesu, kuliko mengine yoyote. Angalia tena msitari wa 15 na 16:
"Nguvu zangu zimekauka kama gae, ulimi wangu waambatana na taya zangu; unaniweka katika mavumbi ya mauti. Kwa maana mbwa wamenizunguka; kusanyiko la waovu wamenisonga, wamenizua ('wamenipigilia') mikono na miguu".
Yalivyofikia hapo
Viongozi wa Kiyahudi walichukizwa sana na Yesu, makundi makubwa ya watu walipokuja kumsikiliza na kuwaleta wagonjwa wao waponywe. Walikuwa wakimwonea wivu na kukasirika. Hawakutambua kuwa, miujiza aliyokuwa akiifanya ilikuwa uthibitisho kuwa, alikuwa Mwana wa Mungu. Wivu na chuki zao ziliwatia giza.
Walipanga mauaji; Yesu auawe. Walimtuhumu kwa kukufuru; tuhuma iliyokuwa ikihukumiwa kifo kulingana na amri za Mungu walizopewa. Kwa vyovyote madai yao yalikuwa ya uongo, lakini hawakujali hilo!
Kwa wakati huo Israeli ilikuwa chini ya utawala wa Kirumi, na ingawa viongozi wa Kiyahudi, makuhani na mafarisayo, walikuwa wamemhukumu Yesu kuuawa, hawakuwa na uwezo wa kutekeleza hilo bila kupata idhini ya mamlaka ya Kirumi.
Jina la mtawala wa Kirumi katika Israeli kwa wakati huo alikuwa akiitwa Pontio Pilato. Wayahudi walimleta Yesu kwa Pilato na kudai kuwa alipaswa kusulubiwa (kuuawa kwa kupigiliwa msalabani). Pilato alifahamu kuwa Yesu hakuwa na kosa, na kuwa Wayahudi walitaka auawe kwa kumuonea wivu tu.
Lakini Pilato aliogopa kusimama kinyume cha Wayahudi, wasije wakamchongea kwa Kaisari, Mfalme Mkuu wa Warumi, akaipoteza kazi yake; alikuwa na makosa yake mengine. Kwa hiyo aliwakubalia ingawa kwa shingo upande, na kumtoa Yesu kwao ili asulubishwe. Kwa hakika hiki kilikuwa kifo cha mateso sana kilichowahi kubuniwa na watawala; na Pilato alijua Yesu hakuwa na hatia.
Warumi nao, kwa vyovyote, walipaswa kubeba lawama kwa yale yaliyompata Bwana Yesu.
Ni kwa nini ilibidi Yesu ateseke kiasi hicho?
Tunapomfikiria Yesu akiwa ananing'inia msalabani na kukumbuka kuwa hakuwa na kosa lolote, tunajiuliza: "Kwa nini ilibidi limpate hili?" Tunajua alikuwa siku zote akifanya mambo yale yanayompendeza Mungu tu!
Kitu kimoja ni hakika: ilikuwa ni njia pekee ya kumwezesha mwanadamu aokolewe na dhambi zake. Yesu alimwomba Baba yake mara tatu, yasimpate yote: "Ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke" (Mathayo 26:39). Hata hivyo alikuwa makini kuongezea, kusema, "Walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe". Mungu angeweza kumwokoa Mwanawe na mateso yale, lakini ilikuwa haiwezekani; ilikuwa ni njia pekee.
Kwa nini Yesu alilazimika kufa?
Adamu alikosa, kwa hiyo alikufa. Mauti yake yalikuwa ni adhabu. Tunaambiwa: "Mshahara wa dhambi ni mauti" (Warumi 6:23). Hii ni sheria ya Mungu isiyoweza kuvunjwa. Kwa hiyo:
Yesu alijaribiwa kama tunavyojaribiwa (na mara nyingine zaidi yetu sisi), hata hivyo hakukosea; hakuanguka dhambini. Katika Waebrania 4:15 tunaambiwa:
"(Yesu) alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi".
Kwa hiyo ilibidi Yesu afe kwa kuwa alikuwa na hulka ya kibinadamu, lakini hakustahili kufa kwa kuwa hakufanya dhambi. Kwa sababu hii Mungu aliweza kumfufua kutoka kwa wafu, bila kuikiuka kanuni yake aliyoweka, ya mauti kuwa mshahara wa dhambi.
Baada ya Yesu kufufuka, Mungu alimpa hulka mpya; hulka ya kutokufa, isiyotokana na dhambi ya Adamu. Ni hulka mpya ambayo pia haiwezi kujaribiwa na dhambi.
Tunaweza kusamehewa dhambi zetu tunapokuwa na ushirika na dhabihu ya Yesu, kwa kuzikiri dhambi zetu, kubatizwa na kutubu. Yesu atakaporudi, tutaweza nasi kuyashinda mauti.
Msalaba unatufundisha nini?
Kuwambwa msalabani kwa Bwana Yesu kulikuwa ni tukio la kutisha. Lilionesha uovu wa wanadamu katika kumchukia na kumuua kikatili Mwana wa Mungu, aliyekuwa mkamilifu wa wema. Kitendo hicho kinaonesha wanadamu wanavyoweza kuwa wabaya, na vile wasivyoweza kamwe kujiokoa wenyewe.
Ni vizuri tutambue na sisi tu wadhambi, na kwamba tunahitaji sana kuokolewa. Tunafanya vizuri kutambua kuwa, Bwana Yesu alikuwa dhabihu ya 'kukubalika'. Alikuwa kama mwana-kondoo asiye na mawaa, na Mungu alimridhia kuwa sadaka hii iliyokuwa kamilifu; kuwa toleo kwa ajili ya wote wanaomwamini. Yesu ni: "Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu" (Yohana 1:29).
Somo lingine la muhimu ni hili: Msalaba wa Kristo unaonesha upeo wa upendo wa Mungu kwetu. Paulo anaweka hivi:
"Yeye asiyemwachia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?" (Warumi 8:32).
Wamoja na Mungu
Mwanadamu alitenganishwa na Mungu na dhambi. Ukarabati wa mtengano huo unaitwa katika Maandiko, "Upatanisho". Hiki ndicho dhabihu ya Bwana Yesu ilichoweza kutufanyia. Imeweza kutuleta, hatimaye, katika u-moja na Mungu; kuwa na mahusiano safi na maelewano. Uhusiano huu mpya unakuja kwa kumhama Adamu na kuja kwa Yesu kupata msamaha wa dhambi zetu. Daudi anasema katika Zaburi:
"Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake. Heri BWANA asiyemhesabia upotovu" (Zab. 32:1,2).
Tuna wajibu gani?
Mungu amefanya kila aliloweza kwa ajili yetu. Ametupa Yesu awe sadaka; awe dhabihu. Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Lakini, bila ya kuamini kikweli kile Mungu alichofanya kwa ajili yetu, dhabihu ya Yesu haiwezi kuwa na maana yoyote.
"Tufanyeje basi?", Baadhi ya Wayahudi walimuuliza mtume Petro swali hili, na jibu lake linatufaa hata sisi leo. Petro aliwaambia:
"Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi" (Matendo 2:38).
Katika kifungu kingine Petro anasema tena:
"Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe" (Matendo 3:19).
Neema ya Mungu na imani yetu
Kwa hiyo tunakuja katika chimbuko lenyewe la Injili. Kwa upendo wake wote, Mungu amemtoa Yesu awe dhabihu kwa ajili ya dhambi zetu. Huu upendo wa Mungu wa bure unaongelewa mara nyingi katika Agano Jipya ukiitwa: "Neema yake". Katika Waefeso 1: 6-8 tunasoma juu ya hiyo neema:
"Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa (Yesu Kristo). Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye ametuzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi".
Tunaweza kuikataa neema ya Mungu na upendo wake, tunaweza kuidharau na kuipuuza, lakini, kama tu-wajanja, hatutafanya hivyo. Ni zawadi ya maana sana hii tunayopewa ya upendo na uzima. Kama tuna akili nzuri, tutataka kuwa miongoni mwa wale Yesu anaowaambia katika Marko 16:16, akisema: "Aaminiye na kubatizwa ataokoka".
Ubatizo ni mwanzo wa maisha mapya
Sisi sote ni wana wa Adamu, na kama Adamu, tunapenda zaidi njia zetu wenyewe kuliko Njia ya Mungu. Lakini Yesu, alipoutoa uhai wake kuwa dhabihu ya dhambi, alituwezesha kuwa 'wana wa Mungu'; kuwa sehemu ya familia ya Kristo. Mwenyewe alisema:
"Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate" (Luka 9:23).
Ni lazima tubatizwe kulingana na agizo lake. Hili lina maana kuwa, badala ya kutembelea njia zetu za dhambi, ni sharti nasi tuifie dhambi, yaani, tufanye kila jitihada kuacha kutenda dhambi. Tunapaswa tutembee na Kristo katika upya wa uzima, wakati wote tukijitahidi kuifuata njia ya Mungu badala ya yetu. Mtume Paulo anatuambia:
"Hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho" (Wagalatia 5:24,25).
Muhtasari
1. Watu wote wanastahili kufa kwa sababu wote ni wadhambi.
2. Mungu, kwa upendo wake kwa wanadamu, ameonesha namna ambavyo dhambi zinaweza kusamehewa.
3. Namna hiyo ni kupitia katika kifo cha Mwanawe wa pekee, Yesu, aliyeishi maisha ya kuishinda dhambi.
4. Ingawa Yesu aliishi maisha hayo kikamilifu, alikuwa na hulka yetu sisi wanadamu inayopaswa kufishwa.
5. Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, kwa kuwa hakuwa na dhambi.
6. Kama tukikubali kuwa tu-wadhambi tunaostahili kufa, tukimjea Mungu kupitia kwa Yesu, atatusamehe dhambi zetu.
7. Kama tukizitambua dhambi zetu na kubatizwa, tunaweza kuwa wana wa Mungu; watu wenye tumaini la uzima wa milele.
Vifungu vya kusoma: 2 Wakorintho 5, 1 Petro 1
Mstari wa kushika : Warumi 5:8
"Mungu anaonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu".