Correspondance Course - Lesson 20

Swahili

Somo la 20

ROHO MTAKATIFU WA MUNGU

SOMO:  Marko 1

“Mungu akasema, iwe nuru, ikawa nuru” (Mwanzo 1:3). Inaonekana kama rahisi sana. Lakini hebu ifikirie hiyo nguvu kubwa ya kiutambuzi na kiuweza iliyohitajika, kabla hiyo nuru haijaweza kupatikana:

“Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” (Mwanzo 1:1).

Fikiri tena juu ya kazi kubwa inayobidi ifanywe, mtu anapotaka kujenga nyumba. Fikiria jinsi inavyobidi kufanya maandalizi na kupanga; haja ya kupata mafundi wa namna mbalimbali, wote wakifanya kazi pamoja. Fikiri ni kiasi gani mtu analazimika kufikiri na kupanga, na ni nguvu au raslimali ngapi zinahitajika!

Tunaambiwa katika Zaburi:

“Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake…..Maana yeye alisema, ikawa, na yeye aliamuru, ikasimama” (Zab. 33: 6,9).

Katika Mwanzo 1:2 tunaoneshwa kuwa, ni Roho ya Mungu iliyotumika katika kuumba:

“Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”.

Pumzi ya Mungu na Roho ya Mungu

Uweza wa Mungu ulitumika tena katika kuziongoza akili za watu walioandika Biblia. Biblia inajulikana kama, ni: “Andiko lenye pumzi ya Mungu”. Mungu aliwatumia watu walioiandika, katika kuyaandika maneno yake. Kwa hiyo tunasoma katika 2 Petro 1:21 kuwa:

“Unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”

Unabii hauna maana ya kutabiri tu; kusema yatakayotokea. Katika Biblia unabii una maana ya kusema anachosema Mungu; iwe ni juu ya mambo ya nyuma, ya wakati uliopo au mambo yajayo.

 Tazama: ni waandishi 30 walioandika maneno yaliyopo kwenye Biblia, kwa kipindi cha zaidi ya miaka 1500. Kama Mungu asingekuwa kwa ‘pumzi yake’ ameongoza uandishi huo, kwa vyovyote kungekuwa na mkorogano mkubwa wa mawazo na utata wa ubora.

Badala yake, Biblia inayaongelea mambo yake yaleyale inayosemea kuanzia mwanzo hadi mwisho, katika mtiririko na uwiano mzuri wa ajabu.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo tunayoambiwa kuihusu Roho ya Mungu.                     

  1. Roho ya Mungu inaweza kuumba.
  2. Mungu, kwa Roho yake, anajua kila kitu.
  3. Mungu amefanya yote aliyoumba kwa Roho yake.
  4. Roho ya Mungu inawajia watu kuwawezesha kufanya mapenzi ya Mungu.
  5. Manabii walijua nini la kusema kwa njia ya Roho ya Mungu.

 

Kama ilivyo katika Mwanzo 1:2

Zaburi 139: 2-12

Zaburi 104:29-30, Ayubu 26:13

Waamuzi 6:34, 11:29 na Wagalatia 5:16

Mika 3:8, Zekaria 7:12, Nehemia 9:30,  2 Petro 1:21

Nini maana ya Roho Mtakatifu?

Neno ‘takatifu’ lina maana ya ‘kilichotengwa’ (kilichowekwa pembeni); kwa kusudi maalumu.

Kwa hiyo tunauzungumzia Uweza wa Mungu ulio Mkuu kama ni Roho iliyo ya kipekee sana; Roho Takatifu, kama mtume Petro anavyosema:

“Unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2 Petro 1:21).

Katika Biblia, Roho Mtakatifu (au Roho Takatifu -‘Holy Spirit’), ni uweza wa Mungu; uweza ambao katika huo Mungu anatimiza makusudi yake. yake.mipango yake.

Neno ‘Mtakatifu’ lililotumiwa na waliotafsiri kwenye Kiswahili, sio sahihi. Linaleta kuhisi kama vile ni ‘mtu’ au ‘nafsi’ badala ya kitu (nguvu/uweza). Maana hiyo haiko kwenye lugha ya asili (Kiyunani, iliyotumika kuandika Agano Jipya), wala katika maneno ‘Holy Spirit’ kwenye Kingereza (tuelewe hivyo, lakini tutaendelea kutumia neno ‘Mtakatifu’ kama lilivyoandikwa, kwa kuwa hatuwezi kubadilisha hapa).

Roho Mtakatifu na Bwana Yesu Kristo

Ni Roho Mtakatifu aliyefanya Bwana Yesu azaliwe. Kwa hiyo tunaambiwa juu ya Yesu kwamba:

“Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba   kwa uweza wa Roho Mtakatifu” (Mathayo 1:18).

Katika ubatizo wake katika mto Yordani, Yesu alipewa Roho Mtakatifu bila kipimo (Yaani, bila kuwekewa kiwango). Tunasoma katika Yohana 3:34 kuwa:

“Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo” (yaani, ….kwa sababu hiyo, Mungu hampi Roho yake kwa kumpimia).

Kwa hiyo, Yesu Kristo alipewa uweza wote. Kwa watu wengine katika nyakati za Agano la Kale na Agano Jipya, Mungu aliwamegea tu kisehemu cha uweza wake. Hakuna mtu mwingine aliyewahi kufaa kupewa uweza kama huo Mungu aliompa Yesu. Yesu aliutumia uweza huo mkubwa katika kufanya miujiza, na ulimsaidia katika kazi yake ya kuhubiri.

Hebu angalia maneno haya kutoka katika Isaya 61:1,2:

“Roho ya Bwana Mungu i juu yangu, kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao……. kuwafariji wote  waliao”.

Hebu kisome hicho kifungu chote katika Biblia yako. Picha unayoipata ni picha ya Yesu akitumia Roho ya Mungu katika kuifanya kazi ya Mungu. Hakuitumia kujijenga au kujinufaisha, bali katika kuwasaidia wengine.

Wanafunzi wake waliahidiwa Roho Mtakatifu

Yesu aliwaahidia wale wanafunzi wake kumi na wawili kuwa, nao pia wangepewa Roho Mtakatifu baada ya yeye kuondoka na kuwaacha kwenda mbinguni. Katika Yohana 14:25, 26 anawaambia:

“….Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia”.

Baada ya Bwana Yesu kuwaacha, wanafunzi hao wangehitaji msaada katika kuhubiri kwao, na katika kuwekea misingi kanisa la kwanza. Mungu pia angetumia Roho Mtakatifu katika kuwawezesha kuliandika Agano Jipya.

Utambue hapa ya kuwa, katika mistari hiyo hapo juu, Roho Mtakatifu angekuwa hapo kuwafundisha na kuwafanya wakumbuke yote yale Yesu aliyosema na kufanya, katika maisha yake hapa duniani. Roho Mtakatifu anazungumziwa hapa kuwa ni ‘Msaidizi’ na kwingine anaitwa ‘Mfariji’.

Yesu, mara kadhaa, anazungumzia Roho Mtakatifu kama vile ni mtu. Ni kwa nini? Ni lugha tu ya picha. Hebu tufungue Zaburi ya 65, na kusoma msitari wa 13. Unasema:

“Na malisho yamevikwa kondoo, na mabonde yamepambwa nafaka, yanashangilia, naam, yanaimba”.

Sasa, tunaposoma hivi, tunapata picha nzuri sana ya mazao mengi ya nafaka yaliyoshonana kwenye bonde, lakini hatufikiri hata kidogo kuwa bonde kweli linaweza kushangilia na kuimba. Ni namna tu ya mwandika Zaburi ya kulisemea jambo; kuelezea shangwe; bonde halina midomo. Ni jinsi tu kitu kinavyoelezewa kwa namna nyingine.

Yesu anaposemea Roho Mtakatifu kama vile ni nafsi fulani inayofanya hili au lile, anatuonesha tu uhalisia wa hiyo Roho kimfano; huo uweza wa Mungu.

Mfano mwingine wa lugha kama hii upo katika Methali 3:13–19. Isome mistari hii na utagundua kuwa, mwandishi anaongelea ‘hekima’ kama vile ni mwanamke mrembo, mwenye maadili. Hii ni namna iliyo dhahiri zaidi ya kusema kuwa, hekima ya kweli inayotokana na kumjua Mungu, sio tu kwamba ni kitu kizuri sana (msichana-mrembo), bali pia ni kamilifu.

Maandiko yanatumia lugha kama hiyo kuihusu Roho ya Mungu, kuonesha vile uweza wake ulivyo mkamilifu na unayofanya yasivyoshindwa. Utaona mifano mingine ya matumizi ya namna hii ya lugha mbeleni.

Roho yawajea wanafunzi

Tumeshaona kuwa Yesu aliwaahidia ‘uweza’ wanafunzi wake, kabla ya kupaa kwenda mbinguni. Aliwataka wasiondoke Yerusalemu: “bali waingoje ahadi ya Baba” (Matendo 1:4).

Aliwataka wabatizwe: “Katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache”  (ms. 5).

Katika Matendo 2 tunasoma vile, walipokuwa wakisubiri pamoja, Roho Mtakatifu alivyowajea: “Kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi” (ms.2). Upepo huo uliitikisa nyumba walimokuwa wakikaa. Ndimi za moto zilionekana kwa kila mmoja wao, na kuanzia hapo, waliweza kufanya miujiza.

Jinsi hiyo Roho inavyotujea

Huo uweza wa kipekee ulihitajika katika kuwaweka pamoja waumini wa kwanza (kanisa) na hauhitajiki kwa sasa. Kuna mengi zaidi juu ya hili katika somo linalofuata. Kwa sasa, Mungu anaongea na sisi kupitia katika Neno lake.

Tumeshaona ya kuwa hao walioiandika Biblia, walifanya hivyo kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Ni vizuri kutambua hapa pia kwamba, maneno haya mawili, Roho Mtakatifu, hayapo katika Agano la Kale. Katika Agano la Kale maneno yaliyotumika ni ‘Roho ya Mungu’. Roho ya Mungu iko katika Neno lake.

Yesu aliwahi kusema: “Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” (Yohana 6:63). Kwa hiyo, tunapolisoma Neno la Mungu, kwa namna fulani tunaipata Roho ya Mungu. Kulisoma Neno la Mungu kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu, na kunaweza kutusaidia kukua katika kumpendeza Mungu.

Hebu basi tulisome Neno la Mungu kwa bidii zaidi na kwa kuomba, tukiyakumbuka maneno ya Petro katika waraka wake wa kwanza, yanayosema: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpata kuukulia wokovu” (1 Petro 2:2).

Tumejifunza nini juu ya Roho Mtakatifu?

  1. Roho Mtakatifu ni uweza wa Mungu.
  2. Biblia iliandikwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
  3. Yesu alizaliwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
  4. Manabii wote wa Mungu walipewa kwa kipimo Roho yake, lakini kwa Yesu ilitolewa ‘bila kipimo’.
  5. Uweza maalumu uliotolewa wa Roho katika karne ya kwanza, baada ya hapo uliondolewa.
  6. Kwa sasa Mungu anatuzungumzia kupitia katika Neno lake, Biblia, iliyoandikwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

Vifungu vya kusoma:     Matendo 10: 34–43,  Yohana 14.           

Jifunze kwa moyo:        Marko 16:15,16.

“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”

 

Swahili Title
Roho Mtakatifu was Mungu
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission