Correspondance Course - Lesson 21

Swahili

Somo la 21

KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU

SOMO:  Matendo 8

Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kuwa wangepewa Roho Mtakatifu. Aliwaambia:

“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya, watashika nyoka, hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17,18).

Wafuasi hao walikuwa wameahidiwa kupewa Roho Mtakatifu kwa uweza maalumu, ili kuwasaidia katika kazi yao. Walikuwa wameambiwa wasiondoke Yerusalemu, “Bali waingoje ahadi ya Baba” (Matendo 1:4). Kwa hiyo waliingoja kama walivyoamriwa.

Tumeshaona jinsi siku moja, katika siku ya Pentekoste, walipokuwa wote pamoja, jambo la ajabu lilipotokea. Nyumba walimokuwamo, ilitikiswa na upepo wa nguvu uliokuwa ukivuma na kwenda kwa kasi, na: “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” (Matendo 2:4). Sasa, ni kwa nini wanafunzi walipewa karama maalumu ya kiroho? Tumeambiwa hapa walisema kwa lugha nyingine!

Zilithibitisha kuwa ujumbe waliotoa ulitoka kwa Mungu.

Yesu alikuwa amesulubiwa, na Mungu alikuwa amemfufua kutoka kwa wafu. Alikuwa amepaa kwenda mbinguni, akikiacha kikundi hiki kidogo cha wanafunzi kumi na wawili (mitume) kwenda ulimwenguni mwote, kuihubiri, “Injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15). Ilikuwa ni kazi kubwa.

Je, watu wangewasikiliza? Mazingira yalikuwa magumu, na walikuwa watu wa kawaida tu wasio na umaarufu wowote. Kwa hakika isingekuwa rahisi watu kuamini habari ya mtu aliyerudishiwa uhai baada ya kufa kwa siku tatu. Agano Jipya lilikuwa bado halijaandikwa.

Kwa hiyo wanafunzi walipewa uweza wa kufanya miujiza na kuongea katika lugha zisizokuwa zao kama ishara ya kuwa, walilokuwa wakisema lilitoka kwa Mungu.

Katika siku hiyo ya Pentekoste, walitoka hapo na kuwahubiri Wayahudi katika lugha ambazo hawakuwahi kujifunza. Ni wazi wasingeweza kuziongea bila ya uweza walioupata kutoka kwa Mungu. Ndio maana watu waliowasikia, tunaambiwa:

“Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao (wanaohubiri) si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?” (Matendo 2:7,8).

Kulikuwa na watu wengi waliotoka katika mataifa mbalimbali pale Yerusalemu siku ile, waliokuwa wamekuja kuidhimisha siku-kuu ya Pentekoste.

Karama hizi za Roho zilisaidia kuliongoza kanisa

Matokeo ya mahubiri yao ya siku hiyo ya Pentekoste ni kwamba, wanaume  na wanawake wapatao 3,000 walijiunga na wanafunzi hao na kuwa Wakristo (Matendo 2:41). Kwa namna hii kanisa la Kikristo lilikuwa limeanza vizuri.

Lakini hebu fikiria vikwazo ambavyo vingevipata. Familia kubwa kama hiyo ya Wakristo ingehitaji mtu wa kuwaongoza, kuwafundisha na kutoa ushauri kuhusiana na mipango waliyokuwa wakipaswa kuifanya kwa ajili ya kuieneza Injili. Wasingejifunza kitu kutoka katika Agano Jipya kwa kuwa, lilikuwa bado halijaandikwa.

Kwa hiyo vipawa vya Roho vilitumwa, sio tu kwa ajili ya kuwahakikishia walio nje ukweli wa ujumbe wa mitume, bali pia kusaidia na kuwafundisha Wakristo hao wa kwanza, na kuyawekea taratibu makusanyiko ya awali yaliyokuwa yakianza.

Karama hizi zilikuwa ni nini?

Tumeshaona kuwa mitume hao waliweza kuongea katika lugha za kigeni, lakini tuaambiwa pia kuwa, waliweza pia kuwaponya wagonjwa.

Katika 1 Wakorintho 12:4-22 mtume Paulo anaonesha jinsi waumini mbalimbali walivyopata karama mbalimbali, na namna kila moja ilivyokuwa atumike kwa ajili ya wengine. Baada ya hapo katika msitari ya 28 na wa 29 anatoa orodha ya hizo karama:

“Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, na wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha”.

Karama za Mungu hazinunuliwi

Mara baada ya wanafunzi kupokea karama za Roho Mtakatifu, walitoka kuanza kuhubiri. Mfuasi wa Yesu aliyeitwa Filipo alishuka kwenda Samaria na kuanza kuwafundisha watu hapo. Wengi waliomsikiliza waliyaamini maneno yake juu ya Yesu na Ufalme wa Mungu unaokuja, na wakabatizwa. Miongoni mwa wale waliobatizwa alikuwapo mtu aliyeitwa ‘Simoni, mchawi’. Alikuwa mtenda miujiza aliyewashangaza wengi katika Samaria kwa miaka mingi, kwa ujanja wake.

Mitume waliokuwa katika Yerusalemu waliposikia juu ya watu wengi kujiunga katika Samaria, walimtuma Petro na Yohana kuongeza nguvu pale.

Petro na Yohana wakiwa ni mitume, waliweza kuwapa wengine uweza wa Roho Mtakatifu, kwa kuwawekea mikono yao. Hiki ni kitu kilichokuwa kikiweza kufanywa na wale mitume wa kwanza tu.

Huyo Simoni, akiwa anatazama, aliona wanaume hao wawili wakiwawekea mikono yao wafuasi wapya na kuwafanya wapate Roho Mtakatifu. Alishangaa! Alianza kufikiri angeweza kutajirika na kuwa maarufu sana, kama angeweza naye kuwapa watu karama hii. Alitaka kuununua uweza huo kwa Petro. Hiki kilikuwa kitu kibaya sana kujaribu kufanya. Petro alimwambia:

“Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyoofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikra hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena ukatika kifungo cha uovu” (Matendo 8:21-23).

Simoni aliogopa, na kumuomba Petro amwombee. Hatuambiwi kilichoendelea.

Habari hii inatuonesha wafuasi wa awali wakitumia uweza wa Roho Mtakatifu katika kuwahubiri watu juu ya Yesu na Ufalme unaokuja.

Soma Matendo 8:15 – 25 na utafakari vizuri yafuatayo:

  1. Msitari wa 18 unasema kuwa, ilikuwa ni kwa kuwekewa mikono na mitume tu ndipo walipopata Roho Mtakatifu.
  2. Simoni hakupata karama ya Roho Mtakatifu alipobatizwa.
  3. Mtume Petro na Yohana waliwapa waumini wapya waliobatizwa karama za Roho Mtakatifu, baada ya kuomba na kuwawekea mikono (hii ilikuwa ni namna ya kuwabariki).
  4. Baada ya Simoni kupokea Roho Mtakatifu kwa namna hiyo, hakuweza yeye kuwapatia wengine; na hiki ndicho hasa alichokitaka.

Hili linatuonesha ya kwamba, ni mitume tu waliokuwa na uwezo wa kutoa karama za Roho Mtakatifu. Walipokufa hakuna karama tena zilizotolewa na zilitokomea na watu wa kizazi kile.

Mwisho wa hizo karama

Tumekwishaona kuwa, katika enzi hizo za Wakristo wa kwanza hakukuwa na Agano Jipya; lilikuwa bado halijaandikwa. Tunafikiri hii ilikuwa ndio sababu ya Mungu kutoa hizo karama kwa kuwa zilikuwa ni za muhimu sana.

Leo tunaweza kusoma wenyewe (au kusomewa) juu ya maisha ya Bwana Yesu, na tunaweza kuzisoma/kusomewa barua ambazo mitume waliwaandikia Wakristo wa wakati wao. Lakini mitume wao hawakuwa na Maandiko hayo. Mitume, manabii na waalimu wenye uweza huo maalumu kutoka kwa Mungu, walikuwa ni msaada wa lazima sana kwa makanisa ya kwanza.

Uandishi wa Agano Jipya ulipokamilika, hapakuwa na haja tena ya msaada wa kipekee kutoka kwa Mungu. Mambo yote ambayo Wakristo wanataka kuyajua, yameandikwa kwa ajili yao katika Biblia. Na, kwa hiyo, karama hizo za kiroho ziliondolewa.

Mtume Paulo alisema hili lingetokea, akiwaandikia Wakorintho. Aliwaambia:

“Upendo haupungui neno (haushindwi) wakati wowote, bali ukiwapo unabii (yaani, karama ya kusema anachosema Mungu) utabatilika (utashindwa); zikiwapo lugha (yaani, karama ya kuweza kuongea lugha zingine bila kuzijifunza) zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika” (1 Wakorintho 13:8).

Inaelekea karama hizi hazikuondolewa haraka wakati Agano Jipya lilipokamilika. Miaka ilivyopita wale Wakristo waliokuwa nazo walikufa, na Wakristo waliofuata hawakuzipewa. Kwa hiyo hazipo.

Kuna aliye na karama hizi leo?

Wapo watu wanaodai kuwa wana hizi karama za Roho. Na hasa wanadai wana uwezo wa kuongea ‘vilugha’ na kuponya wagonjwa. Tuwachukulieje hao wanaodai wanao uweza wa miujiza ya Roho ya Mungu kwa wakati huu?

  1. Tujikumbushe mtume Paulo alichosema katika 1 Wakorintho 13 kuwa, wakati ungefika ambapo karama za kiroho zingeondolewa. Wakati huo ulikuja lini, kama sio muda mfupi baada ya Agano Jipya kukamilika? Haiwezi kuwa inasubiri ujio wa Ufalme, maana wakati huo karama hizo zitaongezwa kuliko ilivyowahi kutokea. Karama hizo zinaongelewa kuwa ni, “kipawa cha mbinguni….nguvu za zamani zijazo” (Waebrania 6:4,5). Wafuasi wa Kristo wa kwanza walipata ‘malimbuko’ tu ya karama hizi zitakazotolewa kwa wingi wakati wa Ufalme.
  2. Tumeona kuwa karama za Roho Mtakatifu zilitolewa ili kulisaidia Kanisa la Kweli. Kanisa la kweli linaliamini na kulihubiri Neno la Mungu. Watu karibu wote (kama sio wote) wanaodai kuwa na uweza huo leo, wanahubiri mambo ambayo hayafundishwi ndani ya Neno la Mungu. Kwa hiyo inatupasa tuyakatae madai yao.
  3. Inatubidi tukiri kuwa, hatuvutiwi na wingi wa ile inayoitwa ‘miujiza’ wanayofanya. Mara nyingi uponyaji wao umeonekana haukuwa lolote baada tu ya muda, na unafuu unaopatikana unaweza kuelezeka kisayansi. Watu wa mazingaumbwe wanaweza mara nyingi nao kufanya hivyo hivyo. Hakuna aliyewahi kumfufua mtu.

Mungu kweli anaweza, na hata sasa anafanya kazi kupitia katika Roho yake leo, lakini haruhusu watu watumie Roho yake. Watu wanaoamini yote yale yaliyoandikwa katika Biblia, hawatadai kuwa wana karama za Roho. Wanatambua kuwa karama hizo ziliwekewa kupita mara baada ya Maandiko ya Agano Jipya kukamilika.

Mungu bado anafanya kazi

Kwa sasa, hatuna uwezo wa kufanya miujiza na kuongea vilugha. Roho Mtakatifu wa Mungu bado anafanya kazi leo, kama kwa mfano, Mungu anapojibu maombi, na Mungu bado anaongea nasi kupitia kwenye Neno lake. Tunapoisoma Biblia, tunakuwa tunafundishwa na Roho ya Mungu, kwa namna iliyo ya hakika sana.

Kama tunataka kumpendeza Mungu, basi hebu tuoneshe tunavyomshukuru kwa yale yote aliyotufanyia kwa kulisoma Neno lake, na kujifunza yote tunayoweza kutokana nalo. Soma 2 Tim 3:16,17.

Muhtasari.

  1. Karama za Roho Mtakatifu zilitolewa kwa Wakristo wa awali tu.
  2. Zilikuwa zikidhi malengo matatu:
    1. Kukamilisha Agano Jipya.
    2. Kuwa ishara kwa wasioamini.
    3. Kusaidia katika kulijenga Kanisa la kwanza.
  3. Zilitolewa tu mpaka Maandiko ya Agano Jipya yalipokamilika, baada ya hapo ziliondolewa.
  4. Hakuna mtu tangu hapo ameweza kufanya miujiza kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
  5. Hao watu wanaodai kufanya miujiza leo wanaweza kuwa na uwezo Fulani usio wa kawaida, kama wacheza mazingaombwe tu lakini sio uweza wa Roho Mtakatifu.

Vifungu vya kusoma:        1 Wakorintho 13 na 14

Jifunze kwa moyo:            1 Wakorintho 13:8

“Upendo haupungui neno wakati wowote, bali ukiwapo unabii utabatilika, zikiwapo lugha, zitakoma, yakiwapo maarifa, yatabatilika”

Swahili Title
Karama za Roho Mtakatifu
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission