Correspondance Course - Lesson 23

Swahili

SOMO LA 23

SOMO: Mhubiri 3

Baada ya kifo – nini?

Kuna nadharia nyingi zinazotofautiana juu ya nini kinatokea tunapokufa. Ni watu wachache wanaopenda kufikiri wanapokufa inakuwa ndio mwisho wao. Hapa kuna baadhi ya nadharia walizonazo:

  • Wapo wanaofikiri wanageuka na kuwa wanyama (huu unaitwa ‘umwilisho’).
  • Wapo wanaofikiri kuna kitu ndani yao kinachoendelea kuishi mahali fulani.
  • Wapo wanaofikiri hakuna tumaini kabisa la namna yoyote ya uhai baada ya kifo.
  • Na wengine wanaamini kutakuwa na siku ya ufufuo wa wafu, ikifuatiwa na hukumu, na uzima wa milele kwa waaminifu.

Biblia inasemaje?

Kama tulivyokwishaona, kifo ni adhabu hutokana na dhambi. Kuwa katika hali ya kufa ni kuwa katika hali ya kutotambua chochote; kutokuwa na mawazo ya namna yoyote. Kwa hiyo, mauti ni mwisho kabisa wa uzima na hakuna kinachoendelea kuishi. Andiko linasema:

“Waliohai wanajua ya kwamba watakufa, lakini wafu hawajui neno lolote, wala hawana ijara tena, maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao imepotea yote pamoja, wala hawana sehemu tena katika jambo lolote lililofanyika chini ya jua” (Mhubiri 9:5,6).

Je, hili lina maana kuwa hakuna tumaini lolote juu yetu? Hakuna tumaini mbele ya kaburi?

Ahadi ya ufufuo na uzima wa milele.

Kusingekuwa na tumaini lolote kama Mungu asingemtuma Yesu Kristo. Yesu mwenyewe alisema: “Msiposadiki ya kwamba mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu” (Yohana 8:24).

Lakini kwa sababu ya kile Yesu alichofanya katika maisha yake yasiyo na dhambi na kwa kufa kwake, tunaweza kuwa na tumaini la uzima baada ya kufa. Neno linasema:

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye” (Yohana 3:16,17).

Tunaweza kusamehewa dhambi zetu kupitia kwa Yesu. Yesu alisemewa na Yohana Mbatizaji kuwa ni: “Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yohana 1:29). Tunakufa kwa sababu ya dhambi. Kama dhambi zetu zinasamehewa kabisa, hatuwezi kubakia tumekufa. Tunakuwa kama ilivyokuwa kwa Yesu.

Jisomee mwenyewe Yohana 6:39,40,44. Tunajua ya kwamba Yesu anaongelea hapa kufufuliwa kwa wafu mara tatu, ‘siku ya mwisho’. Hasa katika msitari wa 40 anasema: “Mapenzi yake baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho”.

Ufufuo wa wafu unaongelewa pia katika Yohana 5:28,29. Yesu anasema:

“Msistaajabie maneno hayo, kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka, wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”.

Nabii Danieli naye alilisemea hili akionesha kuwa, ni sehemu tu ya wale watakaofufuliwa watakaopewa uzima wa milele: “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele” (Danieli 12:2).

Kwa hiyo, kutakuwa na hukumu. Tunaambiwa kuwa, wale watakaokuwa hai wakati wa kurudi Yesu, watahusika pia na hiyo hukumu. Yesu atawahukumu: “Walio hai na waliokufa, kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake’ (2 Tim 4:1).

Hao watu watakaoonekana wanafaa, watapewa nafasi katika Ufalme wa Mungu utakaoanzishwa hapa duniani. Yesu atawaambia:

“Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu” (Mathayo 25:34).

Hawa watu waliokuwa waaminifu watapewa uzima wa milele; maisha yaliyo makamilifu na yasiyo ya dhambi. Tunasoma katika Luka 20:35,36 kuwa, watakuwa kama malaika:

“Wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena, kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kama vile walivyo wana wa ufufuo”.

Tumaini la Mkristo lipo katika ufufuo wa kimwili kutoka kwa wafu, na nafasi katika Ufalme wa Mungu katika dunia hii atakaporudi Yesu.

Wadhambi wanakwenda motoni?

Je, kuna hasa sehemu ya kutisha inayoitwa ‘kuzimu’ watu waovu wanapokwenda kuteswa baada ya kufa? Tumeshaona kuwa, mtu anapokufa, uhai wake unakuwa umefikia mwisho moja kwa moja! Hawezi tena kufikiri au kuhisi chochote. Kwa hiyo ‘kuzimu’ ni nini, na ni wapi?

Neno ‘kuzimu’ ni neno lenye maana ya ‘mahali palipofichwa’ au ‘mahali palipofunikwa’. Ni neno linalotumika katika Biblia kumaanisha mahali palipofichika au palipofunikwa kwa ajili ya wafu; ni kaburi.

Maana ya ‘kuzimu’ ni ‘KABURI’

Katika Agano la Kale, neno la Kiebrania lililotafsiriwa ‘kuzimu’ ni ‘sheol’. Limetumika katika vifungu vifuatavyo:

Katika Zaburi 49:15 mwandika Zaburi anasema: “Mungu atanikomboa nafsi yangu, atanitoa mkononi mwa kuzimu”.

 

Katika Zaburi 55:15 mwandika Zaburi anasema: “Mauti na iwapate kwa ghafla, na washuke kuzimu wangali hai”.

Neno hili ‘kuzimu’ ni neno ‘sheol’; halina maana nyingine. Sio mahali pa ajabu-ajabu, pasipoeleweka.

Katika Agano Jipya, neno lililotafsiriwa ‘kuzimu’ ni ‘hades’ katika Kiyunani.

Katika Ufunuo 1:18 Yesu anasema:

“……..Ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu”.

 

Katika 1 Wakorintho 15:55, mtume Paulo anasema:

“Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako?

U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”

Neno ‘mauti’ na neno ‘kuzimu’, yote ni neno ‘hades’ katika lugha ya Kiyunani; maana yake ni moja (Kiyunani ndiyo lugha ya asili iliyotumika kuandika Agano Jipya lote; lugha zingine zote ni tafsiri).

Hili linatuonesha kuwa, katika Agano la Kale na Agano Jipya, neno ‘kuzimu’ lingeweza kutafsiriwa ‘kaburi’ moja kwa moja.

Maana ya kuzimu ni ‘KABURI’

Kwa hiyo, kuzimu sio mahali pa kutisha pa mateso kwa ajili ya wadhambi wanapokuwa wamekufa.

Yesu alirudi kutoka kuzimu

Baada ya Yesu kufufuka kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, Petro aliwahubiri watu waliokusanyika Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pentekoste. Aliwaambia kuwa, mfalme Daudi alikuwa amemtabiria Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu. Unabii huu unapatikana kwenye Zaburi ya 16, na Petro anauongelea katika Matendo 2:27 akisema:

“Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu”.

Petro anasema kuwa, Daudi alikuwa akimtabiria Yesu Kristo:

“Yeye mwenyewe (Daudi) akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu” (ms.31).

Roho yake Kristo (yaani, Kristo mwenyewe) hakuachwa kuzimu (yaani, kaburini) kwa kuwa Mungu alimfufua siku ya tatu. Mtakatifu wa Mungu hakuona uharibifu (yaani, hakuishia mautini).

Katika Ufunuo 1 Yesu anazungumzia ufufuo wake mwenyewe, na pia ahadi yake ya kuwafufua wafuasi wake waaminifu, anaposema:

“Nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu” (Ufun. 1:18).

Wafuasi wa Yesu waliokwisha kufa, wamefungiwa katika makaburi (au kuzimu). Yesu anao ufunguo (anao ‘uweza’) wa kuyafungua makaburi hayo wakati akirudi, na kuwafufua waliokufa na kulazwa humo.

Kuzimu (‘hades’)

Mara nyingine ‘kuzimu’ kunafikiriwa kuwa ni mahali pa giza au ukungu mnene zinapokaa roho za watu waliokufa. Tunajua hili haliwezi kuwa kweli kwa kuwa Biblia inatuambia: “Wafu hawajui neno lolote” (Mhubiri 9:5).

Hakuna mtu aliyekufa anayejua kitu; anayepata raha au maumivu, kwa kuwa hakuna wanachotambua. ‘Kuzimu’ tumeshaona, ni “kaburi” tu.

Vipi juu ya moto wa kuzimu; wa milele?
Yesu anasema mara tatu katika Marko 9 juu ya ‘moto usiozimika’. Anasema:

“Ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako Jehanum, kwenye moto usiozimika” (Marko 9:43).

Sasa Yesu hapa alimaanisha nini?

Neno ‘Jehanum’ katika msitari huo ni neno ‘Gehenna’ katika Kiyunani, linalotokana na neno ‘Ghi-Hinnom’ katika Kiebrania. Ghi-Hinnom lilikuwa ni jina la bonde lililokuwa nje kidogo ya jiji la Yerusalemu. Ni mahali ambapo miaka ya nyuma wafalme wa Israeli waliteketezea watoto wao kwa moto, wakitambikia miungu ya kigeni (unaweza kusoma juu ya hili katika 2 Wafalme 23:10).

Katika kipindi cha Yesu, hilo ‘Bonde la Hinnom’ (Jehanum) lilikuwa ni mahali mizoga ya wanyama na takataka za Yerusalemu zilipoteketezewa. Moto ulikuwa ukiwaka hapo wakati wote; lilikuwa ni ‘dampo’ la jiji. Palikuwa mahali pa kitu kuteketezwa kitu moja kwa moja.

Yesu alipolitumia neno ‘Jehanum’ walielewa alikuwa akisemea mahali hapo, ikiwa ni ishara ya kuharibiwa au kuteketezwa moja kwa moja; kuangamia. Hakuwa akisema watu kuteseka kwenye adhabu isiyo na mwisho ya moto. Mungu wa upendo hawezi kufanya hivyo. Wangeangamia kwa kufa.

Muhtasari

  1. Biblia inafundisha kuwa kifo ni mwisho wa uhai wote.
  2. Haitoi ahadi ya kwenda mbinguni.
  3. Inaahidi kuwa Yesu atarudi na kuwafufua wafu.
  4. Wakati huo, atawapa wafuasi wake waaminifu uzima usio na mwisho.
  5. ‘Kuzimu’ ni kaburi, mahali ambapo waliokufa wanazikwa.
  6. ‘Jehanum’ ni bonde lililokuwa nje ya mji wa Yerusalemu (Bonde ‘Ghi’ la ukoo wa Hinnom), mahali zilipochomewa taka. Linatumiwa katika Biblia kumaanisha ‘kuteketea’.

Kifungu cha kusoma: Yohana 11:1 – 45

Msitari wa kujifunza: 1 Wakorintho 15: 22,23:

“Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo, baadaye walio wake Kristo, atakapokuja”.

 

Swahili Title
Dhambi na matokeo yake (Sehemu ya 2)
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission