Somo la 24
KWA NEEMA MMEOKOLEWA
SOMO: Warumi 5
|
NEEMA Katika Biblia neema ya Mungu maana yake ni wema wa upendo wa Mungu kwa wanadamu. Ni kitu asichokistahili mtu, na ni zawadi ya bure kabisa inayotoka kwake. Neema hiyo inaeleweka vizuri zaidi katika kumtoa Bwana Yesu kwa ajili ya kutuokoa. (Utahitaji kulikumbuka hili vizuri unavyojifunza somo hili) |
Ni kufa au kupona
Sisi wote tunaelewa vizuri sana kuwa, maisha yetu yatakatizwa hivi karibuni au baadaye kidogo kifo kikija. Mungu alimtuma Mwanawe, Bwana Yesu Kristo, duniani, ili kuifungua njia ya uzima. Hii njia ya wokovu kutokana na mauti ndio âmoyoâ wenyewe wa Injili ya Kikristo.
Dhambi zetu zinatutenganisha na Mungu, ambaye ndiye aliye chanzo cha uhai wote. Yesu alikuja kumrejesha mwanadamu kwa Mungu, kwa kuionesha njia ya uzima. Mtu anaweza akaijua Biblia yake vizuri sana kutoka Mwanzo mpaka Ufunuo, anaweza akawa na ufahamu mkubwa wa mambo Biblia inayofundisha, lakini hili haliwezi kumwokoa. Kama mtu hajaielewa na kuipokea dhabihu Yesu aliyoitoa kwa ajili yake kwa moyo wa ukweli, hawezi kuwa na tumaini la uzima.
Mawazo potofu
Watu wengi wanafikiri kuwa, mambo mazuri wanayofanya na mambo mabaya wanayofanya yanalinganishwa, kuona vile walivyo mbele ya Mungu. Wanafikiri kuwa, kama mema wanayofanya ni mengi kuliko mabaya, wana haki ya kupata upendeleo wa Mungu. Hili sio kweli hata kidogo!
Wengi wanaodai kuwa ni Wakristo, wanaotambua kuwa Mungu amelipa kitu cha thamani kubwa kuwezesha wokovu wao kupatikana, wanajisikia wanastahili kuupata mbaraka huu kwa mambo wanayofanya.
Ni rahisi sana kwetu kufikiri tunastahili kuzipata zawadi za Mungu, lakini, zawadi sio haki, na haziwezi kuwa. Ni mishahara tu inayofanyiwa kazi. Paulo anatuambia:
âMshahara wa dhambi ni mauti; bali karama (zawadi) ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetuâ (Warumi 6:23).
Mungu amefanya mengi sana kwa ajili yetu. Tunahitaji kuonesha shukrani zetu kwa kumpendeza, kwa hiyo tunafikiri kuwa mambo tunayofanya yanaweza âkuilipiaâ mibaraka ya Mungu.
Ni mojawapo ya mafundisho makuu kabisa katika Maandiko kuwa, msamaha wa dhambi na uzima wa milele katika Ufalme wa Mungu ni karama ya Mungu; ni vitu tu vya ukarimu wake. Haviwezi kuwa haki; havilipiwi.
Maandiko yanafundisha kuwa:
- Sisi wote tu-wadhambi na tupo katika hukumu ya kifo.
- Hatuwezi kujiokoa wenyewe (inatupasa tuwe na unyenyekevu wa kulikubali hili).
- Mungu ametoa njia ya wokovu kupitia kwa Bwana Yesu Kristo.
- Njia hii ipo kwa ajili yetu kama tukiiamini Injili, inayopatikana katika Neno la Mungu, Biblia.
Kumwamini Mungu
Yasome maneno haya kwa umakini.
|
Waefeso 2: 4-9 âMungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani (nyakati) zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kupawa (kitu cha kupewa; zawadi) cha Mungu, wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifuâ. |
- Mungu anatupenda sana, ingawa tu wadhambi. Ametupa uhai wa kuwa pamoja na Kristo.
- Wokovu huu ni kitu cha kupewa; ni zawadi.
- Ametupa wokovu huu katika Yesu, ili katika wakati unaokuja aweze kutubariki hata zaidi na uzima katika Ufalme wake.
- Wokovu huu ni tuzo itokayo kwa Mungu. Inabidi tumwamini. Hakuna tunachoweza kufanya kuupata, kwa hivyo hakuna kuringa.
Sasa hebu soma Warumi 3:20-28 kwa makini. Utaona kuwa ujumbe ni huo huo. Hakuna kitu ambacho Wayahudi wangeweza kufanya kwa kuishika Sheria, na hakuna tunaloweza kufanya katika maisha yetu, kutuwezesha tuonekane watu wa haki mbele ya Mungu. Sisi wote ni wadhambi. Lakini, kwa neema yake Mungu, anawahesabia haki wale wanaomwamini Bwana Yesu.
Ni Mungu pekee yake na Bwana Yesu walio wa Haki. Hata hivyo, kama tukiamini kuwa Yesu alitufia, na kuikubali dhabihu aliyoitoa kwa ajili yetu, Mungu atatusamehe dhambi zetu, na kutuhesabia nasi haki. Ona tena mtume Paulo anavyourudia ukweli huu wa muhimu kwamba âyote ni ya Munguâ, na kwamba hakuna mtu anayeweza kuringa kwamba ameokoka:
âBasi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Munguâ (Warumi 5: 1, 2).
Mistari hii inatuambia wazi namna alivyo mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu. Mtu wa namna hiyo ana amani na Mungu kwa kuwa, ameletwa katika ushirika tena na Mungu kupitia katika dhabihu ya Yesu. Amekubalika kwa Mungu na ni raia mtarajiwa wa Ufalme wa Mungu.
Kilichomleta katika uhusiano huo ni imani yake kwa Mungu. Kwa sababu ya mambo haya, anaweza kuwasiliana na Mungu; anaweza kumkaribia kwa njia ya maombi. Mfuasi wa namna hiyo ameifikia neema.
Tunaweza kujali tunavyoishi?
Kwa hiyo tumeona jinsi mtu anavyoweza kumkaribia Mungu, na kuweza kukubalika kwa neema yake. Mtu aliyefikia hapo amekuwa âsawaâ na Mungu.
Lakini hatujasemea chochote kuhusu anavyopaswa kuishi. Tunaweza kuwa huru tena kujifurahisha na kujifanyia tunavyotaka? Mtume Paulo alifikiri watu wangeweza bado kufikiri hivyo; tumesoma juu ya neema ya Mungu kwenye Sura ya 5 ya waraka wake kwa Warumi. Sasa hebu angalia msitari wa kwanza wa Sura ya 6. Unauliza: âTudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?â
Analijibu swali hilo mwenyewe katika msitari wa pili, akisema: âHasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?â
Endelea kusoma hadi msitari wa 14, na hasa uzingatie kinachosemwa katika msitari wa 11 na 12:
âVivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zakeâ.
Kama kweli tunamwamini Bwana Yesu Kristo, tutaishi kama vile tunamwamini. Tutajitahidi sana kufanya anayosema; ndipo tutakapokuwa kikweli wafuasi wake.
Kwa upande mwingine, mtu ambaye hafanyi jitihada yoyote kuyafanya mapenzi ya Mungu na kumtii, hawezi kuwa mfuasi wa kweli. Kama angekuwa ameamini kikweli, angetii. Hana imani iliyo na udhati, na hivyo hajaifikia hiyo neema ya Mungu.
Mtume Yakobo anatuambia: âImani isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwakeâ (Yakobo 2:17). Imani ambayo haimfanyi mtu ajitahidi kuifuata namna ya kuishi ya Mkristo na kuishinda dhambi ndani yake, sio imani lolote.
Kuanza maisha mapya katika Kristo
Tunawezaje kuonesha kutambua kwetu kile Mungu alichokifanya kwa ajili yetu, na nia yetu ya kuishi kulingana na amri zake? Tayari tumeshasoma Warumi 6, msitari wa kwanza na wa pili. Hebu tuiangalie mistari miwili inayofuata:
|
âHamfahamu ya kuwa sisi zote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzimaâ (War. 6:3, 4). |
Yesu alikufa na kufufuka kwa ajili yetu. Tunajishirikisha na dhabihu yake kwa kuzikwa, sio katika kaburi kama ilivyokuwa kwake yeye, bali katika maji. Huu ndio Ubatizo wa Kikristo. Mtu anapoibuka kwenye maji, amekuwa âmtu mpyaâ katika Kristo, na anakuwa tayari kuishi maisha mapya. Anakuwa mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu na anajitambua kuwa yupo âkatika Kristoâ; ni Mkristo.
Ufuasi: Ubatizo ni mwanzo mpya, na dhambi zetu za nyuma zinasamehewa tunapobatizwa. Hata hivyo, hata tukijitahidi kiasi gani, tutakuwa bado tunaendelea kufanya baadhi ya mambo kimakosa na kufikiri mambo yasiyofaa.
Lakini kumbuka: Mkristo ambaye amebatizwa anaweza kumkaribia Mungu kupitia kwa Kristo. Anaweza kukiri kushindwa kwake, na kuonesha kusikitishwa na dhambi yake. Na Mungu atamsamehe kwa ajili ya Kristo.
Kwa hiyo, kamwe tusikate tamaa. Tukiwa na upendo wa Baba kutusaidia, hatimaye tutaufikia Ufalme wa Mungu utakapokuja. Yesu alisema: âBaba yenu ameona vema kuwapa ule ufalmeâ (Luka 12:32). Anayo shauku ya kutuingiza katika Ufalme wake.
Umuhimu wa imani
|
IMANI ni kumtumaini MUNGU |
Mwandishi kwa Waebrania anatuambia, katika Waebrania 11:6 kuwa: âPasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu)â. Kuwa na imani ni kumtumaini Mungu kabisa; kuweka maisha yetu mikononi mwake, kama mtoto mdogo anavyomtegemea baba yake na kumheshimu.
Kama tuna imani ya kumtumaini hivyo, tumeweza kuifikia neema ya Mungu. Lakini hatuwezi kuamini kitu kama hatukijui vizuri; na hatuwezi kuliamini Neno la Mungu mpaka tunapokuwa tumeyaelewa mafundisho yake. Hii ndiyo sababu ya sisi kusisitiza sana kuelewa kile Biblia inachofundisha. Jisomee mwenyewe Warumi 10:13-17. Msitari huo wa mwisho unasema: âImani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristoâ. Hili ni la muhimu sana!
Wafuasi enzi za Agano la Kale
Kama kuamini katika aliyofanya Yesu ni kitu cha lazima kwa wokovu wetu, itakuwa vipi kwa watumishi wa Mungu wakati wa Agano la Kale? Watawezaje kuokolewa wakati waliishi kabla Kristo hajaja?
Wale walioishi katika nyakati za Agano la Kale, walifahamu kumhusu Kristo! Hawakumfahamu kwa jina la Yesu, ila walimjua kama Mwana wa Mungu aliyeahidiwa; Masihi; Mwana-kondoo wa Mungu.
Waaminifu wa kale walitambua kutokana na Neno la Mungu kuwa, watu wote wanahitaji kuokolewa. Waliambiwa kuwa Mungu angelifanikisha hili kwa kifo cha âmtu mkamilifuâ, ambaye angekubali kuwa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Angeutoa uhai wake kwa ajili ya wokovu kwa wanadamu wote.
Ibrahimu alikuwa mmojawapo wa âwakuuâ katika Agano la Kale. Tunaambiwa katika Wagalatia 3:8 ya kuwa: âAndikoâ¦.lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, katika wewe mataifa yote watabarikiwaâ.
Na tunasoma juu ya Yesu akiwaambia Wayahudi: âIbrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahiâ (Yoh. 8:56).
Kwa hiyo, Ibrahimu na wafuasi wengine wengi wa Agano la Kale waliamini katika Kristo, kama ambavyo imekuwa kwetu, ingawa hawakuwa na fursa hii kubwa tuliyo nayo, ya kuweza kuzisoma habari za Injili zinazotuambia juu ya maisha na kazi za Bwana Yesu.
Kwa kuwa maagano yote mawili yanatuambia habari za neema ya Mungu inayofanya kazi kwa ajili ya wokovu wetu, tunahitaji kujifunza Biblia yote, na sio Agano Jipya tu.
|
Muhtasari
|
Vifungu vya kusoma: Zaburi 32, Warumi 4
Usome tena Wagalatia 3; Tito 3:4-6 na 2:11-13
Jifunze kwa moyo: Warumi 5: 1, 2.
âBasi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikilia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Munguâ.