Correspondance Course - Lesson 25

Swahili

Somo la 25

UFUFUO KUTOKA KWA WAFU

Somo: 1 Wakorintho 15

Neno ‘Ufufuo’ maana yake ni kuwa hai tena

Lazima lilikuwa ni tukio zuri sana la ajabu kuliko yote katika historia ya dunia, Yesu alipotoka kwenye kaburi lake, baada ya kuwa mfu kwa siku tatu. Wanafunzi wake walipomwona, hawakuweza kuyaamini macho yao. Walifikiri wanachokiona ni roho, lakini Yesu aliwaambia:

“Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone. Kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo”.

Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia: “Mna chakula chochote hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao” (Luka 24:39-43).

Wakawa, hatimaye, wameamini ya kuwa alikuwa amepata uzima tena. Mungu alikuwa amemfufua kutoka kwa wafu, na kumpa uzima wa milele. Tunasoma juu ya Yesu mwenyewe, akisema: “Tazama, ni hai hata milele na milele” (Ufunuo 1:18).

Yesu atawafufua wafuasi wake

Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuwa, nao pia watafufuliwa kutoka kwa wafu. Hebu uangalie tena msitari huo tuliounukulu sasa hivi. Yesu alisema, yeye ni, ‘Aliye hai’, na alikuwa amekufa. Anaendelea kusema: “Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu (kaburi)”.

Sasa, kama unao ufunguo wa mlango fulani, ina maana ya kuwa unaweza kuufungua huo mlango. Yesu anao ufunguo wa mauti. Hii ni namna ya kusema kuwa, anao uwezo wa kuyafungua makaburi, na kuwaweka huru wale waliozikwa humo. Mamlaka hiyo amepewa na Mungu. Hebu tusome Injili ya Yohana, Sura ya 5: 20-29. Ona hasa analosema Yesu katika msitari wa 21:

“Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao”.

‘Kuhuisha’ ni kufufua; ni kumpa mtu uhai tena. Mungu amempa Yesu jukumu na uweza wa kuwarudishia tena watu waliokufa uhai.

Ibrahimu aliahidiwa ufufuo

Kama tulivyokwisha kujifunza katika Somo la 12, Mungu alifanya ‘maagano’ makubwa sana na Ibrahimu. Kati ya hayo, mojawapo lilikuwa: “Nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele” (Mwanzo 13:15).

Hata hivyo tunajua Ibrahimu alikufa bila ya ahadi hiyo kutimizwa. Ilikuwa ni lazima Ibrahimu afufuliwe kutoka kwa wafu ndipo Mungu aweze kulitimiza Agano hili naye. Bwana Yesu Kristo aliitumia hoja hii kuuthibitisha ufufuo wa wafu. Unaweza kulisoma hili katika Mathayo 22:31,32.

Yesu tena aliwaambia Wayahudi wa wakati huo kuwa, wangemwona Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa Mungu, na wao wenyewe wakitupwa nje (Luka 13:28).

Tumaini walilokuwa nalo waaminifu wote

Watu wa Mungu wa nyakati zote walikufa wakiitazamia siku ambayo wangefufuliwa na kuyarudia maisha. Paulo anatuambia juu ya baadhi ya watu hao, kuwa: “Wakafa katika imani, wasijazipokea (kabla hawajazipokea) zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali” (Waebrania 11:13).

Mbele zaidi anawasemea tena watu hao, ambao walikuwa wamelala mautini katika imani kuwa: “Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi” (Waebr. 11:39, 40).

Tunaona katika msitari huu kuwa, zawadi ya uzima usio na mwisho itatolewa kwa pamoja kwa watu wanaomwabudu Mungu katika kweli.

Wakristo wa awali waliutazamia wakati huo. Mmoja wao alipokufa, walimwongelea kama ‘aliyelala usingizi’ kwa kuwa, kama ambavyo watu wanaamka baada ya kulala, ndivyo ambavyo wafuasi wa Yesu watakavyoamshwa kutoka katika usingizi wao wa mauti.

Katika Sura ya 15 ya Wakorintho wa kwanza, uliyokwisha isoma, Paulo anawaambia wafuasi kuwa, Yesu aliwatokea ‘ndugu’ zaidi ya 500 baada ya kufufuliwa kwake, na kuwa: “Katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala” (ms. 6).

Tumaini hili la ufufuo na uzima wa milele linawaleta pamoja wafuasi wa kweli wa Kristo tangu siku hizo hata sasa.

Yesu na ufufuo

Yesu alikuwa na marafiki watatu, Lazaro na dada zake, Martha na Mariamu, waliokuwa wakiishi Bethania, kijiji kidogo nje kidogo ya Yerusalemu. Hao walielewa juu ya ufufuo. Siku moja Lazaro alipoumwa dada zake walimuagizia Yesu, lakini mpaka alipokuja Lazaro alikuwa amekwisha kufa. Martha alipomwona Yesu, alimwambia: “Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa” (Yohana 11:21).

Yesu anamwambia, “Ndugu yako atafufuka” (ms. 23.) Sasa hebu tuangalie kwa makini jibu analotoa Martha: “Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho” (ms. 24).

Kwa hakika, Martha alijua kuwa kulikuwa na siku ya ufufuo mbeleni. Yesu anamwambia: “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima” (ms. 25). Sasa, ili kuwaonesha wote waliokuwa pale kuwa alikuwa na uweza wa kuwafufua waliokufa, Yesu anamwita Lazaro atoke kaburini; naye anaamka na kutoka!

Tofauti na Yesu, Lazaro hakupewa uzima wa milele alipofufuka.  Ilikuwa afe tena, lakini, kama Martha alivyosema, atafufuka tena katika ufufuo siku ya mwisho. Hili ndilo jambo Yesu alilowafundisha marafiki zake hao, na walimwelewa na kumwamini.

Kitu bora zaidi kuliko maisha yalivyo sasa

Maisha yamejaa matatizo kwetu sisi wote. Walio wengi kati yetu wanajua mtu anavyojisikia akiumwa; tunakuwa na hofu ya mambo mengi. Kifo kinaweza kuwachukua tunaowapenda muda wowote. Tunajua pia kuwa, uzee lazima uje kwa wakati wake, na maumivu yake na uchungu. Ni kweli tunataka kuishi milele katika dunia hii yenye shida?

Maisha ambayo Yesu aliwaahidi wafuasi wake akirudi, ni kitu kilicho tofauti sana na maisha yetu ya sasa na kashkashi zake nyingi. Katika maneno matamu ya Ufunuo 7:16,17 tunaambiwa juu ya wale watakaoupata uzima huo, kuwa:

“Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana, aliye katikati ya kiti cha enzi atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao”

Hawatakuwa tena na miili yenye udhaifu inayoharibika, bali watakuwa washiriki wa maisha ya kiroho ya Mungu mwenyewe. Katika Marko 12:25 Yesu anasema:

“Watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni”.

Wale watakaopewa uzima wa milele na Yesu katika kurudi kwake, watayafurahia maisha ya afya njema na nguvu zisizo na mipaka, na kuwa huru na matatizo ya sasa.

Ufufuo utakuwa lini?

Ni miaka zaidi ya 2000 imepita tangu Yesu afufuliwe kutoka kwa wafu. Atawafufua lini wale ambao wamekufa katika imani? Mtume Paulo anatujibia hili swali, akisema:

“Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja” (1 Wakorintho 15:22, 23).

Tumekwisha kuona tayari ya kuwa, Yesu Kristo anarudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu na kuitawala dunia yote. Atakapokuja kulifanya hili, atawafufua wafu. Baada ya hapo wale waliokuwa waaminifu watapewa uzima wa milele, na wataifurahia fursa ya maana ajabu ya kumsaidia Yesu kuitawala dunia. Tunasoma katika Ufunuo 5:9,10 maneno ya wimbo wanaouimba siku hiyo:

“Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi”.

Wapo watakaokuwa hai wakati Yesu akirudi

Nini kitawatokea wale walio hai wakati Yesu anarudi? Katika 1 Wathesalonike 4:14-17 Paulo anatuambia kidogo juu ya hili. Anasema:

Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani, na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.

Hebu yatazame maneno: “Tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani”.

Unaweza ukafikiri anasemea habari ya kwenda mbinguni hapa. Lakini yachunguze tena. Paulo haongelei juu ya kumlaki Bwana mbinguni; anasema ‘hewani’. Kwa hiyo baada ya ufufuo wa wafu na kukusanywa pamoja na wafuasi walio hai wakati huo wa kurudi kwa Yesu, wale wote wanaohusika watachukuliwa kimuujiza kumtumikia Bwana Yesu katika kazi yake ya kuitawala dunia.

La muhimu kwa wafuasi wote wa Yesu ni kwamba, katika siku hiyo ‘watakuwa pamoja na Bwana milele’, yaani katika Ufalme wake katika dunia.

Huwezi kuwa pande zote

Watu wengi (pengine karibu wote) wanaoamini juu ya uzima baada ya kifo, wanaamini kuwa watu wanakwenda mbinguni wanapokufa. Mwili wa mtu ambaye amekufa unalazwa katika kaburi, lakini, wanasema, mtu anayo roho ambayo inaendelea kuishi. Mtu akifa, hiyo roho inatoka na kwenda mbinguni kuwa na Mungu.

Biblia, kwa upande wake, inasema waziwazi kuwa, Bwana Yesu atarudi katika dunia na kuwafufua waliokufa. Sasa, mawazo haya yote mawili hayawezi kuwa sahihi.

Kusema kuwa roho ambayo imeshakuwa na Mungu mbinguni inarudi kuungana na mwili, alafu mtu analetwa hukumuni, ni upuuzi. Biblia haisemei chochote juu ya mtu yeyote kwenda mbinguni. Inachosema ni kwamba, muumini huyo aliyekufa atalala kaburini akiwa hajitambui na hatambui lolote, mpaka Bwana atakapomfufua kutoka kwa wafu, katika ujio wake.

Kristo atakapokuja

Wote walioisikia Injili wataletwa mbele ya Bwana Yesu Kristo. Wafu watafufuliwa, na walio hai watakusanywa pamoja nao. Kabla hajawapa baadhi yao uzima wa milele, ni lazima kutakuwa na hukumu. Utasikia mengi juu ya hukumu katika somo litakalofuata.

Hebu usome tena 1 Wakorintho 15:51-58. Hapa mtume Paulo anauongelea huo wakati Wakristo waaminifu watakapopewa zawadi hiyo kuu ya uzima usio na mwisho; au kama anavyouita Paulo, ‘kutokuharibika’. Kwa kadri tunavyoutazamia huo wakati, mtume huyu anatutaka, tuimarike, tusitikisike na tuzidi sana kuzitenda kazi za Bwana siku zote, tukijua ya kwamba taabu yetu ‘siyo bure katika Bwana’ (1 Wakor.15:58).

Muhtasari

  1. Mungu amempa Yesu uweza wa kufufua wafu.
  2. Yesu atalifanya hili atakaporudi tena duniani kuusimamisha Ufalme wake.
  3. Kwa wakati huo, atawakusanya wale walio ‘katika Kristo’ wanaoishi wakati wa kurudi kwake.
  4. Wale ambao wameishi kiuaminifu, atawapa uzima wa milele, na wataishi na kuitawala naye dunia.

Vifungu vya kusoma:  1 Wathesalonike 4,  Waebrania 11,

Yohana 11,  Mathayo 22:23-33.

Mstari wa kujifunza:   Yohana 5:28, 29

“Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu (ufufuo wa kukataliwa)”.

 

Swahili Title
Ufufuo kutoka kwa Wafu - Somo la 25
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission