Correspondance Course - Lesson 26

Swahili

Somo la 26

HUKUMU

Somo: Mathayo 25

Ni lazima kumtii Mungu

Mfalme Daudi alipokuwa amekikalia ‘kiti chake cha enzi’ katika jiji lake la Yerusalemu, aliazimia kulirudisha Sanduku la Agano la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu, lilipokuwa limekaa kwa muda. Mkokoteni ulitegeshwa wa kukokotwa kwa mnyama. Yote yalipokuwa yametengemaa, makuhani wa Mungu walitembea kando-kando la hilo sanduku lilivyokuwa likivutwa.

Lilipokuwa likienda, wale ng’ombe walikwazwa na kitu, na bwana mmoja aliyekuwa akiitwa Uza alinyoosha mkono kulizuia sanduku lisitetereke. Tunaambiwa, haraka tukio la kutisha lilitokea: Mungu alimpiga Uza: “Kwa kosa lake, hata akafa pale pale” (2 Samwel 6:7).

Ni kwa nini adhabu kwa Uza ilikuwa kali kiasi hicho, wakati alichofanya kilikuwa ni kulishikilia tu Sanduku la Mungu, tena kwa nia njema? Mungu alikuwa amesema wazi katika Kitabu cha Hesabu kuwa, Sanduku lake lilikuwa ni la kubebwa tu na makuhani mabegani mwao. Kwa hiyo Uza alikuwa ama hakuijua amri hiyo ya Mungu, ama hakuchagua kuitii. Kwa sababu hiyo, alikuwa na hatia mbele ya Mungu.

Habari hii inatufundisha kuwa, Mungu ni Mtakatifu na Mkuu sana. Anataka watu wanaomtumikia wamtii.

Watu wanaoupuuza upendo wa Mungu

Yesu aliwahi kutoa hadithi ya mfalme aliyefanya karamu ya harusi kwa ajili ya mwanawe. Maandalizi yalipokamilika aliwatuma wafanyakazi wake kuwakaribisha walioalikwa, lakini walikataa kwenda.

Waalikwa walipendelea zaidi kuendelea na shughuli zao za kila siku, kuliko kuuitikia wito wa mfalme wao wa kuhudhuria sherehe yake. Kwa sababu hiyo, mfalme alikasirika, na akawatuma watumishi wake kwenda kuwaangamiza hao watu waliodharau mwaliko wake (Mathayo 22:1-4).

Mungu ni Mfalme Mkuu sana. Kama kwa neema yake anawakaribisha watu kuifurahia raha ya Ufalme wake katika dunia, na mtu anasema, kwa makusudi: “Sihitaji hilo Mungu analoniitia, na sitamtii,” basi kutakuwa na siku ya hukumu, na mtu huyo ataangamizwa. Katika Wagalatia 6:7 tunaambiwa: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi, kwa kuwa, chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna”.

Ufufuo na hukumu

Biblia inatufundisha kuwa, kutakuwa na siku ya hukumu baada ya ufufuo. Mungu ana upendo; lakini pia ni mkweli na wa haki. Kama tunavyoambiwa katika Kutoka 34:7, yeye siye: “Mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe”.

Hawezi kutoa uzima wa milele kwa watu ambao wameupuuza upendo wake; ambao, wakiwa wanajua kuwa Yesu aliwafia, hawafanyi jitihada yoyote kumtumikia na kumtii. Kwa hiyo, Paulo anatuambia:

  • “Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu” (Warumi 14:10).
  • “Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya” (2 Wakorintho 5:10).

Lazima uje wakati wa kujibu

Yesu aliwahi kuwaambia wanafunzi wake: “Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo” (Yohana 13:13). Katika wakati wa Agano Jipya, kama mtu alikuwa amemnunua mtu (mtumwa), alikuwa akimmiliki jumla. Mtumwa alikuwa hawezi tena kujipendeza mwenyewe. Jukumu lake lilikuwa moja tu katika maisha yake; kumfurahisha bwana wake.

Sasa Yesu ametununua kwa damu yake, alipoutoa uhai wake msalabani, uwe dhabihu kwa ajili ya dhambi. Kwa hiyo Paulo anatuambia:

“Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu” (1 Wakorintho 6:19, 20).

Maana ya hili ni kwamba, tunawajibika kwa Bwana Yesu kwa namna tunavyoyaishi maisha yetu. Atakapokuja tena, atawapa zawadi ya uzima wa milele waliokuwa waaminifu, na atawaadhibu wale walioibeza njia yake.

Ukweli katika mfano

Ili kuwafundisha wafuasi wake juu ya wajibu wao kwake, Yesu alitoa mfano tunaouona katika Mathayo 25:14-30. Usome, tafadhali, kwa manufaa yako. Ona hasa kinachosemwa kwenye msitari wa 21, kuhusu zawadi itakayotolewa kwa mtumishi atakayeonekana mwaminifu: “Ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako”.

Mtu ambaye hakutii hawezi kutegemea kupata tuzo kama hiyo, kwa kuwa amekuwa mtumwa asiyefaa. Adhabu yake inakuwa kali na amri inatoka: “Mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno” (ms. 30).

Mhukumu wa haki

Yesu atakaporudi, atawafufua wafu na kuwakusanya wale kati ya wanafunzi wake watakaokuwa wakiishi wakati huo. Itakuwa ni wakati wa hukumu. Baada ya mchujo, wale watakaokuwa wamekubaliwa, watapewa uzima wa milele, na Yesu atawaambia:

“Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu” (Mathayo 25:34).

Yesu mwenyewe ndiye atakayekuwa ‘mhukumu’ (angalia Yohana 5:28-30). Atahukumu kwa hekima Mungu aliyompa. Katika Isaya, tunaambiwa:

“Wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili” (Isaya 11:3, 4).

Watu wanaweza tu kuhukumu kwa yale wanaoyaona na wanaoyasikia, lakini Bwana Yesu, kwa kuijua mioyo ya watu ilivyo, hatafanya makosa katika kuhukumu kwake.

Nani watakuwa katika Kiti cha Hukumu?

Wale wote Bwana anaowahesabia kuwajibika kwake, waliosikia wito wa Mungu wa uzima, na kujua kuwa walipaswa kuuitikia, watakusanywa mbele ya Kiti cha Hukumu cha Kristo.

Lakini hawatakuwa ni hao tu. Kutakuwa na watu; wanaume kwa wanawake, walioishi kabla ya Yesu kuzaliwa, na wengine baada ya hapo. Wote wataitwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo kujibu juu ya lile walilofanya kuhusiana na ujumbe wa Injili. Injili ni ‘lulu’ ya thamani kubwa. Wale wasiokuwa waaminifu watakuwa katika kiti cha hukumu pamoja na wale waliojaribu kuishi kwa kufuata mfano wa maisha makamilifu ya Bwana Yesu Kristo. Katika Waebrania tunaonywa:

“Kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao” (Waebrania 10:26, 27).

Yesu mwenyewe anatuambia: “Mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 10:33).

Watu ambao hawakuwahi kumfahamu Mungu wa kweli, na mpango wake wa wokovu, hawatafufuliwa kwa ajili ya hukumu. Unaweza ukawa unaikumbuka mistari ya Zaburi 49 inayosema juu ya mtu kama huyo, kwamba:

“Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake; hawataona nuru hata milele. Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, amefanana na wanyama wapoteao” (Zab. 49:19, 20).

Utakuwa umetambua pia ya kuwa, wazo la kwenda mbinguni tunapokufa ni tofauti kabisa na ukweli. Halitokani na ukweli unaofundishwa kwenye Biblia.

Shangwe kwa wanaokubalika

Wale watakaokubaliwa katika hukumu, watapewa uzima usio na mwisho. Miili yao haitapatwa na uchungu tena au kuchoka, au udhaifu mwingine wowote ule wa kibinadamu. Akili zao nazo hazitavutwa tena kuwaza mawazo mabaya. Utakuwa wakati wa shangwe sana kwa waaminifu.

Katika Biblia, wakati wa kurudi Kristo unazungumziwa kama vile ni Sherehe ya Harusi. Katika Ufunuo tunaambiwa: “Heri walioalikwa karamu ya harusi ya Mwana-kondoo” (Ufunuo 19:9).

Wakati Yesu alipokuwa na wanafunzi wake wakila mlo wa mwisho wa pamoja kabla ya mauti yake, aliwaambia:

“Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli” (Luka 22:29,30).

Ufalme utakapokuja, mitume wale watakuwa watawala juu ya Israeli, nchi itakayokuwa wakati huo taifa-muhimu kuliko mataifa yote duniani. Kila mfuasi atakayekubalika kwa Yesu, atakuwa na sehemu katika hiyo kazi ya kuiongoza dunia. Kwa hiyo tunasoma katika Ufunuo 5 mstari wa 9 na 10 juu ya wafuasi waaminifu wanaoimba wimbo, wakisema:

“Ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi”.

Kitakachowapata wale watakaokataliwa ni nini?

Tumekwishaona kuwa, wote wanaoletwa mbele ya Kiti cha Hukumu cha Kristo watagawanywa kwenye makundi mawili. Kristo atawakubali baadhi yao na kuwakataa wengine, na kuwapa uzima wa milele wale aliowakubali. Lakini kitawatokea nini wale watakaoonekana hawafai? Adhabu yao itakuwa nini?

Hatuufahamu undani wote, ila kuna mambo ambayo ni ya uhakika. Kwanza, watajigundua walivyokuwa wajinga. Wataona walivyopata fursa iliyokuwa nzuri ajabu ya mibaraka ya Mungu na kuidharau. Hili litawaumiza sana mioyo. Yesu anasema juu ya watu hao:

“Kutakuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje” (Luka 13:28).

Mwisho wataangamizwa kabisa. Yesu aliifananisha hukumu na mavuno ambapo, mbegu njema inatenganishwa na magugu yasiyo na kazi; yasiyofaa. Nafaka inahifadhiwa kiuangalifu ghalani, lakini magugu yanachomwa moto (Mathayo 13:36-43). Paulo alifundisha kitu hicho waziwazi, akisema:

“Wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake.…(atawalipiza) kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake” (2 Wathesalonike 1:7-9).

Kuna vifungu kadhaa katika Biblia vinavyoelekea kutuonya tusijiamini sana juu ya hukumu. Yapo pia Maandiko yanayoonekana kututia moyo tuwe na matumaini kabisa. Sio kwamba kuna kujipinga. La kutambua tu ni kwamba, hatuwezi kujiamini sana wenyewe; wote tu-wadhaifu. Hata hivyo, tunaweza kuutumainia kabisa uweza wa kuokoa wa Mungu wetu. Tunaambiwa:

“Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?” (Warumi 8:32).

Ingawa tunaweza kuanza kwa kuogopa juu ya Mungu, tutaweza pole pole kujifunza kumpenda na kumtumainia kabisa. Yohana anasema:

“Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu….katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu” (1 Yohana 4:17,18).

Muhtasari

  1. Kutakuwa na ‘siku ya hukumu’.
  2. Itakuja baada ya ufufuo.
  3. Wote ambao wamejua na kuielewa kweli kumhusu Mungu wataletwa hukumuni.
  4. Watu watakaoshinda katika ‘kiti cha hukumu’ watapewa uzima wa milele.
  5. Watu watakaokuwa wamekataliwa watajuta sana na wataangamizwa.

Kifungu cha kusoma: 2 Wakorintho 5

Mstari wa kuushika: 2 Wakorintho 5:10

“Imetupasa sisi wote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya”.

 

Swahili Title
Hukumu - Somo la 26
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission