Correspondance Course - Lesson 27

Swahili

Somo la 27

UZIMA WA MILELE

SOMO: Yohana 3

Utakuwa umekwishaona katika mafundisho haya ya Biblia ya kwamba, mwanadamu wa kwanza, Adamu, aliumbwa kwa Mungu kuutengeneza mwili kwa udongo, na kisha kuupulizia pumzi ya uhai. Lakini, Adamu na Hawa walikosa, na hivyo walibadilika na kuwa viumbe vinavyokufa.

Watu wote, wanaume kwa wanawake, hatimaye wanakufa, kwa kuwa wote wanakosa; ni wadhambi. Ni kitu kisichokubalika mbele ya Mungu, kwa wadhambi kuishi milele. Haiwezekani!

Kuna mtu mmoja tu ambaye amewezeshwa kutokufa tena, naye ni Bwana Yesu Kristo. Aliweza kuishinda nguvu ya mauti kwa kuishi maisha yasiyo ya dhambi. Hii ndiyo sababu ya Mungu kumfufua kutoka mautini na kumpa uzima usio wa mwisho. Mungu mwenyewe hawezi kufa; yeye ni wa, “Tangu milele, na sasa, na hata milele” (Yuda 25). Ukimwacha Mungu, ni Bwana Yesu Kristo na malaika, ndio tu kwa sasa ‘wasiopatikana na mauti’ (1 Timotheo 6: 15, 16).

Jambo jema sana kuihusu Injili ni kwamba, kwa kuliamini kusudi la Mungu na kazi za wokovu za Yesu, inawezekana ni sisi kuwa na tumaini la uzima wa milele. Paulo anasema, neema ya Mungu:

“Sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu, aliyebatilisha mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili. (2 Timotheo 1:9,10).

Hatuwezi kulipwa uzima wa milele

“Mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama (zawadi) ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 6:23).

Kama tulivyokwisha kuona, uzima wa milele ni zawadi ya Mungu. Hakuna mtu kati yetu, hata awe mwema kiasi gani, anayeweza kuistahili.

Kama wadhambi, la maana zaidi tunaloweza kulitegemea na kujifurahisha kwalo katika maisha haya, ni baadhi ya mambo mazuri tunayoweza kuyapata kwenye Sayari hii, mpaka tunapofikia miaka 70 au 80. Ni wachache wanaovuka hapo.

Hebu angalia ulinganisho ufuatao kwenye Zaburi ya 90:

HULKA YA MUNGU YA MILELE (Zab 90:2)

HULKA YA MWANADAMU

(Zab 9:10)

“Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, na tangu milele hata milele, ndiwe Mungu”.

“Siku za miaka yetu ni miaka sabini, na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; na kiburi chake ni taabu na ubatili; maana chapita upesi tukatokomea mara”.

Kwa hiyo tutakwenda kaburini na kuishia; hatutakuwepo tena, kama hatukuwa na tumaini la Biblia la uzima wa milele uliopo katika Yesu Kristo. Wahusika wote wakuu katika Biblia waliokuwa na imani, walioziamini ahadi za Mungu, walikuwa na tumaini hili la uzima. Waliutazamia wakati ulio bora zaidi wa kuja mbeleni.

Ona kinachosemwa kumhusu Ibrahimu, Sara, Isaka, Yakobo, Daudi na wengi wengineo:

“Hawa wote wakafa katika imani wasijazipokea (‘kabla hawajazipokea’) zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni na wasafiri juu ya nchi” (Waebrania 11:13).

Paulo na Yohana, kama ilivyokuwa kwa mitume wengine, walitazamia uzima wa milele. Walitumaini katika:

“Tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele” (Tito 1:2).

 

“Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele”             (1 Yohana 2:25).

Uzima wa milele sio kwa kila mtu

Kama ingekuwa ni moja kwa moja kila mtu anaweza kupata uzima wa milele, kusingekuwa na haja ya kujitahidi kuzitii amri za Mungu. Ahadi ya uzima usio na mwisho imetolewa kwa wale tu wanaotaka kuuitikia upendo wa Mungu. Kama ukisoma Warumi 2:6,7 utaona kuwa tuna uchaguzi. Mungu atawapa uzima wa daima wale tu ambao:

      “Kwa saburi katika kutenda mema, wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika”.

Kama hatuutafuti, kwa vyovyote hakuna tumaini la kuupata mbeleni.

Maisha ya milele na Uzima wa milele

Utakuwa umegundua kuwa, baadhi ya vifungu tulivyovinukulu vinaongelea kutokuharibika (au uzima wa milele), wakati vingine vinasemea maisha au uhai wa milele. ‘Uhai wa milele’ ni uzima wa kuwa kwa namna Mungu alivyo. Kama tukiishi maisha ya kumcha Mungu, kwa neema yake, atatuzawadia uhai usio na mwisho, ambao ni uzima wa milele.

KUWA NA UZIMA WA MILELE NI KUISHI MILELE KATIKA HAKI KWA UHUSIANO MWEMA NA MUNGU.

Ni lini uzima huo wa milele utatolewa?

Utatolewa na Yesu Kristo kwa waaminifu baada ya kuwafufua waliokufa. Nabii Danieli aliutazamia wakati huo, akisema:

“Wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele” (Dan. 12.2).

Hili litakuwa wakati Yesu atakaporudi na kuwaita wale ‘waliolala’ katika mavumbi ya nchi. Danieli anawaita ‘walalao’ kwa kuwa, Bwana atawaamsha wapate uzima kutoka makaburini walipo.

Katika Yohana, tunasoma: “Saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima” (Yohana 5:28, 29).

Katika Somo la 25 na 26 tulijadili kufufuliwa kwa wafu na hukumu itakayofuata. Wale watakaokuwa wamemfuata Yesu kiuaminifu, watakuwa wale wanaoitwa ‘Watakatifu’; watu wanaopewa kutawala na Mfalme Yesu katika utawala wake wa miaka 1000 kutokea Yerusalemu.

Watu hawa, wanaume kwa wanawake, watapewa uzima wa milele, sio tu kwa kuwa itakuwa ni neema ya tuzo yao kutoka kwa Mungu kwa uaminifu wao katika kizazi hiki, bali pia kwa kuwa itakuwa ni lazima kuwe na watawala walio wakamilifu, wenye afya bora, wasiokufa, katika Ufalme wa Mungu.

Kwa nini ni hivyo?

Katika mifumo yetu ya kiutawala kwa sasa, watawala na wakubwa wengine, kwa nadra wanakuwa watu wa kweli na wa haki. Hawawi na hekima ya kutosha kujua la kufanya, kuondoa uovu ulio katika dunia. Mara nyingi hawawi pia na raslimali au uwezo wa kuyafanya mambo mazuri ambayo wangependa kuyafanya. Na hata aliye bora sana, anapokwenda vizuri na kufanya yaliyo mema kwa ajili ya wengine, anazeeka au kuugua na kufa.

Wale watakaopata uzima wa milele hawatabadilika au kudhoofika, na kwa kuwa wamekuwa wateule wa Mungu, watakuwa na hekima na haki.

                 MTAKATIFU NI MUUMINI WA KWELI

Neno ‘takatifu’ lina maana ya ‘kilichotengwa’ au ‘safi’. Waumini wa kweli hawawi kama watu wa kidunia; wanamcha Mungu.

Watakatifu wasiokufa wataonekanaje?

Wengi wanajiuliza jinsi watakatifu watakavyokuwa, watakapokuwa wamepewa uzima wa milele. Wataweza kutambulika? Watakula na kulala? Ingawa hatuujui undani wote, Biblia inatupa maelezo kadhaa juu ya hili.

Tunafahamu kuwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii watakuwa wakitambulika wakati wa Ufalme (Luka 13:28).

Tunao mfano wa Yesu mwenyewe. Alitambuliwa wazi na wanawake fulani, na mitume pia, baada ya kufufuliwa kwake. Alikula chakula na wanafunzi wake. Mwili wake bado ulikuwa na makovu ya mateso ya kikatili aliyoyapata msalabani, na wanafunzi wake waliruhusiwa kumgusa.

Ni kweli kulikuwa na wakati walikuwa wamejiuliza kama alikuwa ni mtu ama ‘roho’, alipowatokea kiajabu-ajabu mbele yao. Lakini aliwaambia:

“Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili (nyama) na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo (Luka 24:39).

Ni wazi kuwa Yesu akiwa amepata uzima wa milele, alikuwa bado ni mwili wa nyama na mifupa. Neno ‘mwili’ katika msitari huo, kwenye Biblia ya Kingereza ni ‘flesh’ lenye maana ya ‘nyama’.

Andiko halisemi kuwa alikuwa na mwili na damu (kama tulivyo sisi) kwa kuwa, kulingana na Maandiko: “Uhai wa mwili u katika hiyo damu” (Walawi 17:11). Kwa maneno mengine, maisha ya kawaida yanawezeshwa kuwepo na damu, lakini sasa Yesu alikuwa akiishi kwa roho ya Mungu; kwa uweza wake.

Yesu atakapowapa watu uzima wa milele, miili yao ya kibinadamu itakuwa miili ya kiroho: “Hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho” (1 Wakorintho 15:44). Ni, “Sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa” (ms. 53).

Miili yao mipya itakuwa sasa ikiishi kwa roho ya Mungu, badala ya kuishi kwa damu inayokufa. Hakutakuwa na uchungu tena, wala kuugua, wala udhaifu wa kimwili au kiakili. Hakutakuwa na maumivu ya aina yeyote. Neno linasema:

“Naye (Mungu) atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufunuo 21:4).

Maajabu ya uzima wa milele

Kwa hakika itakuwa ni hali nzuri ya ajabu sana ya kuweza kuishi. Katika hali hiyo, tutaweza kufurahia kikamilifu vitu vyote vizuri Mungu atupavyo.

Kutakuwa na mibaraka ya afya njema, nguvu, chakula bora, amani na usalama, na kujua zaidi kuyahusu mambo ya Mungu. Hakutakuwa tena na mapambano dhidi ya dhambi kwa wenye-haki.

Utakumbuka ya kwamba kwa kipindi kifupi katika karne ya kwanza, mitume walipewa karama (zawadi) za Roho Mtakatifu. Wapo walioweza kuihubiri Injili kwa lugha za kigeni, na wengine waliweza kuponya magonjwa ya kimwili na kiakili. Haya yalikuwa ni ‘malimbuko’ tu (mavuno ya kwanza) ya karama hizo, watakazokuwa nazo watakatifu katika Ufalme wa Mungu. Tumepewa kuona kidokezo hicho cha ajabu cha nyakati hizo zinazokuja mbeleni.

Uzima huo sio tu wa miaka hiyo 1000 ya Ufalme, bali ni wa milele. Pengine hili ni gumu sana kwetu kulielewa, kwa sababu ni tofauti mno na maisha ya sasa tunayoishi. Wapo ambao wameshawishika hata kufikiri kuwa maisha yasiyo na mwisho yatakuwa kitu cha kuchosha. Lakini, kamwe Mungu hawezi kuahidia watu wake kitu ambacho hakina mvuto. Andiko linasema:

“Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye” (Isaya 64:4).

Tafsiri hapa ya Kiswahili ameleta shida kupata kinachosemwa. Kwa usahihi zaidi ingekuwa: “….wala jicho halikuona, ila wewe, Mungu, mambo unayotenda kwa ajili ya yeye akungojeaye”.

Hatuwezi kuyaelewa maajabu ya wakati huo, wakati shughuli kubwa na tukufu ya utawala wa Yesu Kristo wa miaka elfu moja itakapokamilika. Baada ya hapo mambo yatakuwa mazuri hata zaidi. Tunaambiwa, Mungu atakuwa: “Yote katika wote” (1 Wakorintho 15:28). Uhusiano kati ya Mungu na vitu alivyoumba utakuwa mkamilifu; umetengemaa. Hivi ndivyo Mungu alivyopanga tangu mwanzo.

Hii ndiyo ahadi ya uzima wa milele.

Muhtasari

  1. Mungu, Yesu na malaika ndio pekee wasio na ‘kutokuharibika’ kwa sasa.
  2. Baada ya hukumu, walio ‘wa haki’, watakatifu, watapewa nao uzima wa milele; watapewa kutokufa.
  3. Watakaowezeshwa kutokufa watapewa miili ya kiroho. Hawatapata shida wala kutenda dhambi tena. Watakuwa na roho ya Mungu.

Vifungu vya kusoma: Danieli 12: 1-3,  1 Wakorintho 15:50-57

Kujifunza kwa moyo: Yohana 3:16

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

 

Swahili Title
Uzima wa Milele - Somo la 27
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission