Correspondance Course - Lesson 29

Swahili

Somo la 29

IBILISI, MAPEPO, SHETANI

Somo: Mathayo 8:14-34

IBILISI NA PEPO

Kuna maneno mawili ya Kiyunani yaliyotafsiriwa ‘Ibilisi’ katika Biblia zetu, na kwa kuwa yanamaanisha vitu tofauti, tutahitaji hasa kujua kila neno lina maana gani. Maneno hayo ni:

   Daimon – lenye maana ya ‘roho mbaya au roho mwovu’

   Diabolos – lenye maana ya ‘msingiziaji au mchongezi’

Tutalichunguza neno Ibilisi (diabolos) katika somo litakalofuata. Neno ‘daimon’ linatumiwa katika Kiyunani tunapoambiwa, Yesu: ‘akawatoa pepo’. Yesu aliponya magonjwa yote watu waliyokuwa wakiugua. Aliwapa vipofu kuona, aliwezesha viziwi kusikia, aliwafanya na walemavu wa miguu kutembea. Yesu aliwaponya pia watu wengi waliokuwa na magonjwa ya kiakili; kichaa na matatizo kama ya kifafa.

Katika siku hizo, kama ugonjwa ulikuwa mgumu kueleweka, watu walisema kuwa mgonjwa huyo alikuwa, ‘ameshikwa na pepo’. Soma kwa makini Mathayo 8:16,17. Tunaambiwa hapa kwamba:

“…wakamletea (Yesu) wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi”.

Yesu akawaambia, Isaya alikuwa ametabiria jambo hilo, aliposema:

“Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu” (Isaya 53:4).

Hili linatufundisha kuwa:

“Kushikwa au kukamatwa na pepo” ni sawa na “Udhaifu na magonjwa”. Yesu aliwaondolea madhaifu na magonjwa hayo.

Sanamu (miungu ya wongo) iliyokuwa ‘pepo’

Katika sehemu zingine kwenye Biblia ambapo neno ‘daimon’ lilitumika, mara nyingi lilikuwa likiongelea ibada za miungu ya uwongo. Tuangalie Zaburi ya 106.

Zaburi hii inatuambia juu ya makosa mengi Waisraeli waliyokuwa wakiyafanya na vile, pamoja na hayo, Mungu alivyoendelea kuwabariki. Soma msitari wa 36-38 mwandika-Zaburi anaposema juu ya wana wa Israeli kuwa:

“Wakazitumikia sanamu zao, nazo zikawa mtego kwao. Naam, walitoa wana wao na binti zao kuwa dhabihu kwa mashetani”.

Neno ‘mashetani’, hapa ni neno ‘daimon’ katika Kiyunani, lililotafsiriwa pia ‘pepo’, kwenye Kiswahili. Katika msitari wa 37 shutuma dhidi yao zimerudiwa, lakini hapa tunaambiwa kuwa: “Waliwatoa wana wao na binti zao kuwa dhabihu kwa mashetani”. Ni wazi basi kuwa, ‘mashetani’ wanaotajwa hapa, walikuwa ni sanamu; miungu ya uwongo ya mataifa yaliyokuwa yakiizunguka Israeli.

Kuna matumizi ya neno hili katika Agano Jipya yanayoleta maana hiyo hiyo katika 1 Wakorintho 10:20. Mtume Paulo anawaambia Wakorintho ya kwamba, vitu vile watu wa kimataifa: “Wavitaovyo sadaka, wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu”.

Kama ukirudi nyuma kwenye msitari wa 19 utaona kuwa, hayo ‘mashetani’ yalikuwa, ‘sio’ kitu. Yalikuwa sanamu; miungu isiyokuwa ya kweli ya watu wa kimataifa, wasiomjua Mungu.

Wakristo wamepewa kumwabudu Mungu mmoja tu aliye wa kweli, miungu mingine yote ni sanamu, hapa ikiitwa ‘mashetani’. Vitu visivyo na uhai watu wanaviabudu bure; ni ukafiri.

Angalizo: Neno lenye maana ya ‘roho mbaya au roho mwovu’ (daimon) kwa kawaida limetafsiriwa ‘pepo’, lakini lisichanganywe na neno ‘Ibilisi’. Sehemu zingine, neno, ‘mashetani’ limetumika badala ya pepo.

SHETANI

Neno ‘shetani’ katika Agano la Kale lina maana ya ‘adui’ au ‘anayepinga’. Mfano wa jinsi lilivyotumika upo katika 1 Wafalme 11:14 ambapo tunasoma, kuwa: “Ndipo BWANA  akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi”. Na mbele kidogo kwenye 1 Wafalme 11:23-25 tunaambiwa: “Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada…Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani”.

Sulemani alianza ufalme wake vizuri akimpenda sana Mungu, lakini baadaye alinasa katika kuabudu sanamu. Matokeo yake, Mungu alimwondokeshea maadui ili asipate amani. Neno hilo ‘adui’ ni neno hilo hilo lililotafsiriwa ‘shetani’ sehemu zingine.

Hadadi na Rezoni walimsumbua Sulemani na Israeli (‘waliwapinga’) na sababu ni kuwa, Sulemani na Israeli walikuwa wamemkiuka Mungu; walikuwa wakifanya dhambi. Hadadi na Rezoni walikuwa ‘shetani’ kwa Sulemani na Israeli.

Lakini, katika Biblia ‘shetani’ sio mara zote anakuwa adui mbaya. Katika Hesabu tunaambiwa juu ya nabii aliyekuwa akiitwa Balaamu, aliyekuwa akienda safari ambayo Mungu hakuwa akitaka aende. Maandiko yanasema:

“Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu (Balaamu) alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga” (Hes. 22:22).

Neno ‘kumpinga’ hapa pia ni neno ‘shetani’ katika Kiebrania. Hapa ‘shetani’ alikuwa ni malaika mwaminifu wa Mungu anayefanya mpenzi ya Mungu, aliyetumwa kumzuia Balaamu njiani asiende kuwalaani wana wa Israeli.

Ni wazi neno hilo haliwezi kumaanisha kiumbe mwovu, au malaika mwovu. Hakuna malaika anayeweza kuwa mwovu. Shetani ni adui, mpinzani; mtu anayepinga. Anaweza kuwa mwema au mbaya.

   MAANA YA SHETANI NI ADUI AU MPINZANI; MTU ANAYEZUIA

Wakati Petro alipojaribu kumzuia Yesu asiiendee njia ambayo Mungu alimtaka aiendee; njia ya msalaba, Petro alikuwa ‘adui’. Yesu alimwambia Petro: “Nenda nyuma yangu, Shetani, u kikwazo kwangu”. Sababu ni kwamba, Petro alikuwa akitaka kumgeuza Yesu asiufuate mpango wa Mungu. Yesu anamwambia, “Huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” (Mathayo 16:23).

Kwa hiyo, Petro alikuwa ‘shetani’; alikuwa hapa akimpinga Yesu; akipingana na kusudi la Mungu. Unaweza kuona; hata katika Agano Jipya maana ni ile ile. Adui mkubwa kuliko wote wa mtu ni hulka yake mwenyewe ya dhambi.

Neno ‘shetani’ linaweza kutumiwa kwa hiyo hulka. Hili linaweza kuonekana tena vizuri kwa kulinganisha Matendo 5 msitari wa 3 na wa 4.

Ms.3: “Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu na kuzuia kwa siri sehemu ya kiwanja?”

Ms.4: “…ilikuwaje hata ukaliweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu....”

Ni mawazo yaliyokuwa potofu ya Anania yaliyomfanya afanye vile. Neno ‘shetani’ limetumiwa katika mstari wa 3 kuiwakilisha hulka ya dhambi aliyokuwa nayo Anania, iliyokuwa ikiyapinga nafsini mambo ya kiroho; mambo ya Mungu.

Lusifa alikuwa ni nani?

Watu wanaoamini juu ya uwepo wa ‘dudu’ ovu linaloitwa ‘shetani’ lisiloonekana, wanapenda kuthibitisha kuamini kwao kwa kunukulu mara nyingi Isaya 14:12-16. Mistari hiyo inasema:

“Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa uliyewaangusha mataifa….”

Maneno, ‘nyota ya alfajiri’ katika Biblia ya Kingereza ni ‘Lucifer’ (Lusifa). Kwa hakika, kama ukikisoma kifungu hicho chote (Isaya 14), utaona kuwa, Lusifa ni mfalme wa Babeli, ‘mwenye kuonea’   (anayeelezewa kwenye mstari wa 4). Ulikuwa ni unabii wa kuanguka kwa ufalme wa Babeli; kitu kilichotokea miaka ilivyopita.

Kwa namna hiyo hiyo, Ezekieli 28:14-16 mara nyingine inasemewa kusemea uwepo wa ‘dudu’ hilo:

“Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu….Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako”.

Ni wazi kuwa ujumbe huu ulikuwa ni kwa ajili ya mfalme wa Tiro, kama mstari wa 12 unavyosema, na hauhusiani na uwepo wa ‘dudu’ lolote hai ovu lisiloonekana.

Ni nini kilichotokea katika Bustani ya Edeni?

Unakumbuka ni nini kilichotokea katika Bustani ya Edeni? Mungu alipomwita Adamu kutoka mahali alipojificha na kumuuliza kama alikuwa amekula kutoka katika mti wa ujuzi wa mema na mabaya, Adamu alijibu: “Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala” (Mwanzo 3:12).

Ukilitafakari jibu hilo utaona kwamba, Adamu alikuwa ni kama anamwambia Mungu kosa sio lake; ni la Mungu. Yeye ndiye aliyempa huyo mwanamke, na mwanamke ndiye wa kulaumiwa kwa kumpa hilo tunda. Lakini, kosa lilikuwa ni la kwake mwenyewe.

Kisha Mungu akamuuliza mwanamke alichofanya ni nini, na mwanamke akajibu: “Nyoka alinidanganya, nikala”. Kwa maneno mengine, alimtupia lawama nyoka; lilikuwa ni kosa la nyoka.

Adamu na Hawa walikuwa na shauku ya kutupia lawama kwingine, badala ya kubeba lawama wenyewe kwa makosa yao. Sisi wote tumekuwa hivyo. Hatupendi kuwajibishwa kwa mawazo na matendo yetu mabaya wenyewe; hatupendi kukubali kosa. Pengine ndio maana watu wengi wanapenda kuamini kuwa, kuna ‘dudu’ hilo lisiloonekana linaloitwa ‘shetani’ linalowadanganya watu wamwasi Mungu.

Mungu alimruhusu nyoka kuongea; sio ajabu sana. Ni kama alivyomruhusu punda wa Balaamu kuongea katika Hesabu 22:28.

Adamu alipaswa kujidhibiti na kumkataa nyoka, lakini Mungu aliwaacha Adamu na Hawa wajaribiwe, na wakaanguka. Nyoka hakuwafanya walile lile tunda; alichofanya tu ilikuwa kuwajaribu. Adamu na Hawa hawakumtii Mungu; walijiamulia wenyewe kufanya walichotaka.

Muhtasari

  1. ‘Pepo’ katika Biblia ni magonjwa yaliyofikiriwa kusababishwa na roho wabaya/wachafu. Yesu alipoyaponya ilihesabiwa ‘ametoa pepo’.
  2. Neno ‘mashetani’ au ‘mapepo’ ni tofauti na neno Ibilisi (tutakalolijadili katika somo lijalo).
  3. ‘Shetani’ maana yake ni adui/mtu anayepinga. ‘Adui’ huyo anaweza kuwa wa kheri au wa shari.
  4. Neno Lusifa katika Isaya 14 kwenye Biblia ya Kingereza linamwongelea mfalme wa Babeli, sio ‘dudu’ hai lisiloonekana.

Vifungu vya kusoma: Mathayo 16:21-28,  Hesabu 22

Mistari ya kushika: Mathayo 8:16, 17

“Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu”.

Swahili Title
Ibilisi (Mapepo) na Shetani
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission