Correspondance Course - Lesson 31

Swahili

Somo la 31

UBATIZO

Somo: Yohana 3

Baada ya kufufuka na kutoka kaburini, na muda mfupi kabla ya kupaa kwenda mbinguni, Bwana Yesu Kristo alisema ifuatavyo kwa mitume wake:

“Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini, atahukumiwa” (Marko 16:15, 16).

Mambo mawili yako wazi sana katika maneno haya:

  1. Kabla mtu yeyote hajaweza kuamini na kubatizwa, ni sharti aijue ile Injili aliyoifundisha Yesu, na kuielewa Habari Njema ya Ufalme wa Mungu.
  2. Hakuna ambaye anaweza kujifurahisha mwenyewe kuhusu Ubatizo. Ubatizo sio kitu ambacho tunaweza kukifanya kama tukijisikia; ni cha lazima! Kama mtu hakuamini na kubatizwa, huyo yuko katika hukumu ya kifo; hana tumaini la uzima ujao.

Kutubu kunaanza kabla ya kubatizwa, mtu anapoisikia (au kuisoma) Injili na kuielewa. Injili inaibadilisha namna yake ya kufikiri na kuanza kuacha kufikiri kikawaida. Anaanza kufikiri kwa namna ya Mungu; kwa namna Mungu anavyotaka.

Ubatizo ni namna aliyoichagua Mungu kwa ajili yetu kuanza maisha mpya. Tunapomgeukia, tunaitii amri yake kwamba tubatizwe, dhambi zetu zinasamehewa, na tunaanza maisha mapya mbele yake.

Yesu alitupa kielelezo

Yesu hakuwahi kufanya lolote baya. Hakuwa na haja ya kubatizwa ili dhambi zake ziweze kusamehewa, kwa kuwa hakutenda dhambi. Hata hivyo, katika Mathayo 3:13-17 unaweza kusoma vile Yesu alivyoshuka katika mto Yordani, na kubatizwa mtoni humo na binamu yake, Yohana.

Yohana alitambua kuwa Yesu hakuwa na kosa, na akasema hakuwa akistahili kumbatiza. Ilikuwa ni kweli tupu, lakini Yesu alimwambia: “Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Mathayo 3:15).

Kwa kubatizwa, Yesu ametupa kielelezo cha kufuata.

Ubatizo unamaanisha nini?

Uligundua katika hicho kifungu cha Mathayo kuwa, Yesu alibatizwa ndani ya mto Yordani, na baada ya hapo, “Akapanda kutoka majini?”

Kuwafanya watoto kuwa Wakristo kwa kuwanyunyizia vimaji au kuwaosha vichwa hakupo kabisa katika Biblia.

Tunafundishwa waziwazi kuwa, kuamini ni lazima kuje kabla ya kubatizwa. Mtoto mdogo anawezaje kuamini, kabla hajawa mkubwa wa kutosha kuelewa?

Wayunani (Wagiriki) walitumia neno linalotafsiriwa ‘kubatiza’ walipokuwa wakiweka nguo rangi. Kitambaa (au nguo) ‘kilibatizwa’ kwa kutumbukizwa chote kwenye maji. Hakuna kipande katika nguo hiyo kilichoachwa nje, ili rangi ikolee.

Biblia inapoongelea Ubatizo inamaanisha kutumbukia mzima-mzima katika maji. Kuna maana yake nzuri kwa kitendo hiki cha kuzikwa mzima kwenye maji na baada ya hapo kuibuka, kama tutakavyoona baadaye.

“Tubuni mkabatizwe”

Kama tulivyokwishaona, huu ulikuwa ndio ujumbe wa Yohana Mbatizaji. Injili inawataka watu wabadili fikra zao na maisha yao, na wamgeukie Mungu. Hii ndio Biblia inayoita ‘toba’.

Petro aliutoa ujumbe huo kwa Wayahudi waliomsulubisha Yesu, katika siku ya Pentekoste baada ya Yesu kupaa. Walikuwa wameifuata njia potofu; hawakuwa wamemtambua Yesu wa Nazareti kuwa alikuwa Mwana wa Mungu.

Walipogundua kosa walilofanya, waliwauliza mitume: “Tutendeje, ndugu zetu?” Tunaambiwa: “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu” (Matendo 2:38).

Ubatizo wa mtume Paulo

Mtume Paulo ni mfano mzuri wa kuelezea jinsi ambavyo toba inavyomfikisha mtu katika Ubatizo. Paulo alikuwa akiendelea katika njia mbaya; alikuwa akiwatesa waliokuwa wafuasi wa Yesu. Hakuamini ya kuwa Yesu alikuwa kikweli ni Mwana wa Mungu.

Paulo alipokuwa akisafiri kwenda Dameski kuwakamata na kuwatesa Wakristo huko, Bwana Yesu alimtokea na kusema naye. Paulo alipomwona, alijifikiria tena. Alimtambua sasa Yesu alikuwa ni nani.

Paulo alipokuwa ametambua alivyokosea, aliyatoa maisha yake yote kumfuata Yesu. Yesu alimtuma mfuasi wake mmoja aliyeitwa Anania kwa Paulo, na Anania alimsaidia aweze kuona tena, na kumwagiza abatizwe (Matendo 9:17,18). Kwa hiyo Paulo alipouamini ukweli aliomhusu Yesu, alisikitika kwa mabaya aliyofanya, na kuanza maisha mapya kwa kubatizwa.

Kuna maelezo mengi katika Matendo ya Mitume, ya watu walioamini na kuigeukia njia ya Mungu na wote walibatizwa.

Habari ya towashi wa Kikushi

Hebu isome hii katika Matendo 8:26-40. Huyo towashi alikuwa ni mtu wa heshima; mtu mkubwa. Alikuwa amekwenda Yerusalemu kumwabudu Mungu. Alipokuwa ameondoka kurudi nyumbani, alikuwa akisoma kutoka katika Isaya 53, ambapo mateso na kifo cha Masihi kinaongelewa. Hakuelewa anachosoma; kifungu kilikuwa kinasema:

“Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya. Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi (Matendo 8:32, 33).

Ghafla alijewa na mfuasi aliyekuwa akiitwa Filipo, ambaye Mungu alikuwa amemtuma kumsaidia. Filipo alimuuliza kama alikuwa akielewa alichokuwa akikisoma, na towashi alimjibu, “Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza?”

Filipo alianza kumfafanulia kifungu hicho, na kumhubiria habari za Yesu. Mara walipofika kwenye maji, towashi alimwambia, “Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?”

Hebu liangalie jibu la Filipo kwa umakini. Alimwambia: “Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana”.

Baada ya hapo, tunaambiwa, wakatelemka wote wawili majini (kwa hiyo lisingeweza kuwa jambo la kunyunyizia vimaji). Hapo Filipo alimbatiza huyo towashi. Baada ya hapo tunaambiwa, walipopanda kutoka majini, Filipo alitoweka, na Mkushi huyo akaendelea zake akifurahi. Alikuwa ameigundua Njia ya Uzima.

Habari ya akida wa Kirumi

Hebu isome habari hii katika Matendo 10. Akida Kornelio alikuwa, “Mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima” (ms.1,2).

Unaweza kufikiri hakukuwa na chochote zaidi cha yeye kufanya kwa jinsi alivyokuwa mwema; lakini kilikuwapo. Mungu alimtuma malaika kwa Kornelio, na malaika akamwambia Kornelio amwagizie mtume Petro aje, ambaye, “Atakuambia (Kornelio) yakupasayo kutenda”.

Sasa Petro, akiwa ni Myahudi, asingeweza kamwe kuingia katika nyumba ya mtu wa kimataifa (asiye Myahudi). Lakini Mungu alikuwa amesema naye kwa njia ya maono, na kumwambia aende na watu waliotumwa na Kornelio kwake. Ni Wayahudi tu waliokuwa wameitwa kwa habari ya Injili, mpaka wakati huo.

Petro alipofika nyumbani kwa Kornelio, alimkuta akida huyo akimngojea na familia yake na marafiki. Alimkaribisha Petro na kumwambia juu ya malaika aliyemtembelea, na kumwambia:

“Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana” (ms. 33).

Petro aliwaambia watu waliokuwa hapo juu ya Yesu; maisha yake, kifo na ufufuko wake. Kabla hajamaliza kusema, karama ya Roho Mtakatifu iliyokuwa imetolewa kwa waumini wa Kiyahudi tu, iliwashukia wale waliokuwa pale wakisikiliza. Hakukuwa na shaka sasa kuwa, Mungu alikuwa amewakubali. Kwa hiyo hatua ya muhimu ya lazima ilifuata. Petro alisema:

“Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo” (ms. 47, 48).

Somo linaeleweka: Hata wanaoishi kwa imani; watu wanaomcha Mungu, wanaweza tu kuwa na sehemu katika ushirika na Kikristo kwa kubatizwa. Ujumbe ni kwamba:

  1. Ni lazima  kwanza watu waupate ujumbe wa Injili
  2. Wauamini kwa mioyo yao yote.
  3. Ni lazima waondokane na kufikiri wanavyojifikiria, na watake kuifuata namna ya Mungu.
  4. Ni lazima baada ya hapo wabatizwe.
  5. Kwa kufanya hivyo wanaanza maisha mapya katika Kristo.

Maana ya Ubatizo

“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”

(Warumi 6:4).

Bwana Yesu alisulubiwa na mwili wake ulilazwa kaburini. Baada ya siku tatu, Mungu alimfufua.

Tukielewa kuwa Bwana Yesu aliteseka na kufa kwa ajili yetu, kama tuna hekima, tutasema kama Wayahudi walivyosema katika siku ile ya Pentekoste, “Tutendeje?” Jibu ni lile lile hata leo: “Tubuni, mkabatizwe”.

Maana halisi ya kubatizwa: Kama mwili wa Yesu ulivyolazwa katika kaburi, katika Ubatizo mwili wako unazikwa kwenye maji. Tunakuwa tumezikwa ‘pamoja naye’. Kwa kufanya hivi tunaonesha kukiri kwamba tunastahili kufa kwa sababu ya dhambi zetu, na ni ishara ya kufa na Kristo. Na kama alivyofufuka na kutoka kaburini, nasi tunaibuka katika maji. Huku ni kuzaliwa upya, na kuanza namna ya maisha mapya.

Kuzaliwa upya

Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa Nikodemo, siku moja alikuja kwa Yesu usiku kumuuliza kuhusu mambo anayofundisha. Yesu alimwambia, “Ni lazima uzaliwe tena”. Nikodemo alifikiri hili haliwezekani, na ni kweli ni hivyo, kama ukiyachukua maneno ya Yesu bila kuielewa maana aliyokuwa nayo.

Yesu alikuwa akisemea kuzaliwa upya kunakotokea katika kubatizwa. Alimwambia Nikodemo: “Amini, amini, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia ufalme wa Mungu” (Yohana 3:5).

Kumbuka maneno tuliyoanza nayo: “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa”. Watu wote ni wadhambi, na dhambi inatupeleka kwenye mauti. Kifo ni mwisho wa uhai, na hakuna lolote la kutazamia mbele ya hapo. Hakuna tumaini mpaka tunapokuwa tumezaliwa upya kwa njia ya Ubatizo.

Maisha mapya

Kuamua kubatizwa ni uamuzi wa maana kuliko uamuzi wowote mwingine mtu yeyote anaoweza kuufanya. Sio kitu cha kuchukulia juu-juu tu.

Kabla ya kubatizwa: Ni lazima tuelewe na kuyaamini mafundisho ya kweli ya Biblia.

Baada ya kubatizwa: Ni lazima tupambane na dhambi, na kujitahidi kutii maagizo ya Mungu na kumtumikia.

Tunaweza tu kufanya hili kama tunalisoma Neno la Mungu. Itatubidi tuache kufanya mambo ambayo tunajua yatamchukiza Mungu. Hili litakuwa na maana ya kutumia muda mdogo zaidi na watu wasiomjali Mungu, hata kama walikuwa marafiki wa karibu, kwa kuwa wanaweza kutuvuta mbali na Mungu. Itakuwa ni jitihada za kila siku, lakini itakuletea zawadi nono sana. Bwana Yesu alisema:

“Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele” (Mathayo 19:29).

Muhtasari

  1. Mungu ametuamuru tubatizwe.
  2. Ubatizo ni kuzamishwa (kuzikwa) kwenye maji.
  3. Ni ishara ya kufa na Kristo, na kuibuka katika maji ni mwanzo wa maisha mapya.
  4. Tunapobatizwa tunaanza maisha mapya ‘katika Kristo’ (Warumi 6:3,4).

Vifungu vya kusoma: Soma tena masimulizi katika Matendo 8, 9 na 10. Soma pia Warumi 6.

Mistari wa kushika: Warumi 6:3,4.

“Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”.

Swahili Title
Ubatizo - Somo la 31
English files
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission