Correspondance Course - Lesson 32

Swahili

Somo la 32

NDOA YA KIKRISTO

Somo: 1 Wakorintho 7

Ndoa ni makubaliano ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja kuishi pamoja. Haitoshi tu kuwa na ‘kaya’ moja. Watu hao wawili ni lazima wajioneshe hadharani kuwa wanakuwa mume na mke, kwa hiyo makubaliano yao yanafanywa mbele ya mashahidi. Lakini, ndoa na Kikristo si hivyo tu.

Kwa ndoa ya Kikristo, ahadi wanazotoa wanaooana mbele ya wanaoshuhudia, zinafanywa pia mbele ya Mungu, na zinakuwa za kudumu. Mungu anachukizwa na kuachana (Malaki 2:16). Kama inawezekana, ni vizuri kuisajili hiyo ndoa Serikalini, muweze kupata na cheti cha ndoa.

Mpango wa Mungu ni kwamba mume mmoja na mke mmoja waishi pamoja wakati wote.

  1. Mungu alipomuumba mwanamke awe ‘msaidizi wa kufanana’ na mume (Mwanzo 2:18), alitaka wasaidiane kwa kila mmoja kumjali mwenzake kwa kila hali; kiroho, kimwili na kifikra.
  2. Mungu aliposema ya kuwa wawe ‘mwili mmoja’ (Mwanzo 2:24), alionesha kuwa walipaswa wawe wamoja, mmoja kwa mwingine: waaminifu, wanaoelekeana, wakweli na wanaotegemeana wakati wote.
  3. Mungu alipowabariki Adamu na Hawa na kuwaagiza wazae na kuongezeka (Mwanzo 1:28) alikuwa akionesha kuwa, ndoa iliyo imara inatoa fursa nzuri ya watoto kukulia ndani yake.

Hata hivyo, sio kila mtu analazimika kuoa au kuolewa. Yesu Kristo hakuoa, na pia, kwa kadri tunavyojua, na mtume Paulo naye, ingawa alisema angeweza kuwa na mke kama angetaka. Ukweli ni kwamba, baadhi ya watu wameumbwa kwa namna ambayo wanapendelea kubakia wenyewe, wakati wengine wanapenda kuwa katika ushirika na msaada wa mwenza; wa mume au mke.

Paulo aliwashauri waliokuwa katika Korintho. Aliowaandikia katika kipindi cha matatizo kwa waumini ya kuwa, waoe (au kuolewa) tu kama walikuwa hasa na haja ya kufanya hivyo. Wapo watu ambao wanaweza kumtumikia Mungu vizuri zaidi wasipooa au kuolewa ( 1 Wakor. 7:32-35), wakati wengine wanahitaji wenza (ms. 2-9). Yote yanategemea tulivyo kila mmoja kimwili na kimawazo.

Ndoa ni mpango aliouweka Mungu. Sio njia rahisi ya kumpata mtumishi wa ndani bure, au kumpata mwanamume wa kukutunza. Kuna kanuni muhimu za kujua na za kuzingatia kama ndoa hiyo itakuwa ni ya kupendeza mbele ya Mungu.

Tutazipitia kuanzia mvulana anapofikiria kumpata mke, au msichana anapoamua kutaka kuolewa. Kuna somo la ziada litashughulikia mazingira tofauti yanayoweza kujitokeza, kutokana na mila za ndoa za kijadi na tofauti zingine za kimienendo.

Ngono kabla ya ndoa

Kitu cha kwanza kuelewa ni kwamba, kujamiiana ni kitu alichokiweka Mungu, lakini hapendi tendo hilo lifanyike nje ya ndoa.

Biblia inalaani matumizi mabaya ya ngono. Kufanya mapenzi kabla ya ndoa na nje ya ndoa, umalaya, ufiraji na ubakaji, ni vitendo vinavyoshutumiwa vibaya sana. Sehemu pekee iliyo sahihi na muafaka ya ngono ni kwa waliooana.

Biblia inasema: “Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti….” (1 Wakorintho 6:9,10).

Kama huko nyuma tulikuwa tumefanya mambo hayo ya kijinga, ni lazima sasa tuache, tutubie dhambi hizo, na kumwomba Mungu atusamehe. Kwa kubatizwa kwetu katika jina liokoalo la Yesu, tunaweza kupata mwanzo mpya wa maisha unaompendeza Mungu.

Mapenzi ndani ya ndoa ni tuzo inayotoka kwa Mungu. Ni mbaraka uliowekwa kusudi, pamoja na mengine, wapatikane watoto ndani ya upendo na uangalizi wa baba na mama. Hakuna amri inayosema Wakristo wanapaswa kupata watoto wengi iwezekanavyo; baadhi ya makanisa yanakazia hili tu ili kuongeza idadi ya wafuasi wao.

Wazazi watapaswa kuifikiria hali ya familia yao kabla ya kuamua wapate watoto wangapi. Kama ilivyo kwa mambo mengine katika familia, mume na mke inawabidi wajadili jambo hili na kufikia makubaliano juu ya ukubwa wa familia wanayoitaka. Lakini kufanya mapenzi ni njia pia aliyoitoa Mungu, ya mume na mke kuoneshana upendo walio nao mmoja kwa mwingine, kwa namna iliyo ya kipekee sana (1 Wakorintho 7:3-5).

Kutafuta mume au mke

Wakati mfuasi wa Kristo anapotaka kuoa au kuolewa, atataka amfahamu huyo anayemtaka ni mtu wa namna gani. Biblia inatoa amri iliyo wazi ambayo watu wanapaswa kuitii.

Muumini ni sharti aoe (au aolewe na) muumini

Kama wawili wanawajibika kuishi pamoja kama washirika wa kiroho, ni lazima imani yao iwe moja; mtume Petro anawaita: ‘warithi pamoja na neema ya uzima’ (1 Petro 3:7).

Ni lazima wawe na uelewa wa pamoja wa kile Biblia inachofundisha. Muumini anayeoa (au kuolewa na) asiyeamini, atapata ugumu na migogoro katika ndoa yake. Kwa maneno mtume Paulo aliyopewa na Mungu kuonya, anasema:

“Msifungiwe, nira pamoja na wasioamini” (2 Wakorintho 6:14). Nira ni kitu kinachounganisha pamoja; ni mfano wa ndoa.

Na kuhusiana na wajane, anasema:

“Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu yeyote amtakaye, katika Bwana tu” (1 Wakor. 7:39).

Maisha ya pamoja

Mwanamume Mkristo anayejali, na mwanamke Mkristo anayejituma, ni mbaraka mkubwa kwao wenyewe, na kwa wale wanaomwabudu Mungu pamoja nao. Mume ni lazima ajitahidi kuufuata mfano wa Bwana Yesu Kristo, aliyekuwa kielelezo cha hali ya juu sana cha upendo wa kuwajali wote wale aliowakuta katika maisha.

Mtume Paulo alipokuwa akiwaandikia Waefeso alieleza kuwa, wanaume wanapaswa kuwa na mwenendo katika familia, kama ule Yesu aliokuwa nao kwa wafuasi wake:

“Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe; kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa; naye ni mwokozi wa mwili…..Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Waef. 5:23 – 25).

Kuwa kiongozi wa familia hakuna maana ya kuwa mume anaruhusiwa kujiweka juu ya kila mtu hapo, akitegemea kila kitu kifanywe kulingana na amri zake, na kusikilizwa wakati wote. Hivyo sivyo Yesu alivyowaongoza wanafunzi wake. Yeye alikuwa miongoni mwao kama ‘atumikaye’ (Luka 22:27). Aliyachukulia mahitaji ya wengine kama vile yalikuwa ya muhimu kuliko ya kwake mwenyewe.

Hili lina maana ya kuongoza kwa ‘kuwa mfano’. Mume ana jukumu la kuelekeza na kudhibiti, kusimamia vipengere vyote vinavyohusu maisha ya familia, na kuyaongea mambo na wanafamilia wake kunapokuwa na maamuzi muhimu ya kufanywa.

Muhimu kuliko yote, mume ataiongoza familia yake katika kuabudu na kuifundisha, katika maombi ya familia na usomaji wa Biblia wa kila siku. Kumhusu Ibrahimu, Mungu alimsifu akisema hivi:

“Nimemjua ya kwamba ataamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu” (Mwanzo 18:19).

Kwa hiyo mume ni lazima ajichukulie mwenyewe kuwa ni mkuu juu ya familia yake, anayewajibika juu ya maisha yao mbele ya Mungu, na aichukulie nyumba yake kama ni kanisa dogo (na kweli, kama hakuna waumini wengine katika mazingira hayo, hiyo ndio fursa pekee atakayokuwa nayo ya kuweza kumwabudu Mungu akiwa na wengine).

Anapaswa kuishirikisha familia yake katika ibada na kuiongoza katika Njia za Mungu; ingawa ni wale tu waliobatizwa watakaoshiriki naye mkate na divai.

Katika baadhi ya nchi, mifumo wa maisha ya kazi, kimila, iko katika namna ambayo wanawake (‘wake’) katika familia ndio wanaofanya kazi ngumu karibu zote. Ndoa ya Kikristo ni ushirika, na mume anayependa kuzishika amri za Mungu, atapenda kushiriki katika kazi zote ngumu katika maisha na mke wake na familia.

Atapenda, “Kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu” (1 Petro 3:7), na kumpenda kama anavyojipenda mwenyewe (Waefeso 5:28). Namna hii ya ushirika wa kiroho unaofanya kazi, utakuwa kitu cha furaha kwa familia yote. Kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana katika majukumu, kutakuwa pia ni njia nzuri sana ya kuwaonesha majirani jinsi Ukristo wa kweli ulivyo.

Mke Mkristo

Mpaka sasa tumeangalia wajibu na majukumu ya mwanamume (‘mume’) Mkristo, lakini anaweza tu kuyafanya mambo hayo kwa mafanikio kama ana mke aliye tayari kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kunaweza kusiwe na wanawake/wasichana wanaoamini wanaoishi karibu, kwa hiyo anayetaka ‘kuwa mume’ atalazimika kumtafuta ‘mwenza’ mwenye kupenda kujifunza Injili ya kweli, aliye tayari kuipokea njia ya wokovu inayofundishwa katika Biblia, kwa kuamini na kubatizwa. Baadhi ya wasomaji wa masomo haya watakuwa wameshaoa (au kuolewa na) wenza ambao hawajifunzi nao mafundisho haya; hili ni jambo tutakaloliangalia katika somo linalokuja.

Lakini mtu anayetafuta mchumba wa kuoa atakuwa ameelewa haja ya kupata mwenza mwenye mwamko wa mambo ya kiroho, mwanamke atakayeweza kushirikiana naye katika mambo yote ya maisha yake katika Kristo. Ni hivyo hivyo pia kwa mwanamke au msichana Mkristo anayetaka kuolewa.

Hawa aliumbwa awe msaidizi wa kumfaa Adamu, na huu ni mpango ambao wanawake walioolewa wote wanapaswa kuufuata. Kuna picha nzuri ya ajabu inayomhusu ‘mke mwema’ katika Methali 31. Anasemewa kuwa ni mke ambaye moyo wa mumewe humwamini, na ambaye, “Humtendea (mumewe) mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake” (Meth. 31:11,12). Anakuwa mchapa–kazi kwa ajili yake mwenyewe na familia yake, na mkarimu na mwelewa, na muhimu zaidi, ni “Mwanamke amchaye BWANA” (ms. 30).

Wanawake wengi waaminifu katika Maandiko waliishi kwa namna hiyo. Waliwatia moyo na kuwasaidia waume zao, huku wakiwaachia wawaongoze. Sara alikuwa miongoni mwao, na alijinyenyekeza kwa Ibrahimu, kiasi kwamba alimchukulia kuwa ni ‘Bwana’ wake, kwa kumtii katika mambo yote (1 Petro 3: 1-6). Mume naye asiitumie vibaya heshima hiyo. Katika familia ya Kikristo, yeye na mke wake ni: “Warithi pamoja wa neema ya uzima” (ms. 7).

Mtume Paulo alimuagiza Tito na wazee wa kike:

“Wawatie wanawake vijana akili (‘wawafundishe’), wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe” (Tito 2:4, 5).

Inawezekana kuwa ajabu kuwataka wanawake wawapende waume zao, lakini hili sio jambo ambalo wana-ndoa wote wanafanikiwa. Wapo wanaoishi pamoja kwa kujinufaisha tu wenyewe na kupata watoto, lakini mara nyingi si hasa kama wanapendana, na wala hawafanikishi kuwalea watoto wao vyema.

Lakini, maisha katika familia ya Kikristo yanamshirikisha Mungu. Kwa ajili hiyo, wakina-mama wana jukumu la kutekeleza katika kuonesha upendo kwa familia nzima; mguso-wa-upole ambao ni wao tu wanaoweza kuutoa, katika kuelekeza kwa ukaribu na kuwafundisha watoto, na hasa wanapokuwa wadogo. Andiko linasema, mzazi ana wajibu wa kumlea: “Mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (Methali 22:6).

Hili ni adili la Ki-mungu: Wanandoa wanaoamini, wanaishiriki mibaraka waliyopewa na Mungu, huku wakiilea familia yao kukua katika kuijua kweli ya Mungu. Kwa namna hiyo, watoto wao na wao, wote watakuwa mbaraka kwa wote watakaokutana nao. Katika maisha yao ya pamoja na ya furaha katika Kristo, wengine wataona mbaraka mkubwa wanaoufurahia, na hivyo Mungu atatukuzwa katika mambo yao yote.

Muhtasari

  1. Ndoa imewekwa na Mungu, na ni kitu kizuri na cha haki.
  2. Wapo watu wanaoridhika kubaki wenyewe, na hili pia ni zuri na la haki. Kukaa hivyo kunaweza kumwongezea mtu fursa ya kumtumikia zaidi Mungu.
  3. Kufanya mapenzi ni mbaraka wa Mungu, lakini ni ruhusa tu kwa mume na mke.
  4. Ngono nje (au kabla) ya ndoa ni dhambi; ni lazima iepukwe.
  5. Ndoa inaruhusiwa tu kufanywa na mtu aliye wa imani yako; muumini aliyebatizwa.
  6. Waume wanapaswa kuwatunza wake zao na watoto wao, na kuongoza familia zao katika mambo yote, na hasa katika ibada kwa Mungu, kusoma Biblia na kuomba.
  7. Wanawake (‘wake’) ni lazima wawatii waume zao na kuziongoza familia zao katika Njia za Mungu.

Vifungu vya kusoma: Waefeso 5, Methali 31:10-31, Timotheo 3, Wakolosai 3:12-25.

Mistari wa kushika: Mathayo 19:5,6

“Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe”.

 

Swahili Title
Ndoa ya Kikristo - Somo la 32
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission