Correspondance Course - Lesson 33

Swahili

Somo la 33

MATATIZO KATIKA NDOA

Somo: Mathayo 19

Mpango wa Mungu kwa ndoa ya Kikristo ni kwa waumini wawili, wa kike na wa kiume, kuishi pamoja kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Lakini, kwa sababu ya mazingira yanayojitokeza, imekuwa sio rahisi wakati wote kulifikia lengo hilo. Matatizo yanatokea, na somo hili linayatazama baadhi; yaliyozoeleka sana. Tunakushauri uwasiliane na mkufunzi wako, kuweza kupata msaada zaidi wa kibinafsi juu ya haya na shida zingine.

Ndoa na Asiyeamini

Muumini ni lazima aoe au aolewe na aliye muumini (2 Wakorintho 6:14). Lakini ni vipi kuwahusu wale ambao wanakuwa wamekwishaoa au kuolewa wakati wanapokuja kulielewa kusudi la Mungu? Watengane, au waendelee kuishi na wenza wao wasioamini?

Hili lilikuwa ni tatizo la kawaida katika karne ya kwanza. Kwa kadri Injili ilivyohubiriwa na watu kuja kuisikia na kuiamini, walibatizwa katika Jina liokoalo la Yesu. Lakini, mara nyingi familia zao zilibakia katika kutokuamini na kulitokea migawanyiko ndani ya familia. Linapotokea hilo inakuwaje; waumini wanajitenga na kutawanyika, au wanaendelea kukaa hapo na kusuluhisha migogoro yao?

Ushauri wa Agano Jipya unaonesha jinsi maisha ya ndoa yalivyo ya muhimu mbele ya Mungu. Tunapooa au kuolewa, tunakuwa na wajibu juu ya wengine. Ni kosa kuwaacha hao; badala yake ni wajibu kujitahidi kuifanya ndoa iendelee, na kuyaweka mambo tunayoamini katika matendo ndani ya familia.

Kwa hiyo, Biblia inatuambia tuendelee na maisha pamoja na wenza wetu kama tunaweza, na kwa mwenendo wetu wa Kikristo tunaweza kuwaonesha waume zetu au wake zetu vile upendo wa Mungu ulivyo, katika Kristo Yesu. Maandiko yanasema:

 

“Ninyi wake, watiini waume zenu kusudi, ikiwa wako wasioamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu (wa kumcha Mungu)”       (1 Petro 3:1, 2).

 

“Mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe. Kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu. Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke” (1 Wakorintho 7:13-15).

 

Maandiko yanatufundisha kuwa, kila linalowezekana lifanywe kuwafanya waliooana waendelee na maisha ya pamoja.

Mungu atachukuliaje? Tunajifunza kuwa, Mungu atachukulia ndoa ile iliyofanywa kabla yeyote kati yao hajaufahamu ukweli wa Kibiblia, kuwa ni mahusiano matakatifu, na watoto hatawachukulia vibaya. Changamoto ni jinsi ya kujaribu kuueneza ukweli wa Kikristo ndani ya familia, kwa aliyeamini kuwa kielelezo cha mwenendo mwema kibinafsi.

Kama matatizo ndani ya ndoa yanajitokeza, ni muhimu yakabiliwe kiusahihi kwa kukumbuka kuwa, kuna wajibu katika mazingira yoyote yale, kuifanya ndoa iendelee. Hili lina maana ya kukubali jambo, hata kama haliridhishi sana. Hivi ndivyo Yesu alivyofanya alipokufa ili tuweze kupata tumaini la wokovu.

Biblia inalinganisha ndoa na uhusiano uliopo kati ya Kristo na kanisa (Wakristo), kwa hiyo mfano wake unaweza kutupa nguvu matatizo yanapozuka. Talaka inaonekana haraka kama suluhu mambo yanapokuwa magumu, lakini ni lazima kukumbuka kabla ya kuchukua hatua kama hiyo kuwa, Mungu amesema:

“Mimi nakuchukia kuachana” (Malaki 2:16)

Ndoa kati ya Waumini

Mungu alipanga ndoa iwe ni mahusiano ya kudumu maisha yote. Ahadi katika kuoana hazifanywi ili zivunjwe; ni ahadi za kudumu kwa maisha yote kwa wanandoa. Mmojawao katika ndoa anapokufa, mwenzake aliyebaki anakuwa huru kuoa au kuolewa tena (Warumi 7:2, 3).

Kanuni ya kipekee iliyo tofauti inakuja tu pale mmojawao anapokuwa sio mwaminifu kwa mambo ya ngono. Kuna wakati Bwana Yesu aliulizwa alikuwa akifikiri nini kuhusu ndugu zake Wayahudi walivyokuwa wakitoa talaka (pengine kirahisi). Waliomuuliza walitaka kujua kama Yesu alifikiri ndoa iliyofutwa ilikuwa imefutwa hivyo mbele ya Mungu.

Bwana Yesu aliwarejesha wasikilizaji wake kwenye ndoa ya kwanza kabisa, kwenye Kitabu cha Mwanzo, Sura ya pili na kuwakumbusha kinachosemwa, kuwa: “Aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Mathayo 19:6). Tunaona hapa ya kuwa, Mungu anachukulia ndoa kama kitu kilichoungwa. Alipoendelea kuulizwa, Yesu alisema:

“Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini” (ms. 9).

Ndoa ya waumini wa Kikristo, kwa hiyo, ni ya kudumu maisha yote. Kama mmojawao anakuwa mzinzi; anafanya mapenzi na mtu mwingine, ndoa yao inahatarika. Lakini ni muhimu bado kujaribu kuifanya iendelee.

Nabii Hosea alikuwa na mke asiyekuwa mwaminifu, lakini alijitahidi sana kumrudisha amrudie. Tunapaswa kukumbuka kuwa, ni lazima tuwe tayari kusamehe baya alilofanya mweza wetu kinyume na sisi, kama tunataka Mungu naye atusamehe tunapofanya mabaya kinyume chake.

Kama mwenza asiye mwaminifu hawezi kurudi, na hatimaye kunakuwa na kuachana, lazima hatua zichukuliwe kuhakikisha athari zake zinakuwa ndogo kwa wengine kwenye familia hiyo. Kama mwanandoa anafariki na aliyebaki anaona inawezekana na inafaa kuishi mwenyewe, ni vizuri zaidi asioe au kuolewa tena.

Matala

Wanaume wengi, hasa katika nchi za Kiislamu na kwa mila za Kiafrika, wanaweza kuwa ni wake wengi, wanapoupokea ujumbe wa Injili ya Kikristo. Wafanye nini: wajitenge na wake zao au waendelee nao? Ndoa za wake wengi (matala), zilikuwepo pia enzi za kale kwenye Biblia.

Mfalme Daudi alikuwa na wake kadhaa. Mfalme Sulemani alikuwa na mamia ya wanawake na mahawara. Lakini mpango wa Mungu umekuwa wakati wote ukitambulika: Mungu alikusudia mume mmoja kwa mke mmoja waishi pamoja kama mume na mke.

Wakati wote mambo mengine yalipofanyika, mara nyingi yamesababisha zaidi matatizo na kuleta huzuni. Yesu aliweka wazi kuwa, ipo sasa njia ya namna moja tu inayokubalika ya kuishi pamoja, kwa kusema:

“Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja” (Mathayo 19:5).

Kwa hiyo, hakuna anayeweza kuchukua zaidi ya mke mmoja baada ya kuwa amebatizwa katika Kristo. Je, wale ambao wanao tayari wake kadhaa, inakuwaje? Ushauri wetu ni kuwa, yeyote ambaye anao wake zaidi ya mmoja, aendelee nao; atambue kuwa bado anawajibika kwao wote. Aendelee kuwa mume mwema kwao na baba wa watu wake wote wanaomtegemea.

Wakristo hawaachi au kukwepa majukumu yao wanapobatizwa; wanajikuta wakiwajibika hata zaidi kwa wategemezi wao. Hata hivyo, Ushirika wetu wa kueneza Injili wa Kikristadelfia (CBM) unashauri kuwa, kwa kuwa matala hayaendani sawasawa na maadili ya Kikristo, ndugu aliyeko kwenye matala hastahili kuwa ‘mzee-kiongozi” kwenye kusanyiko la Kikristadelfia.

Harusi

Matatizo yanaweza kutokea kama inafikiriwa kuwa sherehe kubwa ya harusi ni ya lazima, wakati vijana wenyewe ni wadogo hawajawa na kitu. Hii ndio sababu katika nchi kadhaa watu wanaishi pamoja nje ya ndoa, wakitegemea kufunga ndoa watakapopata uwezo, lakini mara nyingi hawaufikii; na kwa wakati huo watoto wao wanawazaa nje ya ndoa, katika mfumo usioeleweka. Muumini afanye nini?

“Muumini anapaswa kuoa au kuolewa kabla hajaanza kuishi na mwenzake. Kufanya mapenzi kabla ya ndoa ni dhambi. Biblia inasema: “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu” (Waebrania 13:4).

Kitu kinachohitajika tu ni kisherehe kidogo katika kumshirikisha Mungu, familia na marafiki, washuhudie kwamba watu wawili hao wameoana. Kama inawezekana mwende mkaisajili ndoa hiyo Bomani (Serikalini), na kupata vyeti vya ndoa. Hakuna haja ya kuwa na vitu vya gharama kuhusiana na vyakula vinavyoliwa au mavazi, na haijalishi ni wapi sherehe inapofanyikia.

Popote palipo na nafasi ya kutosha kuingiza hao watu wanaokuja kushuhudia, panatosha. Epuka kwenda kanisani kuoana na mtu ambaye hayaelewi mafundisho ya kweli ya Biblia. Ahadi zinazotolewa mbele ya mashahidi, zinamaanisha kwamba wanandoa hao wataishi pamoja mbele ya Mungu kwa maisha yao yote. Usihusishe jambo hili la Kikristo na kanuni za ndoa zenye misingi yake katika upagani. Mkristo anapaswa kuachana na mambo ya kipagani.

Kunakuwa mara nyingine na matatizo kuhusiana na mahari kuwa kubwa, na inaweza kuchukua muda kwa kijana wa kiume kuweka pesa mpaka zitoshe kwa ajili ya msichana aliyemchagua. Kama anamwoa msichana kutoka katika familia ya Kikristo, hawapaswi kwa vyovyote kumtoza mahari ya juu, badala yake watapenda wawatie moyo wanandoa hao wanaooana, waweze kuanza maisha yao ya pamoja bila ya matatizo mengi. 

Lakini kama mahari ni kubwa, hakuna la kufanya isipokuwa ni kwa mvulana anayeoa kusubiri mpaka atakapokuwa na mahari inayotakiwa. Kwa wakati huo, yeye na mwenzake wanapaswa wabakie wasafi, wakijichunga na kuusubiria wakati watakapoweza kuoana.

Kutafuta mume au mke mzuri

Tatizo lililo gumu kuliko yote linaweza likawa kumpata mume au mke wa Kikristo anayefaa, na hasa kama wako waumini wachache tu wanaoishi katika mazingira husika. Kitu cha kwanza kukumbuka ni kwamba, ni hali ya kiroho ya huyo unayemtaka kuwa naye iliyo ya muhimu zaidi; zaidi kuliko anavyoonekana au mali aliyonayo. Mungu huutazama moyo, na sio sura ya nje, na sisi ndivyo tunavyopaswa kutazama (1 Samweli 16:7).

Ni lazima tuoe au kuolewa na mwenzetu wa imani moja; muumini aliyebatizwa.

Uchaguzi wa mume au mke unapaswa ufanywe kuwa jambo la maombi ya dhati. Ibrahimu alipata usumbufu mkubwa kwa ajili ya kumpatia Isaka mke anayemfaa, na tunaweza, kwa kuwa waangalifu, tukalazimika kufanya kama alivyofanya Ibrahimu; kwenda mbali.

Mbaraka kutoka kwa Mungu.

Ndoa ya Kikristo sio kitu cha matatizo tu yanayongojea kutatuliwa, ingawa katika somo hili tumejadili matatizo kawaida yanayojitokeza. Kuoana, kwa upande mwingine, ni mbaraka mkubwa unaotoka kwa Mungu, wa kufurahiwa kwa pamoja.

Maisha ya kifamilia, kama watu wanayaelewa na kuyaishi inavyotakiwa, yana mazuri mengi na yanaweza kufanikisha mengi. Kwa sababu hiyo, ujio wa pili wa Yesu, anapokuja kuusimamisha Ufalme wa Mungu duniani, unafananishwa katika Maandiko na kuanza kwa maisha ya ndoa ya Kikristo. Andiko linasema:

“Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa harusi ya Mwana-kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari” (Ufunuo 19:7).

Muhtasari

  1. Kusudi la ndoa ni kuwaweka pamoja mwanamume anayeamini na mwanamke anayeamini, waishi pamoja kwa maisha yao yote. Tafuta ‘mwenza’ anayeamini!
  2. Kama tumekwishaoa au kuolewa wakati tunapompokea Kristo, ni lazima tubakie na wenza wetu na kujaribu kuwaonesha Njia ya Mungu.
  3. Ahadi tunazopeana wakati wa kufunga ndoa sio kitu cha mzaha, na ni lazima ziheshimiwe. Kama baada ya jitihada kubwa bado ndoa inakwama, ushauri ni lazima utafutwe kwa wazee kwenye Eklesia au kwa wakufunzi.
  4. Kwa wale wanaooa, mume mmoja kwa mke mmoja ndivyo inavyotakiwa. Endapo mwanamume ameshakuwa na zaidi ya mke mmoja wakati anapokata shauri, basi ni lazima abakie katika uaminifu kwa kuendelea kuwa mume wa wake zake wote. Asiongeze mke au wake wengine.
  5. Oa au olewa kisheria mbele ya Mungu; mbele ya mashahidi, hata kama unachoweza kumudu ni kasherehe kadogo tu.

Vifungu vya kusoma: Mwanzo 24,  Mathayo 5:31,32,  Zaburi 128, 1 Timotheo 2.

Msitari wa kushika: Waebrania 13:4

“Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”.

Swahili Title
Matatizo katika Ndoa - Somo la 33
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission