Somo la 34
WAJIBU WETU KWA TAIFA
Somo: 1 Petro 2
|
Angalizo: |
Taifa ni nchi tunayoishi ndani yake (ambayo ndani yake kuna viongozi wake, sheria na taratibu zake). |
Kwa nyakati zote katika historia, Mungu amekuwa akijiandalia watu ambao wanaelewa makusudi yake, na ambao watakuwa washiriki wa mibaraka ya Ufalme wake na kuufurahia Uzima wa Milele. Kwa nyakati za nyuma katika Agano la Kale, watu hao walikuwa wakiishi kama taifa moja ambalo ni Taifa la Israeli, na Mungu alikuwa ndiye Mfalme wao.
Kwa wakati huo hapakuwa na tatizo kati ya taifa na wananchi wake, kwa kuwa wote walikuwa wakihesabiwa kuwa ni waumini. Mambo yalibadilika, na sasa tunahitaji kutafakari wajibu wa Mkristo kwa nchi yake, na hasa kuhusiana na mambo ya kisiasa na vita.
Watu wa Mungu
Mungu bado anaendelea kujiandalia watu, na sasa ni kutoka katika mataifa yote. Ni watu watakaokuwa wa muhimu sana kwa ajili ya mpango wake wa kuweka Ufalme wake katika dunia nzima. Mtume Yohana aliona kwa njia ya maono umati huo, na anauelezea kuwa, ulikuwa ni:
âMkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao, wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwanakondooâ (Ufunuo 7:9,10).
Watu hao watakusanywa pamoja, wakati wa kurudi kwa Bwana Yesu Kristo duniani, kuanzisha âtaifaâ jipya; taifa lake Mungu mwenyewe, na watatawala pamoja na Mfalme Yesu kwa miaka 1000 ya Ufalme huo katika dunia (Ufunuo 5:9, 10; 20:4).
Ufalme wa Mungu uliwahi kuwepo miaka mingi zamani, wakati wafalme walipotawala wakikikalia Kiti cha Enzi katika Yerusalemu na kutawala juu ya Israeli. Hili litatokea tena hapo Mfalme Yesu atakaporudi (Matendo 1:6; Luka 1:32, 33).
Ufalme wa Mungu (nyakati za kale)
Miaka 3,500 iliyopita katika Mlima Sinai, Mungu aliwakusanya wana wa Israeli, waliokuwa ndio wametoroka tu kutoka Misri, na kufanya agano nao (kitu kama makubaliano). Walikuwa waishike Sheria aliyowapa kupitia kwa Musa, baada ya hapo wangeirithi nchi ya Kanaani; ambayo ni nchi ya Israeli (Kutoka 19:1-8).
Sheria za Mungu zilikuwa ndizo Sheria za kuliongoza taifa hilo. Baadaye, Mungu aliteua wafalme kwa ajili ya watu wake. Jeshi la mfalme, lilikuwa ni jeshi la Mungu, na vita vyake vilikuwa ni vita vya Mungu. Mfalme alikuwa hapo kwa ajili ya kufanya Mungu aliyomuamuru.
Baadaye haya yote yalibadilika. Wafalme waliisahau Sheria ya Mungu na kufuata mifano mibaya ya mataifa yaliyowazunguka, na hatimaye, Mungu aliamua kuusitisha Ufalme wake huo katika dunia. Kwa kuanzia, taifa la Ashuru lilibeba mateka makabila ya kaskazini ya Israeli (Ufalme wa Israeli), na baadaye Babeli iliuchukua mateka Ufalme wa kusini; Ufalme wa Yuda.
Watu hao walivyosambaa walikuwa wakimbizi wasio na kwao. Walijikuta wakiishi katika nchi zilizoabudu miungu wengine, ambayo sheria zao mara nyingi zilikuwa zikipingana na hizo za Mungu mmoja aliye wa kweli; Mungu wa Waisraeli.
Jinsi walivyoishi katika mazingira hayo kuna umuhimu mkubwa kwetu kuelewa, kwa kuwa wale wanaokuwa watu wa Mungu kwa sasa, wanaweza nao kukabiliwa na changamoto za namna ya kuishi katika nchi walimo, zilizo na sheria ngumu na mambo yanayofanywa.
Kumtii Mungu au mwanadamu?
Uzoefu wa Danieli na marafiki zake unatupa kielelezo kizuri cha namna ya kuishi katika mataifa tunamoishi kwa sasa. Walikuwa wamebebwa mateka na mfalme Nebukadreza wa Babeli alipoivamia na kuishinda Yerusalemu, kama miaka 600 Kabla ya Kristo. Kuanzia mwanzo wa maisha yao katika nchi ya kigeni, walionesha kutaka kumweka Mungu mbele katika maisha yao. Hebu tuone mifano ifuatayo:
|
TATIZO |
KILE DANIELI NA/AU RAFIKI ZAKE WALICHOFANYA |
KILICHOTOKEA MWISHONI |
|
Danieli na rafiki zake walipewa chakula ambacho iliwezekana kilikuwa kimetolewa sadaka kwa sanamu (nyama iliyotambikiwa). Hawakukubali kuila, ingawa walijua hili lingemuudhi mfalme na maafisa wake. |
Hawakuila ile nyama, badala yake waliomba wapewe mboga za majani. |
Mungu aliwatunza na wakaonekana kuwa na afya bora kuliko wale wengine waliokula nyama (Dan. 1:15-17). |
|
Nebukadreza aliwaamuru watu wote wawe wakiinama na kuisujudia sanamu aliyoisimamisha. |
Marafiki watatu wa Danieli waligoma kuabudu kitu kingine chochote, ila Mungu tu. |
Walitupwa ndani ya tanuru la moto, lakini Mungu aliwaokoa na hawakudhurika. |
|
Maadui wa Danieli walitaka kumwangamiza, kwa kumshawishi mfalme mpya, mfalme Dario, apige marufuku maombi yote, mpaka yanapokuwa yameelekezwa kwake. |
Danieli aliendelea kufanya alivyokuwa akifanya. Alimwomba Mungu madirisha yake yakiwa wazi. |
Danieli alitupwa katika tundu la simba, lakini Mungu alimwokoa na hakudhurika. |
Hii mifano inatufundisha:
- Kumweka Mungu mbele katika maisha yetu.
- Kushikamana na imani yetu na kamwe tusirubuniwe.
- Kwamba Mungu peke yake ndiye wa kuabudiwa.
Lakini Danieli na marafiki zake hawakuwa watu wanaojitafutia matatizo. Hawakuwa wakitafuta fursa za kuzivunja sheria zinapoendana na Sheria za Mungu. Walikuwa watu watiifu sana kwa sheria, na walionekana bora kabisa kati ya watumishi wa mfalme na hata wakawa maafisa wakubwa kabisa serikalini, wakisimamia kazi za mfalme.
Huu ni mfano wa muhimu sana, kwa wote wale wanaomfuata Bwana Yesu Kristo. Pale sheria ya nchi inapoendana na Sheria ya Mungu, nasi tunapaswa tuwe watu tunaoitii sheria za nchi. Sheria nyingi za nchi mara nyingi zinakuwa zinakwenda sawa na Sheria za Mungu. Kama Danieli, ni wazi nasi tutaonekana hakuna kosa kwetu kulingana na tunayofanya (Danieli 6:4, 5).
|
Wakristo ni lazima wazitii sheria za nchi zao, mpaka pale sheria hizo zinapokwenda kinyume na Sheria za Mungu. |
Ufalme wa Mungu: katika siku za Yesu
Kwa miaka kama 2000, watu wa Mungu wameishi katika nchi zilizo na sheria na mawazo yake zenyewe. Ilikuwa hivyo hivyo kwa Bwana Yesu mwenyewe: aliishi Israeli kwa wakati ambao taifa lake lilikuwa nchi ya utawala wa Kirumi, na ni kwa sheria zao aliteswa na kufa.
Lakini kamwe hakuwa mchochezi wa kisiasa, ingawa wengi kati ya Wayahudi wenzake walifikiri angekuwa. Hakujaribu kuiondoa mamlaka ya Kiyahudi iliyokuwa ikitawala, iliyokuwa ikitumia vibaya nafasi yake katika maongozi ya hekalu na katika mambo mengine. Na hakutaka kuwapindua Warumi.
Akiwa ameulizwa wakati fulani vile alivyokuwa akiiona mamlaka ya Kirumi, Yesu alionesha jinsi sarafu ya Warumi ilivyokuwa na picha ya Kaisari; aliyekuwa Mfalme Mkuu wa Warumi. Kwa kuitumia hiyo sarafu, aliweka kanuni ya muhimu sana, akisema:
âMpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Munguâ (Mathayo 22:21).
Hili lina maana kuwa, ni lazima tulipe kodi zetu kama sheria inavyotaka. Paulo naye analiweka hilo wazi katika Warumi 13:7.
Tunatakiwa pia tufanye kila kitu tunachoamriwa, mradi hakipingani na matakwa ya Sheria ya Mungu. Kuna kutofautisha kwa muhimu hapa, na ni utofauti uliooneshwa kwanza na Bwana Yesu mwenyewe. Mara zote alimpa Mungu yaliyo ya Mungu, na sisi tunapaswa kufanya hivyo.
Watawala wa Kiyahudi walijaribu kumzuia Yesu asifundishe na kuponya, lakini Yesu hakuacha. Hata wakati ilipokuwa dhahiri kuwa anawaudhi na maisha yake kuwa hatarini, aliendelea na kazi yake ya wokovu. Sababu ni kuwa, Yesu alijua hiyo ilikuwa ni Kazi ya Mungu, na hilo lilikuwa ni kipau-mbele cha kwanza.
Wakati, hatimaye, Yesu aliposimama mbele ya Pontio Pilato, hali akiwa na fursa ya kuweza kusuluhisha tatizo lake na kujiokoa, aliweka hoja ya msingi wazi. Kwanza alimweleza huyo mtawala wa Kirumi pale kuwa: ingawa yeye, Yesu, alikuwa ni Mfalme, Ufalme wake ulikuwa bado haujaja. Alisema:
âUfalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapaâ (Yohana 18:36).
Ni wazi kabisa Yesu alikuwa akifundisha kuwa, ungefika wakati ambao Ufalme wake ungesimikwa katika ulimwengu huu. Huu ndio wakati tunaoungoja, atakapoitawala dunia kwa mamlaka kutoka Yerusalemu. Wakati huo ulikuwa bado haujafika, na mpaka sasa bado.
Lakini hoja ya pili ya Yesu kwa Pilato ilikuwa kwamba, Mungu alikuwa bado anadhibiti mambo. Nyuma ya matukio yale yanayokuwa yakitokea, alikuwa akiyaelekeza mambo kufanya mapenzi yake yatimie. Alimwambia mtawala huyo wa Kirumi: âWewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juuâ (Yohana 19:11).
Mfano huo wa kiuaminifu wa Bwana Yesu ulifuatwa na mitume. Nao pia walikuwa wakweli; raia waliozitii sheria za nchi. Kamwe hawakujihusisha na mambo ya kisiasa. Walijiweka mbali na taasisi za kitaifa, jeshi la Kirumi, na mamlaka zilizoshughulikia utoaji wa haki. Walikuwa wamejitoa kwa kazi ya Bwana.
Kulipotokea migogoro kati yao na mamlaka za Kiyahudi au za Kirumi, walifanya nini? Walichofanya ni kumweka Mungu mbele na kutii mwongozo wake. Kwa hiyo, mitume walipoamriwa waache kumhubiri Yesu na Habari Njema ya wokovu, walichosema ni: âImetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamuâ (Matendo 5:29).
Ufalme wa Mungu: kwa sasa
Mafundisho haya na mifano ni msaada mkubwa sana kwetu katika kuamua tuishi kwa namna gani, tukiwa ni raia wa nchi zetu, zinazotutaka tufanye mambo yake kadhaa magumu. Kama wafuasi wa Bwana Yesu, kuna mambo kadhaa tunayopaswa tujitenge nayo kabisa, na ajira fulani-fulani tunazopaswa kuziepuka. Tunapaswa kuepusha au kupunguza migongano ambayo inaweza kutupata katika kuitekeleza Sheria ya Mungu na hizo zilizoundwa na watu.
Mungu anawahesabu waumini-wa-kweli kuwa ni sehemu ya watu wake. Unaposoma 1 Petro 2 utagundua kuwa, lugha mwanzoni aliyoitumia Mungu kwa Israeli katika Kutoka 19, imekuwa lugha sasa ambayo Mungu anaitumia akiwazungumzia waumini wa Kikristo; wanaoitwa sasa: âMzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Munguâ (1 Petro 2:9).
Ni jukumu lao kuishi katika njia ambayo inamtukuza Mungu. Unaona hapa ya kuwa, wamekuwa âtaifaâ kwa namna yao iliyo tofauti; ingawa tunajua wametawanyika kati ya mataifa mengi wanamoishi.
Kujitenga na dunia
Waumini ambao kwa sasa wamekuwa sehemu ya taifa la Mungu, (au Ufalme wake), wanamngojea Mfalme wao kurudi katika Yerusalemu. Katika kuja kwake, atawaita pamoja waumini hao kutoa huduma na kufanya kazi pamoja naye. Kwa sababu hiyo, ni sharti wasifanye kitu ambacho kitauharibu uhusiano wao na Mungu mpaka Kristo atakapokuja. Mungu ni lazima awe wa kwanza katika mambo yote wanayofanya.
Hata hivyo, ingawa Mungu yuko kazini nyuma ya matukio yanayotokea ili kukamilisha mpango wake, haiwi wazi wakati wote itakavyokuwa, na watu na mataifa Mungu atakavyoyatumia.
Kwa hiyo basi, ni kosa kujihusisha na mifumo ya serikali za kiwanadamu, katika siasa zake za kimitaa au kitaifa. Watu wa Mungu ni watu wa mpango wake Mungu, na tayari wana Mfalme wao ambaye ni Bwana Yesu Kristo. Ni makosa kujaribu kutumia mifumo ya kisiasa ya watu, kujaribu kuifanya dunia iwe mahali pazuri zaidi. Mungu atalifanya hilo Yesu atakaporudi. Kwa hiyo Mkristo wa kweli atajitenga; atajiepusha na siasa. Hataichangamkia na hatapiga kura.
Kwa namna hiyo hiyo, ni lazima kujiweka mbali na mazingira ambayo hayafai kwa mfuasi wa Kristo; kama kufanya kazi ya kutengeneza silaha za hatari au milipuko. Kufanya kiapo cha uti kwa taifa au kwa mtawala wa kidunia nako ni lazima kuepukwe. Kama tulivyoona, Mkristo atakuwa mtii kwa sheria za nchi lakini kama kutakuwa na utata, achaguzi wake hatimaye atakuwa kushikamana na Yesu.
Kujiunga na jeshi la Polisi au jeshi la Ulinzi sio kitu kizuri pia; ni kazi za kutumia nguvu na kuua. Wale ambao tayari wamekuwa maaskari kabla hawajaja kulielewa hili, watahitaji kumwomba Mungu juu ya jambo hili na kuomba ushauri kutoka kwa wakufunzi wao. Mungu anaweza kumfungulia mtu njia nyingine katika shida zake zote.
Ni vizuri ieleweke vizuri kuwa, haja ya kujitenga na siasa na kazi mbaya, hakuna maana ya kuwa siasa na kazi nyingine za taifa husika ni mbaya. Hizi ni kanuni zinazowahusu kwa namna hiyo hiyo waumini wengine kila mahali. Wapo sasa chini ya âSheria ya Kristoâ (1 Wakor. 9:21) na ni lazima waishi inavyotakiwa. Mtume Paulo alisema juu ya muindo yote ya kidunia:
âTokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana, msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribishaâ (2 Wakor. 6:17).
Kujitenga kwetu na namna na mambo ya serikali za kibinadamu ni sehemu ya kuitwa kwetu tutoke katika dunia, ili tuweze kikweli kuwa watu wa Mungu.
|
Muhtasari
|
Mistari ya kusoma: Danieli 3 na 4; Warumi 13; Mathayo 22:15-22.
Mistari ya kushika: 1 Petro 2:9-11
âNinyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu, mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipinganazo na rohoâ.