Correspondance Course - Lesson 36

Swahili

Somo la 36

KUTEMBEA KATIKA NJIA MPYA YA UZIMA

Somo: Warumi 6

Mwanzo mpya

Tunapobatizwa, tunaanza maisha mapya. Tunakuwa, “tulizikwa pamoja naye (Kristo) katika mauti yake”, wakati tulipotumbukizwa katika maji ya Ubatizo. Maisha tuliyoishi mpaka wakati huo yanakuwa yamefikia mwisho wake; yanakuwa yamepita. Inakuwa:

“Kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (Warumi 6:4).

Mabadiliko ya namna hiyo yanawezekana tu kwa neema ya Mungu. Tukiwa wana wa Baba yetu wa mbinguni, tunaweza sasa kumjea kupitia kwa Yesu. Tutashindwa kumpendeza mara nyingi kwa kadri tunavyojaribu, lakini tunapoomba msamaha, atatusikia kwa ajili ya Yesu. Andiko linasema:

“Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebr. 4:16).

Kujilisha Neno la Mungu

Mtoto anahitaji kula, na anafanya hili lijulikane kwa njia moja ya uhakika; analia! Anahitaji kukua. Chakula ni cha muhimu ili aweze kukua. Na wale ambao wamezaliwa kuyaingia maisha mapya kwa kubatizwa, wanaweza tu kukua katika Kristo, kama maisha  mapya yanalishwa na kutunzwa kwa Neno la Mungu. Mtume Petro anasema:

“Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu” (1 Petro 2:2).

Mungu ametupa Biblia ili iwe kitabu chetu cha kutuongoza. Itatusaidia kutufanya tuishi kwa namna anavyotaka, na kukua kuwa ‘mtu mpya’ katika Kristo kwa Neno lake, kwa kuwa:

“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Tim 3:16, 17).

Kuutazamia Ufalme

Mtume Petro anatuambia kwamba, Mungu, “Hapendi mtu yeyote apotee” (2 Petro 3:9), na katika Yohana 3:16 tunasoma ya kwamba, Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee, Yesu, kusudi: “Kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

Mungu anapenda atupe uzima wa milele katika Ufalme wake. Na kwa hiyo, anatuandaa sasa kwa ajili ya maisha hayo. Amemtoa Yesu kutusaidia, na kupitia kwa Yesu tunaweza kumkaribia Mungu kwa njia ya maombi.

Msaada kutoka kwa Yesu

Bwana Yesu aliwahi kusema: “Msiogope, enye kundi dogo, kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme” (Luka 12:32).

Kuna wakati Yesu alimtolea Mungu maombi kwa ajili ya wale wanaomwamini, wa nyakati zote. Unaweza kuyasoma haya katika Yohana 17. Angalia maneno yaliyopo katika msitari wa 24:

“Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa”.

Kwa hiyo, Yesu naye anatutaka tuwe katika Ufalme wake. Kwa hiyo atatusaidia njiani; kamwe hatatuacha tuhangaike peke yetu. Yesu sio tu Mwokozi ambaye kupitia kwake dhambi zetu zinasamehewa, bali pia ni Kiongozi wetu katika maisha haya. Atakuwa mshirika katika maisha yetu na changamoto zake, katika furaha na majonzi, na kutusaidia kutuingiza kuishi naye katika Ufalme wa Mungu.

Mtume Petro, mtu aliyemfahamu Yesu vizuri alipokuwa duniani, aliwaasa wanaomwamini wamfuate Yesu, huku wakimtwika fadhaa zao zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yao (1 Petro 5:7).

Kuwa sehemu ya familia moja kidunia

“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke, maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu” (Wagalatia 3:27, 28).

Haijalishi wewe ni nani, au upo wapi. Kama umekuwa Mkristadelfia kwa kubatiziwa Kristo, Wakristadelfia wengine wote ni ndugu zako; ni kaka na dada zako. Kumbuka, jina Kristadelfia lina maana ya ‘undugu katika Kristo’. Ni furaha kubwa sana kuwa sehemu ya familia hii, iliyosambaa katika sehemu zote za dunia.

Yesu aliwaambia wanafunzi wake kabla ya kufa, na bado anasema hivyo na sisi leo: “Amri yangu ndiyo hii, mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yoh. 15:12).

Alitupenda sana, kiasi kwamba alikufa kwa ajili yetu. Aliutoa uhai wake kwa ajili yetu, kwa hiyo: “Imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” (1 Yoh. 3:16).

Tunajua tunavyopaswa kufanyiana, lakini, kiuhalisia, ni vigumu sana. Hulka yetu ya awali inachukua muda mrefu kufa! Baadhi yetu wana hasira za haraka-haraka, wengine ni vigeu-geu na wepesi kulipuka n.k. Sisi wote tuna kasoro zetu.

Haya ni mambo, hata hivyo, tunayopaswa kuyapiga vita, na kujaribu kuwaonesha ndugu zetu katika Kristo upendo ule ambao Yesu ametuonesha. Kuna picha ya upendo huo katika 1 Wakorintho 13, ambapo tunaambiwa kuwa:

“Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake, hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote” (1 Wakor. 13:4-7).

Kumpenda jirani yetu

Mwanasheria mmoja aliwahi kuja kwa Yesu na alimuuliza, ni ipi iliyokuwa amri kubwa kuliko zote. Yesu alimjibu:

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 2:37-39).

Hebu uisome hadithi ambayo Yesu aliitoa kuhusiana na ‘jirani mwema’ katika Luka 10:30-37. Kama mtu yeyote ana shida, tunapaswa kumsaidia. Hatupaswi tusite na kujiuliza kama tunampenda au hatumpendi, au kama ni kweli anastahili kupata msaada wetu au hastahili.

Kitu cha muhimu kuliko vyote tunachoweza kuwafanyia wengine, ni kuwapasha Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, ambayo sisi wenyewe tumekuja kuiamini. Kama ambavyo Mungu ametutaka tuzishike Njia Zake na kuwa washiriki wa shangwe ya Ufalme wake unaokuja, nasi ni lazima tutamani kuwavuta na wengine, wawe na ushirika katika mambo haya.

Kuomba na kuabudu

Tunapobatizwa katika Kristo, tunakuwa wana wa Mungu, na tunaweza kumkaribia kwa maombi tukimwabudu na kumwomba atusaidie katika maisha yetu. Lakini ni wajibu tusiusahau Ukuu wake ulivyo, ingawa utukufu na Ukuu wake huo ni vitu vilivyo nje ya upeo wetu wa kuelewa vizuri. Katika Isaya 57:15 tunasoma kuwa:

“Aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu, asema hivi: Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu, tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua mioyo yao waliotubu”.

Yakobo anatuambia kuwa: “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Yakobo 4:6). Hata Bwana Yesu, Mwana wa Mungu, alijisemea mwenyewe kuwa alikuwa ni: “Mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mathayo 11:29).

Tunapomjea Mungu kwa njia ya maombi, tunahitaji kuukumbuka ujumbe kwa Waebrania unaosema: “Tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho” (Waebr. 12:28). Kama tunamjea kwa moyo huu, hakika hawezi kukosa kutusikia.

Heri wenye upole

Katika ulimwengu huu, tunaambiwa wakati wote tupiganie haki zetu. Wale wanaopambana kwa manufaa yao wenyewe kibinafsi, watu wanawahusudu. Swala la muhimu katika mawazo ya kila mmoja yamekuwa: ‘Nifanye nini niweze kujikwamua; niweze kupiga hatua?’

Hii sio namna ya Mkristo. Paulo anasema kwa watakatifu wa Filipi na kwetu kuwa, tuwe wanyenyekevu, na: “Kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake” (Wafilipi 2:3). Hiki ni kitu kigumu kufanya; sisi wote tunapenda kufikiri kuwa tuko bora zaidi kuliko wengine. Lakini tunaambiwa: “Tumikianeni kwa upendo” (Wagalatia 5:13).

Katika hili, kama ilivyo kwa mambo yote, Yesu ni kielelezo kwetu. Muda mfupi kabla hajafa, alipokuwa akila na wanafunzi wake, aliacha kula akajifunga taulo:

“Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga” (Yohana 13:4, 5).

Kumwosha miguu mtu mwingine ilikuwa ni kazi ya mtumwa, na ndicho Yesu alichofanya. Baada ya hapo aliwaambia wanafunzi wake: “Nimewapa kielelezo, ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (ms. 15).

Aliwahudumia wanafunzi wake kwa upendo na unyenyekevu, na sisi ni lazima tuhudumiane. Hivyo ndivyo tutakavyoweza kuwa watu wa namna Mungu anayoitaka katika Ufalme wake. Andiko linasema, “Heri wenye upole, maana hao watairithi nchi” (Mathayo 5:5).

Kumkumbuka Yesu

Tunapobatizwa, tunaanza kuipita njia nyembamba iliyonyoka inayotuongoza kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini bado sisi ni wanadamu sana, na tunaweza kirahisi kusahau lile Yesu alilolifanya kwa ajili yetu alipotufia msalabani.

Yesu alijua jinsi ambavyo kirahisi wanafunzi wake wangeweza kusahau, kwa hiyo aliwaagiza wafanye kitu kujikumbusha. Hebu fungua Injili ya Luka, na usome Sura ya 22: 14-20. Hili lilitokea katika kile chakula cha mwisho, tunachokiita Chakula cha Bwana, tulichokwisha kiongelea, alipowaosha wanafunzi wake miguu yao.

Hebu ona jinsi mkate na divai vilivyokuwa ni kwa ajili ya kuwakumbusha wafuasi wake, jinsi Yesu alivyoutoa uhai wake kwa ajili yao. Aliwaambia: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.

Sasa tusome 1 Wakorintho 11:23-28. Wakristo wa awali walikutana katika siku ya kwanza ya kila juma, kumkumbuka Yesu kwa namna aliyoamuru.

Wafuasi wa kweli wa Bwana Yesu wanakutana pamoja, kama wafuasi hao wa kwanza walivyofanya. Kwa kawaida Jumapili ni siku iliyo nzuri zaidi kwa mikutano hiyo. Wanapokutana wanamwabudu Mungu pamoja na kumega mkate na kula, na kunywa divai, katika kukumbuka vile Yesu alivyoutoa mwili na damu yake kwa ajili ya wokovu wao.

Kwa kadri tunavyokomaa katika Kristo, kumkumbuka Yesu kwa namna hii kutakuwa kitu cha muhimu zaidi na zaidi kwetu, kinachotusaidia kutambua kuwa yupo nasi wakati wote.

KWENDA KATIKA NJIA YA UZIMA KUNAMAANISHA

  • Kujilisha kwa kulisoma Neno la Mungu kila siku:

“Kufafanisha (‘kuyaelewa’) maneno yako (Mungu) kwatia nuru, na kumfahamisha (‘kumwelimisha’) mjinga” (Zaburi 119:130).

  • Kumwomba Mungu na kumsifu wakati wote:

“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6).

  • Kuwapenda ndugu zetu:

“Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu” (1 Yoh. 4:7).

  • Kuwafikiria wengine, na kuwasaidia kila tunapoweza:

“Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo” (Mathayo 7:12).

  • Kuacha kushiriki katika mambo ya kidunia; mambo ya dunia hii:

“Tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana. Msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wakike, asema Bwana Mwenyezi” (2 Wakor. 6:17, 18).

  • Juu ya yote, kumpenda Mungu kuliko vitu vyote:

“Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa nguvu zako zote” (Kumb. La Torati 6:5).

Vifungu vya kusoma: 1 Wakorintho 13;  Luka 10:30 – 37;

                                    Luka 22:14-20;  1 Wakorintho 11:23-28.

Msitari wa kushika: 2 Wakorintho 5:17

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa   kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama! Yamekuwa mapya”.

Swahili Title
Kutembea katika njia mpya ya Uzima - Somo la 36
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission