Correspondance Course - Lesson 37

Swahili

Somo la 37

USOMAJI BIBLIA WA KILA SIKU

Somo: Zaburi 119: 89-112

Biblia ni kama kisima kirefu cha maji safi; kisima ambacho kamwe huwezi kukifikia chini kwa jinsi kilivyo kirefu. Hutaweza kamwe kufikia wakati utakapoweza kujisikia umeijua yote kabisa, huhitaji kulisoma tena Neno la Mungu. Hebu ona jinsi baadhi ya watu walivyolipokea Neno la Mungu.

WAYUNANI WA BEROYA                          PAULO

 ALIVYOWAANDIKIA                                  WATHESALONIKE

“…walilipokea lile neno kwa uelekevu kwa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini” (Matendo 17:11,12).

 

“Mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli” (1 Wathesalonike 2:13).

Kwa hakika ni muhimu sana tukisome kitabu hiki kwa uangalifu! Mungu anaongea nasi katika Biblia! Inatupa tumaini la uzima kupitia kwenye Injili.

Biblia na Yesu

Yesu, kwa vyovyote, alikuwa na Agano la Kale tu. Lakini utashangaa alivyolijua. Kwa kila tatizo na ugumu alioupata, aliliendea Neno la Mungu moja kwa moja kwa ajili ya jibu. Hebu ione mifano hii:

  1. Wakati mafarisayo walipomuuliza kama ilikuwa sahihi kwa mtu kumpa talaka mkewe, Yesu alirudi moja kwa moja kwenye simulizi la Adamu na Hawa kwenye Mwanzo. Aliwaambia: “Tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, (Mungu) aliwafanya mume na mke”. Unaweza kulisoma jibu lote katika Marko 10:5-12.
  2. Yesu alipokuwa peke yake nyikani, majaribu yalimjea yakimtaka aifuate njia iliyokuwa rahisi zaidi kwake, badala ya kuifuata Njia ya Mungu. Aliyashinda mawazo hayo mabaya kwa kuyajibu kwa maneno kutoka kwenye Kitabu cha Kumbukumbu la Torati, mara zote akisema: “Imeandikwa…”
  3. Maaskari walipokuja kumkamata Yesu, Yesu alijua kuwa kingefuatia kifo chake. Alikwenda bila kubisha kwa kuwa, alisema: “Haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia” (Marko 14:49). Maandiko yalikuwa yamezungumzia mauti yake. Kwa maisha yake yote, Yesu alikuwa akitimiza yaliyoandikwa juu yake katika Agano la Kale.

Kukua katika kumjua Yesu

Petro anatusihi tukue: “Katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo” (2 Petro 3:18). Tunaweza tu kumjua Yesu kwa kusoma juu yake; na Injili zote nne zinatupa maelezo ya mambo Yesu aliyofanya na maneno aliyosema, na kwa namna gani aliutoa uhai wake wa ajili yetu.

Vitabu vingine katika Agano Jipya vinatusaidia kuelewa zaidi juu ya yale Yesu aliyofanya kwa ajili yetu katika kufa msalabani, na jinsi inavyotupasa kuishi maisha mapya katika Kristo.

Lakini haiwezekani kuyaelewa mambo haya bila kulisoma Agano la Kale nalo. Msitari wa kwanza kabisa wa Agano Jipya (Mathayo 1:1) unamsemea: “Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu”. Ni lazima turudi nyuma kwenye Agano la Kale ndipo tunapoweza kuelewa Ibrahimu na Daudi walikuwa ni watu gani, na ni kwa nini Yesu anaitwa ‘mwana’ wao.

      Yesu alilisoma Agano la Kale, ni wajibu wetu nasi kulisoma

Inatupasa kusoma kila siku

Mtume Paulo anatuambia jinsi ilivyo muhimu kuyasoma Maandiko Matakatifu katika maisha yetu. Anasema:

“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Timotheo 3:16, 17).

Mwenyezi Mungu anatupatia chakula ambacho miili yetu anakihitaji siku kwa siku. Yesu aliwakumbusha wanafunzi wake hili alipowaambia:

“Waangalieni ndege wa angani ya kwamba hawapandi wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani, na Baba yenu wa mbinguni uwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? (Mathayo 6:26)

Kwa namna hiyo hiyo, uzima wetu mpya ulio katika Kristo utaendelea na utakua kama ukilishwa, na chakula unachokihitaji ni Neno la Mungu.

Ingekuwa hatari kama tungekaa bila ya chakula kwa juma zima, na kujaribu kujifidia kwa kula chakula chote cha juma kwa siku moja. Kwa jinsi hiyo, tunatakiwa kuzilisha akili zetu kwa Neno la Mungu kila siku. Kama tukifanya hivyo litajenga uelewa wetu wa Njia za Mungu, na tutakua katika neema na ufahamu.

Kuyasoma Maandiko yote

Sehemu kadhaa za Biblia kama Zaburi na masimulizi katika Injili, zinasomeka kiurahisi. Lakini kuna sehemu zinazoelezea habari mbaya za uovu na vita, ambazo hatupendelei hasa kuzisoma. Vifungu vingine vina orodha ndefu za majina ya watu au maeneo, na tunaweza hata kujiuliza ni kwa nini vimewekwa humo. Lakini. kama tulivyosoma katika 2 Tim. 3:16, kila andiko ‘lafaa…’ (ni la manufaa). Watu wote wana mahitaji, hulka, mazingira na mazoea yanayotofautiana, na Maandiko yapo kuwaridhisha wote.

Kuanzia msitari wa kwanza wa Mwanzo mpaka msitari wa mwisho wa Ufunuo, Biblia yote ni ‘Andiko’ lenye pumzi ya Mungu. Ni kitabu chote kabisa. Kama tungekuwa ni kujichagulia, tungesoma tu vifungu vile vinavyotupendeza. Kamwe tusingeyajua mafundisho mengine ya umuhimu mkubwa kwenye Biblia, kama yale yanayohusu uovu mkubwa ulio ndani ya mwanadamu, na Utakatifu wa hali ya juu wa Mungu, na unyenyekevu na utii anaoutaka kutoka kwetu.

Unahitajika mpango

Ili tuweze kuisoma Biblia yote, tunahitaji kuwa na mpango wa namna tunavyoisoma. Umekuwa ukiutumia mpango wako wa kusoma Biblia uitwao ‘Bible Planner’? Kama bado, wakati umefika wa kuanza sasa kuweza kuisoma Biblia yako kwa namna inayovutia, na umewekewa mihtasari katika kijitabu hicho kukusaidia kuyaelewa mambo unayosoma.

Sasa, utakapokuwa umemaliza kuisoma Biblia kwa kuutumia mpango huu, nini kitafuata? Jibu ni kwamba, utakuwa umekuwa tayari kuendelea na usomaji wako wa Biblia wa kila siku kwa kutumia kijitabu kingine (au karatasi), chenye majedwali ya siku na miezi, na masomo ya kila siku. Hicho kinaitwa Mshirika wa Biblia (The Bible Companion). Kiambatisho hiki kitakufanya ulisome Agano la Kale lote mara moja, na Agano Jipya mara mbili kila mwaka. Utajiona unakua hasa katika kuijua Biblia yako.

Kumbuka pia kwamba, Wakristadelfia duniani pote wanaisoma Biblia kila siku kwa kumtumia ‘mshirika’ huyu. Wote wanataka kukua katika kulielewa Neno la Mungu, kwa hiyo hauko peke yako katika kusoma kwako.

VIDOKEZO MUHIMU.

Namna ya kusoma

Ni wazo zuri unapokaa chini kuanza usomaji wako wa Biblia wa kila siku, kusoma Sura za siku hiyo moja kwa moja kwanza, kuona kinachozungumziwa. Baada ya kumaliza kusoma, fumba macho yako na ujiulize, ‘hivi nimesoma nini?’ Kuna wakati utakumbuka ulichosoma kirahisi, kuna wakati utaona shida kukumbuka. Kama ni hivyo, utahitaji kuvisoma tena vifungu hivyo.

Kumbuka: kila neno katika Maandiko ni la muhimu (kama hakukuwa na makosa kwa waliotafsiri kwenye Kiswahili).

Misaada mingine kwa kusoma Biblia

Kama Biblia yako haina nafasi ya pembeni iliyoandikwa mistari au haina ramani, au imechapishwa kwa namna tofauti, usijali; bado ulilonalo ni Neno la Mungu. Lakini kwa wale walio na vitu kama hivyo vya kuwasaidia katika Biblia zao, vidokezo vifuatavyo vitawasaidia kuvitumia:

a. Rejea za pembeni/chini

Baadhi ya Biblia zina rejea za mistari pembeni au chini; nazo zitaweza kuwa msaada. Utaona kiherufi kidogo au namba ya neno, na hiyo herufi au namba inaweza kuonekana kwa pembeni au chini ya ukurasa huo. Ukiifuatilia itakuonesha kwa msitari huo kwenye Sura hiyo, Sura na mistari mingine inayosema kitu kinachofanana na hicho ulichosoma. Hili litakusaidia kuelewa zaidi msitari uliousoma.

b. Sura na mistari

Tofauti na vitabu vingine vyote, Biblia imegawanywa katika Mistari na Sura. Mgawanyo huu ulifanywa mamia ya miaka baada ya Biblia kukamilika. Kwa vyovyote huu ni msaada mkubwa kutuongoza kupata tunapopataka, tena kwa haraka.

Lakini sio wakati wote unatusaidia sana. Mara nyingine mgao huo unaikata hadithi vipande viwili, kama lilivyo simulizi la Mathayo 16 na 17, la ‘kugeuzwa sura’ mlima. Msitari wa mwisho katika Sura ya 16 unasema: “Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake”.

Yesu anaongelea hapa maono ya Ufalme waliyopewa watatu kati ya wanafunzi wake: Petro, Yakobo na Yohana. Sura ya 17, inaanza na: “Na baada ya siku sita, Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani”. Kwa hiyo unapoanza kusoma Mathayo 17, inakubidi kuangalia nyuma kwenye msitari wa mwisho ya Sura ya 16 kwanza.

Ni wazo zuri, hata hivyo, wakati wote, kuangalia kinachosemewa kwa Sura unayosoma, kwa kuona kwanza ni nini kilichotokea nyuma, kwa kuitafakari mistari ya karibu.

c. umia ramani zilizopo

Baadhi ya Biblia zina ramani kwa mbele au nyuma. Unaposoma juu ya tukio lililotokea mahali fulani, patafute katika ramani. Kama ukifanya hivyo kila mara kunapotajwa mji, mto, mlima au ziwa, utajikuta unaifahamu nchi ya Israeli vizuri zaidi unavyoendelea. Unaweza kuielewa hadithi hiyo vizuri zaidi pia.

Kwa mfano, utakaposoma Luka 2 (Hatua ya 1, siku ya 3 katika mpango wako wa kwanza wa kujisomea Biblia (Bible Planner), utaona miji ya Nazareti, Bethlehemu na Yerusalemu yote inavyokuja kwenye simulizi hilo. Sasa hebu itazame ramani, na utaona kwamba ilikuwa ni safari iliyokuwa ndefu kutoka Nazareti mpaka Bethlehemu, lakini Bethlehemu na Yerusalemu hapakuwa mbali. Unapata picha zaidi.

Soma Biblia yako kwa maombi

Wakati wote unapokaa chini kuisoma Biblia yako, mwombe Mungu akusaidie katika kulielewa Neno lake. Kuna msitari katika Zaburi ya 119 ambao ni ombi. Unasema: “Unifumbue macho yangu, niyatazame maajabu yatokayo katika Sheria yako” (Zab. 119:18).

Tunahitaji msaada wa Mungu kuweza kuelewa, na yeye wakati wote yupo tayari kuutoa. Kwa hiyo, usisahau kuuomba!

Kusikia na kufanya

Mungu atatufundisha kwa Neno lake, lakini kusoma hakutoshi. Yakobo anatuambia, tuwe: “Watendaji wa neno, wala sio wasikilizaji tu” (Yak. 1:22). Yesu anawaongelea wengine waliokuwa wakimwita “Bwana, Bwana”, lakini hawakuwa wakifanya yale aliyowaamuru wafanye. Soma mwenyewe katika Mathayo 25:31-46.

Sasa fungua Mathayo 7 na uisome habari katika msitari wa 24 mpaka wa 29, juu ya watu wawili ambao wote walijenga nyumba zinazofanana. Mtu anayeyasikia maneno ya Yesu, na kufanya anayosema, anafananishwa na mtu yule mwenye busara aliyeijenga nyumba yake katika mwamba.

Ijee Biblia kwa  unyenyekevu wa moyo

Mwenyezi Mungu amesema:

“Lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye alisikiapo neno langu” (Isaya 66:2).

Muhsatari

Isome Biblia yako:

  • kila siku. Hakikisha kusoma kwako kunavifikia vitabu vyote vya Biblia.
  • kwa moyo uliofunguka, ukiwa unairuhusu ikufundishe.
  • kwa umakini; ufikirie kila msitari na hakikisha unauelewa.
  • kwa kuomba. Mwombe Mungu akusaidie uweze kuelewa kile unachosoma.
  • kwa kunyenyekea; ukiwa unataka kujua vile Mungu anavyokutaka uishi.

Vifungu vya kusoma: Zaburi 19,  Zaburi 119:1-40, Marko 8:34-38.

Mistari ya kushika: Zaburi 119: 33, 34

“Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, nami nitaishika hata mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako. Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote”.

Swahili Title
Usomaji Biblia wa kila siku - Somo la 37
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission