Correspondance Course - Lesson 38

Swahili

Somo la 38

USHIRIKA NA WALIO WA IMANI MOJA

Somo: 1 Wakorintho 3

Mungu alipomuumba mtu, alikifikia kilele cha kazi yake ya uumbaji. Mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu (Mwanzo 1:27). Aliumbwa hivyo ili aweze kuwa kama Mungu; mwenye utashi uliojengeka wa kutambua lililo jema na baya.

Lakini kulikuwa, hata hivyo, na moja lililopungua; Adamu alikuwa peke yake. Kwa huruma na rehema ya Mungu, alitambua kuwa Adamu alihitaji mshirika. Kwa hiyo Mungu alimuumbia mwanamke, akisema: “Si vema huyo mtu awe peke yake” (Mwanzo 2:18).

Ushirika ni nini?

Adamu na Hawa waliumbwa kila mmoja kwa ajili ya mwenzake, na walitakiwa wasaidiane (Mwanzo 2:18). Hawa alipoletwa kwa Adamu, Adamu alisema: “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu” (Mwanzo 2:23). Na mwandishi, akiandika alilosema Mungu anaongeza kuwa, mume na mke wanapaswa, kwa sababu hiyo, kuambatana pamoja; kushikamana, kuwa kitu kimoja (Mwanzo 2:24).

Huu ulikuwa ndio ushirika; kushirikiana katika yote yale Mungu aliyowapa; kufurahiana mmoja kwa mwingine, na kuitambua kwa shukrani mibaraka yote ya Mungu katika maisha yao. Wakati Bwana Mungu alipokuwa akija bustanini kukiwa kumepoa, mtu na mkewe na Mungu walikuwa katika ushirika mzuri, mkamilifu, wa kupendeza. Lakini hili halikudumu.

Dhambi ilipoingia ulimwenguni, ushirika huo ulivunjika. Mungu ni Mtakatifu; hawezi kuikubali dhambi, na wadhambi hawawezi kukaa mbele yake; hawawezi kukaa katika ‘uwepo’ wa Utakatifu wake. Kulikuwa na mtengano uliotokea mara tu Sheria ya Mungu ilipovunjwa (soma Mwanzo 3 tena).

Mungu alipokuja akitembea bustanini siku hiyo ‘wakati wa jua kupunga’, Adamu na Hawa wakijijua kuwa wamekuwa uchi, walijificha; ushirika wao na Mungu ulikuwa umevunjika (Mwanzo 3:7,8).

Hili liliyaathiri pia mahusiano yao ya kibinadamu; Adamu alimlaumu Hawa kwa lile lililotokea. Uhusiano wao wa karibu na Mungu ulikuwa umefikia mwisho. Walikuwa sasa wakiweza tu kuukaribia ‘uwepo wake’ kwa njia aliyoiweka. Walilazimika kuiacha hiyo Bustani, na maisha yakaanza kuwa magumu.

Ushirika na Mungu unabakia katika mpito huo huo, hata kama mazingira ya sisi kuutafuta yamekuwa tofauti sana. Tunapokuwa na ushirika na wenzetu, ina maana kuwa tunaweza kuishiriki mibaraka ya Mungu na wengine wanaoamini tunayoamini, na kuutumainia wokovu ule ule.

Ushirika huo unaweza ukawepo hata kati ya watu ambao hawajawahi kukutana, kwa kuandikiana au kupigiana simu. Ushirika unaweza kufanya kazi, mradi wana imani moja ya Kikristo.

Duniani pote watu wanakuwa na ushirika mmoja, wanapokuwa ndani ya familia ya Mungu. Ushirika sio sawa na kuelewana tu na mtu; ni uhusiano wa kiroho unaojengeka kwa kuamini mambo yanayofanana juu ya Mungu.

Ushirika ni umoja. Ushirika wa Kibiblia una maana ya kuwa na imani moja na matumaini, katika kuabudu pamoja na waumini wenzako.

Roho na Kweli

Katika mojawapo ya safari zake katika Israeli, Yesu alipitia Samaria, sehemu ya nchi walipokuwapo watu waliokuwa wakichukiwa na Wayahudi. Yesu hakuwa na dharau kama wao, na alipopumzika kando ya kisima, aliongea na mwanamke mmoja wa Kisamaria.

Haraka mwanamke huyo aligundua ya kuwa, Yesu hakuwa Myahudi wa kawaida. Alipomuuliza Yesu ni sehemu ipi kati ya maeneo matakatifu ya kukumbukwa, aliyofikiri ni ya muhimu zaidi: Mlima Gezirimu-karibu na walipokuwa wakiongelea, au eneo Yerusalemu ilipo, Yesu alimpa jibu ambalo kwa vyovyote lilimshangaza.

Yesu alimwambia, haupo mlima uliokuwa wa maana zaidi, na kuongeza: “Saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli, kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu” (Yohana 4:23).

Miaka kama 40 baada ya mazungumzo hayo, Yerusalemu na Mlima Gezirimu hayakuwa tena maeneo ya ibada. Majeshi ya Kirumi yalikuwa yameivamia nchi ya Israeli katika mwaka 70 (Baada ya Kristo), na kuyateketeza maeneo yake ya kidini. Wale Wayahudi waliopona katika shambulizi hilo, na ambao hawakutoroka, walichukuliwa mateka na kuuzwa kama watumwa.

Kwa hiyo, kama dini yao ilitegemea uwepo wa mahekalu na maeneo matakatifu, iliwabidi wayaache. Yesu alisema kuwa, ibada ya kweli isingehusiana kwa lolote na majengo au sehemu za ibada, ila na udhati katika kuamini, na katika kweli. Maneno ‘Roho na Kweli’ katika msitari huo hapo juu ni ya muhimu sana.

Kuna watu leo wanaodai kuwa wanaongozwa na roho, lakini unapoongea nao, haraka unatambua ya kuwa hawajui Biblia inachosema. Watakuwa pengine wanaamini juu ya kwenda mbinguni baada ya kufa, wakati Biblia inachofundisha ni kuwa, tumaini la kweli la Mkristo la kuanzishwa Ufalme wa Mungu katika dunia.

Utakuta wanaamini pia kuwa Yesu Kristo ni sehemu iliyo katika Mungu aliye na nafsi tatu, wakati Biblia inafundisha kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, aliyezaliwa na bikira Mariamu kwa muujiza wa Mungu; kwa roho yake. Watu wanaodai kuwa wana ‘roho’ na hawajui ukweli ulio katika Biblia, lazima wamekosea.

Kutokana na hili, wanaomwabudu Mungu kwa dhati; kwa Roho na Kweli, hawatavutiwa na makanisa makubwa au sehemu za kuabudia, au idadi kubwa ya washirika, au kuvuma kwokwote kwa dhehebu. Kanisa la kweli halihusiani na majengo, ila ni watu; na haijalishi ni wangapi.

Cha muhimu zaidi kwao kinakuwa ni kile walichoamini, na namna wanavyomwabudu Mungu. Ni muhimu kuwa na moyo sahihi kiibada, lakini ni muhimu sana kuamini mambo yaliyo sahihi, na kufanya yaliyo sahihi mbele ya Mungu.

‘Jitenge’

Agano Jipya linawaamuru wafuasi wa Yesu kujitenga na dunia. Hili halina maana ya kuiacha dunia; kitu ambacho hakiwezekani. Kinachosemewa ni kuishi kwa namna iliyo tofauti na ‘udunia’, kwa kuzifuata Njia za Mungu. Ibrahimu aliishi pamoja na Wakanaani, lakini alijitenga nao; hakuishi walivyokuwa wakiishi. Anaelezewa kuwa alikuwa ‘mgeni na msafiri juu ya nchi’ (Waebrania 11:13).

Imani na matumaini yake yalikuwa ni kwa Mungu na ahadi zake. Bwana Yesu aliwaombea wafuasi wake Mungu awatenge na maovu ya duniani, na kusema:

“Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni” (Yohana 17:16 – 18).

Yesu Kristo na mitume wake waliichukulia dunia kama mahali pa udhalimu na uovu (1 Yohana 2:16). Imejaa watu wasio na haja na mambo ya Mungu, na wanaoifanya hali iwawie ngumu Wakristo wa kweli, wanaotaka kutii mambo Mungu anayoamuru. Tutambue hapa ya kwamba, hili linawahusu hata watu tunaowaona ‘wa dini’ sana. Wote wanaoupinga ukweli unaomhusu Mungu, wanaweza kuwapotosha waumini katika Njia ya Mungu.

Makao ya Mungu

Wakristadelfia mara nyingi wanaulizwa, “Lipo wapi kanisa lenu?” Watu wanategemea kuona jengo zuri linaloweza kuwavutia na kuwafanya waamini kuwa, ‘hili ni kanisa kweli la Mungu’. Ni vigumu kwa watu hao kutambua kuwa, Mungu anataka watu na sio majengo. Lakini hivi ndivyo hali ilivyokuwa hata katika siku za Yesu na za mitume.

Kulikuwa na majengo mazuri wakati huo ambamo baadhi yao walikwenda humo kuabudu, na hasa Hekalu lililokuwa katika Yerusalemu, lililochukua miaka 40 kujengwa na kurembwa. Lakini Yesu alisema Hekalu hilo lilikuwa ni pango la wezi na wanyang’anyi, na aliwataka wafuasi wake wamfuate, waachane na makuhani.

Yesu hakuwahi kujenga jengo la kanisa au kuwataka wafuasi wake wajenge. Chakula chake cha mwisho kabla hajasulubiwa alikila na wanafunzi wake kwenye nyumba ya mtu, katika ‘chumba cha juu’ katika Yerusalemu, na ndipo hapo mitume walipokwenda kuabudia kwa muda baada ya Yesu kufa na kufufuka (Matendo 1:13 na 12:12).

Ibada za mitume wakati wa kanisa la awali, zilifanyikia majumbani (Wakolosai 4:15) au kwenye vyumba vya kupanga (Matendo 28:23-31). Walitambua ukweli kwamba, wao ndio waliokuwa ‘mahali’ anapokaa Mungu; walikuwa ndio ‘hekalu’ lake. Naye Mungu alikuwa akitaka aishi ndani yao, na pamoja nao, kila siku ya maisha yao. Ni hivyo hata leo!

Mtume Paulo atakuwa alikuwa akizungumzia jengo, wakati alipowaambia waumini wa Korintho kwamba, kazi yake katika Korintho, alipokaa miezi 18, ilikuwa na matokeo ya kuwekea msingi jengo (1 Wakor. 3:10). Alichokuwa akimaanisha ni kuwa, alikuwa ameweka msingi wa Yesu Kristo, kwa kuwafundisha ukweli kama ulivyo kumhusu Mwana wa Mungu, aliyekufa kwa ajili yao na kufufuliwa na Mungu kwa uzima wa milele. Aliwaambia sasa walikuwa wakipaswa kujenga juu ya msingi huo, kwa namna walivyokuwa wakiishi na kuamini (1 Wakor. 3:12-15). Baada ya hapo aliongeza:

“Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” (ms. 16). Paulo analizungumzia hili tena katika Waefeso 2:19-22.

Kumega Mkate

Mkate na divai vinatukumbusha juu ya mwili na damu ya Yesu, vilivyotolewa msalabani kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu. Hakuna la kushangaza au la kutisha juu ya vitu hivi. Mkate haubadiliki kuwa nyama (kuwa mwili) wa Bwana Yesu, na divai haiwi damu, kama watu wengine wanavyoamini kimakosa.

Ni vitu vilivyokusudiwa tu kuwakumbusha wanaoamini, juu ya kazi kubwa aliyoifanya Yesu kwa ajili yao, na ni waumini waliobatizwa tu wanaoshiriki katika kumkumbuka kwa namna hii. Yesu alisema hivi kwa wanafunzi wake: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Luka 22:19).

Kumega-Mkate huku ndipo chimbuko la ushirika wa Kikristo lilipo. Waumini wanafanya kila jitihada kuweza kukutana kila juma (pale wanapoweza), kumkumbuka Bwana wao na wokovu wake mkuu. Wanahitaji kukutana mara kwa mara kuweza kukua pamoja katika upendo na katika kweli. Andiko linasema:

“Tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia” (Waebr. 10:24, 25).

Kuabudu pamoja au kipekee

Kwa namna walivyofanya waumini katika karne ya kwanza, ndivyo Wakristadelfia wanavyofuata. Kila juma kama kuna waumini kadhaa wanaokaa katika eneo moja, wanakutana pamoja mahali ili kumwabudu Mungu. Wanaita kusanyiko lao ‘Eklesia’, neno la Kiyunani lenye maana ya ‘Kusanyiko’, lililotafsiriwa ‘Kanisa’ katika Kiswahili. Kibiblia, kanisa ni watu, sio mahali; sio jengo.

Wanakutana kwa kujengana katika Neno la Mungu, Biblia, na kuweka mipango ya kuihubiri Injili kwa wasio-washirika. Kila juma wanakutana pia kwa ajili ya kumkumbuka Bwana Yesu kwa namna alivyoagiza, kwa kushiriki mkate na divai katika huduma wanayoiita, ‘Kumega-Mkate’.

Kama ilivyokuwa kwa waumini katika karne ya kwanza, hawana wachungaji au mapadri au makuhani kwa ajili ya kuongoza ibada, kwa kuwa Bwana Yesu ndiye ‘Kuhani Mkuu’ wao. Waumini wa kiume wanashirikiana katika kuongoza huduma. Mmoja anasimamia; anapanga nyimbo za kuimbwa, masomo na kuongoza maombi, na anawakaribisha wengine kusaidia katika mambo haya.

Mwingine atakuwa ameandaa mahubiri kutoka kwenye masomo ya Biblia ya siku hiyo, kwa ajili ya kuwatia moyo washirika na kuwaonya. Mawazo ya hao waliopo hapo yanapokuwa yamewekwa sawa kwa mahubiri hayo katika kumkumbuka Bwana Yesu, waumini wote wanashiriki mkate na divai, kama Yesu alivyofanya katika chakula kwenye chumba kile cha juu zamani.

Kama hakuna waumini wengine katika eneo muumini alipo, ni lazima mambo hayo bado yafanyike kwa kadri hali inavyoruhusu. Wajibu wa kuwafundisha watoto na watu wazima juu ya Injili utakuwa jukumu la kila siku la familia, na siku za Jumapili Bwana Yesu ni lazima akumbukwe katika mkate na divai katika umegaji mkate wa kibinafsi.

Utakuwa umeshirikiana na Wakristadelfia wengine popote pale walipo, ambao nao watakuwa wakifanya kitu hicho hicho duniani pote. Mungu anaweza kupenda kuita wapatikane waumini wengine katika eneo hilo, na kuwezesha kuanza kwa Eklesia nyingine ya watu wanaomwabudu kwa hapo.

Muhtasari

  1. Ushirika wa Kikristo au wa Kibiblia una maana ya kuabudu pamoja kwa wale wanaoamini na kuyatumainia mambo yanayofanana, yaliyo sahihi Kimaandiko.
  2. Ushirika wa Kibiblia una maana ya kujitenga na wale ambao hawaamini mambo tunayoamini.
  3. Kwa kuwa sio vizuri kwa mwanamume au mwanamke kuwa peke yake, ni vyema tutafute ushirika na waumini wenzetu mara kwa mara kwa kadri inavyowezekana.
  4. Ni lazima kuutafuta ushirika na Mungu na Bwana Yesu wakati wote kwa njia ya maombi, na kwa kuisoma Biblia na kuitafakari.
  5. Tunamkaribia Mungu, na Bwana Yesu, na waumini wenzetu tunaposhiriki mkate na divai katika ‘Kumega Mkate’ kwetu.
  6. Kutakuwa na ushirika ulio mkamilifu na Mungu katika Ufalme wake duniani.

Vifungu vya kusoma: 1 Yohana 1, Warumi 14-15:7, 1 Wakorintho 10.

Kuweka moyoni:  2 Wakorintho 6:16.

“Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu”.

Swahili Title
Ushirika na walio wa Imani moja - Soma la 38
English files
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission