Somo la 39
UWEZO YA ULIMI
Somo: Yakobo 1
Kiti cha Hukumu
Yesu Kristo atakaporudi kuusimamisha Ufalme wa Mungu, kila mtu aliyeujua na kuuelewa ujumbe wa Injili, ataitwa kumpokea na atahukumiwa naye. Wale ambao wamekuwa waaminifu kwake katika maisha yao watapewa nafasi katika Ufalme huo, na wale ambao hawakuwa, watakataliwa na Bwana na kuondolewa wafe.
Kigezo cha hukumu hiyo kitakuwa, ni kwa kiasi gani tumeufanyia kazi ujumbe wa Injili katika maisha yetu (Warumi 2:16). Katika hili, Yesu atakuwa hasa akiangalia ni kwa namna gani tumeutumia ulimi wetu. Anasema:
âBasi, nawaambia, kila neno lisilo maana watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa, kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwaâ (Mathayo 12: 36, 37).
Yesu hatasikiliza ni nini watu wanasema juu yetu. Pamoja na mambo mengine, atatuhukumu kwa yale tuliyosema juu ya watu wengine; juu ya vile tulivyoutumia ulimi tuliopewa. Kama maneno yetu ni ya âbureâ; kama hatujali tunachosema, kwa hiyo tunasema kwa kuwasononesha wengine, itatupasa kujibu kwa ajili yao kwa Yesu.
Maneno yaliyo bora
Kuna fundisho lingine katika maneno haya ya Yesu, ambalo ni lazima tulifikiri. Wazo la maneno ya âbureâ ni maneno ya kizembe; maneno yasiyo na maana. Yesu alilitumia neno kama hilo katika mfano, wakati alipoongea juu ya wafanyakazi waliokaa bure, âwasiokuwa na kaziâ, waliokuwa wamesimama sokoni (Mathayo 20:3).
Inatupasa tuwe macho juu ya yale tunayosema kwa wenzetu, kwa kutumia maneno yanayosaidia kuwajenga watu wengine. Tutumie ndimi zetu kwa namna ambayo inasaidia katika kuzifanya kazi za Yesu. Kuna njia nyingi za kufanya hili:
- Tutumie ndimi zetu katika kuabudu pamoja na ndugu zetu, tukimsifu na kumshukuru Mungu (Wakolosai 3:15-17).
- Tunaweza kuongea maneno ya faraja na amani, kuleta utulivu kulipo na hasira au ghadhabu (Methali 15:1, Mathayo 5:9).
- Kwa maneno au kwa kutuma ujumbe, tunaweza kuwasaidia na kuwatuliza walio kwenye shida (2 Wakorintho 1:1-11).
- Tunaweza kuwalisha wenye njaa kiroho kwa Neno la Mungu: âMidomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamuâ (Methali 10:21).
Kuna mifano mingi katika Biblia ya wanaume na wanawake waliobadilisha namna zao za kuzungumza walipoiamini Injili. Mtume Paulo anasema: âManeno yenu yawe na neema siku zoteâ. Katika maongezi yetu yote tunapaswa kutambua kitu cha ajabu Mungu alichotufanyia; kutuokoa kwa neema yake.
Pengine mfano mzuri unaofahamika sana ni wa Petro. Yesu alipokamatwa, Petro aliapa akikana kwamba hakuwahi kumjua. Lakini tunaona jinsi ambavyo miaka michache baadaye alivyoandika maneno matamu juu ya namna tunavyopaswa kutumia ndimi zetu katika 1 Petro 3:8-16. Anayahitimisha kwa kusema:
âMwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristoâ (ms. 15, 16).
Huu ni mfano mzuri kwetu kuufuata!
Nguvu ya Ulimi
Katika Waraka wake kwa Warumi, mtume Paulo anasema:
âItoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maanaâ (War. 12:1).
Ni dhahiri kutokana na nyaraka alizoandika Paulo kuwa, maneno haya yalikuwa na maana ya dhati na ya kimatendo kwake. Alipobatizwa alibadilika na kuwa âmtumwa wa Munguâ (War. 6:22), na kutambua kuwa, alimpaswa kumtii Bwana wake mpya katika mambo yote. Katika kila kitu alichofanya na alichosema, Paulo alijaribu kumtii Mungu.
Huu ni mfano tunaojaribu kuufuata katika maisha yetu, tunapokuwa wafuasi waliobatizwa wa Bwana Yesu Kristo. Kama Paulo, tunaona ni kitu kigumu sana kumpendeza Mungu; tunajikuta mara nyingi tukimkiuka, lakini tunamtaka atusamehe kwa njia ya Yesu.
Biblia inatufundisha kuwa, ulimi una nafasi ya muhimu sana katika mapambano yetu na hulka yetu ya kibinadamu. Kile tunachosema na vile tunavyokisema inaweza kuwaonesha watu, zaidi kuliko yale yote tunayofanya, kama tu wafuasi wa kweli wa Kristo au siyo. Tunaambiwa:
âMtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu. Kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wakeâ (Luka 6:45).
Hata tujitahidi kwa kiasi gani kuuficha ukweli huu, maneno yetu yatawaambia watu kile hasa kilichopo mioyoni mwetu; mambo hasa tunayoamini.
Yakobo (ambaye inaaminika alikuwa mdogo wake Bwana Yesu), aliandika maneno mazito sana yanayouhusu ulimi. Tafadhali uyasome katika Yakobo 3 kabla ya kuendelea mbele na somo hili. Tunaweza kuhitimisha Yakobo anayotufundisha kihivi:
- Tusipende sana kufundisha wengine; kutumia ndimi zetu kuwaambia wengine kitu cha kufanya; tuwe vielelezo. Mungu atayahukumu maneno ya wale wanaofanya hivi (ms. 1).
- Ingawa ulimi ni kiungo kidogo sana katika miili yetu, unaongoza mwelekeo wa maisha yetu yote (ms. 3-5).
- Kile tunachosema kinaweza kikaleta shida kubwa sana. Ni kama kuwasha moto (kwa cheche tu), ukalipuka na kushindikana.
Kama tukimuudhi mtu kwa maneno tuliyosema, anaweza akatujibu vibaya, na maneno makali zaidi na zaidi yakaendelea, watu wakashindwa namna ya kuyatuliza (ms. 5-6).
Yakobo anasema hili ni jambo la hatari sana; ni kama kuwashwa, âmoto na jehanumâ. Yesu ni mtu mwingine pekee katika Biblia (ukimwacha Yakobo), aliyelitumia neno âjehanumâ. Tunafahamu kuwa Jehanum lilikuwa ni âdampoâ la takataka nje kidogo ya Yerusalemu, mahali ambapo Wayahudi walitupia takataka zao kuteketezwa. Moto huo haukuwa ukizimika, na Yakobo anatuambia kuwa, hasira na migogoro tunayoweza kuisababisha kwa maneno yetu ya bure; maneno ya kizembe, ni kama moto usiozimika.
4. Hakuna anayeweza kuudhibiti ulimi; umejaa sumu (ms. 8). Haya ni maneno yanayofanana na yale anayosema mwandishi wa Zaburi: âWatu wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao, tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo. Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka, mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake, asiyesikia sauti ya waganga, ijapo wanafanya uganga kwa ustadiâ (Zab. 58:3-5).
Kama ambavyo muumo wa nyoka unavyokuwa wa sumu na unavyoweza kuua, ndivyo ambavyo maneno ya mtu mwovu yanavyoweza kusababisha madhara makubwa kiroho.
5. Tusitumie ndimi zetu kumwabudu Mungu na kumsifu, na tena kwa kuwalaani wengine (ms. 9).
6. Ndimi zetu zinaonesha kilichopo mioyoni mwetu. Tunaporinga au kusema maneno yanayouma kwa wengine, tunakuwa tunasema âuongo juu ya kweliâ (ms. 14, 15).
7. Ni wajibu wetu kuongea maneno yanayoonesha hekima ya Mungu na hulka yake katika maisha yetu, na wakati wote tupende kufanya suluhu; kuleta amani (ms. 17, 15).
Ghadhabu
Ni wakati tunapokuwa na hasira na mtu, tunapojisikia kusema maneno yanayouma. Tunaweza kuwa tumeudhiwa na kitu kilichosemwa juu yetu, na tunataka kumrudishia maudhi. Mfalme Daudi alikuwa mtu aliyelielewa hili vizuri. Alikuwa ameudhiwa mara nyingi katika maisha yake na mambo watu waovu waliyokuwa wakisema juu yake. Kwa hekima kubwa alisema uzeeni:
âUsikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, kama miche mibichi watanyauka.
Umtumaini Bwana ukatende mema, ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa Bwana, naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya. Ataitokeza haki yako kama nuru, na hukumu yako kama adhuhuri.
Ukae kimya mbele za BWANA, nawe umngojee kwa saburi; usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, wala mtu afanyaye hila. Ukomesha hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojeao BWANA ndio watakaorithi nchi.
Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, utapaangalia mahali pake wala hatakuwepo. Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha na wingi wa amaniâ (Zab. 37:1-11).
Ni ushauri wa maana sana uliopo katika maneno haya. Ni sharti tumtumaini Mungu, na sio kujali sana watu wengine wanayosema. Wale ambao ni wapole wa wenye kupenda amani, watairithi nchi lakini watu waovu watatoweshwa milele. Tumwachie Mungu mwenyewe kuhukumu, ni yeye anayeyajua mambo yote; tusiwalaani wengine kwa yale tunayosema juu yao.
Paulo anaongezea kitu katika ushauri huu:
âMuwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatokaâ¦Neno lolote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya. Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyiâ (Waefeso 4:26, 29-32).
Kama tunavyomuomba Mungu kwamba aweze kutusamehe dhambi zetu, na kwamba asiweke hasira juu yetu kwa sababu ya yale tunayofanya, nasi inatupasa tuwasamehe wengine kila siku kwa ajili ya yale wanayosema au wanayotufanyia. Kila siku kabla hatujalala, tunapaswa tuisafishe mioyo yetu na chuki yoyote tuliyoipata juu ya watu wengine. Inatubidi pia tujifunze kuwaomba msamaha wale tunaoweza kuwa tumewaudhi.
Umbea
Umbea ni wakati tunaposema maneno ya âbureâ; maneno mabaya juu ya watu, nyuma ya migongo yao. Inaweza ikawa kitu cha ukweli au kitu cha uongo. Umbea ni dhambi na inafaa tuiepuke kabisa. Tusiwaongee watu wengine kwa ndimi zetu, na haitupasi kusikiliza umbea juu ya wengine. Biblia iko wazi kwenye ujumbe wake juu ya hili. Inasema:
âMtu mshupavu huondokesha fitina; na mchongezi huwafarakanisha rafikiâ (Methali 16:28).
âWalijawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema, ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendaoâ (Warumi 1:29-32).
âBali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu ya kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa. Basi napenda wajane ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, watawale na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumuâ (1 Timotheo 5:11-14).
Kwa bahati mbaya, tunaona habari zinazowahusu watu wengine kama zinavutia, na hasa kama zina taarifa za kuchochewa, au zinakuwa na uovyo fulani. Wakati wote tunapohadithiwa kitu, inatupasa tumsimamishe na kumwambia anayesimulia kuwa, hatuvutiwi. Kuna maswali mawili ya msingi tunayopaswa kujiuliza kuhusu umbea:
- Tungeweza kusema (au kusimuliwa) jambo hilo kama Bwana Yesu Kristo angekuwapo?
- Tungeweza kusimulia jambo hilo kama mtu tunayemsema angekuwa yupo na anasikia?.
Kufuru
Matumizi mabaya, yaliyo mabaya sana ya ndimi zetu, ni wakati tunaposema mambo kinyume cha BWANA, Mungu mwenyewe, au kinyume na Mwanawe. Katika Amri 10, Mungu alisema:
âUsilitaje bure Jina la BWANA, Mungu wako; maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bureâ (Kumb. La Tor. 5:11).
Agano Jipya nalo linasema wazi kitu hicho hicho:
âLakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote: hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenuâ (Wakolosai 3:8).
Neno lililotafsiriwa âmatukanoâ lilipaswa kutafsiriwa âkufuruâ, maana ndilo linalomaanishwa. Ni neno âblasphemyâ kwa lugha ya Kingereza, katika Biblia ya Kingereza (KJV).
Tunapaswa kuliheshimu sana jina la Bwana Mungu na la Mwanawe katika maisha yetu. Tusiyatumie kwa namna isiyo ya heshima. Tusiyatumie kimazoea, au kama sehemu ya lugha-mbaya, au kwa kuapa. Maana ya âkukufuruâ ni âkuchukulia kwa dharauâ. Tunapolitumia vibaya jina la Mungu, ni kama hatumheshimu; tunamdharau.
Bwana Yesu alilipeleka hili mbali zaidi. Alisema tusiape kabisa, tusiape kwa âvichwa vyetuâ (Mathayo 5: 33-37). Leo, kama watu wakitaka kuonesha kuwa wanachosema ni kweli kabisa, wanasema kwa âkuapa mbele ya Munguâ. Hili linakuwa hasa linatakiwa, kama ingetokea kuitwa kutoa ushahidi mahakamani. Kamwe tusikubali kufanya hivyo.
Kama âshahidiâ ni kweli tunaweza tukatakiwa kuapa kwa Biblia, kwamba lile tutakalosema ni kweli kabisa, lakini mfuasi wa Bwana Yesu Kristo hatafanya hilo. Ataomba tu athibitishe kuwa atakachosema ni kweli. Andiko linasema:
âLakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kingine chochote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumuâ (Yakobo 5:12).
Maneno ya upuuzi
Ni rahisi sana kutumia ulimi tuliopewa, kwa namna ya kipuuzi. Tunaweza kushawishika kusimulia habari chafu, yenye matusi ndani yake. Tunaweza kutoa mzaha unaochekesha, unaowafanya wanaocheka wawabeze watu wengine. Tunaweza kuingia katika mjadala usio na maana; usio na manufaa yoyote. Yote haya ni âmaneno ya upuuziâ, hayatusaidii kuwa wafuasi walio bora zaidi kwa Bwana wetu Yesu, na hayatupi kuwa kielelezo kizuri kwa wengine. Neno linasema:
âLakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wala kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuuzi wala ubishi, hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuruâ (Waefeso 5:3, 4).
ââ¦wasimtukane mtu yeyote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu woteâ¦lakini maswali ya upuuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana. Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka tena atenda dhambi; maana amejihukumu hatia yeye mwenyeweâ (Tito 3: 2,9-11).
Mfano wa Yesu
Tunapohitaji hasa kujua namna ya kuongea mmoja kwa mwingine, tunahitaji kumtazama Bwana Yesu Kristo. Alikuwa mkamilifu kwa kila hali; kila neno alilotamka lilikuwa ni la Ki-mungu na sahihi. Nabii Isaya alinena juu yake kuwa:
âHatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashindaâ (Mathayo 12:19, 20).
Yesu hakupiga kelele wala kugombana. Wazo la âmwanzi uliopondeka na utambi utokao moshiâ ni lugha ya kiushairi; anasemea wale walio wadhaifu kiimani. Yesu hakuizima au kuivunja imani yao kwa maneno makali; alifanya aliloweza kuwafanya waendelee na imani yao kwa huruma yake.
Watu walimdhihaki na kumbeza Yesu. Waliolewa (pombe) walitunga nyimbo mbaya juu yake. Watu walimcheka na kumkejeli alipokuwa akiningânia msalabani, lakini bado ikawa hivi:
âAlionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake, kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chakeâ¦.Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; na pamoja na matajiri katika kufa kwake; ingawa hakutenda jeuri wala hapakuwa na hila kinywani mwakeâ (Isaya 53:7, 9).
ââ¦Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwaka. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa hakuogofya (hakutishia). Bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.
Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na mwangalizi wa roho zenuâ (1 Petro 2:21-25).
Hivi ndivyo tunavyopaswa kuutumia uwezo wa ndimi zetu. Hatukupewa nguvu iliyopo katika kusema ili kujitetea, au kufanya mabishano makali. Tumepewa kusema maneno ya Mungu, kufuata mfano wa Bwana Yesu alivyokuwa, katika maisha yetu ya kila siku, kusudi maneno yetu yawe ya kheri wakati wote na ya kumpendeza Mungu.