Correspondance Course - Lesson 40

Swahili

Somo la 40

HUDUMA YA KUMEGA MKATE

Somo: Mathayo 26

Katika somo la 31 tuliona kwamba, ubatizo ni mwisho wa maisha yetu ya kwanza, na mwanzo wa maisha mapya katika Kristo. Tunakuwa sehemu ya familia ya Mungu; wanawe wa kiume na wa kike, na kwa hiyo tunakuwa kwa pamoja ni ndugu katika Kristo. Tunakuwa ‘wafuasi’ wa Yesu; neno lenye maana ya ‘wanafunzi’; watu wanaojifunza kumfuata mtu. Tunaweka maisha yetu katika kuyafuata maneno ya Yesu na mfano wake. Mwenyewe alisema:

“Hakuna aliye na upendo mwingi kama huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa, maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu” (Yoh. 15:13-15).

Hili ni jambo la maana sana. Uhusiano wetu na Yesu unategemea sisi kuyafanya mambo anayotuagiza tufanye. Mojawapo ya mambo ya maana sana aliyotuamuru tufanye, ni kukutana mara kwa mara kula mkate na kunywa divai kwa kumkumbuka:

“Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.

Kwa namna hiyo hiyo alichukua kikombe baada ya kula, akasema:

“Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu” (1 Wakorintho 11:24-26).

Ibada ya pamoja kwa Wakristo wa kweli ni kitu kirahisi na chepesi. Ukiondoa Ubatizo, Kumega Mkate ni kitendo pekee cha kiitikadi Bwana Yesu Kristo alichotuagiza kufanya; mengine ni watu wameongezea tu. Ni lazima tukipe uzito wake unaostahili.

Tunafahamu ya kuwa baada ya Yesu kupaa, wanafunzi wake walikutana kila siku nyumba kwa nyumba kumega mkate na kunywa divai kumkumbuka (Matendo 2:46, 47). Baadaye eklesia zilikutana kila juma siku ya kwanza ya juma; Jumapili, kufanya hili. Kwenye Matendo 20:7 wanafunzi walipokuwa wamekutana katika siku ya kwanza ya juma Kumega Mkate, Paulo aliwahubiria.

Chini ya Sheria ya Musa, Wayahudi walikutana Jumamosi, siku ya mwisho ya juma, kwa ajili ya pumziko; Sabato. Wanafunzi wa Yesu waliamua kukutana katika siku ya kwanza ya juma, kwa kuwa ndiyo siku Yesu aliyofufuka kutoka kwa wafu. Uamuzi huu wa kukutana kila juma kwa namna hii, pengine ulifuatia kipengere cha Kimaandiko kilichohusu chakula cha kila juma,  kilichokuwa kikiliwa na makuhani, kilichoitwa ‘mkate-wa-wonyesho’ katika Agano la Kale (Walawi 24:5-9).

Yesu alipotumia neno ‘ukumbusho’, alitumia neno lisilo la kawaida katika lugha ya Kiyunani lililopo kwenye Walawi 24:7. Kama mkate-wa-wonyesho ulivyokuwa wa kipekee, na wa thamani kwa makuhani katika nyakati za Agano la Kale (na ni makuhani tu walioruhusiwa kuula), ndivyo ambavyo Kumega-Mkate kulivyo kitu cha kipekee, kitakatifu, na cha thamani kubwa kwa wanafunzi wa kweli wa Yesu, wanaoshiriki kitendo hiki leo. Hawakifanyi na watu wengine, hata kama wanajiita Wakristo. Ni wale tu ambao ni ndugu wa kweli wa Kristo.

Kila mahali walipo Wakristadelfia duniani, wanakutana kila Jumapili kushiriki mkate na divai kwa pamoja kwa namna hii. Wanafanya hivi kwa kawaida katika kumbi au vyumba vya kupanga, na mara nyingine nyumbani mwa muumini mwenzao; haijalishi ni wapi.

Huduma yenyewe haina mambo mengi, na inafanana popote pale inapoendeshwa katika dunia. ‘Kumega Mkate’ kama tunavyokuita, ni sehemu ya muhimu sana ya ushirika wetu wa pamoja, na Wakristadelfia wanajua hivyo. Popote wanapokwenda, kama kuna Eklesia, wanaweza kwenda kwenye Eklesia yoyote na kushiriki mkate na divai na wale wanaoabudu pale.

Yesu alitoa maelekezo kadhaa kuihusu huduma hii. Tuyajadili moja moja:

  1. ‘Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’ (Luka 22:19).

Ni Yesu ambaye anayepaswa kuwa chumbuko la mawazo yetu tunapokutana Kumega Mkate. Ndiye msingi, kwa hiyo mawazo yote yanapaswa kuwa kwake. Kama fikra zetu zipo kwenye migogoro na ndugu wengine, au katika matatizo ya kimaisha ya kila siku tuliyo nayo, tunakuwa tumeshindwa kuizingatia amri hiyo.

Neno ‘ukumbusho’ halina maana hapa ya kukumbukia tu kitu tulichosahau; maana yake ni kuijaza akili yetu Yesu. Tunakumbuka kuwa alikufa katika kipindi cha Pasaka. Haya yalikuwa majira ya mwaka ambapo Waisraeli walikumbuka namna  ambavyo Mungu aliwaokoa kutoka katika utumwa, Misri. Alimteua Musa kuwaongoza watoke alfajiri baada ya usiku wa Pasaka, walipomchinja mwana-kondoo kifamilia na kumla pamoja kusherehekea wokovu wa Mungu.

Biblia inatufundisha kuwa, Kristo ndiye Mwana-kondoo wa kweli; alikufa kuwa dhabihu ya kuzichukua dhambi zetu. Kwa hiyo tunashiriki mkate na divai kila juma kukumbukia kuwa, kupitia katika kifo chake, tunaokolewa kutoka kwenye utumwa wa dhambi na mauti:

“Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu (tule mkate na kunywa divai), si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli” (1 Wakorintho 5:7, 8).

Tunapokunywa divai tunakumbuka kuwa, dhabihu ya Yesu ilileta mustakabali mpya wa Agano Jipya. Huu ni uhusiano mpya kati ya Mungu na watu wake. Mustakabali huu mpya unakamilisha ahadi zote za Mungu alizozifanya na watu katika enzi ya Agano la Kale. Yesu ni Mpatanishi wa Agano hili, na kwa sasa yupo mbinguni kuwakilisha maombi yetu kwa Mungu, na kutuombea msamaha wa dhambi zetu tunapoomba kuzikiri:

“(Yesu) sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora” (Waebrania 8:6).

Haya ni mambo yanayomhusu Bwana Yesu, ambayo tunapaswa yatujae katika akili zetu, tunapokuwa katika Kumega Mkate. Lakini kuna lingine zaidi.

Mtume Paulo aliandika maneno haya: “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1 Wakorintho 11:26).

Ni nani tunayemwonesha au kumtangazia mauti ya Bwana? Kwa hakika ni Bwana Mungu, na sisi wenyewe kwa wenyewe. Mkate na divai vinapopita kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine, muumini kwa muumini, kila mmoja wetu anaonesha kutambua haja tuliyonayo ya dhabihu ya Yesu kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu. Tunaona kuwa Yesu alikufa kwa ajili ya ndugu yetu na kwetu pia.

Hili linasaidia kutuunga tuwe kitu kimoja katika ushirika wa kiimani. Tunakuwa mwili mmoja wa waumini wenzetu tunaoishi na kuabudu nao pamoja, wakati tukimngojea Bwana Yesu arudi:

“Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1 Wakor. 10:17)

2. ‘Lakini mtu ajihoji mwenyewe’ (1 Wakorintho 11:28)

Yesu hakusema kwamba tuchunguzane! Hatuendi kwenye Kumega Mkate tukiwa tunachunguza makosa ya wafuasi wengine! Tunajichunguza wenyewe kuona kama makusudi na nia zetu zipo kweli kwenye ibada yetu.

Tunamkumbuka Yesu na maisha yake makamilifu ya utii, na kisha tunajipima kwa kujilinganisha naye. Hili kwa vyovyote litatufunya tujisikie wadhaifu sana mbele ya Mungu, maana ndivyo tulivyo. Kama tuna fikra zozote za kujiona wema-zaidi au bora-zaidi kuliko ndugu zetu, ni lazima tuziondoe kabla ya kula mkate na kunywa divai. Kuna tahadhari anayoitoa Yesu katika Mathayo 5:23, 24. Tafadhali isome.

Kuna wakati ndugu wanashindwa kufanya hili. Wanakuja na ugomvi katika Kumega Mkate, au hawaji; wanajitenga. Wanafanya hivyo kwa kuwa wanashutumiana. Mtume Paulo aliandika maneno makali sana juu ya hao wanaofanya hivyo:

“Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala’ (1 Wakor. 11.27-30).

Hana maana ya kwamba ‘walio hawawezi na dhaifu’ walikuwa kimwili wagonjwa, bali kwamba ni wagonjwa kiroho, wanaelekea kufa. Kama ambavyo tunahitaji chakula halisi kuifanya miili yetu iendelee kuishi, ndivyo ambavyo tunahitaji chakula cha kiroho kwa njia ya mahubiri katika Kumega Mkate, ili tuweze kuendelea kuwa na uhai kiroho.

Tuwe macho! Ni rahisi wakati wote kuona makosa ya watu wengine kuliko kuyaona ya kwetu wenyewe (Mathayo 7:1-5). Tunapokuja kula mkate na kunywa divai, tunapaswa kuwa wakweli kabisa juu ya nafsi zetu mbele ya Mungu. Hata Yesu alijipima kwa namna hii muda mfupi kabla ya kufa msalabani.

Katika bustani ya Gethsemane, alikuwa na uchungu mkubwa alivyokuwa akishindana na nafsi yake. Alimwomba Mungu kwa huzuni amsadie ili aweze kuyafanya mapenzi yake Mungu na kulitimiza kusudi lake; ashinde udhaifu wake. Hivyo ndivyo nasi tunavyotakiwa kufanya tunavyojichunguza kabla ya kula na kunywa kwa kumkumbuka Yesu.

Mkate na Divai

Sasa tuutazame mkate na divai. Luka anaandika maneno yafuatayo kuuhusu mkate:

“Akautwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’ (Luka 22:19).

Tunapouchukua mkate na kuula, haubadiliki kimuujiza na kuwa sehemu ya mwili wa Yesu. Hakuna kitu kinachoitwa ‘mkate mtakatifu’ unaopaswa kutumika; tunatumia mkate wa kawaida katika kuabudu kwetu. Mkate ni alama (au ishara) ya mwili wa Yesu. Unawakilisha kwetu maisha yake yote, jinsi alivyokuwa na hulka kama yetu na alivyojaribiwa kama na sisi tunavyojaribiwa, lakini hakukosea.

Yesu hakufanya dhambi yoyote katika mambo yote aliyofanya; alipenda kuyafanya mambo Mungu anayoyapenda (Zaburi 40:8). Hili lilimfikisha msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Haya ndiyo mambo tunayokumbuka tunapokula mkate.

Kuihusu divai Bwana Yesu alisema: “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:20).

Biblia inasema waziwazi kuwa, kumwagika damu ni kitu cha lazima kwa Mungu kuweza kusamehe dhambi:

“Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo” (Waebrania 9:22).

Katika Sheria kulikuwa na dhabihu za wanyama, lakini hazikuwa na uwezo wa kuondoa dhambi moja kwa moja. Ni kwa kifo cha Yesu, kwa kumwagwa kwa damu yake ndipo Mungu aliporidhia msamaha wa dhambi. Kila wakati tunapokuwa tukinywa divai, tunakumbuka hili. Linatukumbusha juu ya gharama kubwa sana iliyolipwa kwa ajili ya dhambi zetu.

Tunavyokunywa tusiruhusu kiburi chochote kikae ndani yetu. Hakuna nafasi ya chochote kingine zaidi ya kujinyenyekeza kabisa kwa kutambua kuwa, Mungu alitupenda sana, hata akamtoa Mwanawe wa pekee kufa kwa ajili ya dhambi zetu kuzisamehe:

“Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu, bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani, ya Kristo” (1 Petro 1:18, 19).

Mpaka ajapo

Mpaka sasa tumetazama jinsi ibada ya Kumega Mkate inavyotukumbusha juu ya kifo cha Yesu Kristo. Wale ambao wanakula na kunywa kwa namna hii mara kwa mara, wanazijaza akili zao kumbukumbu hii ya Kristo, na hili linawasaidia katika ufuasi wao siku kwa siku. Kuabudu kwa namna hii ni kwa muhimu sana, ili tuweze kuendelea kuimarika kiroho.

Hata hivyo, kuna kipengere kingine katika Meza hiyo ya Bwana, ambacho mara kwa mara tunakisahau. Yesu alikuwa akitazamia kurudi kwake, na kuusimamisha Ufalme wa Mungu katika dunia. Aliwaambia wanafunzi wake:

“Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi Ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli” (Luka 22:28-30).

Bwana Yesu atakaporudi, atakaa na wanafunzi wake na kula na kunywa pamoja nao katika Ufalme wake. Kwa hiyo, tunapokutana Kumega Mkate, tunafanya jambo la muhimu sana kwetu, litakalokamilishwa katika Ufalme wa Mungu.

Kila mfuasi wa kweli anataka kuwa katika Ufalme huo siku hiyo, na ni muhimu asikose kuwa katika ushirika wa Kumega Mkate, katika maisha yake ya sasa. Ni ushirika wa namna hii unaotupa nguvu tunavyoendelea kumsubiri Bwana wetu arudi:

“Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani mwili wake, na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli; kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya; tumeoshwa miili kwa maji safi.

Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. Tuangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane, na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia” (Waebrania 10:19-25).

Swahili Title
Huduma ya Kumega Mkate - Somo la 40
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission