Correspondance Course - Lesson 42

Swahili

Somo la 42

MAISHA YA KRISTO - Dhambi

Somo: Warumi 7

Ulevi wa Dhambi

Kuna nguvu katika maisha ya kila mmoja wetu inayotushinda. Ni ulevi unaozidi ulevi wa pombe, kamari au madawa ya kulevya, nao ni ulevi wa ‘dhambi’. Ni tatizo linalotukamata vibaya; tunakuta tumekosea na inakuwa vigumu kujizuia, na tunavutwa kuendelea hivyo.

Watu wengi hawautambui, na wanakana hawako katika hali ya ulevi huu. Lakini, ni kama mlevi anavyoweza kukana kuwa sio mlevi, kwa kuwa hataki kulikubali tatizo lake. Dhambi inalewesha!

Lakini matokeo yake ni mabaya mno. Biblia inatuambia kuwa, matokeo ya kulewa dhambi ni mauti. Dhambi inaua: ‘Mshahara wa dhambi ni mauti’. Katika Waraka kwa Warumi, mtume Paulo anatuambia juu ya tatizo hili katika maisha yake mwenyewe, akisema:

“Mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo… Ole wangu, maskini mimi!” (Warumi 7:14-24).

Hiki ni kifungu kimojawapo kinachochunguza sana moyo katika Agano Jipya. Paulo anatuambia kuwa, akilini mwake anataka kuzitii sheria za Mungu, lakini vitendo vyake ni vya dhambi. Ni kama yeye ni watu wawili tofauti: mmoja ni mtu mwenye akili inayoelewa kuwa anatakiwa amtii Mungu; na kwa dhati anatamani kufanya hivyo. Lakini, mwingine ni mtu ambaye wakati wote hamtii! Hili ni mojawapo kati ya matatizo makubwa sana ya ‘ufuasi’.

Mara kwa mara tunajua lililo sahihi, lakini hatulifanyi katika maisha yetu. Ni kwa nini tuko hivyo? Sehemu ya jibu ni kwamba, tunaweza kuwa tunafurahia kuwa hivyo; kutofanya lililo sahihi! Hakuna anayetulazimisha kutenda dhambi; tunatenda dhambi kwa kuwa tunajisikia vizuri kufanya hivyo, hata kama tunajua hili linaweza kutufikisha kwenye mauti ya milele. Lakini, juu ya Musa tunaambiwa:

“Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo” (Waebrania 11:24, 25).

Katika Warumi 6 Paulo aliandika juu ya watu kuwa ‘watumwa wa dhambi’. Dhambi ni ‘bwana’, ni mtawala huyu. Dhambi inawatawala watu. Ni vizuri tutambue ya kwamba, ni mtawala jeuri sana huyu, anayewalipa wafanyakazi wake kifo. Anawazalia mauti! Ni mara nyingi Biblia inaionesha dhambi kwa namna hiyo. Ni nguvu inayotawala juu yetu, na hatuwezi kuikwepa kwa jitihada zetu wenyewe.

Sehemu ya pili ya jibu ni kwamba, tunaona vigumu kumtii Mungu. Hata tunapokuwa tunajua lililo sahihi na tunajaribu kulifanya, mara nyingi tunashindwa. Nia ya kuwa wafuasi wa kweli wa Bwana Yesu Kristo inapaswa iwe ndani ya mioyo yetu. Kama tukijaribu kumfuata kwa kulazimishwa, kwa hakika, tutashindwa. Kama tukitaka kumfuata kwa sababu mioyo yetu imejaa kumpenda na Baba yake, kwa ajili ya wokovu uliowekwa mbele yetu, tutakuwa tumeanza ufuasi wetu vizuri; kwa dhamiri iliyo sahihi. Andiko linasema:

“Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa (Yesu)amewajibu vema, akamuuliza, katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Na Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote” (Marko 12:28-30).

Dhambi ni nini?

Dhambi ni kuzikiuka sheria za Mungu, na adhabu yake ni kifo:

“Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti, na hivyo mauti imewafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi… Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Warumi 5:12, 19).

Tunahitaji kurudi nyuma kwenye Bustani ya Edeni ili tuweze kuona kilichokuwa chanzo cha dhambi. Hapo mwanzo, Mungu alipokuwa amemuumba Adamu, alimpa amri moja tu ya kutii. Adamu alikatazwa asile tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 2:17). Mungu alimuonya kuwa kama angekula, kwa hakika angekufa. Ni kwa nini alipewa sheria ya namna hiyo? Adamu na Hawa waliumbwa kumpa Mungu ‘utukufu’ kwa kulitii Neno lake. Waliumbwa wawe na matakwa huru; wachague wenyewe kama wamtii Mungu au wasimtii.

Sheria hii iliwapima walikuwa na moyo wa kujitoa kwa Mungu kiasi gani; wangekuwa na imani ya kumtii Mungu au wangemkiuka. Mungu alikuwa sio tu Muumba-Mkuu aliyeiumba dunia, alikuwa pia ni YEYE aliyekuwa juu ya vitu vyote, ambaye Neno lake halipaswi kuvunjwa. Adamu alipomtii Mungu, alionesha kulitambua hili na kulikubali; alipomkiuka, aliukana uweza wa Mungu na mamlaka yake juu yake. Kifungu kwa Warumi kinasema:

“Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumba ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani uweza wake wa milele na Uungu wake: hata wasiwe na udhuru; kwa sababu walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.

Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakamsujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina” (Warumi 1:19-25).

Ingawa maneno haya hayakuandikwa moja kwa moja kumhusu Adamu na Hawa, hoja nyingi zinazotolewa zinahusiana na maisha yao nao, na zinatusaidia kuona jinsi dhambi ilivyoingia ulimwenguni. Ni kwamba:

  1. Uweza wa Mungu ulioneshwa kwa watu, kwa vitu Mungu alivyoviumba (Zaburi 19). Adamu na Hawa walilipuuza hili.
  2. Dhambi ilianzia kwenye akili ya Hawa, alipoamua kuwa alichokitaka kilikuwa ni cha muhimu zaidi kwake kuliko kuitii amri ya Mungu. Kujaribiwa kwake na dhambi ili amkiuke Mungu, kuliugusa moyo wake na akili yake. Alilitamani lile tunda la ule mti; alitaka hasa kulila (Mwanzo 3:6).
  3. Hawa alifikiri angeerevuka kwa ujanja wake mwenyewe, kwa kulila lile tunda. Kwa kufanya hivi aliukana uweza uliopo katika Neno la Mungu wa kumhekimisha ‘hata apate wokovu’ (2 Timotheo 3:15).
  4. Aliamua kuwa sheria ya Mungu haikuwa hasa kweli, ila uongo; na kama akilila tunda asingekufa kikweli. Kwa hiyo alilila na kumpa mumewe ambaye naye alikula.
  5. Kwa vitendo vyao walijiweka wenyewe mbele na kile walichotaka, kuliko amri ya Mungu.

Walikuwa wakipaswa kumwabudu Mungu, Muumba, kwa kuwa watiifu kwake. Ukweli huu wa mwisho (kipengere cha 5), unatupa ukweli wa muhimu sana. Ibada kwa Mungu ni kuwa watiifu kwake katika maisha yetu ya kila siku; sio tu kwa kukutana pamoja kumsifu siku za Jumapili.

Kwa hiyo, dhambi sio tu kutozitii amri za Mungu; ni kukana pia uwepo wake, kama Muumba aliyetuumba sisi wote. Tukilitambua hili na kulipokea, litabadili mtizamo wetu wote wa maisha.

Kumtupia mwingine lawama

Adamu alijua nini kingetokea hata kabla ya kufanya dhambi, kwa kuwa: “Kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria” (Warumi 3:20).

Mungu alipompa Adamu amri hiyo moja, alimwambia dhambi yenyewe ilivyo na matokeo yake – kifo! Adamu na Hawa waliona shida kuwajibika kwa kitendo chao; na sisi ndivyo tunavyofanya. Sisi wote tunataka kumtupia mtu mwingine lawama kwa makosa yetu. Adamu alisema:

“Huyu mwanamke aliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala”. Na Hawa alijitetea, akisema: “Nyoka alinidanganya, nikala”.

Mafundisho potofu yaliyoenea juu ya ibilisi na shetani, yanatokana na hiyo nia ya kumlaumu mtu mwingine kwa ajili ya dhambi zetu. Tunapokosea, ni rahisi sana kulaumu ‘shetani’ badala ya kukubali kuwa tatizo liko ndani yetu. Tunajidanganya kuwa sisi tuko safi, hatuna dhambi; wa kulaumiwa ni ibilisi, anayesababisha. Nabii Yeremia akilitambua tatizo, alisema: “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha” (Yer. 17:9).

Lakini Biblia haitaki tujiongopee, inasema:

  • “(Yesu)Akasema, kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7:20-23).
  • “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike” (Yakobo 1:13-16).

Nyoka alichofanya kwanza kilikuwa ni kuweka wazo la kula tunda lililokatazwa, kwenye akili ya Hawa. Tangu hapo, kwenye Biblia, nyoka amekuwa ishara ya ‘nguvu ya dhambi na matokeo yake’ katika maisha yetu. Tamaa hii ya kujifurahisha wenyewe badala ya kutaka kumfurahisha Mungu inatuvuta tusimtii; inatuvuta tufanye dhambi. Hebu angalia vifungu hivi vitatu vinavyofuata, vinavyotuambia juu ya watu wasiomtii Mungu:

  • “Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana, kwa kuwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi” (Waefeso 5:6).
  • “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake” (1 Yohana 3:9-10).
  • “Hata alipoona wengi miongoni mwa mafarisayo na masudukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya nini kuikimbia hasira inayokuja?” (Mathayo 3:7).

Katika mfano wa ‘Mpanzi’ katika Luka 8 Yesu anatuambia kuwa, ‘mbegu ni neno la Mungu’ (ms. 11). Kwa hiyo wale wanaolichukua Neno la Mungu katika mioyo yao na katika maisha yao, wanaweza kuelezewa kama wanaochukua ‘mbegu ya Mungu’; wanakuwa ‘uzao wake’. Ni kile Neno hilo linachofanya ndani yao ndicho kinachosaidia kuwafanya wawe ‘watoto wa Mungu’, na kuanza maisha mapya.  Matokeo yake ni kwamba, wanaweza kujitoa kwa Mungu sasa, badala ya kuendelea kuwa ‘watumwa wa dhambi’.

Lakini kila kimoja kati ya vifungu hivyo, kinatuambia pia juu ya daraja lingine la watu. Ni hao wanaoupuuza ukweli wa Neno la Mungu na kuendelea kwa namna zao wenyewe katika maisha. Hao wanaelezewa kuwa ni ‘wana wa uasi’, ‘watoto wa ibilisi’ na ‘wazao wa nyoka’. Wako kama Adamu, aliyemwacha Mungu na kumkiuka kwa makusudi.

Tumeshaona kuwa, mauti ni adhabu inayotokana na dhambi. Kila siku tunavyoendelea kukua na kuwa wakubwa na kuzeeka, na miili yetu inapoanza kuchoka, tunaonesha lilivyo kweli Neno la Mungu. Hatimaye, tunakufa! Tunaweza kumkana Mungu kwa maneno na matendo yetu, tunaweza kujifanya hayupo, lakini hakuna tunachoweza kufanya kuyashinda mauti.

Ni adhabu iliyowekwa juu yetu kwa sababu ya dhambi. Dhambi inatutenganisha na Mungu, lakini kuna lingine linalotokana na dhambi. Inatupeleka mbali na Mungu. Nabii Isaya, anasema: “Maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia” (Isaya 59:2).

Adamu na Hawa walipofanya dhambi, walihukumiwa kifo. Waliondolewa na Mungu watoke katika Bustani ya Edeni. Hili ndilo hasa balaa la dhambi. Adamu alipoondoka katika Bustani hiyo, alipoteza ushirika wake wa kila siku aliokuwa akiufurahia na Mungu. Nguvu ya Mungu na Neno lake katika maisha ya Adamu ilipungua siku baada ya siku.

Mawazo yake yaliendelea kirahisi zaidi kujaa tamaa zake, na hivyo ikawa rahisi zaidi kwake kuendelea kuanguka dhambini. Hii ndio maana ya Yakobo kuongelea, ‘kuvutwa na kudanganywa na uovu’. Maana yake ni kwamba, dhambi inatuvuta mbali na Mungu.

Tunapokuja kutambua mafundisho haya ya ukweli kuhusu ‘dhambi’ kama yalivyo katika Biblia, yatakuwa na mguso mkubwa katika maisha yetu. Tunaweza kuhitimisha kihivi:

  1. Kwanza ni lazima tutambue kuwa, kwa mambo yoyote yale mabaya tunayofanyiana, hatimaye tunayekuwa tumemkosea ni Mungu. Ni neno laki tunalolikiuka.
  2. Kila kitu ambacho kinaikiuka sheria ya Mungu hakikubaliki kwake, na vyote ni ‘dhambi’.
  3. Kama tumeyaweka maisha yetu kwa Mungu kupitia kwa Mwanawe, Yesu Kristo, hatuwezi kuendelea katika dhambi.
  4. Kuyaweka maisha yetu kwa Mungu hakuna maana kwamba tutakuwa wakamilifu, watu wasiokosea. Ni Yesu tu aliyekuwa hivyo!

Mungu hatawakubali watu wanaosema ni wafuasi wa Yesu, lakini hawafanyi jitihada zozote kumfuata kwa namna wanavyoishi maisha yao, wakati wamebatizwa. Maisha yetu ni sharti yabadilishwe na kumfahamu kwetu Kristo. Mwenyewe alisema:

“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).

Kuipata tena Njia ya Mungu

Mwanzoni kabisa wa huduma yake, Yesu alipanda mlimani na kuanza kuwafundisha wanafunzi wake kwa maneno matamu ya mibaraka, akisema: “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Mathayo 5:3). ‘Maskini wa roho’ ni watu ambao wanajua wanavyomhitaji Mungu. Mahusiano yetu na Mungu ndipo yanapotakiwa kuanzia.

Ni hapo tunapotambua mioyo yetu ilivyo na jinsi dhambi ilivyo ndani yetu, na vile inavyotutenganisha na Mungu, ndipo tunapoelewa tunavyomhitaji Mungu katika maisha yetu. Ndipo tunapoweza kuwa tayari kuanza safari ya kumrudia na kumkaribia Mungu kwa maombi, na kuitaka rehema yake na msamaha.

Kama tunamkaribia kwa namna hii, tunajua kuwa atatupokea kama wanawe, kupitia kwa Bwana Yesu Kristo. Dhambi haitakuwa tena ‘bwana’ katika maisha yetu. Mwishoni mwa maneno yale machungu ya kujichunguza katika Warumi 7, mtume Paulo alisema:

“Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu! (War. 7: 24, 25).

Ujumbe mwema wa faraja wa Biblia, ni wa wokovu dhidi ya dhambi na matokeo yake, kupitia kwa Bwana Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kwa hiyo Paulo aliendelea kusema:

“Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Warumi 8:1, 2).

Tunapaswa kwa mioyo yetu kumshukuru Mungu na kufurahi kutokana na hili. Hii ni Habari Njema, ni ujumbe wa Injili unaohitimishwa kwa mstari mmoja:

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16).

Tunapojitoa kwa Bwana Yesu Kristo kuwa wafuasi wake, tunaanza maisha mapya. Dhambi zetu zinasamehewa bure na Mungu aliyejaa huruma na rehema, ambaye hapendi yeyote apotee. Anapenda watu wote wamkubali Mwanawe na kutembea kuuelekea Ufalme wake.

Sehemu iliyobaki ya kozi yetu hii inachunguza mafundisho ya Biblia yanayohusu maisha haya mapya katika Kristo na kile yanachomaanisha kwa kila mmoja wetu. Neno la BWANA linasema:

“Sheria ya BWANA ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa BWANA ni amini, humtia mjinga hekima. Maagizo ya BWANA ni ya adili, huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, huyatia macho nuru. Kicho cha BWANA ni kitakatifu, kinadumu milele. Hukumu za BWANA ni kweli, zina haki kabisa. Ni za kutamanika kuliko dhahabu, kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, kuliko sega la asali. Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi” (Zaburi 19:7-11).

Swahili Title
Maisha ya Kristo - Dhambi
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission