Correspondance Course - Lesson 43

Swahili

Somo la 43

MAISHA YA KRISTO - Kusoma

Somo: Kumb. La Torati 6

Israeli wakiwa Nyikani

Agano la Kale linatupa simulizi la ajabu la namna Mungu alivyowaokoa watu wake, Israeli, kutoka katika nchi ya Misri. Walikuwa wamekaa hapo wakiwa watumwa kwa zaidi ya miaka 200. Walikuwa wameteswa, na mfalme (Farao) alijaribu kuwaua watoto wa kiume wote waliozaliwa kwa Wayahudi. Israeli walimlilia Mungu wakimueleza taabu yao, na Mungu alisikia kilio chao na kumtuma mwokozi wao, Musa, kuwatoa katika Misri.

Wokovu wao ulitegemea kutii kikamilifu maneno ya Mungu kupitia kwa Musa. Kushindwa kuyatii kungewapelekea kuangamia. Waliamriwa kuiadhimisha karamu ya Pasaka kwa pamoja usiku mmoja. Waliagizwa wakae ndani ya nyumba zao mpaka Mungu awaite, alafu, katika usiku huo waondoke Misri kwa pamoja. Mungu aliwaambia kuwa, Musa angewaongoza kwenda kwenye nchi ya Israeli, nchi aliyokuwa amemuahidia Ibrahimu miaka mingi nyuma.

Walipoondoka walifuatiwa na majeshi ya Farao mpaka kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu. Mmoja kati ya miujiza mikubwa kabisa katika Biblia ulitokea; Mungu aliyatenga maji ya Bahari ya Shamu ili Israeli waweze kuvuka kwenda ng’ambo, na alilizamisha jeshi la Misri lilipojaribu kuwafuatia. Mtume Paulo anatuambia kwamba, tukio hili lilikuwa mfano wa ubatizo:

“Baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari” (1 Wakorintho 10:1, 2).

Ndani ya miezi kadhaa, Israeli walikuwa wamefika Sinai kuzipokea sheria za Mungu. Kwa shauku walimuahidi Musa kuwa, wangemtii huyu Mungu aliyewaokoa:

“BWANA akamwita (Musa) toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya… Sasa basi, ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli. Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote BWANA aliyokuwa amemwagiza. Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda” (Kutoka 19:3-8).

Ilikuwa ni katika maisha yao ya kila siku, ambapo sasa Mungu aliwajaribu kuona kama walikuwa na maana kweli kwa lile walilosema. Walipokuwa na njaa na kiu, Je, wangeyakumbuka maneno ya Mungu na kumtumaini, au wangesahau lile waliloitikia?

Mojawapo ya matukio ya kuhuzunisha sana katika Biblia, ni habari ya jinsi watu wazima wote (kasoro wawili), waliokuwa wametoa ile ahadi kwa Mungu, ‘walivyomwangusha’ Mungu. Walikufa humo nyikani kutokana na dhambi yao, kwa hiyo hawakuwahi kuiingia Nchi ya Ahadi.

Muda mfupi kabla ya Musa kufa, aliwafundisha wana wa hao walioangamizwa humo nyikani, somo kubwa kwa ajili ya maisha yao, kusudi na wao wasianguke:

“Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru BWANA, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki; upate kumcha BWANA, Mungu wako, kushika amri zake zote na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama BWANA, Mungu wa baba zako alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.

Sikiza, Ee Israeli, BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako, nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kumb. La Torati 6:1-9).

Jambo moja liko wazi katika nasaha hizo; maneno ya Mungu yalipaswa yawe na sehemu muhimu katika maisha yao ya kila siku. Walikuwa wayaseme wakati wote, na kuwafundisha watoto wao juu yake. Ilikuwa tu ni kwa njia ya kuyafanya Maandiko kuwa sehemu ya kila kitu wanachofanya, ndipo wangeweza kukumbuka umuhimu wa maneno ya Mungu na kuyatii.

Hebu ona ulinganisho kati ya Wana wa Israeli na sisi hapa. Maisha yetu ni kama yao!

Wana wa Israeli

Wafuasi wa Yesu leo

Walikuwa watumwa Misri

Kabla ya ubatizo tulikuwa  watumwa wa dhambi.

Mwana-kondoo wa Pasaka alitolewa na Mungu kuwa dhabihu ya kuwaokoa

Bwana Yesu Kristo ametolewa na Mungu kuwa dhabihu. Amekufa msalabani kutuokoa.

Israeli waliyaacha maisha ya utumwa Misri

Ni lazima tuyaache maisha yetu ya awali ya utumwa wa dhambi.

Israeli waliivuka Bahari ya Shamu

Tumebatizwa.

Waliambiwa maagizo hayo ni lazima yawe sehenu ya maisha yao ya kila siku

Ni lazima tuisome Biblia kila siku, na kuiruhusu itufundishe na kutuongoza katika kila kitu tunachofanya.

Israeli hawakumtii Mungu na wakafa nyikani. Hawakuifikia Nchi ya Ahadi

Kama Biblia haikuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hatutaufikia Ufalme wa Mungu.

Biblia inamaanisha nini kwako

Inashangaza mara nyingine kuona wafuasi ambao hawajali kuisoma Biblia, na kujifunza inachosema katika maisha yao ya kila siku, wakati wanategemea kuwa na sehemu katika Ufalme wa Mungu Yesu atakaporudi. Kama hatuoni jinsi Neno la Mungu linavyosisimua na kutuvutia sasa, kama hatutaki kujifunza kutoka kwake kila siku, tunawezaje kutegemea nafasi katika Ufalme huo ambao Biblia ndiyo msingi wake?

Tafadhali yafikirie maswali yafuatayo, na ujaribu kuyajibu kwa ukweli na moyo wako kwa ajili yako mwenyewe:

  1. Ni kwa nini Biblia ni ya muhimu kwako? Inakufanya ujione ‘wa maana’ tu kuwa nayo, au ni sehemu ya muhimu ya maisha yako?
  2. Unaifungua na kuisoma mara kwa mara kiasi gani: Kila siku? Kila juma? Mara moja-moja? Unaisoma yote au vile vifungu tu unavyovipendelea?
  3. Unaweza kuifungua vizuri: Unajua Zaburi kilipo? Yuda kipo wapi? Mika je?
  4. Unaweza kupata vifungu vya Biblia kuwaambia watu wengine unayoamini?

Kwa nini ni ‘ngumu’ kueleweka?

Sehemu za Biblia ni ngumu kueleweka. Mungu hakuiandika kwa namna ambayo inatupa majibu mara tunapoisoma. Hebu yaangalie maneno haya:

“Mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu, asema BWANA” (Isaya 55:8).

Katika somo letu la nyuma tuliona ya kwamba, toba ni lazima ituongoze kwenye mabadiliko makubwa katika maisha yetu. Ni lazima tuache namna yetu ya kwanza ya maisha, na tuanze maisha mapya ambayo ni ‘ya Ki-Mungu’ (sio tena ya kiubinafsi). Hili ni gumu sana, na hasa mtu anapoanza. Tunajikuta kama hatuwezi kirahisi kuyaelewa maneno ya Mungu. Mawazo yake na fikra anazotupa tunaona ni safi na zakupendeza, lakini akili zetu sisi zinawaza dhambi.

Ni lazima tuanze kufikiri kwa namna nyingine; tuyafanye mawazo ya Mungu na njia zake kuwa zetu. Tunajifunzia wapi haya? Ni katika Biblia, lakini ni lazima tufanye kuyachimbua! Kama tutakuwa Wafalme; ni sharti kwa sasa tuyachunguze Maandiko kuona yote Mungu anayotufundisha kumhusu Mwenyewe na kusudi lake. Hilo ndilo litakalotupa ushirika na Bwana Yesu Kristo katika Ufalme wa Mungu, atakaporudi. Kwa kadri tutakavyofanya hivyo ndivyo imani yetu kwake itakavyojengeka. Andiko linasema:

“Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo” (Methali 25:2).

Neno lenye pumzi ya Mungu

Biblia ina madai ya kipekee juu yake yenyewe; inadai ni neno lenye, ‘Pumzi ya Mungu’, ikiwa na maana tu ya kwamba ‘imetokana na Mungu’. Kama ambavyo tunatumia pumzi (hewa) iliyoko kwenye mapafu yetu kuipa nguvu sauti yetu na kutufanya tusikike, ndivyo ambavyo Biblia inavyotupa picha ya Mungu kusema nasi maneno. Mtume Paulo aliandika juu ya hili katika Waraka wake kwa Timotheo, akimwambia:

“Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa, tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Tim. 3:14-17).

Kuna hoja kadhaa za maana sana zinazotolewa katika mistari hii.

  1. Biblia yote kabisa ni Neno lenye pumzi ya Mungu. Tunapata maelekezo ya kutusaidia na kututia moyo katika vitabu vya Agano la Kale, kama tunavyosaidiwa na kutiwa moyo na  ujumbe wa Injili katika Agano Jipya. Bila ya ‘kila Andiko’, kukua kwetu kiroho kama wanafunzi wa Yesu kusingekuwa kamili.
  2. Tunawezaje kujifunza juu ya ‘tendo jema’ tunalotakiwa tulifanye katika maisha yetu, bila ya kuyasoma matendo mema katika Biblia?
  3. Timotheo alikuwa amejifunza juu ya Mungu katika Biblia. Kujifunza kwake kulimfanya aamini kwa dhati ukweli wa mambo hayo; alifundishwa na ‘kuhakikishwa’. Imani yake ilikuwa imekua. Alikuwa akifundishwa juu ya Biblia tangu utoto wake. Tunapoangalia katika 2 Timotheo 1:5 tunaona kuwa, alifundishwa na mama yake na bibi yake. Hili ni somo la muhimu sana juu ya jinsi tunavyopaswa kuwafundisha watoto wetu na wajukuu wetu.
  4. Sasa alikuwa anapaswa kuendelea katika mambo hayo aliyojifunza na kuyaamini. Hii ilikuwa nasaha ya muhimu sana. Hakupaswa kusema sasa amejua vya kutosha na hahitaji kusoma na kujifunza Biblia tena. Kusoma Biblia kulikuwa kuwe sehemu inayoendelea katika maisha yake ya kila siku. Katika hili Yesu alifundisha kuwa: “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mathayo 4:4). Mtu hawezi kuishi kwa ugali au ubwabwa au ndizi tu. Mahitaji yake ya kila siku ni pamoja na chakula cha kiroho; Neno lililotoka katika kinywa cha BWANA.

Kwa nini ni muhimu kusoma Biblia

Tunajua kuwa, kama hatukula mara kwa mara tutakufa kwa njaa. Chakula cha kawaida ni cha muhimu sana kwa uhai. Chakula cha kiroho nacho ni cha muhimu hivyo hivyo. Bila ya chakula cha kiroho cha kila siku kutoka katika Biblia, tutakufa kiroho na kuukosa Ufalme wa Mungu. Kama tukijilisha Neno la Mungu kila siku, tutakua kiroho. Tunaambiwa, Neno la Mungu:

  • Lina uhai na lina nguvu inayotusaidia kuipima mioyo yetu kiukweli, kuona kile hasa tunachodhamiria (Waebrania 4:12).
  • Linatupa nguvu ya kukabiliana na tamaa za dhambi ambazo zipo ndani ya kila mmoja wetu (Zaburi 119: 9-11).
  • Lina uwezo wa kutujenga na kutuimarisha kiroho (Matendo 20:32, 1 Petro 2:1-2).
  • Linatuonya tunapokosea (2 Tim. 3:16).
  • Linatusaidia kutufanya tujitenge na dunia iliyojaa uovu (Yoh. 17:14-17).
  • Linajenga imani yetu (Warumi 10:17).
  • Linatupa mifano ya namna tunavyopaswa kuishi maisha yetu kama watu tunaomcha Mungu (Wakolosai 3:1-17).
  • Linatufunulia lengo alilonalo Mungu kwa dunia yake, na kwa watu watakaoishi duniani katika Ufalme wa Mungu (Zaburi 72).
  • Zaidi ya yote linatuambia juu ya upendo wa Mungu katika kumtoa Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wetu, na juu ya namna tunavyopaswa kuuonesha upendo huo kwa wengine (1 Yohana 4:7-21).

Neno lililofanyika mwili

Sababu iliyo kubwa kuliko zote ya kusoma Biblia ni kwamba, inatufundisha juu ya Yesu Kristo. Anaelezewa kuwa ni ‘Neno aliyefanyika mwili’. Kwa hili tunaelewa kuwa, aliishi kulingana na Neno la Mungu muda wote siku kwa siku. Kwake yeye kwa kweli Neno la Mungu lilikuwa ni ‘taa ya miguu’ yake, na ‘mwanga wa njia’ yake (Zab. 119:105).

Ni Biblia yake iliyomuonesha namna ya kuishi masaa yote kila siku, kwa namna iliyompendeza Baba yake. Muda mfupi kabla ya kufa, Yesu alimwomba Baba yake kwa ajili ya wanafunzi wake. Tunapata maombi haya katika Yohana 17. Alisema ameikamilisha kazi ambayo Mungu alimpa afanye. Alikuwa amewafundisha wafuasi wake juu ya Mungu; amewapa ujumbe wa Mungu kwa maneno yale yale Mungu aliyosema naye:

“Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo” (Yohana 12:49, 50).

Haya mambo yalikuwa ya muhimu kwake kwa kuwa, alikuwa akikaribia kuwaacha na kupaa mbinguni. Wangehitaji nini ili waweze kuendelea kwa nguvu wakati hayupo? Ni Neno la Mungu! Anawaombea: “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yohana 17:17).

Maombi yake haya ni kwa ajili yetu hata leo. Ni kupitia katika Neno la Mungu katika maisha yetu kila siku ndipo tutakapoweza kukua kiroho kuwa kama Yesu. Litatusaidia kujitenga na uovu uliopo katika dunia, na litatusaidia kuweza kujiweka sawa kumpokea Bwana Yesu Kristo katika kurudi kwake.

Namna ya kukua kiroho

  1. Soma sehemu ya Biblia kila siku. Tumia Mpango wa Usomaji wa Biblia (Bible Reading Planner) au Mshirika wa Biblia (Bible Companion), utakaopewa na mkufunzi wako ili uweze kuhakikisha unasoma sehemu zote za Biblia.
  2. Kabla ya kusoma, muombe Mungu akusaidia uweze kuelewa unachosoma.
  3. Kama unayo familia, watie moyo musome wote.
  4. Weka orodha ya maswali katika daftari lako juu ya kile unachokisoma lakini hukielewi. Unaweza baada ya hapo kumuuliza mkufunzi wako au Mkristadelfia yeyote kukusaidia majibu ya maswali hayo.
  5. Tafakari kile unachosoma. Kama unaweza kupata muda wa kufanya hivi, hili ni jambo jema sana. Lakini, uyafikirie pia mambo unayosoma katika Biblia katika maisha yako ya kila siku, na ujaribu kuyaweka uliyojifunza katika matendo.

 

Swahili Title
Maisha ya Kristo - Kusomo
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission