Correspondance Course - Lesson 44

Swahili

Somo la 44

MAISHA YA KRISTO - Eklesia

Somo: 1 Timotheo 3

Wanaume na wanawake wanapobatizwa katika Kristo, wanakuwa watu wa Mungu, na kuwa sehemu ya familia yake. Mungu aliamuru kuwa wanawe wawe katika jumuia ya kiimani, na ametueleza wazi hili liweje. Amepanga kuwe na kundi moja au jumuia moja ya wafuasi kwa dunia nzima. Neno linasema:

“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani…” (1 Wakorintho 12:12, 13).

Katika Biblia ya Kingereza, umoja huu unaitwa ‘church’, kwa Kiswahili ‘kanisa’, na katika lugha ya Kiyunani, ambayo ndiyo iliyotumika katika kuandikwa Agano Jipya, neno maalumu lililotumika ni neno ‘Eklesia’. Eklesia ni kundi la watu waliokusanywa pamoja kwa lengo maalumu, na kuna matumizi ya neno hilo katika Agano Jipya yanayoonesha hili. Katika Matendo 19 tunasoma juu ya muda Paulo alioutumia katika Efeso, na matatizo aliyoyapata yaliyoletwa na baadhi ya watu wa mji huo:

“Wakati huo kukatokia ghasia si haba katika habari ya Njia ile. Kwa maana mtu mmoja jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi. Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii…. Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi, kwa maana ule mkutano (eklesia) ulikuwa umechafuka–chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja” (Matendo 19:24-25, 32).

Hao mafundi walikuwa wamekusanywa pamoja na mtu huyo mwovu, Demetrio, kumpinga mtume Paulo.

Mungu amewakusanya watu pamoja kuwa eklesia yake kwa lengo la wao kumwabudi na kuwa watu wa familia yake.

Matumizi ya kwanza ya neno ‘eklesia’ katika Agano la Kale la Biblia ya Kiyunani, yako katika kitabu cha Kumbukumbu La Torati. Kinaelezea vile ambavyo wana wa Israeli walivyokuwa tofauti na mataifa mengine yote yaliyokuwa yakiwazunguka. Walikuwa wametolewa Misri na Mungu, na alikuwa anataka kuwaongoza kuiendea Nchi ya Ahadi. Walikuwa wameitwa kwa sababu hiyo na hivyo walikuwa ni eklesia yake; eklesia ya Mungu. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kanisa la Mungu hata leo. Linaundwa na watu walio tofauti na wengine, na wameitwa watoke katika dunia ili Mungu aweze kuwaongoza kuuelekea Ufalme wake.

Bahati ya kuwa mtu wa kanisa la Mungu, ni ya wale tu ambao wamebatiziwa, “Habari njema za Ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo” (Matendo 8:12). Wafuasi wa kweli wanajitenga na ulimwengu, na wanatambua kuwa hawawezi kikweli kumwabudu Mungu na watu wengine wanaojiita Wakristo, wakati hawaelewi au hawaukubali ujumbe wa kweli wa Injili. Wito wa kuwa sehemu ya eklesia ya Mungu ni wito wa kujitenga. Mtume Paulo aliandika juu ya hili kwa eklesia ya Wakorintho na kusema:

“Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana, msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu, wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi” (2 Wakor. 6:16-18).

Ni heshima kubwa kuwa sehemu ya eklesia ya Mungu, na waumini waliobatizwa wanapokutana kuabudu, wakati wote wanalikumbuka hili. Mungu amewaitia mambo haya na wasiyapuuze. Wanaambiwa:

“Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri: wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia” (Waebr. 10:23-25).

Katika Waraka wake kwa Waefeso, Paulo alielezea eklesia kama ni mahali ambapo waumini wanakua kiroho. Alitumia neno lenye maana ya ‘kujengana’. Aliandika kuwa ndani ya mfumo wa eklesia, ndugu wangeweza:

  • Kukua katika uelewa na ufahamu (4:13-15).
  • Kukua katika upendo, na kwa hiyo kuimarisha na kuijenga eklesia (4:15, 16).

Hata hivyo anatuambia kuwa, hili linaweza kutokea tu kama kila muumini katika eklesia anajihusisha na kuichangia (4:16).

Paulo alitumia usemi maalumu kuielezea eklesia. Aliandika kuwa, watu ndani yake ni ‘mwili’ mmoja, na alitumia usemi huu kwa namna hii mara kumi katika barua zake. Kwa mfano:

“Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Warumi 12:4, 5).

Usemi huu ‘mwili mmoja’ unaelezea ukaribu unaokuwapo, ndugu wanavyokuwa wakiishi na kuabudu pamoja kama sehemu ya familia ya Mungu, na Paulo anaandika mambo yafuatayo juu yake:

  1. Kama ambavyo tulivyo na viungo tofauti-tofauti vyetu wenyewe, ndivyo vilivyo viungo tofauti-tofauti kwenye mwili wa kiroho. Sio kila muumini wa kiume na wa kike anafanana na mwingine au wanaweza kufanya kazi moja katika eklesia. Lakini, kila mmoja ni wa muhimu na anathaminiwa na Mungu, na ana jukumu lake la kutekeleza katika mwili wa Kristo. Sisi wote tunahitajiana, kama tunavyovihitaji viungo vyote vya miili yetu, kwa mwili kuweza kufanya kazi vizuri (Warumi 12:4, 5; 1 Wakorintho 12:12, 20).
  2. Mkubwa wa mwili huu ni Kristo (Waefeso 4:15,16). Ni Yeye ndiye mwenye mamlaka juu ya mwili huo, na hakuna mamlaka ya kibinadamu duniani iliyo na mamlaka juu yake.
  3. Tofauti za kirangi au kitaifa, au jinsia, hazina maana. Mungu anawathamini watoto wake wote na wote ni sawa (Wagalatia 3:26-29).
  4. Ingawa kuna mwili mmoja (eklesia moja) ambamo Kristo ndiye kiongozi wake(Waef. 5:23), mwili huo unaelezewa kuwa una matawi mengi. Kwa hiyo Paulo aliliandikia: “Kanisa la Mungu lililoko Korintho” (2 Wakor 1:1) na makanisa mengine. Popote pale wafuasi wa kweli wa Yesu wanapokutana kuabudu, ni eklesia ya Mungu.

Tunahitaji basi kuangalia majukumu mbali mbali yaliyopo katika eklesia, na kufikiria ni nini Biblia inachotuambia juu yake.

Mikutano ya kikazi ya Eklesia

Baada ya kupaa kwa Bwana Yesu Kristo, eklesia iliyokuwa Yerusalemu ilipanuka haraka, na haraka ikaonekana kuwa ilihitaji watu wa ziada kupanga mambo na kuisimamia. Maelezo juu ya hili yanapatikana katika Matendo 6:1-7, na hili linatuwekea utaratibu wa namna eklesia zinavyopaswa kujipanga leo. Tunaweza kuorodhesha vipengere vya msingi kihivi:

  1. Jukumu kubwa la viongozi (mitume) waliokuwa wakisimamia lilikuwa kuhubiri, kuomba na kufundisha Neno la Mungu.
  2. Hata hivyo walihitaji msaada, hasa-hasa kwenye mambo ya kiuchungaji (malezi na ushauri), kwa ajili ya kuwatunza ndugu walioko katika eklesia.
  3. Viongozi hawakufanya maamuzi peke yao, bali waliwaita ndugu wote pamoja kwa mkutano wa kikazi kujadili.
  4. Mitume walitoa miongozo au ushauri wa lile waliloona linapaswa kufanywa, lakini ni eklesia yote iliyofanya maamuzi, na kuwachagua wanaume waliofikiri walifaa zaidi kuzifanya kazi hizo kwa niaba yao. Bila shaka kila mtu alipiga kura alivyoona, lakini kila mmoja alikubalina na uamuzi wa wengi na kuuunga mkono.

Matokeo ni kwamba kama kulikuwa na kutoelewana katika eklesia kulisuluhishwa, na kila mmoja alijisikia kwamba anathaminiwa. Hili lilifanya eklesia iendelee kuhubiri, na hivyo Luka anasema, ‘Neno la Mungu likaenea’.

Hili ni somo la maana sana kwetu. Kama kuna utaratibu mzuri katika eklesia unaomhusisha kila ndugu katika maamuzi yake, eklesia itajizatiti katika kulihubiri Neno. Uamuzi unapokuwa umefanywa kwa haki na walio wengi katika eklesia, washirika wote ni sharti wauunge mkono.

Tunasoma juu ya mkutano mwingine katika Matendo 15, ukiwahusisha wazee na mitume kutoka kwenye eklesia nyingi. Walikuja kukutana kujadili kitu ambacho wengi wao walikuwa wakikipinga. Kulikuwa na hoja nyingi, na tunaona tena kuna mambo ya sisi kujifunza juu ya namna ya kukabiliana na tofauti zinazojitokeza katika eklesia.

  1. Walikutana kuliongelea jambo hilo; hawakutuma barua au kukaa tu nyumbani. Ingawa kulikuwa na hoja nzito, tena zinazopingana, lakini walisikilizana.
  2. Kulikuwa na fursa ya kila mmoja kusema.
  3. Wakati Petro na Yakobo walipoongea, kila mmoja alikaa kimya na kusikiliza kwa kuwa walikuwa viongozi.
  4. Walilitumia Neno la Mungu katika kufanya maamuzi; sio maoni yao wenyewe.
  5. Uamuzi ulipokuwa umefikiwa, wote waliukubali na kuishi kwa kuufuata.

Majukumu ya Wazee

Mtume Paulo alipokuwa akienda katika mizunguko yake ya kuhubiri, mpango uliokuwapo katika eklesia ulikuwa wa muhimu sana kwake. Alitambua kuwa, ndugu wa kike na wa kiume waliokuwa ndio wamebatizwa, walihitaji kuwa na mfumo wa ki-eklesia, kwa hiyo aliteua wanaume katika kila mji kuwa wazee (Matendo 14:23).

Haina maana kuwa, moja kwa moja alichagua waliokuwa wakubwa zaidi kiumri, ndio wawe wazee wa eklesia. Timotheo alikuwa bado kijana lakini alikuwa ‘mzee’ wa eklesia ya Efeso, aliyechagulia kutokana na hali yake ya kiroho. Paulo anatuambia mengi kuhusu sifa tunazopaswa kuziangalia tunapochagua ndugu wa kuwa ‘wazee’ katika eklesia zetu.

Tutambue hapa pia kuwa, sio vibaya kupenda ‘kuwa mzee’ katika eklesia zetu. Ni sababu ya huko ‘kupenda’ iliyo ya muhimu. Paulo anasema:

  • “Mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wakujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi” (1 Tim. 3:1-6).
  • “Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake mwenyewe, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga” (Tito 1:7-9).
  • “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao na shahidi wa mateso ya Yesu, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi” (1 Petro 5:1-3).

Neno ‘askofu’ maana yake ni ‘mwangalizi’. Vifungu hivi vinatupa picha nzuri sana kuhusiana na mchango wa mzee wa eklesia. Anapaswa awe:

  • Mwanamume anayeijua Biblia yake vizuri na anayeweza kuwafundisha wengine ujumbe wa Injili.
  • Mwanamume anayeishi kulingana na Injili.
  • Mwanamume anayejitawala na mwenye kiasi katika mambo yote, anayeyashughulikia matatizo ya eklesia kwa namna ya utulivu na busara (hata yakiwa magumu kiasi gani).
  • Mwanamume asiyekasirika na kulipuka.
  • Mwanamume asiyelewa.
  • Mwanamume mkarimu; anayewakaribisha watu wengine nyumbani kwake.
  • Mwanamume asiyedai malipo kwa kazi ya kuwa mwangalizi, na asiyeiba fedha ya eklesia.
  • Mwanamume asiye na maringo au kiburi.
  • Mwanamume ambaye amejengeka kiroho; sio aliyebatizwa karibuni.

Wapo wazee wanaojiona wenyewe kama wenye-mamlaka au kama viongozi katika makusanyiko yao. Hili linawafanya wajisikie kuringa au wa-maana zaidi kwa namna wanavyowachukulia wengine. Hili linatoa mfano mbaya sana kwa eklesia. Baada ya Yesu kuwaosha wanafunzi wake miguu katika chumba cha juu alisema:

“Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. Amini, amin, nawaambia ninyi, mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo heri ninyi mkiyatenda” (Yohana 13:15-17).

Mzee wa eklesia (Mwenyekiti au Katibu) anapaswa awe mtumishi wa eklesia yake. Anatakiwa awe kama mchungaji wa kondoo anavyowachunga kondoo, na kuwasaidia kwenye njia ya Ufalme wa Mungu.

Nafasi za wanaume na wanawake

Paulo aliandika kwamba:

“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu” (Wagalatia 3:27, 28).

Haya ni maneno ya kusisimua na yanalithibitisha lile wazo la ‘mwili mmoja’. Rangi ya ngozi yetu, tu wanaume au wanawake, yote haya hayana umuhimu kwa Mungu tunapokuwa watu wa nyumba yake; watu wa familia yake.

Hata hivyo Biblia iko wazi kuwa, kuna majukumu yanayotofautiana ndani ya eklesia kwa wanaume na wanawake. Katika eklesia, wanaume ndio wanaoongoza maombi na ibada ya pamoja.

Ni wajibu wa wanaume kufundisha na kuongoza pia katika mahubiri ya hadharani. Wakina dada ni wa kuwasikiliza kimya-kimya wanaume na kuwatii (1 Timotheo 2:8-15). Paulo anasema sababu ya hili ni kwamba, Adamu aliumbwa na Mungu kwanza.

Adamu alipaswa kuongoza katika kumwabudu Mungu akiwa na mke wake, lakini mwanamke, Hawa, alidanganywa na kula tunda. Alipompa mume wake naye alikula bila kujihoji, wakaivunja amri ya Mungu. Kwa kufuata mwongozo wa Mungu kuhusu majukumu yanayotofautiana kati ya wanaume na wanawake katika eklesia, Paulo anasema tunaurudia utaratibu ambao Mungu aliuweka tangu mwanzo.

Hili halina maana kuwa, hakuna shughuli kwa ndugu wa kike. Namna yao ya kushirikisha ni ya muhimu kwa eklesia yoyote. Ni Lidia aliyeweka kielelezo cha ukarimu na wema uliojengeka katika eklesia ya Filipi (Matendo 16). Dorkasi alikuwa dada wa Yafa, aliyefahamika sana kama mfuasi aliyejaa ‘matendo mema’ kwa kuwasaidia maskini (Matendo 9).

Wakina dada wengi wanafundisha Shule ya Jumapili na mara nyingi wanao uwezo na watoto wadogo ambao wanaume hawana. Wanao pia miguso ya kushirikisha katika nyumba zao, kwa namna wanavyofanya mambo, na wanaweka mfano mzuri wa ucha-Mungu kwa watoto wao na kwa waume zao (Tito 2:4, 5).

Namna mojawapo inayotofautisha majukumu kati ya wanaume na wanawake hadharani katika eklesia imewekwa. Wanaume wanatakiwa wasali bila ya kufunika kitu vichwa vyao, na wanawake kufunika (1 Wakorintho 11).

Mikutano ya eklesia

Kila eklesia inapaswa ikutane kila juma, Jumapili kama inawezekana, ili kula mkate na kunywa divai kwa kumbukumbu ya maisha na kifo cha Bwana Yesu Kristo (Somo la 40). Namna inayopendekezwa ya kuendesha huduma ya Kumega Mkate imeoneshwa hapo chini. Hata hivyo ni eklesia iliyo dhaifu tu inayoweza kukutana mara moja tu kwa namna hii. Eklesia, na waumini mmoja mmoja wanapaswa kukua kiroho:

“…ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiunganishwa na kushikamanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili (eklesia) upate kujijenga wenyewe katika upendo” (Waefeso 4:14-16).

Ni usomaji makini katika kujifunza Neno la Mungu, kwa maombi, ndio unaotusaidia kukua (1 Petro 2:1). Eklesia inapaswa kukutana kila juma kwa ajili ya Somo la Biblia, na sio kukutana Jumapili tu. Hili ni lazima litawasaidia ndugu wote kukua-kiimani; kuendelea mbele kutoka kwenye kanuni za kwanza za kiimani, kwa kutafakari kile mwandishi kwa Waebrania anachokiita ‘chakula cha neno’; kukua kutoka ‘kunyonya’ na kufikia ‘kula chakula kigumu’.

Inapaswa pia kuwe na siku nyingine ya kukutana kwa ajili ya kuihubiri Injili, ambapo eklesia inaangalia nje kuwashirikisha watu wanaoishi jirani Habari Njema ya wokovu. Mikutano hii haiwi rahisi kuiandaa na kuiendesha, na hasa kama eklesia ni ndogo.

Hata hivyo msaada upo. Kitengo cha msaada kwa walio kwenye mazingira ya upweke (Christadelphian Isolation League) kipo kwa ajili ya kuwatumia kwa njia ya posta mahubiri yaliyoandikwa, mihadhara, na makaratasi ya masomo ya Biblia, ambayo eklesia inaweza kufaidika nayo.

Ratiba ya Kumega Mkate kwa eklesia za Kikristadelfia:

Wimbo

Maombi

Kusoma sura mbili za masomo ya siku kutoka katika Mshirika wa Biblia (Bible companion).

Mahubiri (yanayotoka katika Biblia kuwaandaa waumini kumega-mkate)

Utangulizi kwa ajili ya Mkate na Divai

Maombi kwa ajili ya Mkate

Maombi kwa ajili ya Divai

Wimbo

Mchango kwa ajili ya eklesia

Matangazo kuhusu mipango ya baadaye

Wimbo

Maombi 

Swahili Title
Maisha ya Kristo - Eklesia
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission