Somo la 45
NAMNA TUNAVYOWAFIKIRIA WATU WENGINE NI MUHIMU KWA MUNGU
Somo: Yakobo 2
Yesu alipojaribiwa siku moja na mmoja wa madaktari wa Sheria ya Kiyahudi, juu ya amri iliyo kuu kuliko zote, alijibu kuwa ni kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, nguvu zako zote, na akili yako yote, na jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Kwa ajili ya kuelezea maana aliyokuwa nayo ya âjiraniâ, aliendelea kwa kutoa mfano wa Msamaria aliyekuwa mwema. Unaweza kusoma juu yake katika Luka 10:25-37.
Tutairudia sehemu hii ya mafundisho ya Yesu katika somo letu lijalo, lakini ni muhimu tuanzie hapa kwa sababu, tunataka kuutumia upendo wa Kikristo katika mahusiano yetu na watu wengine, kama Msamaria-mwema alivyofanya. Tukifanya hivi tutaona kuwa, maagizo mengine tuliyopewa na Yesu na mitume wake, yanaweza kuwa rahisi kuyaelewa na kuyafuata.
Ni rahisi sana kuwa mwema kwa matajiri na wenye nguvu, na kuwadharau na kuwabeza walio wanyonge, maskini au walemavu. Yakobo, mdogo wa Bwana Yesu, anasema, huku ni âkuwa na heshima kwa watuâ, na anatuonya dhidi ya kufikiri kwa namna hiyo (Yakobo 2:1-9).
Kuna mengi ya kufikiri katika maneno haya, na ni muhimu hasa katika nchi na jamii ambazo kuna michanganyiko wa watu walio na asili mbalimbali, makabila au rangi. Kumekuwa na migogoro mibaya na mapambano makali ya watu katika sehemu mbalimbali za dunia katika miaka ya karibuni, inayotokana na ubaguzi. Wapo wanaowaelezea wengine kama vile hawana thamani, sio wakweli, ni washenzi n.k. Ni namna ya kawaida ya kufikiri kibinadamu, lakini ni mbaya sana.
Biblia inachosema ni tofauti. Mawazo na mwelekeo wa kibaguzi ni tabia isiyopaswa kuwa na nafasi katika mioyo na akili za wale wanaokuwa wafuasi wa Yesu Kristo.
Paulo, mtume wa Yesu, aliishi katika nyakati ambazo utumwa ulikuwa ni sehemu ya mifumo iliyokubalika katika Dola ya Kirumi. Kuna maelekezo na ushauri mwingi katika nyaraka za Paulo, kuhusu mahusiano kati ya mabwana na watwana, waliokuwa wameamua kumfuata Bwana Yesu. Mfano upo kwenye Wagalatia 3 mstari wa 26 mpaka wa 29.
Hapa Paulo anasema wazi wazi kuwa, wafuasi wa Yesu walikuwa wote sawa mbele ya Mungu. Hakukuwa na utofauti wa uasili, jinsia, rangi ya ngozi au hadhi ya kijamii.
Tunapoongea na watu tunaoishi nao au tunaofanya nao kazi, ni rahisi sana kutumia maneno makali au maneno ya kukosoa ambayo yanajeruhi au kuwakatisha tamaa wengine. Yakobo aliandika pia juu ya hili (Yakobo 3:5-11). Maneno makali yanapokuwa yametumika, hayawezi kufutika; huwezi kuyarudisha tena mdomoni. Kwa kuwa sisi sote tunatofautiana tulivyo, ni wale wenye hasira za haraka-haraka wanaopaswa kuwa makini zaidi. Mungu, kupitia kwa malaika zake, anajua yote tunayosema.
Kutumia uwezo wetu wa kuhukumu ni kitu cha muhimu kwetu, inapokuwa ni kuamua lililo zuri au baya, sahihi au kosa. Lakini tunapohukumu watu wengine, inatubidi tuwe macho zaidi.
Yesu anatupa ushauri wa maana juu ya hili, na umeandikwa katika Mathayo 7:1-5. Kutokana na maneno hayo, unaweza pengine kuamua usimhukumu tena mtu mwingine, lakini sio rahisi kushikilia msimamo huo. Yesu anakazia maelekezo yake hayo kwa kutoa mfano mdogo. Ufunguo wa kuyaelewa maneno yake ni usemi unaohusu âkuona kibanzi katika jicho la ndugu yakoâ. Huku ni kukosoa wengine hapo kwa hapo, kunakopuuzia kushindwa kwetu wenyewe mbele ya macho ya Mungu.
Kuna wakati tunahitaji kufanya maamuzi kiuangalifu, na Yesu anatoa mfano wa haya katika Mathayo 7:15,16. Nasaha hii kwa vyovyote ilikuwa ya maana sana katika miaka za awali ya imani ya Kikristo, walimu wa uongo walipokuwa wengi mpaka wengine kuitwa âMakristoâ. Ni nasaha ya maana sana hata sasa, wakati ambao kuna makanisa mengi sana na walimu wengi. Namna ya kuwahukumu ni âkuwajua kwa matunda yaoâ. Kwa kawaida, kile wanaume hao (na pengine wanawake) wanachofanya katika maisha yao, kinaonesha zaidi walivyo kuliko kile wanachohubiri.
Yesu alipokuwa amewachagua wanafunzi wake, alianza kuwafundisha namna ya kufanya mambo yanayoweza kumpendeza Mungu; mafundisho hayo yaliyo mengi yapo katika Injili ya Mathayo, Sura ya 5, 6 na 7. Hebu tuangalie pamoja katika Sura ya 5, kuanzia msitari wa 21. Yesu hapa ananukulu kutoka katika Sheria ya Musa iliyotoka wakati taifa hilo lilipotoroka utumwa katika nchi ya Misri.
Hapa anaeleza kuwa, wakati sheria ya zamani ilidhibiti vitendo vya kitabia kwa Wayahudi, sheria yake mpya ingeendelea mbele na kudhibiti mawazo na matendo pia. Anaongelea hasira, lugha chafu, na mawazo ya tamaa. Anaongelea kuvunjika kwa ndoa, ambako mara kwa mara kunatokea kutokana na tamaa ya kufanya mapenzi na wengine nje ya ndoa.
Katika mstari wa 33 Yesu anaonya juu ya kuapa bila kufikiria. Kwa hili ana maana ya maneno watu wanayosema kuwavutia wengine kuamini ukweli wa lile wanalosema. Kwa bahati mbaya, wanatumia maneno ya âutakatifu wa Munguâ na hili lilikatazwa. Hata inapokuwa tunayafikiria tu maneno hayo katika akili zetu, ni muhimu tukumbuke wakati wote kuwa yalikatazwa (Kutoka 20:7). Mwongozo wa jumla wa Yesu ni kwamba: âUsiape kabisaâ (Mathayo 5:34).
Ni vizuri zaidi kuepuka kabisa kuapa wakati wowote, na hili linahusu pia kwenye mahakama kama itatokea tukajikuta mahali hapo. Kwa kawaida kunakuwa na kipengere cha wafuasi wa Yesu âkuahidiâ kabla ya kutoa ushahidi. Matumizi ya viapo kama njia ya kuelezea tunavyowafikiria wengine, yameshughulikiwa na Yesu katika tahadhari yake, kuhusu tunayosema, katika mstari wa 22.
Katika Mathayo 5:44 amri ya kumpenda jirani imepelekwa hatua kadhaa mbele. Yesu sasa anatuagiza tuwapende maadui zetu, tuwabariki wale wanaotulaani, tuwafanyie mema wale wanaotuchukia, na kuwaombea wanaotuumiza. Haitakuwa rahisi kamwe kuzifuata amri hizi kwa kuwa, mwitikio wetu wakati wote uko kufanya kinyume na hivyo. Lakini, kama Yesu alivyoweza kusamehe katikati ya maumivu makali ya mateso aliyokuwa nayo, wale kati yetu wanaotamani kuwa wafuasi wake kwa dhati, ni lazima wajifunze kufuata mfano wake.
Kiburi na maringo yasiwe na nafasi kabisa mbele ya Mungu katika matendo yetu, lakini, muhimu zaidi, katika mioyo na akili zetu.
Kwa kumalizia somo hili, hebu tuyaangalie kwa pamoja maneno fulani ya unabii wa Isaya katika Sura ya 66, mstari wa kwanza na wa pili. Yanatupa dokezo la mambo Mungu anayoyataka kutoka kwetu, na hulka zile katika ubinadamu ambazo zinampendeza.