SOMO LA 47
MAFUNDISHO YA BIBLIA KUHUSU MATESO
SOMO: Waebrania 12
Mateso ni tatizo katika maisha na yanaweza kumpata mtu yeyote. Mtoto anazaliwa kipofu, au amelemaa na tunajiuliza, ni kwa nini? Mtoto hajakosea kitu. Wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, matajiri kwa maskini, wanapatwa na maumivu ya magonjwa ya hatari yanayoweza tu kuishia kwenye kufa. Kwa nini wateseke?
Mateso, maumivu, mauti n.k. ni majanga ambayo yanaletwa kwa mamilioni ya watu na ukiritimba wa mwanadamu, na uharibifu mkubwa unaoletwa na silaha za kisasa. Uhai unaangamizwa na vitendo vya ugaidi na jinai.
Matatizo ya namna hii yamekuwapo katika historia yote ya dunia, lakini kutokana na ongezeko la watu na ongezeko la uwezo wa silaha kuangamiza, kiwango cha majanga haya leo kinatisha. Watu wanajiuliza, ni kwa nini Mungu anaruhusu mambo haya kutokea?
Swali hili linaonekana angalau kukubali kuwa, Mungu ni kweli yupo, ila linategemea kuwa Mungu atakuwa akifanya mambo wakati wote kwa namna iliyo ya kheri. Kitu linachopuuzia kabisa ni sababu ya âuwepo wa matesoâ katika dunia. Sababu inaweza kuhitimishwa ifuatavyo:
- Katika Bustani ya Edeni, mwanadamu alichagua kwenda njia yake mwenyewe badala ya kuifuata Njia ya Mungu, na kujiletea laana iliyoahidiwa ya kifo. Lakini hii ilikuwa ni sehemu tu ya adhabu. Maisha ilikuwa yabadilike na kuwa magumu sana kwa mwanadamu (Mwanzo 3:16-19).
- Kwa sehemu kubwa, mateso wanayopata watu yamekuwa yakitokana na ukatili wa wanadamu wengine. Kuanzia kwenye uuaji wa kwanza, Kaini alipomuua ndugu yake Habili, Biblia inaonesha kulivyokuwa na vita na ugaidi, hila na mauaji, hali ya mambo ambayo tunaielewa vizuri sana. Katika kila kitendo cha ukatili, kunakuwa na shida zingine zinazofuatia. Matokeo ya mambo haya hayakwepeki.
Pamoja na hili kuna suala la mambo yanayofanywa na kizazi kimoja, kuwa na athari kwa vizazi vinavyofuata. Vitu kama vita vya madawa ya sumu yanayoharibu ardhi, bahari au hata urithi wa kimaumbile ya watu na kusababisha ulemavu, upofu, uziwi n.k. yote yametengenezwa na watu.
Mateso na maumivu tunayoyasababisha wenyewe, au yanayosababishwa na wanadamu wenzetu, hayawezi âkutupiwaâ Mungu. Mabomu ya kutegwa ardhini na silaha zingine za maangamizi zinazoua, zimetengenezwa na watu, na zinatumiwa na jeshi kwa amri zinazotolewa na Serikali za kibinadamu.
3. Mwanadamu anaishi katika dunia inayoongozwa na kanuni za kiasili na kimaumbile. Jambo moja linaleta matokeo fulani kwa lingine, na majanga ya asili makubwa kama volkano, matetemeko ya ardhi, mawimbi ya bahari, ukame na mafuriko, yote yanayoleta mateso makubwa kwa watu, hayachagui. Yanawapata wema na wabaya. Kama tunaona kuwa ni Mungu anayeongoza mambo hayo, tujiulize, tungependa kwa namna fulani ayatumie kwa namna ambayo wabaya wanauawa na wema wanaachwa?
Katika Injili ya Luka kuna kumbukumbu ya Yesu, akiulizwa juu ya uhusiano uliopo kati ya dhambi na mateso (Luka 13:1-5). Alichofundisha Yesu kinaeleweka hata kwetu hivi leo. Majanga hayawatafuti tu wadhambi na kuwatokea. Hayo hayatokani na dhambi.
Katika visa hivyo katika Luka, ilikuwa ni ukatili wa utawala wa Kirumi uliosababisha mauaji ya kwenye hekalu na damu kuchanganywa na dhabihu. Kwa kuanguka Mnara wa Siloamu, ambapo watu 18 walikufa, pengine ilikuwa ufundi usiokidhi haja, au tetemeko la nchi.
Yesu alikuwa makini kusema hapo hapo kuwa, wajibu wa mwanadamu mbele ya Mungu sio kujiwazia kishirikina mambo mabaya yanapotokea. Analosema ni kwamba, maisha ya mwanadamu ni mateke, hayana uhakika. Anaweza kufa dakika yoyote! La msingi lilikuwa âkuifikia tobaâ. Kwa hiyo, kuamini na kubatizwa sio jambo la kuahirishwa. Maisha yanaweza kwa mtu yeyote kukatika muda wowote.
Nataka sasa nigeukie upande mwingine wa mateso. Katika Methali 3:11,12 tunaambiwa kwamba, kuna majaribu katika maisha ya wale walio waaminifu. Mistari hiyo inasema:
âMwanangu, usidharau kuadhibiwa na BWANA, wala usione ni taabu kurudiwa naye. Kwa kuwa, BWANA ampendaye humrudi, kama vile baba mwanawe ampendayeâ.
Waaminifu wanajaribiwa na Mungu kwa kuwa Mungu anawapenda. Anawaadhibu kama watoto kwenye familia, mara nyingine wanavyoadhibiwa na wazazi wao wanaowajali. Mungu anawataka wanawe waerevuke na kuelimika kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Paulo alinukulu mistari hiyo ya Methali katika kutoa hoja yake katika Waraka wake kwa Waebrania (Waebr. 12:5-13). Anachosema katika Waraka huo amekielezea vizuri hata zaidi kwenye Waraka wake wa pili kwa Wakorintho (2 Wakor. 12:7-10).
Paulo, akiwa mtume aliyeteuliwa kwa ajili ya watu wa mataifa (watu wasiokuwa Wayahudi), na akiwa mtu ambaye alipata maono ya moja kwa moja kutoka kwa Yesu akimwelekeza na kumsaidia, alikuwa na tatizo fulani la maumivu lililompa kitu kama ulemavu. Lilimpa shida katika kufanya kazi zake.
Alimwomba Mungu mara tatu kwamba amponye. Jibu alilopewa lilikuwa:
âNeema yangu yakutosha, maana uweza wangu hutimilika katika udhaifuâ (ms. 9).
Kwa maneno mengine, hakuitikiwa; aliambiwa âbakia hivyo-hivyoâ! Ni wazi Paulo aliyakubali majibu hayo kutoka kwa Mungu na kuendelea na kazi yake ya kusafiri na kuhubiri mpaka siku alipokuwa mfungwa wa Warumi.
Na sisi tunapaswa kujifunza somo hili kutoka katika maneno hayo ya Mungu. Udhaifu au shida ni kitu ambacho ni lazima tukikubali katika maisha yetu. Tusikiruhusu kiyaharibu maisha yetu na tusikiruhusu kiingilie na kuathiri ibada yetu kwa Mungu na kwa Mwanawe, Bwana wetu Yesu Kristo. Tunaweza hata kuyaelewa mateso kama njia ya kujivua anasa na mivuto ya kidunia inayotuzunguka, ili tuweze kupata ukaribu zaidi kimahusiano na Mungu na Yesu.
Hivi kwa hakika ndivyo ilivyokuwa kwa wengi kati ya watumishi wa Mungu katika nyakati za Agano la Kale kwa kuwa, walijaribiwa sana katika maisha yao. Imani yao kwa Mungu iliimarika katika kujaribiwa kwao. Wengi kati ya watu tuliowaona katika masomo haya, wanaume kwa wanawake, walijaribiwa: Ayubu, Ibrahimu, Sara, Yusufu, Hana, Eliya, Danieli, Yeremia na wengineo.
Mpaka sasa tumeangalia tu zaidi mateso kwa wanadamu, na sasa nataka nikutake umfikirie BWANA Mungu mwenyewe. Aliumia wakati watu wake, Israeli, walipomkataa. Anaumia hata hivi leo kutokana na ugumu wa mioyo ya wanadamu, na ukatili wanaoufanya kwa wanadamu wenzao.
Hebu ifungue Biblia yako katika Injili ya Yohana 3:14-17. Hapa, kwa hakika tunaona mateso makubwa kwa Mungu, katika kuruhusu Mwanawe wa pekee apigwe na kuuawa kwa kuwambwa msalabani, ili dhambi za wanadamu ziweze kusamehewa, na watu wa-imani waweze kuwa na tumaini thabiti la ufufuo na uzima wa milele.
Yesu alikuja katika hali ya uanadamu, yalimpata yanayotupata na alivumilia majaribu kutoka ndani na dhiki kutoka nje. Ni hali ambayo ni ya kawaida kwa watu wote. Maisha yake ya kipekee aliyoyaishi kwa manufaa ya wengine; kwa manufaa yetu, yanaelezewa katika Waebrania 2:10-18.
Hapa tunaona somo lingine la maana sana kwa ajili yetu. Yesu alikamilishwa kupitia katika mateso (ms. 10), ili aweze kuwasaidia wale wote wanaojaribiwa (ms. 18). Katika Waebrania 5:5-8 tunasoma kuwa Yesu alijifunza kutii, kwa mateso aliyoyapata.
Kama basi Mungu aliteseka, na kama kwa kumtii Baba yake, Yesu aliteseka, tunaweza kulitazama tatizo lote la mateso ya mwanadamu kwa mwanga tofauti. Bila ya kuelewa kwamba Mungu alipata shida kwa ajili ya Kristo ili kutuokoa, kuna uovu mkuu unaotungâangâania.
Tukiwa na imani na mfano wa Yesu mbele yetu, tunaweza kuelewa kuwa, mateso yanaweza kuitakasa imani yetu. Inaweza ikawa njia ambayo Mungu anaitumia katika kumleta mfuasi anayeteseka karibu naye.
Kuadhibu kwa Bwana ni sharti kuchukuliwe kama âkurudiwaâ kwa namna ya Ki-mungu. Kama tunaona âhaturudiâ tumshukuru na kumwabudu, na kama âtunarudiwaâ, basi tuwe na subira, tuvumilie na kumkaribia Mungu wetu tukijua ya kuwa, naye aliteseka; anatukusudia tuimarike na kumtii kwa yale yanayotupata.