SOMO LA 48
KUISHI KWA HOFU
SOMO: Kumb. La Torati 26
Ni rahisi sana kwa wale wanaoishi katika nchi zenye serikali nzuri, zenye amani na utangamano, kusema kuwa hofu ni kitu unachopaswa tu kukikubali. Kuna useme wa kisasa unaosema, 'kabili hofu zako'.
Katika miaka ya karibuni, hata watu waliokuwa wakiishi katika nchi zilizokuwa na utulivu, imewabidi wajifunze kuishi kwa hofu mchana na usiku. Kutegameana na wapi walipo duniani, kumekuwa na matukio ya kutisha: vita, majanga ya asili kama matetemeko ya nchi, milipuko ya kivolkano, mafuriko, vimbunga n.k.
Hofu inakuja kutokana na kutojua ni nini kitakachofuata; iwe ni kuweza kujiokoa mwenyewe, familia yako na marafiki, au mali. Matukio ya ghafla na misituko yake ni hali inayoweza kutupata sisi sote. Somo hili limeandikwa kuonesha namna ya kuyachukulia mambo haya, na kuikabili hofu isiyoondoka. Hii ni hofu ambayo tunakuwa nayo mchana na usiku kwa siku kadhaa, miezi na hata miaka.
Kuna mifano mingi katika Biblia inayoweza kutuonesha watu walivyoikabili hofu. Mmoja upo katika Kutoka 14:10 wakati wana wa Israeli waliokuwa wameutoroka utumwa katika Misri na kugundua ghafla kuwa, walikuwa wakifuatiliwa na jeshi kali la Wamisri nyuma yao. Bahari ilikuwa mbele yao, Wamisri nyuma; kwa vyovyote waliogopa sana.
Mfano mwingine, kwa sasa ni katika Kumb. La Torati 26:63-67. Unaposoma hapo utaona kuwa, maneno hayo yanaielezea ile hofu isiyokwisha. Mungu anawaambia watu wake kuwa, hofu hii itawapata kama wakimuacha na kuanza kuabudu miungu ya uongo; ya miti na mawe. Wayahudi walimuacha Mungu, na historia yao mpaka siku ya leo inaonesha walivyoishi miaka mingi maisha ya hofu. Katika Ujerumani kwa mfano, kati ya mwaka 1939 na 1945, Wayahudi milioni 6 waliuawa kwa sababu tu kuwa Wayahudi.
Hofu ni mbaya zaidi inapokuwa ni ya kitu kisichojulikana. Inaweza ikaathiri makundi makubwa ya watu. Inapenyezwa kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine kwa njia ya mazungumzo. Hili linapokupata, kitu cha kwanza unachoweza kufanya kibinafsi ni kutaka kujua chanzo cha hiyo hofu. Ni vizuri pia kujua, inaletwa na nini au na nani.
Ukifanya hivyo ndipo utakapoweza kuona ni nini ufanye juu ya chanzo hicho. Mara nyingine kuihama nyumba, kijiji, familia au marafiki zako inaweza kuonekana kuwa suluhu pekee ya maana pengine kwa muda.
Tangu mwanzo wa kanisa la Kikristo, wafuasi wa Yesu walikuwa wakiteswa kama inavyowatokea watu wengine hata sasa. Mara nyingi hili liliwapata kwa sababu ya kuwa Wakristo. Hata hivyo mateso hayakuwafanya waache kuwa wafuasi. Badala yake, inaonekana walikuwa shupavu zaidi kwenye imani yao na kwa utii wao kwa Yesu.
Kitabu cha Matendo kinatuambia juu ya kazi ya kuhubiri iliyofanywa na mitume, katika nchi za kaskazini ya Bahari ya Kati (Mediterranean Sea). Tunaoneshwa kuwa, popote walipokwenda walitishiwa na vikundi vya Wayahudi waliokuwa wakiishi maeneo hayo.
Mitume walipigwa, waliuawa kwa kupigwa mawe na kufungwa, lakini hatuoni wakirudi nyuma au kushindwa; tunachoona ni kinyume chake. Mungu kuna wakati aliwaokoa. Tunaona, kwa mfano, akituma malaika zake kufungua milango ya magereza (Matendo 16:22-29). Hebu jaribu kufikiri ilivyokuwa kwa Paulo na Sila, wakiwa wanaumwa kwa kipigo walichopata na kukosa usingizi, lakini wanaimba wakimsifu Mungu (pengine kutoka kwenye Zaburi).
Tangu mwanzo wa kanisa la Yesu, wafuasi walijua kuishi kwa hofu kulivyokuwa, lakini hawakuiruhusu iyatawale maisha yao; iwarudishe nyuma. Yesu alikuwa ndiyo nguvu iliyoyatawala maisha yao. Mfano wake uliwapa nguvu. Katika siku ile ya kutisha, Yesu akijua ya kuwa watu wakatili wangekuja kumkamata na kumchukua akasulubiwe, alivyoendelea mbele, aliacha kielelezo kikubwa kwa wafuasi wake. Anaweza kuwa kielelezo hivyo kwetu pia hata leo.
Katika Luka 22:39-44 tunasoma wakati huo ulivyokuwa wa hofu kubwa kwa Yesu. Alijua kutokana na utabiri mwingi wa Kimaandiko lile ambalo lingempata, na kwa kuwa alikuwa mwanadamu kama sisi, alitishika sana. Kilichosaidia ni kuwa, alikuwa pia Mwana wa Mungu, akijua kifo hiki cha uchungu mkubwa kilivyokuwa gharama iliyotakiwa kulipwa kwa ajili ya dhambi za wanadamu.
Kwa moyo mkuu alisimama kutoka pale alipokuwa ameinama akiomba, na kuondoka mahali pale pa utulivu kwenda kuonana na wanaomshutumu, na kifo chake.
Yesu hakuwahi kuwaahidi wafuasi wake maisha yasiyo ya shida na hofu. Badala yake aliwaonesha kuwa, maisha tunayoishi sasa ni dhiki inayoutangulia Ufalme wa Mungu. Kuna baadhi ya wanaomfuata ambao wangekufa kwa sababu ya kuwa Wakristo, lakini katika kusudi la Mungu kamwe wasingesahaulika; wasingepotea. Katika siku ya ufufuo, watasimama duniani pamoja na wale ambao wameishi na kufa katika hali ya amani.
Hebu yatazame maneno ya Yesu katika Luka 12:4-7. 'Jehanum' katika msitari wa tano hapo ni kaburi, na wale wasioupokea wito wa Mungu wa wokovu, wanakaa humo daima. Kama tukijiweka sisi mikononi mwa Mungu, tutakuwa tumeweka tumaini letu mikononi mwa Muumba, mwenye uweza wote. Ndiye Mungu aliyetuumba na kutuweka duniani hapa kwa ajili ya mpango wake mwenyewe wa ajabu.
Ili kutunyanyua juu zaidi ya matokeo ya hofu, tunayo maneno ya kututia moyo yaliyo katika Wakorintho wa kwanza, Sura ya 3 mstari wa 16. Msingi wa maisha yetu ni Yesu, kama tumebatizwa katika jina lake. Mstari wa 12 mpaka wa 15 upo kutuonesha wazi kuwa, hata kama mali zetu zote zinapotea, kama tunaishikilia imani yetu, bado tupo salama katika kusudi la Mungu.
Hebu sasa turudi tena kwenye Kutoka 14, tuone kilichowapata Wana wa Israeli. Kumbuka kuwa walikuwa kabisa katika hali ya kuangamia, wakiwa wamenasa kati ya Bahari ya Shamu na Majeshi yanayokuja mbio ya Wamisri. Tazama sasa mstari wa 13 na endelea kusoma mpaka mwisho wa Sura hii. Umeona ushauri wanaopewa na Musa. Anawaambia: "Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA" (ms.13).
Hebu tazama sasa 1 Yohana 4:15-19. Mstari wa 15 unatoa wito kwa wale wote walio na mawazo ya kubatizwa, lakini bado hawajaamua. Kama mtu yupo katika Kristo, anazungukwa na upendo wake mkamilifu, na upendo huo mkamilifu unaondoa hofu.
Kuna maneno kadhaa ya faraja katika Zaburi ya 34; hebu isome. Ni maneno yanayoweza kubadili kabisa mtazamo wetu wa maisha. Ufikirie hasa mstari wa 4 mpaka wa 8. Katika mstari wa 9 tumepewa wazo jipya. Kama kunakuwa na hofu katika maisha yetu, na iwe basi hofu na namna tofauti, iliyo nzuri zaidi, hofu iliyo ya kutufaa...hofu ya kumcha Mungu. Kama unausoma mstari wa 11 utaona kuna wito unaotolewa na Daudi, aliyeiandika Zaburi hii.
Alikuwa ni mtu ambaye, alipokuwa kijana, alitoka kwenda kupigana na Mfilisti 'kibonge', aliyeitwa Goliati, kwa manati, akiwa amejiandaa na kokoto chache na imani iliyojaa kwa Mungu wake. Daudi anatupa nasaha njema. Hofu ya Mungu ni nzuri na ni safi kwetu. Hili lina maana kwamba tutakuwa wakati wote tukitambua uwepo wake. Tutamheshimu Mungu wakati wote na kutambua jinsi alivyo karibu nasi kupitia kwa malaika zake.
Mambo tunayofanya katika maisha yetu yatakuwa ni kwa uaminifu na wema, na tunavyompenda Mungu, ndivyo itakavyokuwa rahisi kwetu kuwapenda wanadamu wenzetu kama alivyofanya Yesu. Kumbuka hapa ya kuwa, hata wakati alipokuwa akining'inia msalabani kwa uchungu mkali, alimwomba Baba yake kusamehe, akisema: "Wasamehe Baba, kwa kuwa hawajui walitendalo".
Mtume Yohana anatuambia mengi juu ya upendo katika maisha yetu, lakini anatuambia pia juu ya hofu ya mwanadamu: "Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu" (1 Yoh 4:18).