SOMO LA 49
NI SAWA KUWA NA TAMAA?
SOMO: Mathayo 18
Maelezo ya Mathayo juu ya maisha na mafundisho ya Yesu, ni pamoja na misemo kadhaa inayohusu tamaa za kibinadamu. Maelezo hayo yote yanalaani au kutuonya dhidi ya msukumo wa tamaa, ambao ni kitu chenye nguvu katika hulka yetu.
Wanafunzi wa Yesu walielekea kuwa na tatizo la: nani angekuwa mkubwa zaidi katika kikundi chao, ukimwondoa Yesu? Inaonekana lilikuwa jambo waliloliona la muhimu kwao kwa wakati huo, na inaelekea walibishania mara nyingi.
Swala lingine lililowapa shida ni: nani ambao wangepata nafasi za juu zaidi katika Ufalme ambao Yesu alikuwa akiwaahidia? Yesu alitambua mabishano hayo. Walipomuuliza wazi wazi, aliwajibu kwa kuwapa fundisho fupi linaloeleweka. Tutaanzie hapa uchunguzi wetu.
Angalia kwanza Mathayo 18:1-4. Swali lilikuwa: "Nini aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?" Jibu la Yesu lilikuwa kuwapa kielelezo cha mtoto, aliyemweka mbele yao: Mpole, mkweli, mnyenyekevu mbele ya wakubwa, mwaminifu. Ujumbe wa Yesu kwao ulikuwa ni: ye yote ajinyenyekezaye mwenyewe akawa kama mtoto huyu, ndiye atakayekuwa mkubwa.
Sasa angalia linalofuata katika Mathayo 20:20 ambapo tunasoma juu ya mama mmoja wa-wawili kati ya wanafunzi pale, aliyekuwa akiwaombea nafasi za heshima wanawe hao; Yakobo na Yohana.
Ni kitu cha kawaida mzazi kutamani lililo bora zaidi kwa ajili ya mwanawe, lakini kwa mara nyingine tena Yesu anakuwa makini kujibu. Alitambua hiyo ilikuwa namna ya kawaida ya kufikiri kibinadamu, lakini haikuwa ikiwiana na mahitaji na malengo ya kanisa lake au na Ufalme wake unaokuja. Mambo yote ya ajabu kabisa Mungu aliyoyaandaa kwa ajili ya wale watakaopata nafasi katika Ufalme huo katika dunia, watayapata atakaowaona wamestahili.
Hebu sasa pitia jibu lote Yesu analolitoa kwa mama huyo wa Yakobo na Yohana, katika mstari wa 22 na 23. Sio juu yetu kwa sasa kuwa na tamaa za madaraka katika kanisa au katika Ufalme unaokuja.
Katika mstari wa 24 tunasoma, kunatokea tatizo wale wanafunzi wengine kumi wanaposikia juu ya ombi hilo, na unaweza kuona wanavyokasirika. Yesu sasa anatumia uhusiano kati yake na wanafunzi wake hao 12 kuwa kielelezo. Yeyote anayetaka kuwa mkubwa ni lazima atumikie kwanza.
Mfano wetu mwingine uko katika Mathayo 23. Yesu anawaonya wanafunzi wake wawe macho, wasijifanye kuonekana kwa nje wasafi na watakatifu, wakati hasa misukumo waliyonayo katika mioyo yao ni ya kiburi na tamaa za kibinadamu. Kama ukisoma mstari wa kwanza mpaka wa kumi na mbili, utaipata picha ya lile analofundisha. Maelekezo hayo yanatuhusu na sisi leo, kama tunapenda kweli kuwa wanafunzi wake. Ni kwa ajili pia ya wote kati yetu ambao wamebatizwa.
Yesu aliwatumia viongozi wa dini wa wakati wake, kukosoa namna isiyo sahihi ya kumwabudu Mungu. Katika mstari wa kwanza tunaambiwa kuwa, wanafunzi wake nao walikuwa sehemu ya mkutano uliokuwa ukisikiliza mafundisho yake. Mafarisayo kwa vyovyote walichukizwa, hata hivyo ujumbe ulikuwa ni ule ule kama aliokwishatoa kwa wanafunzi wake; yeyote anayetaka kuwa mkubwa katika Ufalme, ni sharti awe kama mtumwa kwa wengine kwa sasa.
Sasa fundisho hili lililo wazi kutoka kwa Yesu, sio namna wanadamu wanavyoyaendea mambo, sio? Wapo watu ambao kwa jinsi walivyo, hawana tamaa, wanatosheka na maisha tu yaliyo; wako mara zote tayari kutumikia; hawana tamaa ya kuwa wakubwa juu ya wengine.
Lakini wengine sisi wote tunakuwa na tamaa kazini kwetu au katika jamii zetu. Tunakuwa tunatamani kupata heshima katika jamii tunamoishi, iwe ni katika jiji, mji au kijiji. Katika sehemu hizi zote wapo watu wengi wanaojitahidi kwa nguvu zao zote kupata nafasi juu ya wengine. Mafundisho ya Yesu Kristo yanakuwaje kwa tamaa ya namna hiyo?
Sasa kumbuka kuwa, mafundisho yote ya Yesu yalikuwa ni kwa kuwalenga wanaume na wanawake ambao hatimaye wangekuwa wafuasi wake. Chochote kile ambacho kilikuwa kikiingiliana na 'kuwa mwanafunzi' wa Yesu, kilikuwa na lazima kichunguzwe. Ndivyo inavyopasa hata leo. Hakuna mashaka kuwa, Yesu alijionesha kuwa mfano mzuri katika jambo hili alipowaosha miguu wanafunzi wake (Yohana 13:3-15).
Kama Yesu ambaye ni Mwana wa Mungu, aliweza kupiga magoti sakafuni mbele ya kila mwanafunzi na kumwosha miguu yake, kazi ya mtumishi wa chini kabisa, basi wanafunzi wake wote tangu wakati huu wanapaswa wawe tayari kutumikia, zaidi kuliko kutoa amri.
Kwa kutegemeana na jamii tunamoishi na desturi za nchi hiyo, kuwaosha wageni wanaoheshimika bado kunaweza kuwa kitu cha kufanywa. Kwa sehemu ambazo sio hivyo, somo hilo bado ni la muhimu; linahitaji kutafsiriwa kwa namna ambayo ni ya kuwatumikia wengine kwa njia zingine. Tunaweza kuzisaidia familia zetu, majirani, wafanyakazi wenzetu na watu wengine wowote tunaokutana nao njiani kila siku, kwa namna fulani fulani.
Kwa hiyo, tujiulize: tamaa zetu za kibinadamu ni mbaya? Jibu ni kwamba, itategemea kama kuna ambaye tamaa hizo zinamuumiza. Kama tunafanikiwa kupata kile tunachohitaji kwa kuwasukumia mbali wengine; kwa kutumia ujanja na mbinu zisizofaa, basi jibu ni lazima liwe 'ndio'. Kama tunapata kazi kwa kuwaangusha wengine, au tunapanda cheo au hadhi kwa kuwaponda wengine, tunakuwa hatukutii mwongozo wa Yesu.
Ni wazi yote yanategemea kusudi letu hasa ni nini. Ni kujisikia tumepanda hadhi au kulipiza kisasi kwa wale wasiotupenda, au tunalotaka kufanya litawanufaisha wengine? Tunaweza kuwa viongozi wazuri wanaofaa? Tunaweza kuwa watu wanaoweza kuganga migawanyiko kati ya watu? Haya ni maswali tunayohitaji kujiuliza, na kuna mifano mingi katika Biblia inayoweza kutusaidia kufanya hivyo.
Angalia kwanza katika kitabu cha Esta, Sura ya 3, mstari wa 1 mpaka wa 9. Hapo utamkuta mtu aliyekuwa akiitwa Hamani, aliyekuwa mshauri wa kutegemewa katika Ikulu ya mfalme wa Uajemi. Hamani alikuwa kizalia cha Waamaleki na adui mkubwa wa Wayahudi. Alibuni mpango wa kuwafanya Wayahudi wote chini ya Dola ya Kiajemi wauawe.
Matokeo ya mpango wake huo ulipogunduliwa, yapo kwenye Sura ya 4 mstari wa 3. Kwa jinsi alivyopanga hili litimie, inaonesha Hamani alivyokuwa na nia ya kiovu ya kuwadhuru wengine. Kama utakuwa na muda wa kukisoma kitabu chote utagundua kuwa, kinasisimua kusoma, na kitakuonesha mfano wa namna Mungu alivyokuwa akiwaangalia na kuwachunga watu wake kwa namna isiyotegemewa.
Mfano mwingine ninaotaka tuutizame uko katika Danieli; mtu wa imani kubwa sana kwa Mungu. Alikuwa mtu wa uwezo mkubwa na unyenyekevu wa hali ya juu. Katika maisha yake yote yasiyo ya kawaida, Danieli wakati wote alimpa Mungu sifa kwa miujiza yote iliyofanyika, na kamwe hakudai kuwa na uwezo wa kipekee yeye mwenyewe. Angalia sasa katika Danieli 2:26-30.
Tamaa ya kibinadamu inaweza kuwa na msisimko unavyojitahidi kwa kila njia kufanikisha unachokitaka, lakini ni muhimu kuufikiria mfano wa Sulemani, aliyekuwa mfalme mkubwa kuliko wote wa Kiyahudi. Aligundua kuwa, unapokuwa umefikia hatimaye lengo lako, unalokuwa umepata haliwi la kutosheleza hasa! Unaweza ukawa umejaribu kila kitu na kupata kila kitu, lakini kamwe hutajisikia kabisa umetosheka.
Kuweza kutambua ilivyokuwa kwa Sulemani, angalia Mhubiri 2:1-11. Sulemani anasema katika mstari wa 26 kuwa, kitu kilicho bora zaidi ni kuifuata njia ya Mungu.
Kwa hiyo, Njia ya Mungu basi ni ipi? Ni njia ambayo imeoneshwa vizuri kabisa na Yesu. Ni njia ambayo wale wote watakaokuwa wakubwa, watakaoongoza, lazima pia wawe 'watumikaji'; watu wanaowatumikia wengine. Ni njia ambayo hulka ya mtu mume, au mtu mke, inaongozwa na upendo na huruma. Inaongozwa na moyo wa rehema na dhamira ya kuwasaidia wale wanaotuzunguka.
Mfano wetu wa maana kabisa utakuwa wakati wote ni Yesu mwenyewe, ambaye, ingawa atakuwa Mfalme mkubwa kabisa juu ya mataifa yote atakaporudi duniani, aliweza kuutumia muda wake na nguvu zake kuwahudumia maskini na wagonjwa. Alikuwa na muda na walemavu na vipofu, wakoma na waliokuwa na matatizo ya magonjwa ya akili.
Hatutaweza kuiponya huzuni inayotuzunguka kila siku, ya hali mbaya aliyonayo mwanadamu kama Yesu alivyofanya, lakini tunaweza kuifanya nia yoyote tuliyo nayo kuwa mpango unaotekelezeka, katika kuwasaidia wengine kwa njia yoyote tunayoweza.