Correspondance Course - Lesson 50

Swahili

SOMO LA 50

UAMINIFU MBELE YA MUNGU NA MBELE YA MWANAWE YESU KRISTO

SOMO: Matendo 5

Katika somo hili, nataka tuangalie kwa makini mambo tunayofanya kila siku. Baadhi yake yatakuwa ni kwa ajili ya Mungu na Yesu, kama kuhubiri kwa wengine au kuwasaidia wagonjwa na wazee. Mengine yatakuwa ni kwa kuhudumia familia au kuipa mwelekeo fulani, au wale tunaowajibika kwao.

Matendo mengine yote yatakuwa yakiwahusu watu tunaokutana nao kila siku kwenye shughuli, au safari au kwenye lolote linaloweza kutokea.

Uaminifu ni kitu kinachohusu kutii sheria au kanuni. Ni hivyo zaidi kwa sheria za Mungu, lakini pia kwa sheria za jamii tunayoishi ndani yake. Wakati mwingine kunapokuwa na vita au majanga mengine, sheria za kibinadamu zinavunjwa, lakini mfuasi wa Yesu hajiachii tu kuzivunja. Sababu ni kwamba sheria alizoziweka Mungu na kuelezewa kwa umakini sana na Yesu na mitume wake, zinakuja kwanza katika maisha yake.

Katika somo mojawapo la nyuma tulitazama pamoja fundisho lililopo kwenye Zaburi 34:7. Haya ni maneno ya maana sana na ni faraja kubwa kwetu katika nyakati za shida, lakini maneno hayo yanafanya kazi kwa namna mbili. Kama malaika wa Mungu wapo karibu na watu wa imani katika maisha yao ya kila siku, basi wapo pia karibu kusikiliza na kuona tunapofanya ujanja na kukiuka maadili; tunaposema uongo au tunapochukua kitu ambacho sio chetu.

Njoo nami sasa kwenye maneno ya Paulo juu ya mada hii, tuweze kuona anachotaka kusema. Tuanze na Waraka wake kwa Warumi Sura ya 12 mstari wa 17. Paulo anaonekana kuzingatia hapa jinsi watu wasio Wakristo wanavyomtazama mtu anayemfuata Yesu. Kumbuka hapa kuwa, kuhibiri sio tu yale tunayosema kwa wengine. Kunahusu pia yale tunayofanya na namna tunavyoyafanya. Paulo anaendelea katika Warumi 13:12-14 kusema juu ya ‘matendo ya giza’; mambo ambayo watu wanayafanya kwa kuvunja sheria, wakifikiri kuwa hawataonekana.

Yesu alilitumia wazo hili alipokuwa akiongea na Nikodemo (Yohana 3:19-21). Kusudi analokuwa nalo mfuasi wa kweli wa Yesu, ni kufanya mambo yote kwa namna ambayo yanaweza kuonwa wazi na yeyote; na Mungu na wanadamu wengine. Hili ni fundisho lililo wazi kabisa, au siyo?

Katika Waraka wake kwa Wafilipi, Paulo anatushauri tuwekee mambo fulani-fulani kanuni katika maisha yetu (Wafilipi 4:8). Mambo kama: ukweli, staha, haki, usafi, mambo ya pendeza, yenye sifa njema n.k. ni mambo yatakayowaonesha wengine kuwa ni kweli tunamfuata Yesu, na kwa wakati huo huo yatakuwa ni njia iliyo bora kabisa ya kuwahubiria. Kama tutakuwa tunawazungumzia majirani zetu habari za Yesu na Injili yake ya Ufalme wa Mungu tukiwa na hulka hizo, watakuwa tayari zaidi kuamini tunachosema.

Ni kitu kinachoshangaza kusoma katika nyaraka za Paulo na Petro ushauri wanaotoa, juu ya namna tunavyopaswa kuwachukulia wale walio na madaraka juu yetu. Serikali zinatofautiana duniani, zipo zilizo nzuri na zingine mbaya. Zipo zenye mifumo ya kisheria iliyo ya haki, wakati zingine sheria zake ni kali na za kikatili. Hata hivyo, mitume walishauri utii kwa mamlaka zote. Hebu angalia waraka wa kwanza wa Paulo kwa Timotheo, Sura ya 2, mstari wa kwanza mpaka wa tatu.

Maneno haya yaliandikwa katika wakati ambao dola ya Kirumi ilikuwa ikiwatesa Wakristo. Ni lazima lilikuwa somo gumu kwa wafuasi kulipokea na kulitekeleza wakati huo, lakini ni somo lililopo hapo na kwetu pia kulifuata.

Yesu aliwafundisha wafuasi wake kulipa kodi zao kwa mfalme wa Kirumi na, kwa maneno yake, anatupa nasi kitu kingine cha ziada kukumbuka. Maneno yake katika Mathayo 22:17-22 ni maelekezo ya kuilipa nchi kiuaminifu kodi na ushuru mwingine, na kumpa Mungu upendo wetu na maisha yetu yote kwa kumtumikia.

Paulo aliwapa Wakristo wa Kifilipi nasaha za maana sana. Kuna usemi: “Ikiwapo sifa nzuri yoyote” (Wafilipi 4:8). Ulikuwa ukimaanisha nini? Haya ni mambo ambayo yalikuwa kwa ujumla yamekubalika kwa wote kwa wafuasi wa Yesu kufanya. Hayakuwa tu kwa namna mtu anavyoona, bali wote walivyoona kwa ujumla, wakiwepo wale ndugu wa-kutegemewa zaidi katika eklesia. Kwenye Matendo 6:3 kuna mfano kama huo ambapo maoni ya pamoja ya wafuasi wote yalitumika.

Ilikuwa ni muhimu kwa wakati huo kuwateua watu wakufaa zaidi waliokuwapo. Walikuwa wawe mashemasi; viongozi wa kuwaongoza wengine. Pengine ni uchaguzi mzuri waliofanya; tunayo taarifa ya wawili kati ya hao, walioonekana kuwa watumishi wazuri katika eklesia, wenye uwezo wa kuongoza na kuhubiri kwa bidii.

Kuna somo katika Agano Jipya linalorudiwa-rudiwa, kuwa, tufuate mafundisho ya Yesu, na miongozo makini na maelezo ya mitume wake. Ingawa kuna ushauri huu wa Kibiblia, kikawaida tunaelekea kuwategemea zaidi marafiki na jamaa zetu kwa ushauri wa kibinadamu.

Uliwahi kufikiri ni nini hasa kilichopo kwa mtu mwingine, kinachokufanya wewe ufuate ushauri wake? Pengine imekuwa: ni mtu mzima, mwenye uzoefu na hekima, au ni mkweli. Hebu tuangalie mifano miwili ya watu waliotoa ushauri. Wa kwanza tunamwona katika Hesabu 13, ukingoni mwa Nchi ya Ahadi. Musa alikuwa amewatuma wapelelezi 12 mbele ya taifa lote la Israeli kupeleleza. Waliporudi taarifa zao zilitofautiana (ms. 26-33).

Kati yao kumi walirudi wakiwa wamejaa hofu na mashaka, na ni wawili tu waliokuwa na imani na uhakika kuwa, kwa msaada wa Mungu hakuna kisichowezekana.

Tunapoendelea kusoma kifungu cha 14 tunaweza kuona maneno ya Kalebu na Yoshua katika mstari wa 6 mpaka wa 9. Unafikiri wananchi waliwaamini nani? Ilikuwa, kwa bahati yao mbaya, ni wale waliowakatisha tamaa. Ghadhabu ya Mungu juu ya lile walilochagua inatuonesha ni nani kati ya wale kumi na wawili waliokuwa wakweli na wa kuaminika; watu wa imani. Ilikuwa ni Kalebu na Yoshua. Zawadi yao ilikuwa kuvuka na kuiingia Nchi ya Ahadi na familia zao, wakati wengine wote waliokosa imani wakiangamia nyikani.

Mfano mwingine ni wa marafiki waliotoa ushauri kwa Ayubu, unaopatikana katika kitabu cha Ayubu. Ayubu alikuwa amepoteza kila kitu alichokuwa nacho. Akiwa amekaa kwenye dampo la takataka za mji akijikuna, alitembelewa na marafiki watatu waliompa ushauri. Lakini haukuwa ushauri mzuri na mwishowe tunasoma kuwa, Mungu aliwalaumu marafiki hao watatu kwa ushauri wao potofu (Ayubu 42:7-10).

Ilikuwa ni vizuri kwa Ayubu kwamba alipuuza ushauri ule wa rafiki zake hao, na kuing’ang’ania imani yake kwa Mungu. Kitu cha muhimu cha kugundua hapa ni kwamba, watu hao watatu hawakujaribu kumsaidia Ayubu; walitumia muda mwingi kujaribu kumfariji tu katika huzuni yake (Ayubu 2:13). Hawakutumia kanuni za Mungu katika ushauri wao kwa Ayubu, badala yake walitumia hekima ya kibinadamu inayoshindwa. Huu ndio utofauti tunaohitaji kuuchunguza tunapochukua ushauri kwa marafiki.

Mambo mengine yanayohusu uaminifu yanaonekana kuwa madogo sana na yasiyo na umuhimu, lakini tukumbuke kuwa, kwa Mungu mambo madogo madogo sana tunayofanya, yana maana sana. Tuangalie sasa unabii wa Mika 6:8. Baadhi ya mifano imetolewa katika mstari wa 10 na wa 11.

Hebu jaribu kuwafikiria wenye maduka walio na mizani, ambazo zimefanyiwa ujanja zitoe bidhaa pungufu kuliko kile mteja anacholipia. Mwenye duka anaweza kufikiri ni ujanja mzuri, na ni kitu cha kawaida, lakini Mungu anachukizwa na uovu huu uliojificha. Lakini unaweza usiwe na duka au genge, sasa maneno haya yanakuhusuje?

Katika maisha yetu, tunafanya mambo kwa ajili ya watu wengine. Tunaweza tukawa na ajira, kwa mfano. Tunaweza katika kufanya kazi tukawa tunajituma na kufanya kazi kwa bidii au kufanya kidogo tu. Tunaweza kupata au kutopata mshahara wetu. Ni hivyo hivyo inavyokuwa tunapofanya mambo kwa ajili ya Mungu. Tunaweza tukajitoa sana au kidogo tu. Uongo unakuja tunapojifanya kwa Wakristo wengine kuwa, tumejitoa kwa yote tuliyonayo wakati sio kweli.

Tunapokuwa tumepewa wajibu wa kutekeleza kwa ajili ya wengine au kwa ajili ya kipato, ni lazima tulikumbuke somo hili. Bila kujali ni kwa kiasi gani tunajaribiwa kuzembea kutekeleza wajibu tuliopewa, Mungu anajua tunavyofikiri na kile tunachoweza kufanya kwa siri. Inaweza ikawa rahisi kuyaficha matendo yetu kwa wengine, lakini hatuwezi kumficha Mungu.

Kuna fundisho kali kuhusiana na hili, katika Matendo ya Mitume, Sura ya 5, mstari wa kwanza mpaka wa tano. Hapa mtu na mkewe walijaribu kusema uongo kwa Mungu mbele ya mitume. Hukumu waliyopata ilikuwa ya kutisha. Unaweza ukaona kuwa, huu ulikuwa ni uovu kama ule wa kuwa na mizani batili, au mawe ya kupimia yasiyo sawa sokoni, na tunasoma katika Mika kuwa Mungu anachukizwa na hili.

Kitendo hicho cha Anania na Safira ni lazima lilionekana kibaya sana, kiasi kwamba hatua ya hapo kwa hapo ilibidi ichukuliwe. Hili ni tukio pekee katika Agano Jipya, ambapo uweza wa Roho Mtakatifu umetumika kuua. Kwingineko pole umetumika kuponya na kurudishia uhai kwa wale waliokufa.

Yesu alipojiachia achukuliwe na wale askari, apigwe na kisha asulubiwe, alijitoa kwa kila kitu kwa ajili yetu. Alifanya hivyo ili watu waweze kufunguliwa njia ya wokovu kutoka katika mauti ya milele.

Hapakuwa na udanganyifu katika Yesu; alikuwa wakati wote mkweli kabisa na mwema kwa wote waliomjea. Katika hotuba yake juu ya kuishi Kikristo, ametupa vigezo kadhaa vya kipekee vya kulenga katika kumwitikia (Luka 6:35-38). Maneno ya mwisho katika mstari wa 38 yanatukumbusha haja ya kutoa kwa uaminifu, kama tunahitaji kupokea urithi wa Ufalme.

Swahili Title
Uaminifu mbele ya Mungu na mbele ya mwanawe Yesu Kristo
English files
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission