Correspondance Course - Lesson 51

Swahili

SOMO LA 51

MATUMIZI NA UDHIBITI WA HASIRA

SOMO: Mwanzo 34

Hasira ni hisia ya ajabu sana ndani ya uanadamu wetu. Pengine ina nguvu hata zaidi katika ulimwengu wa wanyama, ndege na samaki. Katika Biblia kuna ushauri mzuri unaotolewa wa namna ya kuidhibiti hasira, na kuna maonyo kadhaa ya wazi kuhusiana na nini kitatokea kama tukiiachia hasira itutawale.

Hasira imekuwa na mwanadamu tangu mwanzo wa historia yetu; sio kama ni tatizo la leo. Kama ukiangalia Mwanzo 4:5, utaona maelezo ya mambo ya kutisha hasira inayoweza kumpelekea mtu kufanya. Kaini alimuua ndugu yake. Tunasoma kwamba, “Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana”.

Kwa kawaida inawezekana kumtambua mtu akiwa na hasira kali kutokana na kubadilika kwa sura yake. Mara nyingi, na hasa kama ni mweupe, kunakuwa na kubadilika hata kwa rangi ya ngozi yake.

Kutokana na somo hilo katika Mwanzo tunahitaji kukumbuka kuwa, Kaini alikuwa ni mtoto wa kwanza wa Adamu na Hawa, na kwa hiyo alikuwa mtu wa tatu kuishi katika dunia. Kama angekuwa amechukia tu, isingekuwa neno sana. Lakini, kwa kuwa Mungu alikuwa ameikubali dhabihu iliyokuwa imetolewa na mdogo wake Habili kwa kuikataa yake, chuki iliipandisha hasira ikawa ghadhabu, iliyomfanya Kaini amuue Habili, ndugu yake.

Kwa hiyo ilikuwa kwamba, katika mwanzo kabisa wa historia yetu, uuaji ulifanyika kutokana na wivu na hasira. Tunajifunza hapa kuwa, hasira ni ya hatari! Katika tukio hilo, ilileta balaa kubwa katika familia yote. Ilipelekea Habili kupoteza uhai wake, na Kaini kufukuzwa. Adamu na Hawa wakawa wamewakosa vijana wao wote wawili.

Mfano mwingine upo katika maneno ya unabii yaliyotamkwa na mwasisi wa taifa la Israeli; Yakobo. Alipokaribia kufa aliita familia yake pamoja na akatabiria hatma yao yote ambavyo ingekuwa. Kifungu cha Mwanzo 49:5-7 kinawaongelea wawili kati ya wana wa Yakobo, Simeoni na Lawi.

Hawa wanaume wawili walikuwa wamejionesha kuwa, walikuwa watu wa hasira kali isiyo na maana. Hebu kifungue hicho cha 34 ukisome mwenyewe. Haya yalikuwa matendo ya giza, na ya aibu katika siku za mwanzo kwa taifa la Israeli; yakivunja ahadi na kukiuka matarajio kimakusudi. Kilichofanya hili litokee kilikuwa ni hasira.

Kitu kinacholeta hofu juu ya haya yote ni kwamba, sisi wote tunapatwa na hasira mara kwa mara. Kama tusingepatwa, tungekuwa watu wa ajabu sana. Hasira inakuja kutokana na kutotimia malengo, kushindwa, wivu, kuchukizwa, na mara nyingine hata kuchoka tu. Tunaweza tukaipata hasira kwa ajili ya watu wengine na pia dhidi yao.

Kama tunajisikia mtu mwingine ametufanyia ubaya tunaweza kujikuta tumechukia, na ni rahisi sana kujihesabia wenyewe sababu iliyotufanya tukasirike kuwa ni halali. Kwa namna hii tunaihalalisha hasira, lakini ni mbaya.

Kuna watu waliozaliwa na hasira za haraka-haraka, wakati wengine wanakwenda pole pole zaidi. Ni wazi kuwa wale wanaokasirika kwa kasi, wana wajibu wa kufanya la ziada kuishinda hiyo hulka. Maneno makali yanayosemwa kwa hasira hayawezi kirahisi kufutika. Fungua na mimi kitabu cha Methali, Sura ya 15, mstari wa 1 mpaka wa 3.

Katika mistari hiyo, kuna ushauri wa maana. Tunaonywa kuepuka mashindano; ‘Neno liumizalo huchochea ghadhabu’. Hekima na upumbavu vina nafasi ya muhimu katika nafsi ya mtu. Kwa maneno mengine, kama tukifikiri kwa makini kabla ya kusema, tunaweza tukaepusha matatizo.

Hili sio jambo rahisi kufanya, lakini ni la maana sana kama tukijizoeza kufanya hivyo. Katika mstari wa 3 swala hili limewekewa uzito hata zaidi kwa kuwa tunaambiwa, macho ya BWANA yako kila mahali, ’yakimchunguza mbaya na mwema’. Anatambua yote tunayofanya na tunayosema. Hili ni la mguso, na hasa kwa wale ambao tayari wamemkaribia Mungu mioyoni mwao, kwa kuwa Mungu anawajali sana wale wanaompenda.

Mahusiano kati ya hasira na upumbavu yanayojitokeza tena katika kitabu cha Mhubiri. Tunaambiwa: “Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu” (Mhubiri 7:9). Unajisikiaje juu ya maneno haya? Ni nasaha nzuri?

Ningependa sasa tugeukie Agano Jipya na kuifungua barua ya Paulo kwa Wakolosai, Sura ya 3. Paulo anawaandikia wafuasi wa Yesu; watu waliobatizwa, walioahidi kuufuata mfano wa Yesu katika maisha yao. Katika sura hii, wasomaji wa waraka huu wanakumbushwa umuhimu wa ubatizo: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Wakol. 3:1).

Kufufuliwa hapa kunamaanisha kuibuka kwenye maji ya ubatizo, kama ambavyo kutumbukizwa kwa muda ndani ya maji kunavyowakilisha kufa pamoja na Kristo. Paulo alitumia kielelezo hicho aliposemea hili katika Wakolosai 2:12.

Muumini anapobatizwa, anapaswa baada ya hapo ayatafute maadili ya kiroho, na sio kuhisi kwa namna ya wale ambao hawamfuati Bwana Yesu Kristo katika maisha yao. Baada ya hapo Paulo anatoa orodha ya mambo ambayo mfuasi ni lazima ayaondoe akilini mwake. Haya mambo, anasema Paulo, yanaweza yakatuletea ghadhabu ya Mungu (Wakol. 3:6).

Nataka tuangalie sasa mstari wa 8 ambapo hasira na mabaya mengine yanatakiwa yawekwe mbali na maisha ya Mkristo. Alilielezea hili vizuri zaidi alipowaandikia Waefeso (Waef. 4:17-24). Picha anayoitoa ni ya mfuasi-mpya anayeziacha namna zake za maisha ya awali, na kuuvaa utu mpya, ‘katika haki na utakatifu wa kweli’. Haya yanapaswa yawe ndiyo matokeo ya kubatizwa ndani ya muumini.

Paulo anatambua ya kuwa, hulka ya ndani ya mfuasi mpya inachukua muda kubadilika, kwa hiyo katika mstari wa 26 anaongelea hasira, akisema: “Mwe na hasira, ila msitende dhambi”. (Waef. 4:26). Alikuwa anakubali kuwa kutakuwa na wakati ambapo hata mfuasi madhubuti kabisa wa Yesu atapatwa na hasira na kwamba, katika mazingira ya namna hiyo, itamfaa akasirike lakini ajidhibiti asitende dhambi. Hasira iwe akilini, lakini isimfanye atende kitendo kinachotokana na kukasirika huko.

Ametuachia tufikirie wenyewe ni kwa nyakati gani hali hiyo inatupata, na itakuwa ni zoezi la maana kwako kutafakari hili, na kuona maelekezo hayo kwa namna maisha yako yalivyo. La muhimu sana katika ushauri huo ni kwamba hasira hii inapotujea, ni muhimu iwe ya muda mfupi; iondoke kabla ya jua kutua. Anasema: ‘Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka”.

Huu hakika ni ushauri mzuri sana, na hasa kunapokuwa na karaha za kimahusiano kati ya mume na mke. Hasira isiachiwe iende siku ya pili; mmojawao ni lazima apende suluhu; awe ‘mpatanishi’.

Tumeshawafikiria watu wale ambao wanazaliwa na hasira za haraka-haraka; wenye uwezo mdogo wa kujidhibiti. Hebu sasa twende pamoja kwenye barua Paulo aliyomwandikia Tito, Mkristo kijana aliyempa jukumu la kufungua eklesia katika kisiwa cha Krete. Katika Tito 1:1-7 alimpa mwongozo wa kuweka waumini ambao wangekuwa ‘wazee’ wa eklesia hizo, na utaona kuwa mojawapo ya sifa za kuangalia ilikuwa ni wasiwe, ‘wepesi wa hasira’.

Ni Yesu mwenyewe aliyekuwa ametoa kanuni zote za maisha ya mfuasi. Katika hotuba yake ya Mlimani, mojawapo ya mambo ya muhimu aliyosema Yesu ilikuwa ni kuhusu hasira. Hebu soma Mathayo 5:21-22 upate mwenyewe anachosema. Kama tukiyachunguza maneno yake, tutakuta kuna maswali kadhaa yanatujea.

Tunaweza tukawaelezea watu wengine kama ni ‘wajinga’ katika namna yetu ya kuongea ya kila siku, lakini mara nyingi ni maneno yanayosemwa kwa kilipuka au mzaha kidogo na yanapokelewa kihivyo na mtu tunayeongea naye. Ni wakati maneno hayo yanaposemwa kwa hasira na kwa kukaziwa, ndipo yanapomuuma mtu wa pili na hayakupaswa kutumika.

Katika mstari wa 23 mpaka wa 26 Yesu anaruhusu hali ambayo, kama tumefanya vibaya au kusema vibaya kitu, tunaleta tena kuelewana. Ushauri wake uko wazi: “Upatane kwanza na ndugu yako” na “Patana na mshitaki wako upesi”. Hili linafanya kazi kwa upande wa pili pia, maana kuna neno lingine la maana analilolitumia Yesu katika kuwafundisha wanafunzi wake; neno ‘msamehe’ (Luka 17:3,4).

Mtu anapokuja kwako na kusema ‘nisamehe’, kubali ombi lake na usilifanye jambo hilo kuwa kubwa kwa kuwa mgumu. Katika Injili zote tunafundishwa kuwa, kama unategemea Mungu akusamehe makosa yako, ni lazima na wewe uwasamehe wengine.

Nataka nimalizie somo hili kwa kuongea kidogo juu ya hasira ya ‘haki’. Hii ni aina ya hasira au ghadhabu inayoonekana katika Biblia, na ipo kwa sababu nzuri. Hasira inayotokana na ujinga wetu, kutotii kwetu au dhambi zetu, ni hasira inayostahili kuwepo kwa Mungu aliyetuumba. Yeye peke yake ndiye aliye na haki kamilifu ya kukasirika, na tunasoma mengi juu ya hili hasa katika Agano la Kale.

Mungu alimuumba mwanadamu kwa namna ya kipekee kati ya viumbe wengine wenye uhai katika sayari hii. Sisi ni watu tunaoguswa sana tunapofanyiwa mabaya, lakini ni wajanja-wajanja sana. Tunaweza kuwa na upendo, lakini tuna hila na tunalipuka-lipuka mara nyingine. Tangu Adamu na Hawa wafukuzwe katika bustani ya Edeni kwa sababu ya kiburi, mwanadamu wakati wote amekuwa akimhuzunisha Mungu.

Agano la Kale linaongelea ghadhabu ya Mungu kwa taifa la Israeli. Hili halina maana kuwa haoni uovu walionao wanadamu leo; ni kinyume chake kabisa. Mungu alimtoa Mwanawe pekee awe dhabihu kwa ajili ya dhambi za watu, na kwa sababu hiyo anataka mwitikio wa maana kutoka kwetu. Na sisi tumepata bahati ya kuwekewa lengo lote la Mungu mbele yetu kwenye Biblia.

Historia ya taifa la Israeli imehitimishwa katika unabii wa Hosea, katika Sura ya 13, mstari wa 9 mpaka wa 11. Kitu kibaya kuliko vyote walichofanya ilikuwa kumkataa Mungu, na kuchagua kuabudu miungu ya miti na mawe (sanamu). Baada ya hapo walimtaka Mwana wa Mungu auawe, likatokea. Kwa sababu hizo, Mungu alipatwa na hasira juu ya watu wake.

Kuna fundisho la maana kwetu leo kwa kuwa, kama ukimwangalia tena Hosea, kwenye Hosea 14:1-4 utauona upendo wa Mungu kwa watu wake Israeli, kwa namna ambavyo atawabariki mbeleni. Katika somo la mbeleni tutalirudia tena somo hili la upendo wa Mungu kwa kuwa ni la muhimu.    

Swahili Title
Matumizi na udhibiti wa hasira
English files
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission