SOMO LA 52
MFUASI NA NCHI
SOMO: Warumi 13
Mtume Petro alipokuwa akiziandikia eklesia zote katika Asia alisema kwamba, wafuasi wa Yesu ni lazima wamche Mungu na kumheshimu mfalme (1 Petro 2:13-17). Kwa wakati huo, mfalme pekee alikuwa Mfalme wa Kirumi, na kwa wakati huo wa mwisho-mwisho wa maisha ya Petro, mfalme huyo alikuwa Nero, aliyekuwa âbalaaâ kwa ukatili wake na kwa jinsi alivyowatesa Wakristo.
Tatizo la kuwa mfuasi wa Yesu, na wakati huo huo kuishi katika dunia ya watu iliyojaa ubadhilifu, ukatili na utovu wa maadili, ni lazima lilionekana gumu kwa Wakristo hao wa kwanza. Tatizo hilo halijapungua makali hata leo; linaendelea. Somo hili litaonesha maelekezo ya Kibiblia kwa ajili ya wafuasi wote wa Yesu waliobatizwa, na wale ambao wamekuwa wakiifuatilia kozi hii ya Biblia kwa njia ya posta.
Itajaribu kusaidia wote wale wanaoona shida kuelewa mahusiano yanavyopaswa kuwa, kati ya mfuasi wa Yesu na Serikali katika nchi anamoishi. Masuala tutakayoangalia ni:
- Huduma za kijeshi
- Ushiriki katika shughuli za kipolisi, mgambo n.k
- Kutumikia mahakama au kuwa sehemu ya mfumo wa kisheria
- Kushiriki katika maandamano yoyote ya kupinga.
- Kuituma haki ya kupiga kura.
Kwa kuwa somo hili limeandikwa kwa ajili ya kutumika katika nchi nyingi, ni lazima litoe maelezo kuhusu sheria za namna tofauti, na kanuni zinazowatawala raia wa nchi hizo. Ni muhimu pia liseme kwa uwezekano kwamba, nchi yako inaweza ikawa na tatizo la vita kwa wakati huu. Katika baadhi ya nchi, vijana wanalazimika kujiunga na jeshi na kupambana vitani. Inakuwaje kwa mfuasi wa Yesu?
Kusimama mbele ya maafisa wanaowaandikisha vijana kwa nguvu, au mbele ya mahakama kudai haki ya uhuru wa kutojiunga na jeshi la nchi yako, vyote vitahitaji moyo wa ujasiri wa hali ya juu. Lakini, vitahitaji pia kuzijua sababu za Kimaandiko za kwa nini unafanya hivyo. Mkufunzi anayekufundisha, anaweza kukupatia vijitabu vya Kikristadelfia vinavyoongelea mada hii kuifafanua zaidi, lakini sababu za kawaida zimeelezwa hapa.
Tuangalie kwanza katika Injili ya Luka, Sura ya 22, mstari wa 35 mpaka wa 38. Mtu anaweza akanukulu mistari hiyo kwako kuonesha sababu ya kupambana, lakini ni muhimu uangalie kwa umakini matukio yote katika usiku ule ambao Yesu alikamatwa. Wawili kati ya wanafunzi wake tayari walikuwa wamebeba silaha, na tunajua ya kuwa mmojawao alikuwa Petro (Yohana 18:10). Fundisho kwa wanafunzi wake na kwetu pia limeandikwa katika Injili ya Mathayo: âWote waushikao upanga, wataangamia kwa upangaâ (26:51-53).
Yesu alitaka kuweka wazi kwa wafuasi wake kuwa, hawakupaswa kutumia nguvu; hawapaswi kulazimisha. Alionesha kimatendo kulivyo âkuwapenda maaduiâ kulingana na mafundisho yake, kwa kumponya askari yule wa Kuhani Mkuu aliyeshambuliwa na Petro, kwa kulirudishia sikio lake (Mathayo 5:44, Luka 33:50, 51). Ili uweze kuwashawishi wakubwa walioko madarakani kuwa ni kweli unafuata na kuitii miongozo ya Yesu, itakubidi uoneshe imani yako kwa namna unavyoishi. Ukiweza kufanya hivyo watu wengine wataweza kutambua ya kuwa uko tofauti.
Yesu analielezea hili kwa namna nzuri sana akisema: âNuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguniâ (Mathayo 5:16).
Paulo alitoa maelekezo hayo kwa Wakristo waliokuwa wakiishi Rumi. Anaweka wazi jukumu la mfuasi la kuwa mtii kwa sheria za nchi yake, na wajibu wake wa kulipa kodi zote (Warumi 13:1-7). Katika waraka wake kwa Timotheo anaamuru tuwaombee wafalme na wote wenye mamlaka, tukiomba waweze kuendelea kuturuhusu kumwabudu Mungu kwa namna anavyotutaka.
Miaka zaidi ya mia tano nyuma Mungu alikuwa ametangaza kuwa, ndiye aliyekuwa akiongoza katika ufalme wa binadamu, na ndiye aliyekuwa akiwaweka watawala madarakani kulingana na anavyoona (Danieli 4:25).
Pamoja na jeshi, kuna kazi zingine zinazowataka watu wavae âYunifomuâ, wabebe silaha na kuapa viapo maalum vya utii kwa taifa. Kutokana na sababu tulizozisema, na haja pengine ya kuelezea kwa nini unapingana na kuingia vitani, isingekuwa jambo la busara kuipokea ajira ya namna hiyo; hata kama inatoa mshahara mzuri na maisha bora zaidi kwa familia yako.
Bwana Yesu alipokuwa akihukumiwa mbele ya mtawala wa Kirumi, Pilato, alisema kuwa Ufalme wake ungekuwa kwa wakati mwingine. Haungekuwa wa kuwekwa kwa nguvu za kijeshi, na wafuasi wake wasingehitaji kupambana (Yohana 18:36).
Nchi zile zenye mfumo wa kisheria unaotokana na ule wa Kingereza, zitakuwa kwa kiasi kikubwa zikitumia âwazee wa mahakamaâ kukaa katika mahakama ya kisheria, kuamua hukumu ya mtuhumiwa aliyefikishwa mahakamani. Katika nchi ya Uingereza na Amerika, inachukuliwa kuwa ni haki na wajibu wa raia wote kufanya kazi hiyo wakitakiwa. Kama hili likikutokea itakubidi kuamua kama ni sawa au sio sawa kuwa na sehemu katika baraza hilo. Hapa kuna mwongozo unaotoka kwenye Biblia, unaoweza kukusaidia.
Pamoja na Paulo kutoa maelekezo ya kuwa raia wema, la kwanza kukumbuka ni kwamba wajibu wetu wa kwanza ni kwa Mungu; âkumcha Mungu, na kumpa mfalme heshimaâ (1 Petro 2:17). Petro na wanafunzi wenzake kadhaa walipoletwa mbele ya baraza la Kiyahudi lililokuwa likitawala, wakishutumiwa kwa kuhubiri Injili kinyume cha sheria, jibu la Petro lilikuwa kusema: âImetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamuâ (Matendo 5:28, 29).
Bwana Yesu yuko wazi katika maelekezo yake kwetu kuwa âtusihukumuâ (Mathayo 7:1). Maana yake hapa ni kuwa, tusilaani au kutolea adhabu makosa ya wengine. Hili liko wazi kutokana na maneno yake yaliyofuata na mfano mdogo aliotoa kumhusu mtu mwenye boriti kwenye jicho lake (ms. 2-5).
Yesu anatutegemea tuwe na maamuzi yenye umakini katika mambo na matukio mengi katika maisha yetu. Hatupaswi kuwa mahakimu. Yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa mhukumu mkubwa wa wote, atakaporudi duniani. Sio juu yetu kuwatolea hukumu watu wengine; tunalohitajika kufanya ni kuwa waangalifu tu na wale wanaotaka kututenga na Yesu.
Katika waraka wake kwa Wafilipi Paulo anaeleza kuwa, kumfuata Yesu kulitakiwa kuwe kipau-mbele chao namba moja. Uraia wetu upo naye mbinguni kwa kuwa huko ndiko aliko kwa sasa. Hatuna sehemu katika michakato ya serikali za kibinadamu, na mifumo ya kisheria ya nchi yoyote ndio msingi wa taifa hilo. Kwa hiyo, hatuwezi kuwa na sehemu katika kuhukumu.
Hili lina maana ya kwamba, tutaona shida kujiunga na kazi ya uhakimu au kushiriki katika namna haki inavyotolewa. Kuwa âmzee wa barazaâ ni kushiriki katika namna haki inavyotolewa. Kuwa âmzeeâ kunamuweka mtu katikati ya mchakato huo.
Kutokana na vifungu tulivyovitazama katika somo hili, inaeleweka kuwa, kama wafuasi wa Yesu ni lazima tujitenge wenyewe na dunia na mengi ya mambo watu wanaotuzunguka wanayoona ya kawaida; ya kukubalika. Paulo alitoa nasaha nzuri kwa Wakorintho katika waraka wake wa pili kwa Wakorintho, Sura ya 6, mstari wa 14 mpaka wa 18. Kama tumekuwa wafuasi wa Yesu, ni kwa kuwa Mungu ametuita kwa ajili ya fursa hii ya ajabu.
Watu walioko madarakani kwa kawaida hawajihesabii kuwa wapo hapo kuyafanya mapenzi ya Mungu. Wanafuata sera za chama kilichopo madarakani. Katika mataifa ya magharibi watu wote wanapofikia umri fulani wanakuwa na haki ya kupiga kura, kwa ajili ya wanasiasa watakaokuwa madarakani katika serikali za mitaa na serikali kuu. Haki ya kupiga kura kwa sehemu fulani ni fursa iliyopatikana miaka ya karibuni, na ilipatikana baada ya jitihada kubwa. Sasa ni nini anachopaswa kufanya mfuasi wa Yesu kunapokuja uchaguzi?
Tunafahamu kutokana na unabii mwingi kuwa, Mungu ndiye anayeongoza na kudhibiti hatma ya mataifa, na tumeona mojawapo ya unabii huo katika Danieli. Tunajua kuwa kama tunampigia kura mwanasiasa, tunawajibika kwa kile mtu huyo anachofanya. Tunafahamu kuwa, wanasiasa walio wengi wanafuata maamuzi ya viongozi wa vyama vyao na kwamba, maamuzi yanayofanywa na wanadamu, ni mara chache yanakuwa yakiizingatia Sheria ya Mungu.
Kwa hiyo hakuna sababu ya sisi kumpigia kura mwanasiasa, au kujihusisha na mambo ya siasa kimitaa au kitaifa. Hakuna namna ambayo tunaweza kujishirikisha katika maandamano yanayotokea kupinga sera ya serikali. Sheria ya Kristo kwa maneno ya Paulo ni; âMwe radhi (âmtoshekeâ) na vitu mlivyo navyoâ, na, âBwana ndiye anisaidiayeâ (Waebrania 13:5, 6).