Correspondance Course - Lesson 56

Swahili

Somo la 56:

ZAWADI YA HALI YA JUU YA TUMAINI KATIKA MAISHA YAKO

Somo: Maombolezo 3

Tumaini ni mojawapo ya zawadi za maana sana zinazotoka kwa Mungu. Kwa upendo wake kwetu, alijua ni kwa kiasi gani mwanadamu angehitaji hili, na kwa namna alivyoushughulikia uanadamu wetu, ametuwezesha kuwa nalo hata katika mazingira yaliyo mabaya sana. Hebu funua Biblia yako usome waraka wa pili wa mtume Paulo kwa Wathesalonike, Sura ya  pili, mstari wa kumi na sita na kumi na saba.

Kutoka kwenye kurasa za mwanzo kabisa za Biblia, tunaweza kuyafuatia maisha ya watu waliosukumwa na tumaini kufanya mambo kadhaa katika maisha yao. Kuna mahusiano makubwa yaliyopo kati ya tumaini na imani, na tutaiangalia imani katika somo la 57.

Katika Waebrania, Sura ya 11, mstari wa kwanza, tunasoma ya kuwa, imani ni uhakika wa mambo yatarajiwayo. Tunapokuwa tuna-tumaini, tunaweka akilini mwetu picha za mambo ambayo tungependa yatokee, mambo ambayo tungependa kuyafanya, na kwa kuwa tu-wanadamu, vitu ambavyo tungependa kuvipata.

Tumaini ni mojawapo kati ya mambo matatu ambayo Paulo aliyaona kuwa ya msingi, katika hulka ya mfuasi wa kweli wa Kristo, anayosema ni: imani, tumaini, na upendo (1 Wakor.13:13). Kwa hiyo hebu twende sasa na kuwaangalia baadhi ya watu katika Biblia, waliokuwa na tumaini, na wachache waliokosa.

Tutaanza na Yesu kwa kuyatazama maneno ya Petro, aliyekuwa mmoja kati ya wafuasi wake wa mwanzo. Yapo katika Matendo 2:26. Petro alikuwa akimuongelea Yesu, lakini akitumia maneno ya mfalme Daudi yaliyopo katika Zaburi ya 16 mstari wa 9. Kama unaweza kujiweka katika nafasi ya Yesu alipojiachia mwenyewe akamatwe, na kuteswa, na kuuawa msalabani, utaweza kutambua jinsi unabii huo uliofanywa na Daudi katika Zaburi hii, ulivyokuwa wa muhimu kwa Yesu.

Sasa tutaangalia maneno kadhaa ya nabii Yeremia, aliyeteseka sana kwa sababu ya kusema bila kuogopa, ujumbe uliotoka kwa Mungu, kwa watu katika Yerusalemu. Aliwaambia watu na mfalme wao kuwa, ili waishi iliwabidi wajisalimishe kwa jeshi la Babeli. Walimchukulia Yeremia kama msaliti, na kumtumbukiza katika handaki refu sana jijini hapo (Yeremia 38:6). Katika Maombolezo 3:1-6 Yeremia anaongelea hofu aliyokuwa nayo na hali yake ilivyokuwa mbaya sana.

Somo la maana sana kwetu ni kwamba, katika dhiki yake na hatari iliyomkabili, Yeremia aliweza kuyaona mambo kwa namna iliyokuwa nzuri zaidi (ms. 18). Tunaweza na sisi kujisikia hivyo wakati wa hali ngumu katika maisha yetu, lakini endelea kusoma sasa mstari wa 19 mpaka wa 21. Katika dhiki yake, Yeremia ghafla anakumbuka kuwa bado yupo hai, na maneno yake matamu ya sisi kukumbuka, yanafuatia:

“BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, kwa hiyo nitamtumaini yeye. BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA, na kumngojea kwa utulivu” (Maombolezo 3:24-26).

Kwa hiyo, tumaini ni kitu cha subira; tunahitaji kuwa watulivu tunapoungojea wokovu unaotoka kwa Mungu.

Mengi yameandikwa kuhusu kurudi kwa Yesu duniani, akiwa ni Mfalme. Tungependa hili liwe leo; kuna matatizo mengi mno katika dunia hii yanayohitaji ufumbuzi. Watu wanaonekana hawaliwezi hili hata wafanyeje. Ni hapa ndipo maneno ya Yeremia yanapokuwa ya muhimu kwetu kukumbuka. Tuna wajibu wa kuungojea kwa utulivu wakati ambao Mungu ameuweka.

Sasa hebu tuutafakari mfano wa Abramu, aliyehama mji na kuacha kila kitu, kufuata maono aliyopewa juu ya wakati wa mbeleni. Mungu alipokuwa amemuahidi mambo ambayo yalikuwa mbali sana mbeleni, ilikuwa wazi kwa Abramu kuwa, angehitaji mwana wa kuendelea baada yake, na hata mjukuu na kitukuu pia! Hebu angalia uone ni kwa muda gani ilimbidi Abramu angojee kabla ya Isaka kuzaliwa. Abramu alikuwa na miaka 75 alipoondoka Harani, na miaka 100 Isaka alipozaliwa; miaka 25. Ni muda mrefu kusubiri kwa imani!

Ni vibaya kiasi gani kuishi bila tumaini! Kwa kipindi kifupi Ayubu alikuwa hivi (Ayubu 7:3-7). Kama ukisoma juu ya mabaya yote yaliyompata yeye na familia yake, ni rahisi kuelewa ni kwa nini alijisikia hivyo. Hata hivyo, baada ya kupima namna ya kufikiri ya kibinadamu ya marafiki zake, namna yake ya kuyaona maisha iliboreka. Katika Ayubu 19, pamoja na hali yake kuwa mbaya sana, ghafla anabadilika katika maombolezo yake, na kusemea mambo ambayo nasi tunayaamini hata leo kuhusiana na mada ya kifo na ufufuo.

Ni sawa tushangae jinsi ilivyomjea picha nzuri ya ajabu, na tumaini zito ambalo lilikuwa liwe muhimili wa hulka ya mtu huyu wa imani sana. Anasema, anajua ya kuwa mtetezi wake yu hai na kwamba, hatimaye atasimama katika nchi na kumhesabia haki (Ayubu 19:25-27). Haya ni maneno matamu sana ya kuyageukia, tunapokuwa kwenye taabu na maisha yenyewe yanapokuwa hayaeleweki.

Kwa hiyo, tumaini ni kitu cha maana sana cha kuwa nacho; tumaini juu ya kutimia kwa Ahadi za Mungu kwa dunia hii, kwa namna ambayo maisha ya watu wote yataboreka sana. Lakini kuna namna nyingine ya ajabu zaidi ya vile tunavyoweza kulielewa hili neno ‘tumaini’.

Mitume wa Yesu walilitumia neno ‘tumaini’ kwa namna iliyoelezea mambo yote waliyoamini, kumhusu Yesu na Ufalme wake unaokuja. Maneno waliyotumia ni: “Kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu” (Tito 3:7), “tumaini la wokovu” (1 Wathes. 5:8) na, “tumaini la utukufu” (Wakolosai 1:27).

Paulo aliandika hata kwa Warumi katika Warumi 4:18 kuwa, tunaokolewa kwa njia ya ‘tumaini’. Katika 1 Wakorintho 15:19 anatutaka wote tutulie na kufikiri. Kama katika maisha haya matumaini yetu ndipo yalipo tu, anasema, basi sisi ni watu wa kusikitisha sana. Kutegemea kuwa wanasiasa, wanadiplomasia, majeshi, mashirika ya misaada ya kimataifa n.k wataibadili dunia iwe mahali bora zaidi kwa watu wote kuishi, ni kitu ambacho hakitakaa kitokee.

Paulo anasema kuwa, ni tofauti sana na kuwa na tumaini kwa Yesu maana, Yesu alifufuka kutoka kwa wafu, yupo hai na anarudi duniani. Atakaporudi, atausimamisha Ufalme wa Mungu, na wafuasi wake wote wa enzi zote katika historia yote, watafufuliwa kutoka mautini, na kama waliishika imani, watapewa uhai utakaoendelea daima katika dunia iliyoboreshwa sana, yenye amani.

Bwana Yesu Kristo atakuwa Mfalme juu ya mataifa yote, na atatawala kwa mamlaka inayotoka kwa Mungu, kwa haki na hekima na upendo.

Kubatizwa katika Jina la Yesu kunaifungua njia ya mambo haya mazuri sana, na mtume Petro anaandika katika waraka wake wa kwanza, kuwa:

“Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili, tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu” (1 Petro 1:3).

Kubatizwa ni kuzaliwa upya ili kuwa mfuasi wa Yesu. Hili kwetu leo ni tumaini lililo hai, na moja ambalo tunaweza kujisikia vizuri sana kuwashirikisha wengine. 

Swahili Title
Zawadi ya hali ya juu ya tumaini katika maisha yako
English files
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission