Correspondance Course - Lesson 57

Swahili

Somo la 57:

IMANI NA KUUFANYIA UKRISTO KAZI

Somo: Waebrania 11

Mara nyingi katika masomo yetu haya, tumetumia neno ‘Imani’. Sasa ni wakati wa kutazama na kuona ni nini waandishi katika Biblia wanachotutaka tuelewe juu ya neno hili. Ni neno linaloweza kutumika katika lugha yetu ya kawaida kwa namna kadhaa.

Mfumo wowote wa kiibada unaweza kuitwa ‘Imani’. Kama tunalazimika kuvuka kikorongo au kijito kwa kupita juu ya kigogo, tutahitaji kuwa na imani kuwa kidaraja hicho kina uwezo wa kuuhimili uzito wetu na kimewekwa vizuri; vinginevyo hatutathubutu.

Paulo katika waraka wake kwa Waebrania, Sura ya 11, anatupa maelezo juu ya imani. Anasema, imani ni kuwa na uhakika wa kitu tunachokitarajia, tusichokiona. Ni hili lililowafanya watu waaminifu wa kale wasifiwe.

Unajua kutokana na masomo haya mengi uliyopitia kuwa, katika Agano la Kale Mungu alionekana kuwa karibu sana na Ibrahimu na familia yake, kuja mpaka wakati wa manabii. Watu waliokuwa wakiishi enzi hizo, hawakuwa mbali na mojawapo ya matukio makubwa ya kutisha. Pengine ilikuwa ni rahisi zaidi kwao kuwa na imani kwa Mungu na kwa ahadi zake. Mungu aliwatarajia watu hao wawe na imani na alipendezwa nao na kuwazawadia walipokuwa nayo.

Katika wakati wa Yesu, ni miujiza iliyowafanya watu katika nchi ya Israeli waamini kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Mungu na Masihi (angalia Yohana 11:44, 45, kwa mfano).

Leo hatuna miujiza ya waziwazi kama maji ya Bahari ya Shamu kutengana, yaliyowaachia wana wa Israeli walitoroke jeshi la Kimisri (Kutoka 14 na hasa mstari wa 13). Hatuna manabii wa Mungu wanaozunguka katika nchi zetu, na hatuna uwezo wa kusimama na kuiona miujiza iliyofanywa na Yesu.

Ulicho nacho ni Biblia yako ambamo matukio haya yote, na ahadi na maonyo yameandikwa humo kwa uweza wa Mungu, kwa ajili yetu wote kusoma. Ni ili tuwe na kumbukumbu ya wakati wote ya kusudi la Mungu kwa dunia hii, na ‘ofa’ anayoitoa kwako kibinafsi, ya wewe kuwa na sehemu kwa mambo yanayokuja.

Kwa hiyo, imani kwa leo ni ridhaa ya moyoni utakayokuwa nayo moyoni na akilini mwako. Utakuwa nayo kutokana na mambo unayoyasoma kwenye Biblia yako au kufundishwa na wengine, ambao nao wana imani na Neno la Mungu.

Ninalotaka kufanya sasa ni kukuonesha kuwa, Mungu anatutaka tuweke imani yetu katika matendo. Mtume Yakobo katika waraka wake analielezea hili (Yak. 2:14-18). Kuwa uhusiano mkubwa unaopaswa kuwepo, kati ya imani na matendo. Lingine la kufikiria lipo katika maombi, ambayo pia ni unabii kwenye 1 Samweli 2:3. Hapa tunaambiwa kuwa, Mungu anatutazama na kuyapima matendo yetu. Kwa hiyo kile tunachofanya kwa sababu ya kuwa na imani, ni cha muhimu sana kwake.

Mungu anajua tunahitaji msaada kuweza kufanya hili, na ametupa mifano mingi jinsi imani inavyoweza kuwa matendo.

Kuna mifano miwili katika Sura tuliyoisoma katika waraka kwa Yakobo. Ilikuwa ni Sura ya pili, na sasa tuangalie mstari wa 21 mpaka wa 24. Kama ukirudi nyuma kwenye Mwanzo 22: 1-18 unaweza kuyapata maelezo yote hapa. Ili kuweza kutambua sawasawa imani ya Ibrahimu ilivyokuwa, ni vizuri ukumbuke kuwa, Mungu alikuwa amempa Ibrahimu ahadi ya muhimu sana alipomtoa katika mji wa Uru katika Ukaldayo (Mwanzo 12:1-3).

Ahadi hiyo kutimia, ilitegemea Ibrahimu kupata mtoto wa kiume, na familia yake kukua na kuwa taifa kubwa. Tunajua, hatimaye Ibrahimu aliweza kumpata mtoto huyo, Isaka, wakati yeye na mke wake wakiwa wazee sana. Hili linatusaidia kuelewa jinsi Ibrahimu alivyokuwa na imani kubwa, na vile alivyojaribiwa alipotakiwa amtoe Isaka kuwa sadaka.

Paulo anatuambia kile Ibrahimu alichokuwa akiwaza, wakati alipokuwa akipanda na Isaka kwenda mlimani Moria (Waebrania 11:17-19). Isaka alikuwa kijana wa muhimu sana katika ahadi Mungu aliyokuwa ameitoa. Bila ya Isaka hakuna ambao lingeweza kutimia. Mungu alipomtaka Ibrahimu amtoe Isaka afe, Ibrahimu aliamini Mungu angeweza kumrudishia tena uhai.

Kwa vyovyote hili lilihitaji kuwa na imani sana. Lingine la maana sana kuhusiana na tukio hili ni kwamba, Mungu hakulifanya hili ili kumpima Ibrahimu tu. Alikuwa tayari akijua imani ya Ibrahimu ilivyokuwa, na unaweza kuliona hili katika Mwanzo 15:3-6. Amri yake kwa Ibrahimu kwamba amtoe Isaka, ilikuwa ni kumfundisha Ibrahimu jinsi yeye Mungu alivyokuwa akikusudia kuleta wokovu kwa wanadamu, kwa njia ya dhabihu ya Mwanawe.

Tendo hili lilimfundisha Ibrahimu kuwa, siku moja mbeleni, yeye Mungu, akiwa ni Baba, atamwachia Mwanawe Yesu awe sadaka kwa ajili ya dhambi za dunia; awezeshe msamaha kwa ajili ya dhambi kupatikana, ufufuo na uzima wa milele kwa watu wenye imani kwa Mungu, na kwa Mwana wake, Yesu Kristo.

Mfano mwingine uliotolewa na Yakobo ni wa Rahabu. Huyu alikuwa, kwa kumwona haraka, mtu asiyefaa. Hakuwa Myahudi na anasemewa alikuwa malaya, akikaa katika mji wa Kikanaani wa Yeriko. Alikuwa ni mtu pekee hapo aliyeonekana kuwa na imani juu ya Mungu wa Wayahudi.

Kwa namna fulani alikuwa amefahamu kuwa, umati mkubwa wa watu waliokuwa wamepiga kambi upande wa pili wa mto Yordani, wangekuja na kuidai nchi yao ya zamani, nchi Mungu aliyokuwa amempa Ibrahimu (Yoshua 2).

Kuta za mji huo zilipoanguka kwa muujiza, ni Rahabu tu na familia yake waliookolewa kwa kuwa, Rahabu alikuwa amejihatarishia maisha yake kwa kuwahifadhi wapelelezi wa Kiisraeli. Tukio hili kwa vyovyote lilikuwa la kipekee sana, kiasi kwamba Yakobo na Paulo walimtumia Rahabu kama kielelezo cha mtu wa imani.

Waebrania 11 imejaa mifano ya imani kwa matendo, na ninataka sasa kuutazama mmoja tu zaidi. Nuhu aliishi katika nyakati ambapo kulikuwa na uovu mwingi sana kati ya watu, enzi ya ustaarabu wa kale (Mwanzo 6, 7 na 8 na hasa Mwanzo 6:5-7). Tunaoneshwa miaka ilivyopita Nuhu akiwa anajenga meli kubwa, kwa kuona kinachosemwa kwenye Mwanzo 5:32 na Mwanzo 7:6. Kwa hiyo alichukua miaka 100 kujenga hiyo Safina, ambao ni  muda mrefu sana kwetu. Kwake yeye haukuwa, kwa kuwa aliishi miaka 950.

Kuna mashaka kama kuna mtu aliyewahi kujenga mashua kubwa kama hiyo nyuma. Kwa miaka hiyo yote Nuhu alikuwa akilazimika kukata miti, kujifunza namna ya kutengeneza misumeno, kukata mbao na kuzisawazisha zinyoke, ziweze kufaa kivipimo, zikipigiliwa maji yasipenye.

Safina hiyo ilipaswa iwe kubwa sana, iwe mahali pa usalama kwa wanadamu na wanyama, ndege na wadudu, kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kwa jitihada yote hii na kwa miaka yote hiyo ya kujenga, kilichomsukuma Nuhu kufanya yote ilikuwa ni imani yake kwa Mungu. Paulo anahitimisha mfano huu wa hali ya juu wa Nuhu katika Waebrania 11:7.

Tulichojifunza ni nini mpaka hapo? Tumejifunza:

  • Kwamba imani ni kuwa na uhakika kuwa Mungu yupo na kwamba wakati wote atatimiza kile alichoahidi.
  • Kwamba haitoshi kusema kuwa tunaamini; Mungu atakuwa akijua wakati wote kama ni kweli.
  • Kwamba imani peke yake haitoshi, tunahitaji kuifanyia kazi katika maisha yetu.
  • Kwamba Mungu anatutarajia mara nyingine tuendelea na kitendo cha kiimani tunachokifanya kwa muda mrefu.

Kama unafikiria kuamua kubatizwa au kama umeshampokea Yesu kwa njia ya Ubatizo, utahitaji kujua kama hili lina maana gani kwa maisha yako ya siku kwa siku. Unaiwekaje imani yako katika matendo? Yafuatayo ni mapendekezo kadhaa kutoka kwa Paulo, katika waraka wake kwa Warumi, kwenye Warumi 12:9-18.

Yasome kwa umakini na uyatafakari jinsi yanavyoweza kuyagusa maisha yako. Paulo anatuambia kuwa, tunapaswa kuiheshimu Serikali katika nchi tunamoishi, hata kama ni mbaya. Hili lina maana kuwa, ni lazima tuviheshimu vyombo vya dola (Warumi 13:1-5). Hili linahusu pia kulipa kodi kiuaminifu (ms. 6, 7).

Masharti muhimu mengine yanatoka kwa Yesu mwenyewe, katika Mathayo 25. Anatuambia hasa namna ya kuyaweka mafundisho yake katika matendo maishani mwetu (ms. 31-40). Ni muhimu sana kuyakumbuka maneno hayo.

Yesu anaongelea siku ya hukumu kuwa, katika siku hiyo, hatatupima sisi kulingana na mambo tuliyoyajua, bali kwa namna tulivyojitahidi kuyaweka aliyofundisha katika matendo katika maisha yetu; jinsi tulivyoufanyia kazi Ukristo wetu.

Swahili Title
Imani na kuufanya Ukristo kazi
English files
Swahili file
PDF file
Arabic file
African text
Christadelphian Bible Mission