Correspondance Course - Lesson 59

Swahili

Somo la 59:

MUHTASARI WA MAFUNDISHO YA BIBLIA

  1. Injili

Hii ni Habari Njema inayohusu Ufalme wa Mungu utakaoanzishwa hapa duniani, Yesu akirudi. Ni ujumbe unaopatikana katika Agano la Kale na Agano Jipya.

 

Mwanzo 22:17, 18

Mathayo 4:23

  1. Biblia ni Neno la Mungu

Waandishi wote 40 wa vitabu 66 vya Biblia waliandika waliyoandika kwa kuongozwa na Mungu.

 

Zaburi 68:11

2 Petro 1:21

  1. Mungu ndiye aliyeiumba dunia

Kila kitu katika dunia kiliumbwa na Mungu kwa manufaa ya wanadamu, kwa lengo la dunia kuweza kujazwa na Utukufu wake. Yesu Kristo ni kiini cha lengo hilo la Mungu.

 

Mwanzo 1:1

Hesabu 14:21

Zaburi 103:8-11

Isaya 45:18

  1. Yesu atarudi duniani

Yesu alikuja miaka 2000 iliyopita kuihubiri Injili na kutoa uhai wake akiwa kama “Mwana-kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu”. Kwa sasa yupo mbinguni, lakini atarudi na kuwa Mfalme wa dunia.

Mathayo 25:31-34

Matendo 1:10-11

Matendo 3:20, 21

Ufunuo 22:20

  1. Kurudi kwa Yesu kuko karibu sana

Unabii wa Biblia unaendelea kutimia na kuna ishara nyingi leo kuwa, kuja huko kwa Yesu kumekaribia sana. Mifano: Wayahudi na uwepo tena wa Taifa la Israeli; kuporomoka kwa maadili; ugaidi; njaa; magonjwa na matetemeko ya nchi.

 

Luka 21:10-11

Luka 21:24-33

2 Timotheo 3:1-5

  1. Ufalme wa Mungu utakuwa duniani

Huu ni ujumbe wa msingi katika Biblia. Ufalme tunaouombea katika ‘Sala ya Bwana’ utakuwa na makao makuu yake katika Yerusalemu, Israeli, ambapo Bwana Yesu atatawala kwa miaka 1000 juu ya mataifa yote kwa amani. Baada ya hapo hapatakuwa na dhambi na mauti tena duniani.

 

Yeremia 3:17

Mika 4:1-8

Ufunuo 11:15

  1. Mungu alitoa Ahadi kwa Ibrahimu

Kwa sababu ya utii wake wa kiimani, Ibrahimu alipewa ahadi na Mungu kuwa, yeye na familia yake wataimiliki nchi ya Kanaani (Israeli), na kwamba mmoja kati ya uzao wake (Yesu), atakuwa Mfalme wa dunia.

 

Mwanzo 12:1-3

Mwanzo 15:5-6

Mwanzo 22:15-18

Wagalatia 3:8,16,29

  1. Wayahudi ni Watu wa Mungu

Waliwekwa wawe mashahidi juu ya uwepo wa Mungu na uweza wake. Lakini hawakumtii, kwa hiyo walitawanywa duniani mwote. Biblia ilitabiria kuwa, katika ‘siku za mwisho’ watarudi tena katika nchi ya Israeli.

 

Isaya 11:11, 12

Isaya 44:8

Ezekieli 37:21-22

Warumi 9:3-5

  1. Yerusalemu itakuwa ni Makao Makuu ya dunia

Yesu alikuwa Myahudi. Wengi kati ya uzao wa Kiyahudi uliomsulubisha utamkubali kama Masihi (Mwokozi) wao. Yerusalemu utakuwa Makao Makuu ya Ufalme wa Mungu, na Israeli itakuwa ‘kichwa cha mataifa yote’. Wasafiri kutoka katika kila nchi watakuwa wakienda Yerusalemu kuabudu.

 

Yeremia 3:17

Mika 4:1-2

Zekaria 14:16

Mathayo 5: 34-35

  1. Mungu alimpa Daudi ahadi

Mfalme Daudi aliambiwa kuwa, angekuwa na mzao (mwana) ambaye angekaa katika Kiti chake cha Enzi milele. Huu ni unabii uliokuwa ukimhusu Yesu.

 

2 Samweli 7:12-16

Luka 1:30-33

  1. Yesu ni Mwana wa Mungu

Alizaliwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu na mama yake, Mariamu. Kwa namna hii alikuwa ni ‘Mwana wa Mungu’ na pia ‘mwanadamu’. Yesu alisema wakati wote kuwa, Baba yake (Mungu) alikuwa ni mkubwa kuliko yeye. Hakuna kitu katika Biblia kinachosemea kuwa Yesu alikuwa Mungu.

 

Mathayo 1:20-25

Yohana 14:28

Warumi 1:3-4

Wagalatia 4:4

  1. Yesu hakutenda dhambi

Ingawa alikuwa mwanadamu, Yesu alikuwa Mwana wa Mungu, na kwa hiyo aliweza kuyashinda majaribu yote na kuishi maisha makamilifu. Aliweka kielelezo kwa ajili ya wafuasi wake wote.

 

Isaya 53:5, 12

2 Wakorintho 5:21

1 Petro 2:22

  1. Yesu alikufa msalabani kwa ajili yetu

Ilikuwa ni lazima afe kama ilivyo kwa watu wote, kwa kuwa alikuwa uzao wa Adamu, kama sisi sote. Lakini kwa kuwa hakutenda dhambi, alikuwa dhabihu kamilifu (‘Mwana-kondoo wa Mungu’) katika kufa kwake. Kwa sababu hii ameweza kuzichukua dhambi za wale ‘wanaokufa naye’ kwa njia ya ubatizo.

 

Yohana 1:29

Yohana 3:16

Wagalatia 1:4

 

  1. Yesu alifufuliwa kutoka kaburini

Kwa kuwa hakufanya dhambi, kaburi halikuweza kumng’ang’ania. Mungu alikuwa sawa kumrudishia uzima mtu huyu mmoja pekee aliyekuwa wa haki. Kwa kufufuka, Bwana Yesu Kristo ni ‘limbuko’ la waliokufa (tunda la kwanza la waliokufa); ni uthibitisho wa kwamba wale walio katika Kristo, watafufuliwa kutoka kwa wafu, atakaporudi.

Matendo 2:24

Matendo 17:31

1 Wakor. 15:22-23

  1. Roho Mtakatifu ni uweza wa Mungu

Uweza wa Mungu unaonekana kwa yale yote aliyoumba. Mungu anapoitumia Roho yake kwa kusudi maalumu, uweza wake huo unaitwa ‘Roho Mtakatifu’. Roho Mtakatifu sio kitu kilicho nje ya Mungu; kilicho na uwezo wa kufanya kazi chenyewe; sio nafsi. Ni uweza wa Mungu ule ule. (Neno sahihi zaidi lingekuwa Roho Takatifu (Holy Spirit), na sio Roho Mtakatifu. Herufi ‘M’ inaleta kufikiri kama ni nafsi, kwa namna fulani (kwenye Kingereza utata huo haupo).

Isaya 61:1-3

Luka 1:35

Matendo 10:38

2 Petro 1:21

  1. Mshahara wa dhambi ni mauti

Kifo ni adhabu inayotupata wanadamu wote kwa sababu ya dhambi. Tangu Adamu amkiuke Mungu kwa kutomtii mwanzoni, watu wote wameangukia kwenye dhambi (tukimuondoa Yesu), na kwa hiyo wote tunakufa. Wanaume kwa wanawake, wote wataishia makaburini kama hawakulifahamu kusudi la Mungu na kuuitikia mwito wa Injili.

Mwanzo 3:17-19

Warumi: 5:12

Warumi 6:23

  1. Karama ya Mungu ni uzima wa milele

Uzima wa milele sio malipo; hakuna anayeweza kuustahili. Lakini Mungu, kwa upendo wake ameahidi kuwapatia huo wale wanaoliamini Neno lake, wanaoweka matumaini yao katika Bwana Yesu na kujitahidi kuyafanya mapenzi yake.

 

Yohana 17:1-3

Warumi 2:6-8

Warumi 5:1-5

Warumi 6:23

  1. Kutakuwa na ufufuo wa wafu

Lakini sio kila mtu atafufuliwa. Yesu atawatoa makaburini wale tu waliopata fursa ya kuweza kuuitikia ujumbe wa Injili kwa ajili ya wokovu wao.

 

Yohana 5:28-29

1 Wakorintho 15:12-19

2 Timotheo 4:1

  1. Kutakuwa na hukumu

Wale wote waliouelewa wito wa Injili, ni lazima watasimama mbele ya Mfalme atakaporudi duniani, ama kuadhibiwa kwa mauti ya pili (na ya mwisho), ama kukirimiwa uzima usio na mwisho. Kutakuwa pia na hukumu kali kwa watu wa dunia watakaompinga Yesu katika kurudi kwake.

Danieli 12:1-2

Yohana 5:28-29

2 Wakorintho 5:10

2 Wathesalonike 1:7-9

  1. Uzima wa milele

Wale watakaopatiwa uzima wa daima watapata fursa ya maana sana ya kumtumikia Bwana Yesu duniani, na chini yake watawatawala watu wengine (watu wa dunia ambao hawajapata uzima huo; watu wanaokufa). Watu hao hatimaye watakufa na kufufuliwa tena kwa hukumu mwishoni mwa miaka 1000 ya Ufalme wa Mungu. Watakatifu (wale waliopewa uzima wa milele) wataifurahia afya bora kabisa na kila kitu, wakati wakiihubiri ‘Injili ya milele’ na kuifanya dunia kuwa mahali pazuri kabisa pa kuishi kwa kila mtu.

Zaburi 37:9-11,22

Danieli 7:27

Ufunuo 20:4-7

  1. Malaika ni Watumishi wa Mungu

Mungu aliumba malaika wawe watumishi wake anaowatuma milele. Hawafi na wanatekeleza maagizo ya Mungu kama yalivyo, katika ulimwengu wote. Wanawachunga pia wale katika dunia walioitwa na Mungu kuwa ‘watakatifu’ wake.

Kutoka 23:20-21

Zaburi 103:20

Waebrania 1:13, 14

  1. Ibilisi na Shetani

Katika Biblia ‘ibilisi’ ni neno lililotumiwa kuelezea nguvu ya dhambi iliyopo ndani ya watu wote. Wote wanaoyapinga mapenzi ya Mungu mara nyingine wanaitwa ‘shetani’. Hakuna kitu katika Biblia kinachohusu uwepo wa malaika mwovu au mungu wa namna fulani nje ya mtu, anayemfanya mtu akosee.

Mathayo 16:23

Yohana 8:44

Matendo 10:38

Yakobo 1:14

  1. Sisi sote tunapaswa kutubu

Mungu anatutaka tuzitambue dhambi zetu, tuzijutie, na tujitahidi kuishi maisha ya kuikataa dhambi. Hatuwezi kuwa na tumaini la wokovu mpaka tuwe tumefanya hili. Maisha ya toba ni maisha mapya ya kumfuata Yesu; maisha ya kupingana na dhambi.

Zaburi 51:1-10

Mathayo 4:1-7

Luka 13:1-5

Matendo 3:19

  1. Ubatizo wa mtu mzima kwenye maji

Huu ni wa muhimu sana, lakini ni lazima tuelewe na kuyaamini mafundisho ya Biblia na amri za Yesu Kristo kabla hatujaweza kubatizwa. Ubatizo ni ishara ya kufa pamoja na Kristo kwa ajili ya dhambi zetu, na kufufuka tena kwa ajili ya maisha mapya.

Mathayo 28:19-20

Marko 16:16

Matendo 2:38

  1. Wakristo hawapambani

Mfuasi wa Kristo hawezi kutumia nguvu au kujiunga na huduma za kijeshi au za kipolisi. Ni sharti awapende maadui zake kama anavyowapenda rafiki zake.

Mathayo 26:52

Luka 6:27-29

Luka 22:25

Warumi 13:1-2

  1. Ndoa ya Kikristo

Biblia iko wazi kabisa kuwa, Mungu alimkusudia mwanamume awe na mke mmoja, na kwa pamoja wailee familia yao katika njia za Mungu. Kwa sababu hii, Mkristo hapaswi kutengana na mwenza wake.

 

Mwanzo 2:21-24

Mathayo 19:3-6

Waebrania 13:4

  1. Wajibu wetu kwa Taifa

Wakristo wanazitii sheria zote za nchi zao, mpaka zinapokuwa zikipingana na amri za Mungu. Kwa kuwa wao ni raia wa Ufalme wa Mungu, hawawezi kuutoa muda wao na nguvu zao kwa siasa za serikali yoyote ya kidunia. Tunaweza kujikuta tukipingana na Mungu, kama tukifanya hivyo.

Mathayo 22:21

Warumi 13:1-7

1 Petro 2:17

  1. Wakristo wanaweza kuomba msamaha wa dhambi zao

Hii ni fursa ya kipekee ya kuwa katika Kristo (yaani, ya kuwa umebatizwa). Bwana Yesu yuko mbinguni, akiwa mpatanishi kati ya wafuasi wake na Mungu; akimwomba Mungu asamehe udhaifu wao.

Wafilipi 4:6

1 Timotheo 2:5

Waebrania 7:24-26

1 Yohana 1:9

  1. Kusoma Biblia kila siku ni muhimu

Kusoma Biblia ni kama kula; ni kitu cha kila siku. Mwenyezi Mungu anasema nasi kupitia katika Neno lake. Tunajifunza kutoka katika mifano ya Kimaandiko, ambapo kuna vifungu na mistari inayotufaa kwa matatizo yetu na mahitaji yetu.

Zaburi 119:89-112

Matendo 17:11-12

2 Timotheo 3:16-17

  1. Ushirika na kifo cha Yesu

Wakristo-wa-kweli wanakikumbuka kifo cha Bwana Yesu kwa ‘kumega mkate’ na ‘kunywa divai’ kila juma, kama Yesu alivyoagiza katika chakula kile kwenye chumba cha juu. Kumbukumbu hii ina ahadi kwa wafuasi wake, ya kula pamoja naye katika Ufalme wa Mungu.

Marko 14:22-25

Luka 22:14-20

1 Wakorintho 11:23

  1. Ushirika wa Kweli

Hiki ni kitu kinachowaleta pamoja wale tu walioamini, wanaotaka kuyafanyia kazi mambo ya kweli waliyojifunza kwenye Biblia, yaliyofundishwa na Bwana Yesu na wanafunzi wake, katika karne ya kwanza. Wakristadelfia wanao ushirika wa hali hii na maelefu ya ndugu zao waliopo katika nchi nyingi duniani.

Yohana 17:16-18

Matendo 2:41-42

Waebrania 10:24-25

  1. Wito wa Injili

Mungu anawaita watu kutoka katika mataifa yote wamfuate Yesu na kujiandaa kwa ajili ya Ufalme wake unaokuja.

Mathayo 16:24-26

1 Wakorintho 1:26-27

Wagalatia 3:27

Matendo 15:14

Je, utaupokea wito huu?

Mstari wa mwisho wa kujifunza: Matendo 17:30-31

“Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana, ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu”.

 

Swahili Title
Muhtasari wa mafundisho ya Biblia
English files
Swahili file
PDF file
African text
Christadelphian Bible Mission