155. BALAAMU
“Usiwalaani watu hawa; kwa maana wamebarikiwa.”
Somo la mwisho liliwaacha Wana wa Israeli wakihangaika kutoka kusini kuelekea nchi ya ahadi. Walipokuwa wakisafiri kuelekea kaskazini, nchi ilibadilika na suala la kwenda likawa rahisi. Wakipanda upande wa mashariki mwa Moabu, Mungu aliwapa ushindi mkubwa juu ya majeshi ya Wafalme wa Waamori, Sihoni na Ogu (tazama ramani). Kisha wakakaa katika tambarare za Moabu zinazoelekea ukingo wa mashariki mwa Yordani (Hesabu 22:1). Tunaposoma jinsi Balaki alivyoitikia uwepo wa Israeli tunafundishwa kwamba, mipango ya Mungu haiwezi kuzuiwa. Somo hili linaonyesha jinsi Mungu alivyogeuza laana za maadui wa Israeli kuwa baraka.
Hesabu 22-25
BALAKI ANAMWITA BALAAMU.
Balaki mfalme wa Moabu aliwaogopa Waisraeli na akatuma watu waende kumwita nabii Balaamu huko Mesopotamia. Kwa ujinga wake, alitumaini kwamba Balaamu angeweza kuweka laana juu ya Waisraeli ambayo ingewaangamiza (ms. 5-6). Lakini, Balaamu alionywa na Mungu asiende pamoja na wajumbe wa Balaki (ms. 12) na kwa hiyo, Balaki akatuma baadhi ya watu wake wakuu kwa Balaamu na ahadi za utajiri mwingi (ms. 15-17). Mwanzoni Balaamu alikataa na hatimaye akaambiwa na Mungu kwamba, kama watu hao wangemwita tena, yeye aende lakini angesema tu yale ambayo Mungu alimwambia (ms. 20). Balaamu alikuwa na shauku sana ya kufuata thawabu iliyotolewa na Balaki, hivyo ni dhahiri kwamba hakungoja watu wamwite bali alitandika punda wake na kwenda mwenyewe (ms. 21 - linganisha Yuda 11; 2 Petro 3:15-16).
MALAIKA ANAMPINGA BALAAMU.
Shauku ya Balaamu ya kwenda ilimkasirisha Yahwe ambaye alimtuma malaika kuzuia njia yake (Hesabu 22:22). Ijapokuwa hakuonekana kwa Balaamu, punda huyo aliweza kumwona malaika na kugeuka kando kwenda shambani (mst. 23). Balaamu alimkasirikia punda wake na kumpiga. Malaika akatokea tena mbele ya punda huyo na kumfanya anyemelee upande mmoja na kuuponda mguu wa Balaamu ukutani. Balaamu alikasirika na yule mnyama alipoanguka chini yake mara ya tatu akampiga sana. Ndipo Mungu akafungua kinywa cha yule punda na kusema na Balaamu. Fikiria mshangao wake kusikia punda wake akizungumza. Licha ya upuuzi huo wa kuongea na mnyama alijibu na kutishia kumuua kwa tabia yake.
Kisha Mungu akafungua macho ya Balaamu na akamwona malaika aliyesimama njiani. Balaamu aliogopa sana na angerudi nyumbani kwake lakini malaika akamwambia aende kwa Balaki, lakini akamwambia kwamba ni lazima aseme maneno ambayo Mungu angempa.
Inafurahisha kuona katika sura hii kwamba, neno la Kiebrania “shetani” limetumika mara mbili na kutafsiriwa kwa usahihi kama “kumpinga” (mst. 22) na “kukupinga” (mst. 32). Mkanganyiko mkubwa umezuka kwa sababu sehemu fulani neno “shetani” limehamishiwa katika lugha ya Kiswahili ili kutoa dhana potofu kwamba kuna malaika aliyeanguka mbaya zaidi kuliko wanadamu kwa ujumla anayeshawishi wanadamu kutenda dhambi. Katika hali zote ambapo neno hili linapatikana lina maana ya “mpingaji” (iwe nzuri au mbaya).
LAANA ILIGEUKA KUWA BARAKA.
Balaki alimchukua Balaamu hadi kwenye mlima mrefu ambapo angeweza kutazama chini kwenye kambi ya Israeli. Lingekuwa jambo la kuvutia kuona safu ndefu za mahema zenye mpangilio zilizopangwa katika makabila na Hema la kukutania katikati yao. Baada ya kutoa dhabihu, Balaki na Balaamu walijitayarisha kuwalaani Israeli. Lakini Mungu alimtokea Balaamu na kumwambia cha kusema (Hesabu 23:4-5). Kwa hiyo, Balaamu alilazimika kumwambia Balaki kwamba, watu wa Israeli walikuwa wamekusudiwa kuwa taifa kubwa duniani (mst. 7-10). Balaki alishtuka na kumpeleka Balaamu mahali pengine pa juu ambapo utaratibu uleule wa kutoa dhabihu ulirudiwa na Balaamu akaanza tena kulaani Israeli.
Tena Balaamu alipewa ujumbe na malaika na kwa mara ya pili laana aliyokusudia ikageuzwa kuwa baraka (ms. 18-24). Balaki alikasirika na kumpeleka Balaamu kwenye sehemu mbili zaidi za kutazama ili tu kusikia baraka zaidi juu ya watu (sura 24:3-9; 15-24). Tunaweza kuona jinsi uvuvio wa roho wa Mungu ulivyokuwa na nguvu, ingawa Balaamu alitaka kuwalaani Israeli na kupokea thawabu, aliweza tu kusema kile ambacho Mungu aliruhusu (cf. 2 Petro 1:20-21).
BALAAMU ANAWASABABISHIA SHIDA WAISRAELI.
Ingawa hakuweza kutamka laana juu ya Israeli, Balaamu alitaka kuleta anguko lao kwa njia nyingine. Nia yake ilikuwa kujipatia thawabu ya Balaki, kwa kuwa alikuwa mtu mwenye pupa. Shauri la Balaamu kwa Wamoabu lilikuwa kufanya urafiki na Israeli na kuwatia moyo wajiunge na ibada ya miungu ya Wamoabu. Ndipo Yahwe, Mungu wa Israeli, akawakasirikia watu wake na kuwaangamiza. Ushauri huu ulifuatwa na kuwafanya wengi katika Israeli kugeukia njia mbaya za Wamoabu. Waliabudu sanamu na kufanya uasherati na wanawake wa Moabu, hata Mungu akatuma tauni kati ya watu hadi wakavunja urafiki wao na Moabu (cf. Hesabu 31:16 pamoja na Ufunuo 2:14 na Yuda 11). Ni muhimu kwa Ndugu katika Kristo kujitenga na mazoea mabaya ya ulimwengu. Ndivyo ilivyo hasa katika mawasiliano yetu na vijana ambao shinikizo lao la kwenda pamoja nao kwenye anasa za kiulimwengu lingeharibu imani na upendo wetu kwa Mungu.
Ilikuwa ni msiba ulioje kwa wale wanaokaribia nchi kuuawa wakiwakaribu mwisho wa kutangatanga nyikani. Hata hivyo, katika hilo kuna onyo lililo wazi kwetu. Tunaukaribia Ufalme wa Mungu kwa kasi. Katika siku hizi za mwisho za maandalizi yetu kwa ajili ya Ufalme tusijaribiwe na watu wa kidunia kutenda dhambi na kuangamia, wakati ujio wa Kristo umekaribia sana.
BALAAMU AUAWA.
Siyo tu kwamba ushauri wa Balaamu ulishindwa kuwaangamiza Israeli, bali hasira ya Mungu iliwaka dhidi ya Wafalme wa Midiani ambao walikuwa wamemlinda Balaamu na kumsaidia Balaki. Kwa hiyo, jeshi la askari wa Israeli lilitumwa dhidi ya Wamidiani. Nguvu za Midiani zilivunjwa na Balaamu akauawa (Hesabu 31:1-12).
SOMO KWETU:
Mungu ameahidi kuwalinda wale wanaomtii na kutembea katika njia zake (Zaburi 34:7). Hata hivyo, tunapokengeuka na kufuata njia mbaya za watu wanaompuuza Mungu, ataruhusu matokeo mabaya yatakayofuata. Ni lazima tuwe macho kila wakati ili kuona kwamba hatukiuki sheria zozote za Mungu katika tamaa yetu ya kuwa na urafiki na watu wengine (Yakobo 4:4).
Wala hatupaswi kudumishaa mazoea ya pupa ili tuwe tayari kumpa Mungu kisogo na njia zake kwa ajili ya kupata faida za kimwili.
MAKTABA YA MAREJEO:
“Hadithi ya Biblia” (H. P. Mansfield)—Kitabu. 2, Nambari 8
“Mkono wa Mungu Uonekanao” (R. Roberts)—Sura ya 19
MASWALI YA AYA:
- Kwa nini Balaamu alitaka kwenda na wakuu wa Moabu?
- Eleza jinsi Balaamu alivyojifunza kwamba Mungu alimkasirikia kwa ajili ya kwenda kwa Balaki.
- Nia ya Balaki ya kuwalaani Israeli ilishindwaje?
-
- Balaamu alifaulu vipi kuleta anguko la Israeli?
- Kuna ubaya gani kuwa na urafiki na ulimwengu?
SWALI LA INSHA:
- Onyesha jinsi Balaamu alivyozuiwa awali asiwalaani Israeli lakini hatimaye aliwafanya Israeli watende dhambi?
- Ni masomo gani tunajifunza kutoka kwa hadithi ya Balaamu
- Manabii wa uwongo - yaani watu wanaotumia Neno la Mungu kwa faida yao wenyewe, na
- Kuwa na urafiki na watu wa kidunia? Onyesha jinsi ilivyo muhimu kujitenga na mazoea ya kiulimwengu tunapojitayarisha kwa ajili ya kuja kwa Kristo.