194. MAELEZO YA DANIELI KUHUSU HISTORIA YA YA UTAWALA WA ULIMWENGU
"Mungu amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa katika, SIKU ZA MWISHO"
Ukweli ni kwamba Mungu ndiye anayemiliki falme za wanadamu unadhihirishwa katika sura hii. Nguvu za watu wa Mataifa zinahukumiwa na kuonekana kuwa chini ya mapenzi ya Mungu. Na utukufu wa mwanadamu unaonekana kuwa kivuli kinachotoweka. Ingawa Nebukadreza alijifikiria yeye mwenyewe kuwa alikuwa na uwezo wa kuamua hatima yake, anapewa ufahamu wa kutambua yeye siyo kiti isipokuwa ni chombo katika mkono wa BWANA. Ndilo la kwanza katika matukio matatu yanayomthibitisha BWANA, kuwa mwenye hekima yote (Danieli 2:47), mwenye nguvu zote (Danieli 3:28-29) na mwenye mamlaka yote (Danieli 4:37).
MTIHANI ALIOPEWA MFALME - Danieli 2:1-9
Mungu, kwa njia ya ndoto (upitia), alimfunulia Nebukadreza "mambo yatakayokuwa siku za mwisho" (mstari 28) ndoto hiyo ilmwacha mfalme katika hali ya kufadhaika. Alisisimka na kuchanganyikiwa na akawaita watu wake wenye hekima, wanajimu na wachawi ili wamsaidie. Siuyo tu kwamba alitaka wamwambie maana ya ndoto ile, bali pia hata wamjulishe ile ndoto yenyewe. Wale waliojiweka kuwa wenye hekima waliwekwa katika kuchanganyikiwa na walimwomba mfalme ili awajulishe ile ndoto. Lakini Mfalme alisisitiza kuwa "Najua hakika kuwa mnataka kupata nafasi, kwa kuwa mmeona kuwa lile neno lenyewe limeniondoka" (mstari 8). Ndipo mfalme alipowatishia kuwa atawaua iwapo wangeshindwa kumjulisha ndoto ile na maana yake. Kwa kukata tamaa ndipo wale watu wenye hekima wakambembeleza mfalme wakisema; “Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo." (mstari 10).
AMRI YA KUWAANGAMIZA WENYE HEKIMA YATANGAZWA - Danieli 2:10-16
Mwitikio wenye hekima kwa ombi la mfalme lilimghadhabisha zaidi naye akaamrisha mara moja kuwa watu wote wenye hekima wauawe. Tangazo hili lilimhusu Danieli pia, ingawa yeye na rafiki zake watatu, walikuwa bado hawajahitimu mafunzo yao ya miaka mitatu, hata hivyo walikuwa wakihesabiwa katika kundi la watu wenye hekima (linganisha Danieli 1:5 na Danieli 2:1). Ingawa amri ilipotangazwa hawakuwepo, walishangazwa sana walipomwona Arioko, akida wa walinzi wa mfalme au "mkuu wa wauaji" (mstari 14 pembezoni). Uhakikisho wa Danieli kuwa angeisema ndoto ile, ulimshawishi mfalme kuruhusu muda wa nyongeza, ingawa ombi lililokuwa limetangulia kutoka kwa Wakaldayo, viongozi wa dini Babeli lilikuwa limekataliwa (mstari 8).
NGUVU YA MAOMBI -Danieli 2:17-23
Danieli na wenzake wakalifanya hili hitaji kuwa ni jambo la wote kuomba kwa pamoja (mstari 17). Na kama BWANA alivyokuwa amewabariki kuweza kuwa na msimamo wao dhidi ya unajisi (Danieli 1:8-17), vivyo hivyo waliamini kwamba Mungu angeweza kufunua "Mungu hataacha kuwafunulia watumishi wake manabii siri" (Amosi 3:7). Tunaweza kuwa na ujasiri wa namna hiyohiyo kwa kuwa Mungu ameahidi kusikia maombi (Mathayo 7:7), na kuwapa hekima wamchao (Zaburi 25:14; Yakobo 1:5). Waliomba, ili kwamba "wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli" (mstari 18), na katika kufanya hivyo walifanya kwa utaratibu sawasa na Ibrahimu, aliyemwombea Lutu "hasha, isiwe hivyo ukamwua mwenye haki pamoja na mwovu;mhukumu wa ulimwengu wote asitende haki?" (Mwanzo 18:25). Kwa mara nyingine tena kupitia ndoto (mstari 19).
Mungu alimfunulia Danieli ile ndoto ya mfalme na tafsiri yake. Mara moja Danieli aliitikia kwa njia ya kushukuru na kwa kumsifu Mungu, siyo kwa sababu uhai wake usingekuwa katika hatari, bali kulitukuza jina la ajabu la BWANA, kwa kuwa ni mwenye hekima na mwenye nguvu katika kutawala hatima ya falme za Wanadamu. Danieli alijisikia katika vilindi virefu vya shukrani kwa kujulishwa siri ya Mungu. Mungu alijifunua yeye mwenyewe kama alivyowahi kutenda kwa mababa siku za kale. Danieli akamwita, "Mungu wa baba zangu" na kumshukuru yeye. Na sisi vilevile tuwe wenye kuthamini maandiko na nguvu ya maombi katika maisha yetu.
DANIELI MBELE YA MFALME - Danieli 2:24-31
Kwa haraka Danieli aliletwa mbele ya mfalme, lakini kabla ya kuieleza ndoto ile na maana yake, Danieli alikuwa mwangalifu kwa kumfahamisha Nebukadreza kuhusu ukweli kuwa "yuko Mungu mbinguni afunuaye siri" na kwamba alikuwa ni Mungu huyu aliyemjulisha yey ndoto hiyo na maana yake (mstari 28). Ndipo sasa Danieli kwa uhakika akaeleza ndoto hiyo jinsi alivyokuwa tofauti ukilinganisha na washauri wa mfalme ambao walikuwa wamekosa ufahamu.
NDOTO YENYEWE - Danieli 2:21-35
Danieli aliielezea jinsi sanamu yenyewe ilivyokuwa ikionekana kuwa ilikuwa kubwa sana na yenye mwangaza mwingi sana ikiwa na umbo la kutisha. Ilikuwa umeundwa kwa madini ya aina mbalimbali - kichwa kilikuwa cha dhahabu, kifua na mikono ilikuwa fedha, tumbo na mapaja ilikuwa shaba, miguu ilikuwa chuma na nyayo zake ilikuwa nusu chuma na nusu udongo. Na jiwe lililochongwa, "bila kazi ya mikono" maana yake bila ya kazi ya mikono ya mwanadamu, likaipiga sanamu miguu yake ikasababisha sanamuianguke. Madini yakavunjika na kuwa vumbi na jiwe lile ambalo liliipiga sanamu likaongezeka kuwa mlima mkubwa likaijaza dunia yote.
TAFSIRI YA NDOTO - Danieli 2:36-45
1. KICHWA CHA DHAHABU - DOLA YA BABELI.
Ingawa Nebukadreza kwa upuuzi alifikiri kuwa kwa uwezo wake mwenyewe ndiye aliyehusika na nguvu yake, Danieli alimfunulia kwamba "Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu" (mstari 37, 41). Mungu alikuwa amempatia Nebukadreza, ufalme juu ya mataifa yote (mstari 38; Yeremia 27: 4-5) na kwa kuwa aliwakilisha ule mji wa dhahabu (Isaya 13:19, 14:4) ilikuwa ni sahihi yeye kutajwa kuwa ndiye "kile kichwa cha dhahabu".
2. KIFUA NA MIKONO YA FEDHA - DOLA YA UAJEMI.
Ufalme wa Babeli ulitekwa na Dario, pamoja na Koreshi, Mwajemi, katika mwaka 539 (K.K), Majeshi ya Dario yalielekeza maji ya mto frati sehemu nyingine na majeshi ya Dario yakaingia kwa kupitia ukingo wa mto na Babeli ikatekwa (sura 5, Isaya 45:1-3). Kwa hiyo dola ya Babeli ikaangushwa na "kifua na mikono ya fedha" ukasimama badala yake ufalme duni zaidi wa Wamedi na Waajemi. Utawala wake ulikuwa dhaifu zaidi ukilinganisha na ufalme wa Babeli lakini ulidumu yapata kama miaka 200. Hii ilikuwa kwa sababu ya baraka ya Isreali na mwasisi wake, Koreshi (Ezra 1:1-4; 2 Mambo ya Nyakati 36: 22-23).
3. TUMBO NA MAPAJA YA SHABA - DOLA YA WAYUNANI
Ufalme wa Wamedsi na Waajemi kwa zamu yake ulifuatiwa na "ufalme mwingine wa shaba, ambao uliitawala dunia yote" (mstari 39). "Tumbo na mapaja" yanajibu kuwa ni dola ya Wayunani, katika mapigano mawili ya vita vya maamuzi makubwa, ya Graniko na Issu katika mwaka wa 334, na 333 K.K. Alexanda Mkuu wa Uyunani alipindua nguvu ya Uajemi na upesi akaeneza utawala wake. Na baada ya kifo cha ghafla cha Alexanda, maafisa wanne wa jeshi lake wakagawana dola yake.
4. MIGUU YA CHUMA - DOLA YA RUMI
Pole pole Rumi iliongezeka kukua kuwa "utawala na nguvu mfano wa chuma, kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote; ndivyo utakavyo vunja vunja na kuseta" (mstari 40). Majeshi ya Rumi yaliitawala Ulaya, Uingereza, Hispania, na nchi za Mesopotamia kwa kutumia chini ya kisigino chake (Uajemi, Umedi, Uyunani na Babeli). Katika mwaka 70 B.K, Yerusalemu "wakaanguka kwa makali ya upanga" (Luka 21:24; Kumbu kumbu la Torati 28:48-57). Lakini faida moja ya matokeo ya dola Rumi ilikuwa ni ujenzi wa barabara katika Asia na Ulaya ambazo ziliwezesha kuenezwa kwa Injili kwa Jina la Kristo aliyefufuka. Na kisha ulimwengu ule uliojulikana uliweza kupinduliwa "ulimwengu ulipinduliwa" kwa nguvu za ujumbe huu (Matendo ya Mitume 17:6), ukiacha alama juu ya wanadamu iliyo na nguvu kuliko nguvu ya dola ya Rumi. Ni jambo la kushangaza kwamba hapakutokea dola ya dunia iliyoishinda Rumi, Dola ilisambaratika; iligawanyika katika mataifa - madogo 10.
Mataifa haya 10 yakawa ndiyo mwanzo (msingi) wa mataifa ya Ulaya ya leo ambayo yanawakilishwa na vidole kumi vya nyayo za sanamu ile. Zile nyayo zilikuwa nusu chuma na nusu udongo, ikionyesha kuwa mataifa mengine yangekuwa na nguvu na mengine yangekuwa dhaifu. Kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo, "au kushikamana" (mstari 43), wala hali ya kugawanyika kwa Ulaya pamoja hisia kali za kitaifa kati za nchi za Ulaya hairuhusu muungano kamili wa serikali.
5. JIWE LILE DOGO - UFALME WA MUNGU
Nebukadreza alikuwa ameona katika ndoto yake ile sanamu ikisimama kwa nguvu zake zote na ikiwa na mwangaza mwingi sana, na sanamu hiyo ikavunjwa vipande vipande na jiwe lile dogo, Danieli alisema hayo yangetokea "siku za mwisho" (mstari 28). Katika siku za mwisho mataifa yote yanawakilishwa na madini ya thamani mbalimbali yangeungamanishwa katika "taifa moja lenye nguvu chini ya utawala wa mabavu, kwa jina unaitwa Urusi. Mamlaka hii itapata nguvu kutoka katika majimbo ambayo hapo mwanzo yaliitwa katika utawala wa Babeli, Umedi, Ugiriki, Uyunani, na Dola ya Rumi. Muungano huu wa nguvu nyingi wa mataifa chini ya utawala wa Urusi, utasababisha hofu kubwa katika mioyo ya watu wote ambao wangepinga nguvu yake”. Unabii mwingi kama unavyofafanuliwa katika Ezekieli 38, Daniele 11, Yoeli 3, Zakaria 14, na Danieli 2, hutuonyesha sisi waziwazi kwamba ni kusudi lake Mungu kuuangusha ufalme huu wa wanadamu kwa kuuangamiza utawala huu ambao ni muungano wa Warusi. Huu muungano mkubwa utaonekana kuitawala dunia, usioweza kutekwa. Lakini pamoja na kuwa nguvu zake simba, ukali wake kama dubu, wepesi kama wa chui, na uchu wake usio na utashi kuitamalaki dunia, itayumba na kuanguka mkononi mwa jiwe lile dogo. Itafikia mwisho wake utaangushwa "bila kazi ya mikono ya wanadamu" (Danieli 8:25 Biblia ya Union Version). Ninani huyu ambaye ni nguvu za jiwe? Hakuna mwingine isipokuwa ni Bwana Yesu Kristo (Mathayo 21:42-44). Angalia kwa makini Danieli 2: 44 ambapo tafsiri imetolewa.
Katika ndoto ya mfalme huenda ilionekana katika akili ya Nebukadreza kwamba haiwezekani jiwe dogo liweze kuharibu sanamu kubwa kama ile.
Hata siku ya leo watu hawatambui uweza mkuu wa Mungu, na kwamba ataleta mabadiliko katika siku chache zijazo. Na kwa hiyo itakuwa ya kwamba "Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme amabo hautaangamizwa milele... nao utasimama milele na milele" (mstari 44).
Kwa keli tunaweza kutazamia wakati ambao ufalme wa Mungu utaanzishwa katika dunia hii na mataifa yote watakwenda Yerusalemu kumwabudu Kristo akiwa ndiye mfalme, "ndoto hii ni ya hakika na tafsiri yake ni thabiti" (mstari 45).
FUNDISHO KWETU
Kama Danieli alivyohitimisha, "ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti" (mstari 45). Na sisi tukubaliane na Nebukadreza kwamba, kama ukweli ulivyo, kwamba Mungu wetu ndiye Mungu wa miungu na BWANA wa mabwana na Mfalme wa wafalme, na mwenye kufumbua siri (mstari 47). Danieli sura 2 ni mfano kamili wa Mungu wa kutupatia sisi ufunguo wa kuelewa kusudi la Mungu. Tunaishi katika siku za mwisho kumalizia siku za nyakati za mataifa, wakati ambao matukio ya sasa ya taonyesha waziwazi uthibitisho wa usahihi wa neno la unabii. Historia na karne ya ishirini zinatuthibishia sisi ya kuwa "Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu" (Danieli 4:17), ikituhakikishia sisi kuwa karibu ataufikisha mwisho wa nyakati za Mataifa pamoja na ujilio wa utukufu wa Mwana wa Mungu. Ushiriki wetu katika kueneza ufalme wa Mungu sehemu nyingine ni kwa njia ya kualikwa. Hebu na sisi sasa tujiandae kwa bidii kwa ajili ya wakati ambapo "Na ufalme na mamlaka na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii" (Danieli 7:27).
MAKTABA REJEA:
Historia ya Biblia (H.P.Mansfield) - Kitabu cha 6, Namba 10, Ukurasa 148-154
"Ufafanuzi wa unabii wa Danieli" (J.Thomas) - Sehemu ya 1-2.
"Elpis Israel" (J.Thomas) - Sehemu ya tatu, Sura ya 1.
"Danieli" (M.Stewart)
MASALI YA VIFUNGU:
1. Fafanua ndoto ya Nebukadreza?
2. Kwa kifupi ainisha maana ya ndoto ya Nebukadreza?
3. Je, ni nani ambaye ni "jiwe" katika ndoto na kazi yake ni ipi?
MASWALI YA INSHA
1. Fafanua kwa ufasaha ndoto ya Nebukadreza, jinsi ilivyotafsiriwa na ina maana gani.
2. Je, ni nani ambaye ni "jiwe" katika ndoto na kazi yake ni ipi, na ni lini mambo haya yatakapotimia?