CSSA 3-3-305 - THE TEMPLE OF SOLOMON

Swahili

305. HEKALU YA SULEMANI

" Nyumba ambayo ninajenga ni kubwa; kwani Mungu wetu ni mkuu wa miungu yote”

Daudi, Mfalme mashuhuri wa Israeli alitamani kujenga hekalu kwa jina la Bwana. Hili halikukubaliwa na Bwana na nafasi hii ilitunukiwa mwanawe Sulemani ambaye ufalme wake ulijulikana kwa amani, kujenga nyumba hii tukufu ambayo ilidumu kwa miaka 350 mpaka ilipoharibiwa na Nebukadreza.

Lengo letu katika somo hili ni kuona ukuu wa Hekalu na kujifunza masoma ya kiroho katika kujengwa kwake na sherehe yake ya ufunguzi.

1 Wafalme 5-8; 2 Mambo ya Nyakati 2-7

SULEMANI ANATAYARISHA VIFAA VYA UJENZI (1 Wafalme 5; 2 Mambo ya Nyakati 2).

Baada ya amani kuimarishwa katika ufalme, Sulemani  alianza kujitayarisha kwa kazi ya ujenzi wa Hekalu. Alipata msaada kwa kuwa  vifaa ambavyo vingetumika katika ujenzi wa Hekalu vilikuwa vimekusanywa na Daudi hapo awali (Taz.1 Nya. 22:14-16). Daudi alikuwa pia amewajibika katika baraka nyingine ambayo ilimsaidia Sulemani katika ujenzi wa Hekalu. Tunajifunza kutoka 1 Wafalme 5: 1 kwamba Hiramu Mfalme wa Tiro alikuwa “anampenda Daudi sana” na alifurahi wakati Sulemani aliomba mierezi kutoka Lebanoni. Mkataba wa Amani ulifanyika dhidi ya Hiramu na Sulemani na utoaji wa mbao ukahakikishwa. Sulemani alikuwa atafute wafanyikazi na takriban wafanyikazi 30,000 walipangwa kwa shughuli hii. Ili kuhakikisha kwamba watu hawa wangefurahishwa na kazi yao Sulemani aliwagawanya kwa vikundi vya watu 10,000 kufanya kazi kwa mwezi mmoja Lebanoni na kisha miezi miwili wangekaa nyumbani kabla ya zamu yao tena (1 Fal. 5: 13-14).

Kando na wanaume hawa 30,000 kulikuwa na wa wafanyikazi 70,000 zaidi ambao walihusika na shughuli tofauti na wengine 80,000 ambao walihusika na kazi ya kuchonga mawe kutoka milima iliokuwa karibu na Yerusalemu. Wafanyi kazi hawa  150,000 walitoka kwa wageni waliokuwa wakiishi kwenye taifa hili; na hivyo pamoja na wafanyikazi wa Tiro, na watu wengine wengi wa mataifa walihusika katika ujenzi wa  Hekalu la Mungu wa Israeli (Liganisha 2 Nya. 2:17).

Waangalizi 3,300 walikuwa maofisa wa Sulemani mwenyewe (1 Fal. 5:16). Hivyo jumla ya watu 183,300 walikuwa wameajiriwa katika kazi za ujenzi wa nyumba kwa utukufu wa Jina ya Bwana.
 

UJENZI WA HEKALU (1 Wafalme 6: 7; 2 Mambo ya Nyakati 3: 4).

 Sehemu iliochanguliwa kujengwa Hekalu ilikuwa Mlima Moria pahali ambapo Mungu alikuwa amemtokea Daudi. Ujenzi ulianza katika mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa Sulemani na ulikamilika katika mwaka wa 11 mwezi wa nane. Hivyo miaka saba na nusu ilitumika katika ujenzi. Hekalu haikuwa kubwa ikilinganishwa na majengo ya mataifa yaliozunguka Israeli, lakini utumizi wa dhahabu ambayo ilitumika kupamba upande wa ndani wa hema; na wingi wa hazina ambazo ziliwekwa, ziliipa Hekalu utukufu mkuu.

Kama Saduku la Agano hapo awali, muundo wa Hekalu, samani zake, na huduma za kikuhani zilikuwa mfano wa kazi ya ukombozi ya Yesu Kristo, Mwana wa Daudi, ambaye alikuwa mkuu zaidi kuliko Sulemani. Mpangilio wa hekalu ulikuwa  sawa na ule wa Hema, lakini kubwa zaidi na mapambo ya dhamani zaidi.

Jengo hili lilihusisha ukumbi wa mbele wenye mita 10, upana wa mita 5, Mahali Patakatifu palikuwa mita 10 upana, mita 20 urefu na Mahali Patakatifu Zaidi palikuwa na mita 10 mraba kamili (tazama michoro, kurasa 31, 32).

Upande wa Nje wa Hekalu:

  1. Madhabahu ya shaba, ambapo sadaka zilitolewa;
  2. Bahari ya kuyeyushwa ilioshikiliwa na ngombe kumi na wawili, ilitumika kuosha makuhani
  3. Birika kumi za shaba, ambazo zilitumika kuosha sadaka.


Wanafunzi wanapaswa kuwa na ufahamu wa kiroho wa vitu hivi katika masomo yao kuhusu ya hema (Rejelea Hatua ya 1 ya maelezo, somo la 22).

Mbele ya Mahali patakatifu palikuwa na nguzo mbili za shaba, moja ilitwa "Yakini" (“ataanzisha”) na ya pili iliitwa “Boaz” (“Nguvu”). Nguzo hizi mbili ziliwakilisha mtu aliyepewa nguvu na kuimarishwa na roho wa Neno la Mungu (tazama michoro, kurasa 31, 32).

Katika Mahali Patakatifu palisimama:

1.Vinara kumi vya dhahabu, vitano kwa kila upande;
2. Meza kumi za dhahabu, tano kila upande, za mkate iliokwa.
3. Madhabahu ya dhahabu ya ubani, ambapo pengine palikuwa mahali mbele ya pazia kabla ya Mahali Patakatifu Zaidi.

Pazia, ambayo iligawanyisha Mahali Patakatifu na Mahali Patakatifu Zaidi, ilizungumzia upatanisho na mafanikio ya Mungu kwa Yesu, na ilikuwa ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na ilitengenezwa kwa kitani nzuri na kupambwa na makerubi.

Katika Mahali Patakatifu Zaidi, mahali pa ukamilifu, palikuwa na makerubi mawili ya dhahabu ambayo yalitizamia pazia na mabawa yao yalikuwa yamenyooshwa, hivyo kwamba yaligusana kwa kila upande wa ukuta. Baada ya kuingia Mahali Patakatifu Zaidi, kuhani mkuu angekuwa ametizama makerubi wenye mabawa yaliyonyooka katikati mwa chumba. Chini ya bawa zilizonyooka za makerubi kulikuwa na Agano ambalo kwa sasa lilikuwa na vipande viwili vya mawe vilizokuwa na amri.

Kando ya Hekalu na samani zake, vitu vingine vya muhimu vilitengenezwa, kama vile, nyungu, vijiko, miiko na majembe. Vitu hivi vilitengenezwa na Hiramu, mfanyakazi mwenye ujuzi wa vyuma kutoka Tiro.
 

HEKALU LINAFUNGULIWA (1 Wafalme 8, 2 Mambo ya Nyakati 5).

Baada ya miaka saba na nusu ya ujenzi, ni lazima lilikuwa tukio la furaha wakati Hekalu lilikamilika na kuwa tayari kufunguliwa. Baada ya kuweka vilivyostahili, Sulemani akaleta hazina  ambazo Daudi babake alikuwa amekusanya kwa ajili ya Nyumba. Kisha akakusanya wazee wote wa Israeli na wakuu wote kushuhudia tukio hili la ajabu la kuletwa kwa Agano na kuwekwa  na katika mahali pake  katika Hekalu. Ilikuwa ni mwezi wa saba ya sikukuu ya Vibanda wakati makuhani walileta Agano, pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa katika hema, na vikaletwa katika mlango wa Hekalu. Pale Sulemani na watu wote  wakatoa sadaka, idadi kubwa ya  kondoo na ngombe ilitolewa kwa Bwana, na kwa mapambo, Agano likapelekwa hadi Mahali Patakatifu Zaidi, ambapo liliwekwa chini ya mabawa ya makerubi.

Kilele cha sherehe za ufunguzi ilikuwa imefikiwa. Wakati makuhani walikuwa wanaondoka katika Mahali Patakatifu, waimbaji wa Asafu, Hemani na Yeduthuni, wana wao na ndugu zao waliimba nyimbo za sifa na shukrani kwa Bwana wakitumia vinanda na vinubi na 120 makuhani wakipiga tarumbeta. Kama walivyomwimbia Bwana “kwa kuwa ni mwema, na fadhili zake ni za milele", Hekalu likagubikwa na wigu, udhihirisho wa utukufu wa Mungu. Utukufu huu ulikuwa mkubwa, hata makuhani wakashindwa kusimama na kuendelea na huduma zao.

 

MAOMBI YA SULEMANI KATIKA KUBARIKIWA KWA HEKALU (1 Wafalme 8, 2 Mambo ya Nyakati 6).

Bila shaka Sulemani alishangazwa na tukio hili kuu wakati alitazama jengo hili tukufu lililojaa utukufu wa Bwana. Hapa kuna kutimizwa kwa Ahadi kuu iliofanywa kwa babake Daudi. Kwa moyo uliojaa furaha, aliinua mikono yake kwa Bwana juu mbiguni na mbele ya  watu wote akaomba sala ya shukrani na sifa. Katika maombi yake Sulemani alisifu fadhila za Bwana kwa uaminifu na huruma yake kubwa ya kuwaruhusu kujenga Hekalu hili kubwa kama Makao yake. Lakini Sulemani alitambua kwamba Mungu hangeweza kuishi katika jengo hilo dogo wakati hata mbigu yote haikumtosha; “lakini Mungu sasa ataishi pamoja na binadamu humu duniani?;  tazama mbigu zote haziwezi kutosha; tizama ukubwa wa nyumba hii niliojenga"(2Nya. 6:18; linganisha Mdo 7: 47-49).

Tambua hili na jinsi taifa lilikuwa  katika nafsi ya Mungu mkuu, Sulemani kisha akamsihi Mungu kutunza nyumba alioijenga kwa Jina Lake, daima kusikiza maombi ya watu wake katika shida na mafanikio. Sulemani aliogopa kwamba historia itajirudia na Israeli watageuka na kutoka katika njia za Bwana. Kwa hivyo akaomba msamaha jambo kama hilo likitokea (2 Nya. 6: 22-39).

Ni muhimu sana, kwamba katika maombi yake Sulemani alifanya kutaja maalum kwamba mgeni yeyote atakaye tamani kumwabudu Mungu wa Isaeli. Hakukuwa na pingamiza kwa Waisraeli katika fikra za Sulemani (mst.32, 33).  Alikuwa na hamu kwamba ulimwengu mzima ungejifunza kuhusu Mungu na kumwabudu kwa Kweli. Hatimaye alitoa wito wa dhati kwa Mungu kusikiza dua zote zitakazo fanywa katika mahali pale na kulinda  kiti cha enzi cha Daudi (Mst.40-42). Kwa Sulemani kuitoa Hekalu kulikuwa  mwanzo wa siku zijazo za utukufu wakati utukufu wa Bwana utajaza dunia nzima na watakatifu wake watavikwa wokovu.

 

KUKUBALIKA KWA MAOMBI YA SULEMANI NA MUNGU NA KUJITOLEA KWA WATU (2 Mambo ya Nyakati 7: 1-11).

Wakati Sulemani alimaliza maombi, moto ukashuka kutoka mbiguni na kuteketeza sadaka. Hapa, katika njia ya ajabu, Mungu alikuwa anawaonyesha Sulemani na watu kwamba maombi yao yalikuwa yamekubalika. Moto kutoka mbiguni and utukufu uliojaa katika Hekalu ulitia alama kwa watu. waliinama chini na kumsifu Bwana, wakisema “kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele" (mst.3).

Ilikuwa ni wakati wa Sikukuu ya Vibanda, ambayo inaongea kuhusu kukusanyika kwa mataifa yote katika shughuli ya Mungu (Zek. 14:16.), ambapo Hekalu lilifunguliwa (2 Nya. 5: 3). Idadi kubwa ya watu ilikuwa imefika kutazama sherehe ya ufunguzi wa Nyumba ya maombi. Sadaka nyingi zilitolewa na Sulemani na watu- Sulemani pekee alitoa ngombe 22,000 na kondoo 120,000. Kulikuwa na nyimbo na kusifu. Unaweza kupata hisia za furaha katika maneno yafuatayo “ na katika siku ya tatu na ya ishirini ya mwezi wa saba aliwatuma watu kwa hema zao,wakiwa na furaha na kuchangamka moyoni kwa wema ambao Bwana alikuwa amewaonyesha Daudi na Sulemani, na kwa Israeli na watu wake. Hivyo Sulemani akamaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; yote  yaliokuwa ndani ya moyo wa Sulemani kufanya katika Nyumba ya Bwana, na nyumba yake akayafanikisha "( 2Nya. 07:10; 11)
 

MUNGU ANAMUONYA SULEMANI (1 Wafalme 9: 1-9, 2 Mambo ya Nyakati 7: 12-22).

Mungu alikuwa ameonyesha kukubali Kwake kwa maombi ya Sulemani kwa kutumia moto kutoka mbiguni. Baadaye akamtokea Sulemani usiku na maneno ya kumtuliza na kumuonya. Alisisitiza ahadi yake ya kubariki Israeli, kama wangemgeukia kwa Kweli, akamwambia Sulemani kwamba macho yake yatakuwa daima yamefunguliwa na masikio yake yatasikia maombi yatakayo tolewa katika Nyumba yake. Hata hivyo mambo ambayo yalimkabili Sulemani na watu wake yalikuwa wazi. Kama Sulemani angetembea mbele ya Mungu kama vile Daudi babake alikuwa amefanya, basi Mungu angekuwa pamoja naye and ufalme wake ungedumu; “Hakutakosa mtu wa kuwa kiongozi katika Israeli” (mst.18) Kwa upande mwingine, kama Sulemani akageuka na kutoka kwa njia ya Bwana na kuacha amri za Mungu au kuanza kuabudu miungu mingine, basi sio tu Hekalu tukufu lingekuwa bure lakini pia Waisraeli wangetolewa katika nchi yao na kuwa wa kudharauliwa na mataifa.

Kwa onyo kama hili, ungefikiria kwamba Sulemani angeshika njia ya Ukweli, lakini pia yeye alitoka kwenye njia ya Bwana na utabiri wa kutisha ulioandikwa katika Mambo ya Nyakati.7: 20-21 ukatimia.

HEKALU YA SULEMANI MFANO WA HEKALU YA SIKU ZA USONI

Hekalu la Sulemani lilijengwa kama mahali pa kuishi pa Bwana, lakini pia ilionyesha alama na mifano  ya jinsi Waisraeli wa kweli watakavyo enda mbele ya Bwana na hivyo pakakuwa mahali pa kuishi pa Mungu. Katika Hekalu ya siku za baadaye litaloanzishwa Yerusalemu, Waisraeli na watu wa mataifa walio waaminifu watapata mahali pa kuishi milele katika uwepo wa mwana mkuu wa Daudi, Bwana Yesu Kristo.

Kuna mafunzo mengi ya kiroho yanayopatikana katika ujenzi wa Hekalu la Sulemani. Maandiko yanaonyesha Hekalu kama mfano wa Nyumba ya maombi kwa mataifa yote kuanzishwa wakati Kristo atakaporudi. Maelezo kamili ya Hekalu Tukufu yametolewa katika katika Ezekieli 40-48. Kuna zoezi la kuvutia la kujaribu kuchunguza mafunzo mengi na ya Hekalu ya Sulemani. Baadhi yameandikwa hapa chini;-

  1. Jiwe la Hekalu lilichongwa kutoka milima ilioko karibu na Yerusalemu mbali na Hekalu na kuletwa hadi sehemu ya ujenzi. Vivyo hivyo watakatifu, viumbe vya duniani, wameundwa kwa neno la Mungu ili wawe mawe yalio hai ya Hekalu la kiroho la Mungu (1 Pet. 2: 5; Efe. 2: 19-22).
  2. Mbao aina tatu zilitumika. Mwerezi, ukiwa wa kudumu, ulimaanisha hali ya kutoharibika (Zaburi. 92:12). Mti wa Miberoshi ulikuwa wenye nguvu, na ulisimamia Nguvu zilizotoka kwa Mungu (Hab. 3:19). Mzeituni, ambao unazalisha mafuta taa, ni ishara ya ufunuo wa Mungu na ukweli (Zek. 4:. 3). 
  3.  Waisraeli na watu wa mataifa walihusika, Isaiya anaeleza kuwa sio kusaidia kujenga hekalu la siku la baadaye tu “Wageni”, (Isa. 60:10), lakini "utukufu wa Lebanoni" utashuka na kurembesha nafasi ya mapumziko ya Mungu.
  4. Tiro alimsaidia Sulemani, na katika ulimwengu ujao, Tiro wa wakati huo atakuwa mmoja wa wale watakao msifu yule atakuwa mkuu kuliko Sulemani (Zab. 45:12.).
  5. Sulemani hakujenga Hekalu tu, lakini pia alitengeneza nyumba ya mwana wa Farao, mke wake (1 Fal. 7: 8). Wale wanaofikia maisha ya milele, baada ya kutoka katika Misri ya kiroho, pia watapata mahali pa kuishi  na Kristo kama "bi harusi" (Zab. 45: 10-11, 14-15).
    Zaburi 45 inaweza kuwa msingi wa ndoa wa Sulemani binti ya Farao.
  6. Kama vile utukufu wa Bwana ulijaa ndani ya Hekalu wakati wa sherehe ya ufunguzi, hivyo Ezekiel anaonyesha kwamba Hekalu ya Siku za usoni itajaa utukufu wa Bwana (Eze. 43: 4).
  7. Sulemani alitamani Hekalu iwe nyumba ya sala, sio tu kwa waisraeli lakini “ kwa watu wote duniani” (2 Nya. 6:33). Hekalu la siku zijazo bila shaka itakuwa “nyumba ya Maombi kwa mataifa” wakati utukufu wa Mungu utajaa dunia nzima(Isa. 56: 6-8.).
  8. Ufunguzi wa Hekalu la Sulemani ulikuwa wakati wa sikukuu ya Vibanda. Mwaka hadi Mwaka watu watakuwa wanaenda hadi Yerusalemu kumwabudu Bwana na kuweka sikukuu ya Vibanda (Zek. 14:16.).
     

MAMBO TUNAYOJIFUNZA:

  • Ingawa Hekalu la Sulemani lilikuwa jengo tukufu, halingekuwa na manufaa yoyote kama mioyo ya Sulemani na  watu wa Israeli haingekuwa sawa mbele ya macho ya Mungu. Daima kulikuwa na hatari ya kudhania kwamba Jengo lile lilishirikisha utakatifu bila kujali mtazamo wao.
  • Sisi pia, kama vijana wa Mungu, lazima tutambue kwamba Eklezia hawawezi kutupatia haki, lakini ni mtizamo wetu wa kibinafsi ambao ni wa muhimu mbele ya macho ya Mungu. Kuna hatari  katika kuweka dhamani  katika mtizamo wa nje, wakati Mungu anaangalia roho ya mtu “Maana Bwana asema aliye juu na anayeishi milele, ambaye jina lake ni takatifu; Ninaishi mahali patukufu, pamoja na yule mwenye roho ya kunyenyekea,  kufufua roho ya walionyenyekea na pia kufufua mioyo wa wale waliotubu "(Isa. 57:15).
     

MAKTABA YA KUREJELEA:

  • "The Story of the Bible" (H.P. Mansfield)—Tol.4, Nam. 8
  • "Law and Grace" (W.F. Barling)— Sura. 5
  • "Law of Moses" (R. Roberts)—Kur. 95-154

MASWALI YA AYA:

  1. Vitu gani vinafananishwa na jinsi Sulemani alitumia watu wa mataifa  katika ujenzi wa Hekalu?
  2. Kwa njia gani Hekalu la Sulemani lilikuwa tofauti na Hema?
  3. Ni masomo gani tunayosoma katika sala ya Sulemani wakati wa ufunguzi  wa Hekalu?
  4. Ni onyo gani Mungu anatoa kwa Sulemani wakati ambao Hekalu linafunguliwa rasmi?

 

MASWALI YA INSHA:

  1. Toa maelezo ya Hekalu la Sulemani na samani zake na kwa kifupi, na utoe muhtasari wa masomo ya kiroho tunayopata.
  2. Elezea jinsi ujenzi na ufunguzi wa Hekalu la Sulemani ulifafanishwa na Hekalu la siku za usoni.
  3. Ni pointi gani kuu Sulemani anagusia katika maombi yake wakati wa kutakaswa kwa Hekalu? Nini ilikuwa jibu la Mungu? Kwa kifupi elezea mambo tunayojifunza katika mambo haya.
     

Katika mwaka wa nne wa utawala wake, Sulemani akajenga  “ nyumba ya Bwana”. Kama hema hapo awali, msingi, samani na  huduma za kikuhani zilikuwa kama mafumbo ya kazi ya ukombozi ya Kristo kabla ya kuwekwa wazi -"kivuli cha mambo ya mbinguni" (Kut. 25:40; Ebr. 8:. 5; 9: 9. 23, 24). Lilikuwa jengo zuri sana na likakuwa kipenzi cha taifa (1 Nya. 22: 5, 1 Fal. 10: 5; Isa. 64:11.). Maelezo ya msingi wake na kutakaswa kwake yameandikwa mara mbili  (1 fal. 5-8; 2Nya. 2-7.).

Utawala wa Sulemani ulitabiria ule wa  Messia na Hekalu iikuwa mfano wa “Nyumba ya maombi kwa mataifa yote” itakayo jengwa na mwana mkuu zaidi wa Daudi na mridhi (Isa. 56: 7; 2 Sam. 07:13; Zak. 6:12, 13).

ENEO: Mlima Moriah, ambapo awali Ibrahimu alikuwa “amemtoa” Isaka, na Daudi  alikuwa amefanya sadaka ili pigo lisitishwe (linganisha 2 Nya. 3: 1; 1 Nya. 21: 22-30, 22: 1; Mwa. 22 : 2, 14; Kum.12:11)

WAKATI WA UJENZI; ulianza mwezi wa pili wa mwaka wa nne wa Sulemani na ulikamilishwa katika mwezi wa nane wa mwaka wa kumi na moja (1 Fal. 6: 1, 37, 38; 2Nya. 3: 2).

NGUVU-KAZI: Maseremala, wabeba mizigo na wachogaji mawe walitoka Israeli na Tiro, wakati  maafisa wakuu walikuwa watumishi wa Sulemani (1 Fal. 5: 6, 13-18; 2Nya. 2:17 linganisha Isa. 60: 10-13).

MPANGO WA JUMLA: Sawia na Hema, lakini vipimo vya msingi vilikuwa mara mbili zaidi na mapambo ya dhamani zaidi.

VIPIMO VYA NDANI:   Urefu wa mita 60, upana wa mita 20 na urefu wa mita 30. Hekalu Ilikuwa imegawanyishwa katika sehemu tatu; Mahali Patakatifu Zaidi, Mahali Patakatifu, na Mahakama.

  • Kuta zilikuwa zimetengenezwa na mawe ya kuchibwa na  kuchongwa kwa ajili ya ujenzi. Kisha kulainishwa na mierezi, makerubi, mitende, maua na buyu zilizofunikwa na dhahabu (1 Fal. 6: 7, 15, 18, 21, 29).
  • Sakafu ilitengenezwa na miberoshi  na kufunikiwa na dhahabu (1 Fal. 6:15, 30).
  • Paa zilitengenezwa kwa mihimili na mbao ya mierezi na kufunikwa na dhahabu (1 Fal. 6: 9, 22).
  • Milango ya Mahali Patakatifu Zaidi ilitengenezwa na Mzeituni na kuchongwa pamoa na mkerubi, mitende na Maua yaliyo wazi na ilifunikwa na dhahabu (1 Fal. 6: 31-32).
  •  Milango ya Mahali Patatifu ilkuwa miwili iliotengenezwa na miherezi na ilikuwa imeundwa sawia (1 Fal. 6: 33-35).

 

NYENZO — MAANA YA KIROHO

  1.  JIWE:  Mawe haya yalichukuliwa kutoka ardhini na yakachongwa kulingana na maagizo ya Mungu. Kwa njia sawia waumini,  “mawe yaliyo hai” ya nyumba ya kiroho ya Mungu watalewa kwa watu wa mataifa na kutayarishwa  kama makazi ya Mungu ya kudumu (1 Fal. 6: 7; 1 Pet.2: 5; Yn. 14: 23).
  2.  MBAO.
    Mwerezi- wa kudumu= na usioharibika (Zab. 92:12; 1 Kor. 15:53​​.).
    Mberoshi- Wenye nguvu= Nguvu za Mungu (Efe. 6:10;. Hab.3:19).
    Mzeituni- ulitoa mafuta yalioangaza mahali patakatifu= ufunuo wa dunia ya Kiroho (27:20 Kut; Zab. 119:. 130; Neh. 9:20, 30; Zek. 4:14; Mdo. 10:38 , Ufu.1:20).
     
  3. VYUMA: Dhahabu ilitumika rasmi katika Mahali Patakatifu na Mahali Patakatifu Zaidi (tazama maelezo ya Mahali Patakatifu Zaidi) Shaba ilitumika katika Mahakama (tazama maelezo ya madhabahu ya Shaba)

MAHAKAMA YA NJE

Mahali ambapo ibada iliyokubalika Ilianza= UTAKASO WA FIKRA

Vyombo Maalum:

  1. MADHABAHU YA SHABA (2 Nya. 4:. 1). Ilikuwa “Patakatifu Zaidi” (Kut. 29:37.) = Kristo (Ebr. 13:10). ilifanya “Takatifu” kile kilichogusa (Ebr. 2:10). Ilikuwa ni kitu cha kwanza ambacho kilizuia njia ya moja kwa moja  hadi Mahali Patakatifu na ilizungumzia mahitaji ya kujitolea katika altari ya Kristo (Rum 12:. 1, 2). Shaba= Dhambi ya mwili (Hes. 16: 38-39; 31: 22-23; 21: 8; Kut. 38: 8; Ebr. 2:14; Rum. 8: 3).
     
  2. BAHARI ILIYOYEYUKA (2 Nya. 4: 2-5; 1 Fal. 7: 23-26.) Sawa na Birika. Mikono na Miguu (matendo na kutembea) ya kuoshwa na maji (= Neno la Mungu, Efe. 5:26; Mdo.26:16), Kabla madhahabu ya shaba kufikiwa (Zab. 26:6; Kut.30:18 -21). Kulikuwa na  Ngombe dume 12 (12 = makabila ya Israeli, na ng'ombe = huduma). Kabla sisi tutoe ibada ya kukubalika ni lazima tuoshwe na kuelimishwa na Neno (Yn.15: 3; 17:17).
     

BIRIKA KUMI na nguzo zake (1 Fal. 7:. 27-39). Kulikuwa na tano kwa kila upande wa mahakama, na  zilitumika kuosha sadaka za kuteketezwa (2 Nya. 4: 6; Law. 1: 9).

NGUZO MBILI za shaba mbele ya Mahali Patakatifu (1Fal. 7.: 15-22). Moja iliitwa Yakini (= ataanzisha) na Boazi (=Nguvu) Ziliwakilisha “mwili” uliosafishwa na kupewa nguvu na kufanywa  kusimama kwa ukombozi wa Mungu(Ufu; 3:12; Dan. 10: 18-19; 12:13).

KUPAA (1 Fal. 10.: 5) Ebr. "Ola", neno linalotafsiriwa  "sadaka ya kuteketezwa" (linganisha Eze. 40:26.). = kujitoa kwa huduma ya Bwana na kwa hivyo harufu tamu kwa Mapua yake (Efe. 5:. 2).
 

MAHALI PATAKATIFU

Ilikuwa katikati, katika hatua ya pili, na sehemu ya KUOSHWA KWA NAFSI ilihitaji wakati mtu anatembea kuelekea kwenye ufalme wa Mungu (1 Yn. 3: 3). Ilikuwa ni fumbo la kiroho kwa Israeli katika hali ya kuwa katika uhusiano wa mkataba na Mungu. Madhabahu ya shaba na bahari iliyoyeyushwa ziko nyuma na uwepo wa Bwana upo mbele yetu.

Vyombo Maalum:

1. TAA KUMI za dhahabu, tano kwa kila upande wa Mahali Patakatifu (2 Nya. 4:. 7, 1 Fal. 07:49.) = Yesu na Ekklesia ambaye mwanga wa ujuzi wa Ukweli kusambaa katika ulimwengu wa giza (2 kor. 4: 6; Yn. 1: 9; Flp. 2:15, Ufu. 1:20; Mt. 5: 14-16; 4 Kum. 6; Zab. 119:. 105; Ufu. 06:23 ).

MAFUTA- yalitolewa na Waisraeli wote, na hivyo taa ilisimamia taifa (Kut. 27:20, 21.).

MATAWI SABA – Saba ilikuwa nambari katika Agano la Musa na hivyo walikumbushwa uhusiano na Mungu (5:15 Kum; Kut. 31: 16-17; Law. 26: 15,18, 21, 24, 34,35). Pia inasimamia ukamilifu wa maarifa na hekima ya kumtumikia Mungu (Ufu. 4: 5; 5: 6; Zek.4: 2; 3: 9).

KUMI – ukamilifu, Hitimisho (Luka 19; 13; Mwa. 31: 7; Hes. 14:22; Dan.1:20; Zek. 08:23; Law 26:26, Ayu. 19: 3; 1 Sam 1 : 8). Hivyo “ kumi” inahusishwa na taa zenye mwanga, zinazowakilisha Kristo,  ambaye ndani yake hekima inakamilika (Kol 2: 8-10; 1 Kor. 1: 18-24, 30.).

2. MEZA KUMI YA MIKATE ILIOKWA (2 Nya 4:. 8, 19, 1 fal. 07:48.),na mikate 12 kila upande (Law. 24: 5-9.). 12 = 12 makabila ya Israeli; mikate = sadaka ya chakula, matunda ya kazi zao; na Haruni na makuhani waliwakilisha Mungu. Wakati makuhani walikula “Mkate wa Mungu”  (Law. 21: 6)., Mungu alikuwa mfano wa kukubali tunda la kazi yao. Ubani kwa mkate uliochomwa, na kutoa harufu ya kupendeza, kuonyesha kuridhishwa kwa Mungu (Law. 24: 7).  Mkate ulibadilishwa “kila Sabato”- siku ambayo ilikuwa “Alama ya Agano” ukumbusho wa kuokolewa kutoka kwa utumwa (Kum. 5:15; 31:16 Kut, 17).

3. Madhabahu ya kufukizia uvumba wa mierezi yaliyofunikwa na dhahabu (1Fal. 6:22). Kupaa kwa Uvumba = Maombi ya watakatifu katika madhabahu ya Kristo (Zab. 141: 2; Lk. 1: 7-10; Ufu. 5: 8 ; 8:34).  Ilikuwa ni ya makao ya ndani ama Mahali Patakatifu (1 Fal. 6:22). Hivyo "sala" zilifika “mbiguni” (Ebr 6:19;. 9:24). Ni moto kutoka kwa madhabahu ya shaba ambayo yangetumika katika mafunzo yakiwa maombi yanakubalika tu katika  hali ya kusamehewa dhambi  kupitia Kristo. Hakuna  “Uvumba mgeni” ulikubaliwa- ila tu ule ambao ulikuwa umekubaliwa kutumika (Kut. 30: 9, 34; Law. 16:12; Mt. 4:12 na Yn.15: 4-5).

PAZIA (2 Nya. 3:14) Ebr. "paroketh" = "kutengana". Ilikuwa kizuizi kilichowagawanyisha Waisraeli na Mungu. Kwa hivyo ilikuwa ni ishara inayofaa ya umuhimu wa Sheria ya Musa kuvuka mipaka ya mwili na kuwapa uhai (Gal. 3:21; Rum. 8:3). Hivyo inawakilisha “mwili” na sheria ambayo iliwatenganisha na Mungu (Ebr. 10:20). Ilikuwa imetengenezwa na sanda nyeupe (= haki za watu wa Mungu, Ufu. 19: 7-8) na kuzungushwa na rangi ya Buluu (= Sheria ya Mungu, Hes. 15:38) Zambarau (= ukombozi, Yn. 19: 2) , na nyekundu (= binandamu na dhambi, Isa 1:18; Mt. 27:28; Law. 14: 4, 6). Kanuni ya upatanisho ilifanywa katika mwili wa Kristo na kwa utii kamili pazia likapasuka na kufungua njia ya Mahali Patakatifu Zaidi (Ebr.2: 10-14; 5.: 5-8; 10:20; Mt. 27:51).

MAHALI PATAKATIFU ZAIDI

Hatua ya mwisho, lengo la maisha ya kiroho ya Israeli, inawakilisha -
(1) Uwepo wa Mungu au "Mbingu yenyewe" (Kut. 25: 21-22; Ebr 6:18-20; 9:24).
(2) UTAKASO WA KIMWILI, hali ya kutoharibika, kutokufa katika ufalme (Ebr. 10:34; Kol. 3: 3-4; 1 Kor. 15: 50-54).

Vyombo Maalum

1. UMBO - Mraba kamili (1Fal. 6:20) = Iklezia amekamilika, na kuwa mmoja na Mungu (Ufu. 21:16, 3).

2. DHAHABU – iliyofunika kila kitu. Ni ya thamani na isiyoharibika na inasimamia utajiri wa "urithi usioharibika, na usio na hitilafu" - uzima wa milele (1 Pet 1: 4-7; Ufu. 21:18; Zab. 45: 9, 13), na pia imani iliodhihirika, na ambayo hali ya maisha ya milele inapatikana (Ufu. 3:18; Ayu. 23:10).

3 Makerubi (1 Fal. 6: 23-28) = Iklezia amekamilika, umoja wa mwili wa Kristo-, sasa baada ya kukamilisha lengo (Eze. 1; 43.: 1-3; Ufu. 4: 7; 5: 9- 14). Katika hema mbawa  zilitupa kivuli juu ya kiti cha rehema, lakini hapa mbawa zimenyooka, kukubaliana na kipengele cha ufalme wa Sulemani (1 Fal. 4:21, 24, 34).

4 AGANO – ilikuwa imewekwa meza za kudumu za agano (2 Nya. 5:10) = Makao ya Mungu  matakatifu(Hes. 7:89, 80 Zab: 1; 2 Kor. 5:21; Yn. 1:14, "anaishi" = "hema").

5. KITI CHA REHEMA = Kristo, ambapo Mungu atakutana nasi (Kut. 25:22;.. Rom 3:25 "suluhu" = "kiti cha rehema"). Mungu ni kiumbe mwenye maadili na atakutana nasi tu kwa msingi wa mapenzi yake ya maisha matakatifu kama ilivyo elezewa katika amri 10 zilizoandikwa juu ya mbao mbili za mawe chini ya kiti cha rehema.

6. MITI iliwachwa katika agano na ilichomoza katika Mahali Patakatifu (1 Fal 8: 8). Hivyo ilikuwa tayari kwa  safari na somo  tunalosoma katika Hekalu la Sulemani  ni kwamba hapa hapakuwa mahali pake pa mapumziko, bali ni mahali pa maskini na wenye majuto moyoni, ambao wananyenyekea kwa Neno lake (Mt. 7:. 47-49; Isa. 66: 1 -2; 2 Kor. 6:16).

Kiti cha rehema kilimwagiliwa damu ya kutakasa mara moja kwa mwaka ili kupata msamaha (Law. 16:. 14-15). Hivyo hakuna ushirika ulikuwa unawezekana ila kwa misingi ya "kumwaga damu". Hata hivyo baada ya kutakaswa, basi, "ushirika" na Mungu ulipatikana, kama kuingia katika Mahali Patakatifu zaidi kunavyoashiria.

MAFUNZO YA JUMLA yameonyeshwa katika Kut.25:8, “Wacha wanifanye mimi ngome yao ili niweze kuishi pamoja nao”. Hekalu lilionyesha jinsi binadamu anaweza patanishwa na Mungu. Kwa upande wa nje wa mahakama, Binadamu alikuja; na  katika Mahali Patakatifu, Mungu alikaa. Hatua ambazo ziko katikati  zinaonyesha jinsi binadamu kwa, kufuata masharti ya  Mungu naweza kupata ukombozi na hatimaye maisha ya milele. Hivyo Mtakatifu Zaidi anawaashiria Waisraeli kuja mbele na kusimama kama lengo. Hapa palikuwa kama uhai wa mahali patakatifu uwepo wa Bwana Mwenyewe, hali hii inafaa kwani inonyesha ushirika na Yeye Ambaye aliwaokoa Waisraeli na kuonyesha utukufu wake kupitia kwao.

NYUMBA YA KWELI

Hekalu la Sulemani lilikuwa la kupendeza na Mungu alikuwa ameonyesha utukufu wake ndani yake, haingeweza kutoshea nafsi. Hata wajenzi walitambua hili (1 Fal. 8:11., 27). Hakuna nyumba iliojengwa na binadamu ingeweza kutosha nafsi yake, lakini Yeye Mwenyewe  amekiri kwamba ataishi pamoja na binadamu “wale wenyenyekevu na wenye  roho nzuri” (Isa. 57:15; 66.: 1-2). Kwa imani amepata nafasi ndani ya nyoyo zao na utiifu wao unadhihirisha kwamba yupo pale. (Efe. 3: 16-19; 2:. 21-22). "Kwa mtu yeyote anayenipenda, atashika maneno yangu; na babangu atampenda, na tutakuja kwake na kuishi naye” (Yn.14:23).

Uovu ulisababishwa utukufu wa Mungu kuondoka katika Hekalu la Sulemani na Wababeli wakaliharibu (Eze. 10: 4, 18, 19; 11:23, 2 Fal. 25: 8-17). Katika mahali pake Mungu akaweka jiwe la msingi la nyumba tofauti kabisa: "Tazama, naweka katika Sayuni jiwe la msingi, jiwe lililojaribiwa, Jiwe la pembeni, la msingi hakika". Binadamu, kama mawe yaliyo hai, wamealikwa kujenga juu yake kwa msingi wa imani: "Yeye aaminiye hatafanya haraka" au kuwa na aibu (Isa 28:16; Rum. 9:33, 10.: 11-12; Efe. 2: 19-22; 1 Pet. 2: 4-7).. "Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu ... Yeye aliye na sikio, na asikie".

MAKTABA YA KUREJELEA:

"Story of the Bible" (H.P. Mansfield) tol. 4, Nam. 8.

"Law and Grace" (W.F. Barling) Sura 5

"Law of Moses" (R. Roberts) pp. 95-154.

Inapatikana kama nyongeza ya Biblia kutoka maandiko ya huduma ya Kristadelfiani.

 

Swahili Title
305. HEKALU YA SULEMANI
Sub type
Sub sub type