342

Swahili

342.  MFANO WA KUTAFUTA “WALIOPOTEA"

“Itakuwa furaha kubwa mbuguni kwa ajili ya kila mwenye dhambi anayetubu . . .”

 

Yesu alisisitiza jinsi lilikuwa jambo la muhimu kwa yule anayetaka kuwa mwanafunzi wake;  kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyonayvo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Lk 14:33).

Majibu ya ombi lake yalitoka katika kundi fulani la watu wa Israeli- watoza ushuru wote na wenye dhambi wakamsongelea wale na yeye: " (Lk 15: 1). Ilikuwa ni Mafarisayo na walimu wa Sheria waliotaka kumdhoofisha Yesu “Mtu huyu anawakaribisha wenye dhambi na anakula nao” (Lk 15: 2) waliona makosa kwa sababu alishirikiana na watu ambao waliwafikiria kuwa hawafai kuwa miongoni mwa watu wenye haki.

Kutokana na hali hii Yesu alitoa msururu wa mifano mitano inayoitwa “mifano ya waliopotea” (Lk. 15 na 16). Tutangalia mifano mitatu ya kwanza. Tazama Luka 15:3 inasema, “na Yesu akawaambia mfano huu” Neno “huu” linamaanisha mifano yote mitatu ya sura 15 na sio wa kwanza pekee. Mifano yote inazungumzia hadithi moja lakini inaelezea pande mbalimbali. Tizama kwamba inanenwa “kwao” yaani Mafarisayo na walimu wa Sheria.

Lengo la somo hili ni kuonyesha jinsi huruma za mungu ni kubwa kwa wale wanaotubu.

 

Luka 15

MWANAKONDOO ALIYEPOTEA (Lk. 15:3-7)

Katika mfano wa kwanza wa Yesu aligusia ujuzi wao kuhusu kuwatunza kondoo: “ Ni nani kwenu, akiwa na kondoo mia moja, agundue kwamba mmoja amepotea, atafanya nini? Ila kuwaacha wale tisini na kenda na kwenda kumtafuta aliyepotea, mpaka atakapompata?”. Hili lazima liwe lilikuwa jambo la kawaida, la sivyo hadithi haingekuwa na athari inayofaa. Lakini kwanini wangewaacha kundi nzima la kondoo kumtafuta mmoja aliyepotea? Kwa sababu kila mmoja alikuwa wa dhamani halisi, kibiashara na ingawa ilikuwa kwa maksudi au kwa ajali, kondoo  amepotea hii ilikuwa hasara kwa mchungaji. Hivyo basi kwa umakini usiogawanyika na kwa nguvu zake zote ingebidi kumtafuta “aliyepotea”. Angepanda juu ya milima, apite juu ya vichaka, kwa jua linalochoma au baridi ya usiku, akiita na kusikiza “mlio” utakaompa matumaini,  “mpaka atakapo mpata” (Mst4).

Anapompata, uchungu na uchovu wa mchungaji unaondolewa  na “furaha” na mzigo mzito mabegani mwake unakuwa mwepesi kwa sababu ya furaha ilio moyoni mwake (Mst.5).  Baada ya kurudi nyumbani huwaita marafik na majirani zake wajiunge naye katika kusherehekea.

MAANA

Mungu ni mchungaji na sisi ni kondoo malishoni mwake. Wasiwasi wake kwa ajili yetu unaonyeshwa katika juhudi zake zake zisizo na kifani ili tubaki katika sehemu ya kaya yake. Huzuni yake wakati sisi “tunapotea” inatoshana na nia yake ya “Kututafuta” aturejeshe (2 Pet 3:9). Mafarisayo na walimu wa Sheria walijiona kuwa walinzi wa sheria ya Mungu, lakini hawakuelewa nia ya Mungu ya kupanua uwezo wake wa kuokoa wote. Waliweka watu kwenye makundi ya “walio na dhambi” (Mst.2), na walifikiria kwamba kuwa na haki kulihusisha kuwa tofauti na wao. Hawakuona haja ya kuiga bidii ya wachungaji ya kwenda kwa wale “waliopotea” kwa dhambi, na kuwahimiza kutubu. Wakati Yesu aliwaelezea kile Mungu aliwahitaji kufanya, walisema alikuwa “Mtenda dhambi”, kwa sababu alijihusisha na  wale wasiowapenda.  Walijiona kuwa “wenye haki” wasiohitaji kutubu (Mst.7)! Waliongezea dhambi zao kwa kushindwa kuwatafuta wale “Waliopotea” na kwa kuwakemea wale walivyofanya hivyo. Katika mahali pengine Yesu aliwaita " makaburi chokaa ", Wasafi kwa nje lakini wanafiki kwa ndani.

Mungu hawezi kuwaokoa wale “wenye haki yao wenyewe”, kwani hawakuona haja ya kutubu, na walijiona wazuri kuliko wengine. “Viongozi” wa Israeli walikuwa kwa kundi hili. Mungu hakukubaliana na maoni yao. Alihitaji binadamu kila mahali kutubu. Hapo awali Yesu alikuwa ameonya: maana haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi n mafarisayo hamtingia kamwe katika ufalme wa mbiguni (Mt. 5:20).

MFANO WA SARAFU ILIYOPOTEA (Lk. 15:8-10)

Mfano huu unafanana na ule wa kwanza lakini funzo ni tofauti kidogo. Mwanamke akiwa na sarafu kumi za shaba apoteze moja (Mst.8). Wakati huu sarafu  haina uhai na haina wajibu wa kupotea uliokuwa na kundi lililotajwa kama; Kondoo “alienda” nyikani, lakini sarafu ilipote ndani ya nyumba. “Nyumba”  inawakilisha inawakilisha nyumba ya Mungu, au Iklezia. Iklezia pia inawakilishwa na mwanamke, bibi harusi wa Kristo, "mabikira" nk, na hivyo kuna wajibu kwa upande wake kuangalia watu wa jamaa yake. Sarafu ina dhamani, lakini wakati inapotea, “haielewi” dhamani yake halisi.

MAANA

Katika siku ile mfano huu ulinenwa, dhamani ya sarafu ilikuwa kubwa. Hivyo ndivyo kila mtu katika familia ya Mungu ana dhamani kwake. Hivyo basi Ikklezia lazima awe na uhakika kwamba kila mtu anachangia sehemu yake kwa mwili nzima. Kama ndugu “amepotea” katika nyumba, anashiriki shughuli za Eklezia lakini hachangii dhamani yake ya kweli. Kama vile mwanamke “huwasha mshumaa”, hivyo Iklezia lazima ahakikishe kwamba Neno la Mungu linasemwa na kutendwa. Mwanga wa Neno unapenya katika giza la maisha yetu, na kufagiliwa kwa ufangio kunafunua vumbi, kutoka kwa sarafu iliyopotea. Kufagia kwa chumba kunawakilisha bidii ya ndugu katika kuongea neno katika msimu, katika kutembelea mayatima na wajane,n.k. Lazima  tufanye kazi kwa ajili ya wema wa wengine, kuongeza thamani ya nyumba na kuhakikisha kwamba hakuna inayopotea. Kufurahia kunaofuatia kupatikana kwa sarafu na mwanamke akawaita majirani zake kufurahikia nao. Hivyo pia kuna furaha wakati wenye dhambi anatubu (Mst.10) au ndugu  “aliyepotea” katika Iklezia anafufua maslahi yake, bidii na mchango wake katika jamii.

 

MFANO WA MWANA MPOTEVU (Lk. 15:11-32)

Yesu anaunganisha mifano hii miwili  na watatu ambao unaelezea vizuri zaidi kuhusu masuala halisi ya maisha. Katika mfano wa Mwana Mpotevu “aliyepotea” hakua mnyama ama chombo kisichokuwa na uhai, lakini kijana, na yule aliyempoteza ni baba. Masomo haya kwa hivyo ni ya maana.

Hadithi hii inaonyesha kijana mdogo akiondoka katika nyumba ya babake na kwa Ukweli na kwenda kutafuta raha za dunia katika "maisha ya uasherati." Wale ambao wanafanya hivi wanapoteza “mali”  na siku moja wakakumbana na “ukame mkuu”- wahisi upungufu na majuto ya nafsi (Mst.14). Alikuwa maskini, amerarukiwa na yatima: “akawa akitamani kijishibisha na maganda ambayo nguruwe walikula” (Mst.16).

Akiwa amefika mwisho akakumbuka hali yake ya hapo awali. Alifikira kwamba ingekuwa bora zaidi kama angejinyenyekeza na kurudi nyumbani na kuwa mtumishi wa kuajiriwa. Katika mstari wa 18 anaonyesha maana ya kweli ya kutubu; kukiri dhambi, na kutambua kutofaa kwake kupokea baraka kutoka kwa babake.

Baba yake, hata hivyo, alitamani kurudi kwake, na licha ya kupita kwa mda, alitizama viwanjani akitumainia kwamba mwanawe aweza kurudu. “Alipokuwa angali mbali’ babake alimwona! Hii inaonyesha jinsi Mungu anawatafuta wale walipotea. Alikuwa amejawa na huruma na alikimbia kukutana naye. Akamwangukia shingoni na kumbusu sana (Mst.20). Akiomba kwamba huruma kama hio haifai na sio haki, kijana mdogo alitaka baba yake apunguze furaha yake. Lakini pingamizi zake hazikufaulu. Neema juu ya neema, baraka juu baraka zilipewa kwake. Baba yake alimpa joho nzuri, pete kidoleni na viatu miguuni. Akatoa amri kuchinjwa kwa ndama aliyenona na kufanya karamu. Kulikuwa na sherehe kubwa na sababu ilitolewa: “Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana" (Mst24).

Baada ya kuonyesha kwa mara nyingine  jinsi Mungi anafurahi pale mwenye dhambi anatubu, mfano unarejelea nduguye mkubwa. Alisikia sauti za sherehe na kutaka kujua sababu yake.  Maelezo aliyopewa na watumishi inaoyesha jinsi ndugu wanapaswa kuwaangalia wenzao katika huduma ya Ukweli: “ ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona kwa sababu amempata akiwa yu mzima (Mst.27) Hasira ya nduguye mkubwa ilionyesha roho yake ilikuwa tofauti na ya babake; “alikataa kuingia ndani” kushiriki katika katika sherehe (linganisha Mathayo 21:31-32).

Kiwango cha uvumilivu wa Mungu kinaweza kuonekana kutokana na ukweli kwamba baba “alitoka na kumkumbatia”. Kijana mkuu alionyesha kuchukizwa kwake kwa sababu ya “kukosa haki” kwa baba yake na maneno yake yanaonyesha jinsi alivyotambua hali yake mwenyewe ya haki; miaka hio yote, mimi nimekutumikia, wala sijakosa amri yako wakati wowote: lakini hujanipa hata mwana-mbuzi nisherehekee na marafiki zangu” (Mst.29). Alitambua yote aliyokuwa amemfanyia babake. Alikuwa amesahau mapendeleo aliyokuwa amepokea kutoka kwa baba yake na alimtia babake kwenye deni la huduma yake kwake. Alichukuliwa kwamba malipo lazima yawe katika misingi ya sheria na kazi liyofanyika, na hakuweza kutambua roho ya neema. Hakuweza kuelewa kwanini baba yake anaweza kumsamehe na kumtukuza mtu ambaye alikuwa mwovu na aliye asi.

Jibu la baba lilimhakikishia usahihi wa matendo yake kuelekea kwa mwana yule mpotevu,na kwa wakati ule ule akamwomba mwanawe mkuu atambue roho yake: “ ilikuwa inatubidi tufanye sherehe, na tufurahi kwani ndugu yako alikuwa amekufa na sasa amefufuka; alikuwa amepotea na sasa amepatikana” (Mst.32).

Kuna kejeli ya kutisha katika mfano huu. Kijana mkuu, aliona kiburi kwa kuwa mtiifu wakati aliwekwa katika mtihani wa undugu wa kweli, alikuwa “amepotea”, alishindwa kufurahia juu ya kubadilika kwa roho kwa ndugu yake. Hapa palikuwa na kijana kwenye nyumba, lakini alikuwa “amepotea”, kama ile sarafu moja. Aliwakilisha wenye haki binafsi “kundi la mafarisayo” wa umri wote.

Ndugu mdogo hapo awali hakutambua dhamani halisi ya utajiri wa kweli. Baada ya muda alipata ufahamu na kutubu, na akajitupa kwa huruma ya baba yake. Aliwakilisha “Watoza ushuru na wenye dhambi ambao walimsogelea” na kutubu dhambi zao za njia yao ya maisha ya hapo awali na kufuata maisha ya Bwana wao mpya (MSTl) 

MAMBO TUNAYOJIFUNZA:

  • Mungu anatupenda na anasikitika wakati sisi tunatoka katika Ukweli.
  • Yeye ni mpole wa hasira na anatamani kurejesha wale waliopotea. Mapenzi yake ni kila mtu aokolewe (1 Tim 2: 4).
  • Inawezekana  "kupotea" wakati bado tuko katika nyumba ya imani.
  • Ndugu mkubwa alikuwa "amepotea" kwa sababu alishindwa kutambua na kuonyesha neema ya baba yake.
  • Lazima sisi, kama Mungu, tutafute na kuwaokoa wenye dhambi, hata kama wamemwondokea Mungu na kwenda mbali sana (Yak. 5: 19-20).

 

MAKTABA YA KUREJELEA:

"Parables of the Messiah" (J. Carter)—Nam. 72-74

"Nazareth Revisited" (R. Roberts)—Kurasa. 252-254

MASWALI YA AYA:

  1. Kwa nini Yesu aliongea kuhusu mifano ile mitatu "Mifano ya Wapotevu?
  2. Ni masomo gani tunayojifunza kutokana na mfano wa mwana kondoo aliyepotea?
  3. Ni masomo gani tunayojifunza kutokana na mfano wa sarafu iliyopotea?
  4. Nini, kilikuwa na makosa na tabia ya ndugu mkubwa katika mfano wa mwana mpotevu?

MASWALI YA INSHA:

  1. Andika insha kulinganisha mifano ya kondoo aliyepotea, sarafu iliopotea na mwana mpotevu.
  2. Katika Mifano ya Wapotevu, ni nini majibu ya mchungaji, mwanamke na baba wakati:
    a) kondoo, sarafu na mwana, wanapotea kwa mpangilio huo?
    b) Baada ya mwanakondoo, sarafu na mwana, kupatikana? Je, majibu haya yana maana gani kwako?
  3. Elezea mfano wa Mwana Mpotevu, ukiweka mkazo juu ya masomo ya binafsi ambayo yanaibuka kutoka humo.
  4. Jinsi gani neema ya Mungu ilionyeshwa katika mifano ya mitatu ya wapotevu?
  5. Jinsi gani mfano wa Mwana Mpotevu unaleta vyema masomo ya mifano ya  Mwana-kondoo aliyepotea na Sarafu iliopotea?
  6. Nini masomo gani ya kibinafsi na mashauri gani yanayoibuka katika "Mifano wa Wapotevu?

 

 

Swahili Title
342. MFANO WA KUTAFUTA “WALIOPOTEA"
Sub type
Sub sub type