340

Swahili

340. USO WA YESU UNAGEUKA

"Huyu ni mwana wangu mpendwa, msikilizeni"

Katika Kaisarea Filipi, Yesu aliweka matumaini ya Kimasihi kwa wanafunzi wake kwa mtazamo unaofaa. Ilikuwa kweli kwamba Yesu alikuwa Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Lakini pia hii ilimaanisha ni lazima angeteseka kabla ya kupata utukufu wa Ufalme. Wafuasi wa Yesu hawakuelewa hili na hivyo Yesu kuanzia wakati huu alisisitiza kwamba Msalaba lazima uje kabla ya taji.

Wafuasi wake walichanganyikiwa kusikia kwamba lazima angeteseka mambo mengi  na kwamba matumaini yao ya kwamba ataokoa Yerusalemu hivi karibuni yalionekana kuwa mbali katika siku za usoni. Lakini ingawa hawakuwa sahihi, ni wachache waliopendelewa wangeonja ufalme huo: “Amini amini nawaambieni kwamba, kuna baadhi katika hawa wamesimama hapa,ambao hawataonja mauti,  mpaka watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa Nguvu  (Mk. 9: 1).

Lengo la somo hili ni kuona jinsi kugeuka sura kulimsaidia Yesu kustahimili msalaba, na jinsi maono yaliyo wazi ya Ufalme wa Mungu yatatusaidia sisi pia kushinda ulimwengu.

Marko 9:1-32

 YESU AWACHUKUA WANAFUNZI WATATU MLIMANI

Yesu aliwaambia wanafunzi  wake kwamba kuna wale kati yao ambao hawatakufa kabla wauone ufalme wa Mungu ukija kwa Nguvu. Je, alimaanisha nini? Katika injili tatu pale ambapo maneno haya yanapopatikana, yanafuatia na kugeuka sura kwa Yesu. Basi tunabaki bila shaka yeyote kuhusu kile Yesu alikuwa anaashiria. Petro anaelezea kwamba tukio hili la kugeuka sura kwa Yesu kunadhibitisha utabiri wa Yesu wa “Nguvu na Ujio” wa Bwana (2 Pet. 1: 16-18).

Tunasoma kwamba Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana hadi juu ya mlima faraghani peke yao (Mk 9: 2). wafuasi hawa watatu walikuwa  wana bahati ya kuwa na Yesu katika tukio la muujiza wake mkubwa zaidi na baadaye wangeshiriki naye huzuni yake kuu (Mk. 14:33). Hatujaambiwa ni mlima gani ambao Yesu na wafuasi wake walienda, lakini wilaya ya Kaiserea Filipi imejaa milima, na kulikuwa na milima mingi iliyojitenga katika upande wa Labanoni iliyofaa shughuli hii waliokuwa nayo. Yesu alijua kile kingetokea kule mlimani, na Luka anatwambia walipofika mlimani Yesu alianza kuomba (Lk. 9:28). Kwa kufanya hivi alidumisha umoja wa fikra na Baba yake. Pengine, aliwaombea wanafunzi wake. Alikuwa amewaleta mlimani kama mashahidi, ili waweze kuongezwa nguvu ya kuendelea na kazi baada ya Yeye kupaa. Lakini wakati Yesu alikuwa akiomba, wafuasi wakahisi uchovu na kwa vile kulikuwa usiku wakalala (Lk 9:32).

USO WA YESU UNAGEUKA (Mk. 9:2-3).

Yesu aliendelea kusali na alipokuwa akisali jambo la ajabu likatokea. Marko anatuambia kwamba sura yake iligeuka (Mk 9: 2). Maana yake alibadilika umbo. Kwa kuunganisha rekodi kutoka kwa Injili tatu, tunajifunza kwamba mavazi ya Yesu yaligeuka na kuwa  “meupe mno kuliko barafu, na hakuna kitu duniani kulikuwa cheupe kuyaliko”, yakimetameta na kung’aa. Uso wake wote ukabadilika na kungaa kama jua  (Mt 17: 2; Mk 9: 3; Lk 9:29).

Maneno haya yanatumika kwengineko kuelezea utukufu wa kiumbe chenye uzima  wa milele. Danieli anaelezea wale watakao pata uzima wa milele kama “ wang’aao kama mwanga wa jua” (Dan 12: 3). Yesu hapo awali alisema maneno sawa; kisha, wale wema watang’aa kama jua katika Uflame wa Baba yao” (Mt. 13:43). kwa Malaika aliyeondoa jiwe kutoka kwa kaburi la Yesu ilisemwa kwamba "uso wake ulikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji" (Mt. 28: 3).Hivyo kwa kipindi kifupi Yesu anawaonyesha Utukufu na Nguvu zilizoahidiwa kwake baada ya msalaba.
 

MUSA NA ELIYA WANATOKEA KWA UTUKUFU (Mk. 9:4).

Musa na Eliyaa walitokea ghafla katika utukufu na kuongea na Yesu kuhusu kifo chake, ambacho angemalizia Yerusalemu (Lk. 9: 30-31). Kutokea kwa watumishi hawa wawili wakuu wa Mungu,  Musa akiwakilisha Sheria na Eliya akiwakilisha manabii, bila shaka hili lilikuwa jambo la kutia moyo kwa Yesu kwani siku ya kusulubishwa kwake ilikuwa inakaribia. Hawa wawili walisimama juu ya Mlima Sinai katikati mwa mtetemeko wa ardhi na moto na walisikia Jina la Bwana likitangazwa (Kut. 34: 4-7; 1Fal. 19: 8-12). lakini sasa walinena na yule aliyekuwa anawakilisha Sheria na Manabii- neno likafanywa Mwili.

Wakati Yesu, Musa na Eliya walikuwa katika mazungumzo wanafunzi wake wakaamka. Ili kusisitiza utukufu mkuu wa Yesu, Luka anaandika: Waliona utukufu wake, na wanaume wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye” (Lk 9:32). Ilikuwa muda mfupi baadaye wakati wanafunzi walitambua kwamba utukufu wa Kristo ni mkubwa.

Watatu hawa walikuwa wamepata neema kuona utukufu kama huo. Kwa kweli "Ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu" kama vile Yesu alivyosema.

MUSA NA ELIYA WANAANZA KUONDOKA (Mk. 9:5-6).

Tukio hili lilikuwa la muda mfupi. Musa na Eliya wakaanza kuondoka. Petro, kwa mshangao hakuwa anataka hili litokee, akamlilia Yesu, “Bwana ni vyema sisi tuwe hapa: ni bora tujenge vibanda vitatu, kimoja chako, kingine cha Musa na kimoja cha Eliya ; bila kujua alichokisema” (Lk. 9:33).

Pengine Petro alifikiria kwamba kutokea kwa Yesu katika utukufu pamoja Musa na Eliya ilikuwa ishara kwamba utukufu ulikuwa karibu. Lakini wakati Musa na  Eliya walioondoka, matumaini yake yalikatizwa. Kwa haraka, bila kujua alichokuwa akinena, alipendekeza kwamba  vibanda vitatu vijengwe ili wakae mle- kimoja cha Yesu, kingine cha Musa na kingine cha Eliya. Bila kutambua alikuwa amewatoshanisha watatu hawa. Mungu angelekeza fikra zake kwa Mwana wake Mpendwa kama mkuu kuliko wote.

Lakini Petro hakuwa ameelewa tukio hili kwa kikamilifu. Ufalme ungekuja kwa wakati uliowekwa na Mungu. Kwa sasa, walikuwa watambue kwamba utukufu lazima utanguliwe na sadaka ya Mwana wa Mungu ambaye alikuwa amekuja kutimiza Sheria na Manabii.

TANGAZO LA MUNGU (Mk. 9:7-8)

Wakati Petro alikuwa anaongea wingu jeupe likawaghubika. Sauti ikazungumza nao kutoka kwa wingu, "Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa naye, msikilizeni" (Mt. 17: 5., Lk.9:34, 35) wanafunzi waliposikia sauti ile wakaanguka kifudifudi, wakiwa wamejawa na woga. Wakati Yesu alifika akawagusa, akasema, "Inuka, msiogope" (Mt. 17: 6, 7).  Walipoinua macho yao, Yesu pekee ndiye aliyebaki (Mt. 17: 8; Mk 9: 8). Musa na Eliya walikuwa washaondoka- Kwa kweli Yesu alikuwa mkuu. Na hadi Musa alikuwa amesema kwamba Kristo ndiye ambaye kila mtu anapaswa kusikiliza (Kum. 18:15). Miaka mingi baadaye Petro alikumbuka matukio haya kama ushahidi kwamba hawakuwa wanafuata hadithi tu (2 Pet 1: 16-18). Tukio hili halingesahaulika kamwe na wafuasi hawa watatu.

ELIYA KUJA KWANZA (Mk. 9:9-13)

Siku iliyofuata Yesu aliwakataza watatu wale na kuwaambia “msimweleze yeyote kile kilichotokea, hadi Mwana wa mtu atakapofufuka kutoka kwa wafu” (Mt. 17:9). Lakini maneno “kufufuka kutoka kwa wafu” yaliwashangaza. Wafuasi walionekana kuwa na mtizamo kwamba Yesu angekuwa nao milele (Yn.12:34).  Walishindwa kuweka kifo na ufufuo katika mtizamo wa Masihi. Maswali mengine yaliwatatiza. Kwanini Eliya alikuwa kwenye Mlima? Je si angepaswa kutokea kabla “siku kuu na ya kutisha ya Bwana?" (Mai 4: 5-6). Jinsi gani Masihi angeweza kufa baada ya kutokea kwa Eliya?

Hivyo basi wakamuuliza Yesu: “ kwanini Waandishi hunena kwamba  Eliya yuapaswa kuja kwanza?”  (Mk. 9:11). Yesu akawaambia kwamba ni kweli Eliya atakuja kwanza “kurejesha upya yote” kabla ya siku ya Bwana (Mt. 17:11). Lakini andiko pia limetabiri mateso ya Mwana wa Mtu kabla ya siku hiyo kubwa.

Yesu alielezea kwamba, Eliya alikuwa ametokea kwa mfano wa Yohana mbatizaji. Yohana alihubiri "katika roho na nguvu ya Eliya" (Lk. 1:17). Yeye alihubiri kutubu kabla ya kuja kwa Yesu, na alikuwa amefariki. Kama walivyomfanyia Yohana, ndivyo wangemfanyia Bwana wake (Mt. 17:12).

Hivyo Yesu hakupinga mafundisho ya Waandishi kuhusu Eliya. Aliwaonyesha kwamba andiko halikuongea kuhusu mtangulizi kabla ya kurudi kwa Kristo katika utukufu, lakini kabla ya mateso na kifo chake.

UGOMVI KATIKA MKUTANO NYIKANI (Mk. 9:14-19)    

Yesu na wanafunzi waliteremka na kuwakuta wanafunzi waliobaki. Waliaibika kwa sababu hawakuweza kumponya mtoto aliyekuwa kiziwi na aliyeteswa na kifafa (Mk.9:17, 18). Wafuasi walikuwa miongoni mwa umati na Waandishi walikuwa wanawauliza maswali, walimkimbilia wakiwa na  matumaini kwamba angeweza kumponya. Waandishi pia walikuja kwa Yesu.  Walikuwa wakiwakejeli wafuasi, na walinyamaza pale Yesu aliwauliza, “Mnajadiliana nini na wao?” (Mk. 9:16). Ikabaki kwa Baba aliye na majonzi kuelezea: “Bwana, nimemleta mwanangu, ambaye ana pepo bubu,  na kila ampagaapo humbwaga chini; naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe; wasiweze (Mk 9: 17-18). Tazama tofauti iliokuwepo katika utulivu kule mlimani na kuteseka na ghasia huku chini nyikani. Na Kama akitamani wakati wa Ufalme, Yesu aliwakemea wote- akiwakejeli Waandishi, wafuasi wasioamini, baba mwenye wasiwasi- “Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Niandamane na nyinyi hadi lini? Mleteni kwangu” (Mst. 9). Kukemea hakukuwa kukataa.

YESU ANAMTIBU YULE MTOTO (Mk. 9:20-29)

Mtoto aliletwa kwa Yesu, lakini alipomwana Yesu “alianguka chini na kutokwa na povu” (Mst.20). maneno ya babake yalidhibitishwa.

Hapakuwa na shaka kwamba Bwana alimwonea mtoto yule huruma, lakini kwa muda alikuwa anatafakari kuhusu imani ya baba ya yule mtoto ambayo ingeweza kumwokoa mwanawe. Kulikuwa na hali ya ghasia na wasiwasi ambayo haifai kwa imani. Yesu alitaka kuwe imani ya kutosha kabla atende muujiza. Alimgeukia baba ya yule mtoto na kumuuliza ni kwa muda gani mtoto alikuwa kwa hali ile. “tangu utotoni”, alijibu, na ili kujaribu kumhimiza Yesu zaidi kuhusu haja ya kumtibu, aliendelea kuelezea jinsi mwili ulivyopoteza nguvu katika viungo vyake vyote, akianguka kwa moto na maji (Mst. 21-22).  Kwa shaka aliongezea:  “lakini ukiweza nena neno lolote, basi tuonee huruma na utusaidie” (Mst.22). Alitilia shaka nia na uwezo wa Yesu.

Hakukuwa na haja kwake yeye kusihi huruma kutoka kwa Yesu, Miujiza yake ilionyesha alikuwa na ruhuma na nia. Hivyo swali halikuwa kama Yesu alikuwa na nia; lakini swali lilikuwa kama mtu yule angeamini. Yesu  alibadilisha msisitizo wake kwa imani ya mtu yule kwa swali; “ yote yanawezekana kwa mtu yule anayeamini” (Mst.23)! Changamoto hii ilikuwa na matokeo mazuri kwani kwa unyenyekevu wa fikra ya baba yule alilia kwa machozi. “Bwana, Naamini, kutokuamini kwangu” (Mst.24).

Hili ndilo Yesu alilotaka kuona: imani kama ya mtoto ambayo inaweka imani yote kwa nguvu za Mungu kuokoa. Mungu anatarajia hayo kutoka kwetu. Inaonekana katika tukio hili Yesu alikuwa amemvuta yule mtu na mwanawe kando na umati. Aliona watu wakiwajia tena, hakuchelewesha kuamuru “Pepo bubu na kiziwi” kumtoka yule mtoto (Mst.25) kwa hili kijana akatoa kilio, na kutetemeka kwa kifafa, kwa nguvu na kuzirai. Watu walidhani kuwa amekufa, tunaweza elewa hisia za babake wakati waliposema kwamba  “amekufa” (Mst.26) Lakini Yesu alisema, “kwani nyinyi hamwamini...” akamshika kijana mkono na kumwinua na kurejesha kwa baba yake akiwa mzima kabisa (Mst.27: Lk 09:42).


MAMBO TUNAYOJIFUNZA:

  • Tukio la kugeuka kwa sura lilikuwa jambo la kumtia moyo Yesu alipoweka uso wake kuelekea Yerusalemu. Mwandishi wa Waebrania anaelezea kuwa "kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake" Mwana wa Mungu "alivumilia kifo msalabani, bila kujali aibu" (Ebr 12: 2).
  • Sisi hatujaitwa kuteseka kama Mwana wa Mungu, lakini picha ya utukufu wa ufalme inaweza kututia sisi motisha. Inatusaidia kuona thamani ya kuhudhuria mambo ya Mungu na kuweka "vivutio" vya dunia hii katika mtazamo unaofaa.
  • Tukio la mtoto mwenye kifafa linatufundisha kwamba imani ambayo Mungu anahitaji ni ilio na nguvu, ambayo inafuta tu ufalme wa Mungu na haki yake. Kwa imani tunaweza fanya mambo yote, na kukanyaga kwa kujiamini kwa njia ambayo itatuongoza kwa ufalme.

MAKTABA YA KUREJELEA:

"A Life of Jesus" (M.Purkis)—Kitabu 5, Sura 8

"Nazareth Revisited" (R. Roberts)—Sura 37

"The Gospel of the Son of God" (L. G. Sargent)—Kitabu V, Sura 1
 

MASWALI YA AYA:

  1. Yesu alimaanisha nini aliposema: "... Eliya anakuja kwanza kutayarisha yote... Lakini nawaambia kwamba Eliya amekwisha kuja nao walimtendea jinsi walivyotaka"?
  2. Kwa nini Yesu alimwambia baba mtoto mwenye kifafa, "Kama unaweza, amini, mambo yote yanawezekana kwake aaminiye"?

MASWALI YA INSHA:

1. Orodhesha lengo la kugeuka uso:
(a) kwa Kristo
(b) kwa wanafunzi.
2. Orodhesha matukio ambayo yalitokea wakati Yesu aligeuka sura.
3. Elezea uponyaji wa mtoto mwenye kifafa. Ni masomo gani tunaweza kuchukua kutokana na tukio hili?
4. Eliya na Musa walikuwa pamoja na Yesu juu ya mlima wakati wa kugeuka sura. Kwa njia gani ilionyeshwa kwamba Yesu alikuwa mkuu wa wote watatu?
5. Furaha iliyowekwa mbele ya Yesu ilimwezesha kuvumilia msalaba. Ni sehemu gani ya kugeuka sura ilionyesha hili? Kwa nini muhimu kwetu?
 

Swahili Title
340. USO WA YESU UNAGEUKA
Sub type
Sub sub type