Jinsi ya Kuhubiri
Jinsi tunavyohubiri hufanya tofauti kubwa kwa jinsi tunavyokuwa na matokeo. Ikiwa sisi ni wakali, tukikasirika kwa urahisi au kutumia lugha mbaya, haitaleta hisia nzuri.
Paulo alimshauri Timotheo, “Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli” (2 Timotheo 2:23-25).
Watu husikiliza walimu wenye fadhili na wenye kupendeza. Tunapaswa kujibu watu, “kwa upole na kwa hofu.” (1 Petro 3:15). Ni lazima “wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.” (Tito 3:2).
Hatuwezi kutarajia kila mtu tunayekutana naye atupende. Yesu alieleza tatizo, “Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.” (Yohana 3:20). Kama vile si kila mtu alimpenda Yesu, ndivyo sivyo wote watatupenda. Yesu alituambia tena, “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.” (Yohana 15:18).
Hata tukikutana na watu wenye hasira na wasio na adabu, hatupaswi kukasirika sisi wenyewe. “watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.” (1 Petro 3:9). Paulo anasema, “Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.” (1 Wakorintho 4:12,13). Hivi ndivyo tunavyoonyesha sisi ni tofauti nao, na jinsi tunavyowafundisha kwa tabia zetu.